Header Ads

RAIA WA KIGENI KORTINI KWA DAWA ZA KULEVYA

Na Happiness Katabazi

KWA mara nyingine tena serikali imewaburuza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, raia wanne wa kigeni wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kuingiza dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 81 zenye thamani ya Sh bilioni 2.8.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mustapher Siyani wakili mwandamizi wa serikali Biswalo Mganga aliyekuwa akisaidiwa Prosper Mwangamila na Theophili Mtakyawa aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Dinnis Chukwudi Okechukwu,Paul Ikechukwu Obi ambao ni raia wa Naigeria, Stani Hycenth raia wa Afrika ya Kusini na Shoaib Mohammed Ayazi ambaye ni raia wa Pakstani ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Brigson Sheiyo.

Wakili Mganga alidai kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili.Shtaka la kwanza ni la kula njama kuingiza dawa za kulevya nchini Tanzania katika kipindi cha Machi 4 mwaka huu na Septemba 26 mwaka jana,katika maeneo tofauti bila kibali cha serikali ya Tanzania washtakiwa hao ambao ni raia wa Nigeria, Pakstani na Afrika Kusini kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama na kuingiza dawa za kulevya hapa nchini.

Mganga alidai kuwa shtaka la pili ni la kusafirisha dawa hizo kuja hapa nchini kinyume na kifungu cha 16(11)b(i) cha Sheria ya Kuzuia dawa za Kulevya ya mwaka 2002 , kuwa Machi 4 mwaka huu, huko Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote waliingiza nchini gramu 81,000 aina ya Heroin yenye thamani ya Sh 2,835,000,000.

Hata hivyo washtakiwa hao hawakutakiwa kusema chochote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo kwani Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi.

Kwa upande wake wakili wa washtakiwa hao, Sheiyo aliomba mahakama itoe amri ya kuwataka polisi warejeshe simu za washtakiwa ili washtakiwa hao ambao ni raia wa kigeni waweze kuzitumia kuwasiliana na ndugu zao.

Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa vikali na wakili wa serikali Biswalo Mganga ambaye alidai kuwa ombi hilo alijaletwa chini ya kifungu chochote cha sheria na kuongeza kuwa kifungu cha 38 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, inawaruhusu polisi kushikilia vitu vya mshtakiwa ambavyo wanaamini vinaweza kuwasaidia kwenye upelelezi wa kesi husika na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri wakusikiliza kesi hiyo.

Akitoa uamuzi wake kuhusu ombi hilo la wakili wa washtakiwa, Hakimu mkazi Siyani alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba na ndiyo maana baada ya upande wa Jamhuri ulivyomaliza kuwasomea mashtaka washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote na kumhoji wakili huyo wa washtakiwa kuwa kama washtakiwa hao wanahitaji simu hizo ili waweze kuwasiliana na ndugu zao ,Je washtakiwa walimpataje yeye aje kuwatetea mahakamani wakati tayari simu zao zilikuwa zimeishaanza kushikiliwa na jeshi la polisi na akaairisha kesi hiyo hadi Machi 21 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Februali 23 mwaka huu, serikali ilifikisha mahakamani hapo raia wanne wakiwamo raia wawili wa Pakstan wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha kilo 179 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.2.

Wakati huo huo;Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Gabriel Mirumbe jana alishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro na wenzake kwasababu ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Boniface Stanslaus kushindwa kutokea mahakamani hapo kwasababu alikuwa akiiudhulia kesi nyingine Mahakama Kuu.

Hakimu Mirumbe alisema kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana na leo na akaiarisha hadi leo ambapo Jamhuri italeta mashahidi wake ili waweze kuendelea kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 8 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.