Header Ads

SERIKALI YAKWAMISHA KESI YA KIBANDA





Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa shahidi wa pili katika kesi ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na wenzake kwasababu wakili Mwandamizi wa Serikali anayeendesha kesi hiyo Prospa Mwangamila kuwa na udhuru.

Wakili wa serikali Beatha Kitau na Inspekta wa Polisi Hamis Said mbele ya Hakimu  Mkazi Waliarwande Lema  aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo leo ilikuja kwaajili ya shahidi wa pili wa upande wa jamhuri kuendelea na kutoa ushahidi na kwamba leo waliwawaleta mashahidi wawili ambao ni Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza toka Kitengo cha Sheria cha jeshi hilo, George Mwambashi na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi(SSP), David Hizza toka Jeshi la Polisj kwaajjli ya kuja kutoa ushahidi wao lakini hilo halitawezekana kwasababu wakili Mwangamila amepata udhuru.
Hoja hiyo haikupingwa na wakili wa utetezi Mabere Marando  ambapo hakimu Lema aliarisha kesi hiyo hadi Desemba 6 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na Januari 14 mwaka 2013 itakapokuja kwaajili ya mashahidi hao kutoa ushahidi wao na kuwataka wafike bila kukosa.

Mbali na Kibanda mshitakiwa mwingine ni mwandishi makala
Samson Mwigamba ambaye ni mwandishi wa makala wa gazeti la Tanzania Daima na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd.

Machi 7 mwaka huu, Wakili Elizabeth Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda. Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo, Mlinzi mmoja aitwaye Said Masudi Amiri (27), amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la wizi wa mafuta aina ya dizeli 125 zenye thamani ya sh 250,000 mali ya Tanzania telecomunication  (TTCL).Inspekta wa polisi Hamis Said alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Oktoba 30 mwaka huu, huko eneo la Ubungo lakini mshitakiwa huyo nalikanusha mashitaka  na alikwenda rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi Novemba 19 mwaka huu,itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 8 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.