Header Ads

ATIWA HATIANI KWA MAKOSA YA KUFANYA BIASHARA HARAMU YA KUSAFIRISHA BINADAMU



Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imemtia hatiani mfanyabiashara wa ngozi nchini, Salim Ally (61) kwa makosa ya kusafirisha binadamu na kuwatumisha na kumhukumu kwenda jela miaka 10 au kulipa fidia ya jumla ya milioni 17.

Hukumu hiyo ya kesi hiyo ya ki historia na ya kwanza kutolewa katika Mahakama hiyo tangu Sheria ya Usafirishaji haramu binadamu ya mwaka 2008 ilipotungwa na bunge, ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ilvin Mugeta.

Akitoa hukumu hiyo hakimu Mugeta alisema  upande wa jamhuri ambao ulikuwa ukiwakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Arafa Msafiri, Prosper Mwangamila na Hamid Mwanga katika kujenga kesi yao walileta jumla ya mashahidi watano wakati mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu alijitetea yeye mwenyewe bila kuleta shahidi yoyote.

Hakimu Mugeta alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa ilidaiwa mahakamni hapo na upande wa jamhuri kuwa Agosti 8 mwaka 2010 alimsafirisha Abduswamad na wenzake kwenda nchini Yemen na kwenda kuwatumisha kwa nguvu na bila ya kuwalipa ujira wao kinyume na kifungu cha 4(1)a,6(2)c, cha Sheria ya Usafirishaji haramu wa binadamu ya mwaka 2008.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na vielelezo ,mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake na kwamba baadhi ya ushahidi uliotolewa na mshtikakiwa na wakili wa Magafu ulikuwa unatofautiana kwani Magafu katika majumuisho yake alidai Abduswamad  alijisafirisha mwenyewe kwenda Yemen akusafirishwa na mshtakiwa lakini Mshtakiwa katika utetezi wake alidai yeye aliwasaidia fedha washtakiwa kwenda Yemen kwasababu washtakiwa hao walikuwa wakiitaji fedha za kwenda Yemen kufanyakazi kwa mtu mwingine na yeye akaamua kuwapatia kwa makubaliano kuwa wakimaliza kufanyakazi kwa mtu huyo wataenda kufanyakazi kwenye nyumba yake iliyopo Yemen na kwamba fedha hizo alizowaazima watakuwa wakimlipwa katika fedha watakazokuwa wanalipwa kutoka kwa mtu waliyokuwa wamekwenda kumjengea nyumba.

“Mahakama hii inasema upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake kwani ushahidi ulitolewa ambao upande wa utetezi umeshindwa kuupinga umetosha kuifanya mahakama hii iamini kuwa ni mshtakiwa ndiye aliyewasafirisha watu hao kutoka Tanzania kwenda Yemen kuwatumisha bila kuwa ujira na kwasababu hiyo mahakama hii inamtia hatiani kwa makosa hayo”alisema hakimu Mugeta.
Baada ya kumtia hatiani wakili Msafiri alidai mahakama haina rekodi ya mshtakiwa ambayo inaonyesha ni mhalifu mzoefu na kwasababu hiyo hii ni kesi yake ya kwanza kutiwa hatiani na kwamba anaomba mahakama imwamuru mshtakiwa amlipe  faini waathirika(waliosafirishwa) na itoe adhabu stahili.
Kwa upande wake wakili mshtakiwa, Magafu aliomba mahakama isimpe adhabu ya kwenda kutumikia kifungo gerezani kwani mshtakiwa ni mtu mzima sana,ana matatizo ya kiafya na kwamba akifungwa jela ,watanzania watapata hasara kwasababu kodi zao zitatumika kumtunza wakati mshtakiwa huyo hawezi kufanya kazi ngumu.

Aidha Hakimu Mugeta alisema amesikiliza maombi ya mawakili hao na kwamba ana mwamuru Ally kwenda jela miaka 10 au kulipa faini ya Sh.milioni saba pamoja kumlipa fidia Abduswamad na mwenzake sh milioni 10.

Hata hivyo ndugu wa mshtakiwa walilipa kiasi hicho cha fedha na hivyo kumfanya mshtakiwa huyo aliyesota gerezani kwa zaidi ya miezi nane sasa kuwa huru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 29 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.