Header Ads

HUKUMU YA KESI YA PONDA YAOTA MBAWA




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kutoa hukumu ya kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na wenzake 49 kwa maelezo kuwa hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Victoria Nongwa hayupo na wala hajaituma hukumu hiyo kwa uongozi wa mahakama.

Hakimu Mkazi Alocye Katemana ndiye aliyeairisha kesi hiyo ambapo alianza kwa kusema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutolewa hukumu, lakini hukumu hiyo haitatolewa kwasababu hakimu anayesikkiliza kesi hiyo hayupo na wala hajatuma hukumu ya kesi hiyo.

‘Kwa sababu hiyo naairisha kesi hii hadi Mei 2 itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kwamba Mei 9 mwaka huu, itakuja kwaajili ya kutolewa hukumu na hivyo kuamuru mshitakiwa wa kwanza na watano(Ponda na Mukadamu Swalehe) kurudishwa rumande kwasababu hadi sasa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP).Dk.Elizer Feleshi ajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alifika mahakamani hapo tangu saa moja asubuhi ,alishuhudia kundi la watu zaidi ya mia moja wakiwa wamesimama nje ya uzio wa mahakama hiyo karibu na ofisi ya Maktaba ya Taifa tayari wakisubiri kuingia ndani ya geti la mahakama hiyo kwaajili ya kukaguliwa kwa vifaa maalum na wanausalama  ambapo hata hivyo waliruhusiwa na kuingia ndani ya viwanja vya mahakama, lakini ni wafuasi wachache ndiyo walioruhusiwa ndani ya chumba cha wazi Na. mbili cha mahakama hiyo kwaajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya kuarishwa kesi hiyo askari magreza waliondoka na msafara wa magari yao ambao ulikuwa ukiongozwa na askari polisi waliokuwa wamevalia sare na wale ambao hawajavalia sare za jeshi hilo, na wakati wakitoka ndani ya viwanja hivyo tayari kwaajili ya kuelekea katika gereza la Segerea anapoishi Ponda na Mukadamu ,wafuasi hao walianza kupaza sauti huku wakimpungia mkono Ponda na kusema ‘ Takbirii Abkbaru ’.

Aprili 3 mwaka huu:Mawakili wa upande wa Jamhuri ,Tumaini Kweka na Jessy Peter na mawakili wa utetezi Juma Nassor na Njama waliwasilisha majumuisho yao mahakamani hapo kwa njia ya maandishi ambapo mawakili wa upande wa jamhuri waliiomba mahakama iwaone washitakiwa wote wana hatia na wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria.

Wakati mawakili wa utetezi waliiomba mahakama iwaone washitakiwa hawana hatia na iwaachilie huru kwa sababu hawakutenda  makosa yanayowakabili na kwamba upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao.

Machi 21 mwaka huu;Sheik Ponda, mshitakiwa wa tano Mukadamu Swaleh walijitetea.Na washitakiwa wenzake wa nne nao walijitetea siku hiyo na hivyo kufanya jumla ya washitakiwa 48 wa kesi hiyo kumaliza kutoa utetezi wao.Na siku hii ndipo upande wa utetezi walifunga utetezi wao na Hakimu Nongwa aliipanga tarehe ya jana ndiyo angetoa hukumu ya kesi hiyo.

Machi 4 mwaka huu:  Hakimu Nongwa atoa uamuzi wake ambapo aliwaona washitakiwa wote wana kesi ya kujibu na akatupilia mbali hoja ya mawakili wa utetezi iliyokuwa ikidai kesi hiyo ni ya madai na kwamba ifutwe.

Oktoba 18 mwaka jana, Ponda na wenzake walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza ambapo wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano na makosa hayo ni kama yafuatayo.
shitaka la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2012,kwamba Oktoba 12 mwaka huu, huko eneo la Chang’ombe Markasi washitakiwa wote walikula  kwa nia ya kutenda kosa hilo.

Shitaka la pili wakili Kweka alidai linawakabili washitakiwa wote ambalo ni la kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa  kinyume na kiufungu cha 85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu  na kwamba  Oktoba 12 mwaka huu,  huko Chang’ombe  Markasi , kwa jinai  wasipokuwa na sababu  za msingi  washitakiwa hao waliingia  kwenye kiwanja kinachomilikiwa kampuni ya AgriTanzania  Ltd  kwania ya kujimilikisha  kiwanja hicho isivyo halali.

Kabla ya washitakiwa hakubali au kataa shitala hilo Ponda aliripoka na kusema yeye anakanusha shitaka hilo na kwamba washitakiwa wenzake nao wanalikanusha shitaka hilo,jambo ambalo lilikataliwa na Hakimu Sanga ambaye alimrisha kila mshitakiwa ajibu shitaka hilo kwa kinywa chake ambapo kila mshitakiwa kwa kinywa chake alikanusha shitaka hilo kinyume na alivyokuwa anataka Ponda iwe kwa yeye kukanusha shitaka hilo kwa niaba ya wenzake.

Wakili Kweka alilitaja shitaka la tatu kuwa ni  kujimilikisha  kiwanja kwa jinai kinyume na kifungu cha 86 na 35 cha sheria hiyo  na kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu huko Chang’ambe  Markasi  pasipo na uhalali wowote washitakiwa wote  katika hali  iliyokuwa ikipelekea  uvunjifu wa amani  walijimilikisha  kwa nguvu ardhi  ya  kampuni ya Agritanza Ltd.

Shitaka la nne, wakili Kweka alidai ni la wizi  ambalo ni kinyume na kifungu cha 258  cha sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, na kuwa kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu,  washitakiwa hao waliiba vifaa na malighafi,matofali 1500,nondo,Tani 36 za Kokoto vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya Sh 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Aidha shitaka la tano Kweka alidai ni la uchochezi ambalo linamkabili Sheikh Ponda peke yake  ambalo ni kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha sheria hiyo  kwamba kati ya Oktoba 12-16 mwaka huu katika eneo hilo la Chang’ombe Markasi  kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu(T) aliwashawishi  wafuasi wake ambao ni washitakiwa hao  kutenda makosa hayo  na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu pamoja na kuwasomea mashitaka hayo ambayo yanadhamana kwa mujibu wa sheria, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Elizer Feleshi kwa mkono wake amenituma kuwasilisha kwaniaba yake mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana kwa mshitakiwa wa kwanza (Ponda) peke yake chini ya kifungu cha  148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2012’alidai wakili Kweka.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 18 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.