Header Ads

JINA LA NYERERE LISITUMIKE VIBAYA

Happiness Katabazi

HAKUNA ubishi kwamba jina la mhasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na picha yake, tangu atutoke Oktoba 14 mwaka 1999, hadi sasa baadhi ya wananchi wamekuwa wakivitumia kwa ajili ya kukidhi matakwa yao.


Wengi miongoni mwa wanaotumia jina la Nyerere na picha yake kwenye taasisi zao wamekuwa wakifanya hivyo kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Kwa makusudi kabisa, wameamua kutumia jina la Mwalimu kwenye shughuli zao kibiashara kama shule, bahati nasibu, mihadhara mbalimbali kwa kigezo cha kumuenzi.

Ieleweke wazi kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiiga sera, mavazi misimamo na matendo yaliyokuwa yakitendwa na kuvaliwa njuga na viongozi wa kisiasa wa mataifa mbalimbali duniani na pia wamekuwa wakisimama katika matendo sahihi yaliyokuwa yakifanywa na viongozi hao ambao wengi ni waasisi wa mataifa yao.

Lakini leo hii hapa nchini kwetu mambo yamekuwa ndivyo sivyo, wengi wetu tumekuwa tukiwaenzi viongozi hao kwa maneno badala ya vitendo, hukariri yaliyofanywa na waasisi hao kwa ajili ya kujibia mitihani na tukishamaliza, yanahama kwenye vichwa vyetu.

Tunaimba sera walizoziasisi siku za kumbukumbu za vifo vyao na pindi tunapotaka kuomba fedha kwa wafadhili. Baadhi ya wanasiasa wakati wa kampeni husimama majukwaani wakiomba kura wananchi na kutamba kuwa wanamuenzi Nyerere kwa vitendo wakati kwenye uchaguzi ndio vinara wa kutoa rushwa.

Tukubaliane kimsingi kwamba hadi sasa nchi yetu bado haijatunga sheria ya kudhibiti matumizi holela ya picha ya Nyerere na jina lake, hivyo hata hawa wenzetu wanaotumia jina na picha hiyo kwa ajili ya kuchumia matumbo yao, wanakuwa hawajavunja sheria zozote za nchi yetu kwa hiyo wanaendelea kupeta.

Licha serikali yetu kipindi cha nyuma kuahidi kwamba inakusudia kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ya kuthibiti matumizi yasiyo sahihi ya jina na picha ya Mwalimu, lakini hadi leo serikali haijatueleza mchakato huo umefikia wapi.

Na matokeo yake hivi karibuni tumeshuhudia chama kipya cha siasa, CCJ kilichopewa usajili wa muda mapema wiki iliyopita, nyuma ya kadi za chama hicho kuna picha ya Mwalimu Nyerere.

Katika mazingira kama haya ya taifa kutokuwa na sheria ya kuthibiti matumizi holela ya picha ya mhasisi wa taifa hili, kadiri siku zinavyosonga mbele vyama vya siasa vipya vitasajiliwa na kutumia picha ya Mwalimu Nyerere kiholela. leo ni CCJ kadi yake inapicha ya Nyerere, kesho watatokea Watanzania wengine wataanzisha vyama vya siasa ambavyo kadi zao pia zitakuwa na picha ya mhasisi huyo au marais wengine wastaafu au wataweka picha za waasisi wa vuguvugu la vyama vingi nchini.

Aidha kadri miaka inavyozidi kusonga mbele, ndiyo watanzania wanavyozidi kuvumbua mbinu mpya za kujiingizia kipato. Wataibuka watu waanzishe madanguro, nyumba za kulala wageni na biashara nyingine haramu kisha wazibatize jina la Mwalimu Nyerere au majina ya marais wastaafu.

Na hili linawezakana, ni suala la muda tu, tusubiri tuone. Kwani hata hao wanaoongoza vyama vya siasa na wanaojigamba wanamuenzi Nyerere kwa vitendo hawastahili kabisa kujinasibu kuwa wanamuenzi kwani miongoni mwao wanakabiliwa na tuhuma za ukosefu wa maadili, ikiwemo rushwa.

Na tukiruhusu tufikie huko, tukae tukijua wazi heshima na hadhi ya viongozi wetu hao wa nchi itaporomoka.

Nihitimishe kwa kutoa rai kwa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwamba wakati umefika sasa wa Bunge lake kutunga sheria ya kudhibiti matumizi holela ya picha ya mhasisi wa taifa hili, na iainishe picha na jina linatakiwa litumikeje au wanaotaka kulitumia jina hilo kwa ajili ya shughuli zao za kibiashara ni vyema wakaomba ridhaa kwa familia yake na wale wanatakaobainika kulitumia vibaya wakumbane na mkono wa dola.

Naomba kutoa hoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano la Machi 10 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.