Header Ads

KESI YA SHEIKH PONDA KUANZA KUSIKILIZWA NOVEMBA 29




  
Na Happiness Katabazi
KATIBU wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49,jana walikanusha  madai ya upande wa jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa Sh milioni 59  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa Baraza Kuu la Waislamu nchini(BAKWATA), siyo chombo cha kuwakilisha waislamu wote hapa nchini.

Wakili wa washitakiwa hao Mansoor Nassor mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ndiye alikanusha madai hayo kwa niaba ya washitakiwa muda mfupi baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao ambapo ndani ya maelezo hayo alidai BAKWATA ni chombo kinachotambuliwa na serikali na kipo kwaajili ya kuwawakilisha waislamu wote.

“Mheshimiwa hakimu wateja wangu wamenituma nikanushe madai ya kuwa BAKWATA ni chombo kinachotambulika na serikali na kipo kwaajili ya kuwawakilisha waislamu wote”alidai wakili Mansoor.

Kama ilivyo ada ya kesi hiyo ijapo mahakamani hapo, ulinzi mkali ulitawala tangu saa 12 asubuhi ndani,na nje ya viwanja vya mahakama hivyo ambapo wanausalama walisimama getini wakiwa na vifaa maalumu vinavyoweza kumtambua mtu ambaye amebeba silaha zinazoweza kuhatarisha usalama pia ndugu na wadhamini wa washitakiwa hao huku wakiwa wamevalia mavazi ya kanzu na Baibu walianza kumiminika tangu saa 12:30 asubuhi ndani ya viwanja vya mahakama hiyo na kesi hiyo ikaanza kusikilizwa saa 9:011 asubuhi ambapo Ponda na Mkadamu waliletwa asubuhi na maofisa wa jeshi la Magereza waliokuwa wamevalia mavazi maalum ya kujikinga na hatari yoyote, gari la maji ya kuwasha “Kikojozi”  gari za polisi aina ya defenda nne zilizokuwa zimejaa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia zilimleta na kurudisha gerezani Ponda na Mukadamu.

Kabla ya  kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, wakili Kweka alianza kwa kuimbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kubadilisha hati ya mashtaka kwasababu wanamuongeza mshtakiwa mmoja ambaye ni Kiongozi wa taasisi inayoongozwa Ponda, Mukadam Abdal Swalehe(45) ambaye amekuwa mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo ya jinai Na.245/2012 na pia Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi amewasilisha hati ya kumuondoa mshitakiwa 35 katika kesi hii Rashid Omary chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2012, kwasababu hana haja ya kuendelea kumshtaki  Omary hicho kufanya sasa hati ya mpya ya mashtaka kuwa na washitakiwa 50 tu.

Baada ya kumaliza kutoa maelezo hayo Wakili Kweka alianza kwa kuwasomea upya mashtaka yanayowakabili ambapo alisema wanakabiliwa na makosa matano.

Kosa la kwanza alidai ni la kula njama ambalo linawakabili washitakiwa wote,kosa la pili ni kwaajili ya washitakiwa wote ambalo ni la  kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha  85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Oktoba 12 mwaka huu huko Chang’ombe Markas, wasipokuwa na sababu za msingi waliingia kwa jinai kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia ya iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi ambapo baada ya kuvamia waliiba vifaa na malighafi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza na kosa la tano ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo sasa kosa hili la uchochezi litamkabili Mukadamu na Ponda peke yao  kuwa wakiwa ni viongozi wa jumuiya hiyo , Oktoba 12 mwaka huu ,waliwashawishi wafuasi wao watende makosa hayo hata hivyo walikanusha mashtaka yote.

Akiwasomea maelezo ya awali wakili Kweka alidai washtakiwa na makosa hayo na na kwamba BAKWATA  ni taasisi iliyoundwa  ili kutoa miongozo  pamoja inatambulika  kama inawawakilisha  waislamu wote Tanzania.

Kwamba Baraza  chini ya wadhamini wake ,BAKWATA  inamiliki  mali  kama viwanja na majengo mbalimbali  na miongoni mwa mali za BAKWATA  ni kiwanja kilichopo eneo la Chang’ombe Markas Kitalu Na.311/3/4/Block T.

Wakili Kweka alidai  Juni 18 mwaka 2011 ,BAKWATA  kupitia wadhamini  wake waliingia katika makubaliano ya kupangisha  kiwanja hicho cha Chang’ombe kwa kampuni ya Agritanza Ltd  kwaajili ya kuuza au kubadilisha  mali hiyo ambayo ni kiwanja kwa kampuni hiyo.

“Mabadilishano hayo  yaliyofanywa kati ya BAKWATA na kampuni ya Agritanza  yaliambatana na fedha  na kubadilishana kiwanja kilichopo Kisarawe mkoani Pwani na kutokaa na makubaliano hayo  ardhi ya kiwanja kilichopo Chang’ombe Markas  kiliingizwa kisheria kwenye umiliki mpya wa kampuni ya Agritanza’alidai Kweka

Ailiendelea kueleza kuwa Oktoba 12 mwaka huu, baada ya kampuni ya Agritanzaa kuanza kumiliki kiwanja hicho toka mikononi mwa BAKWATA , kampuni hiyo ilianza kukiendeleza kiwanja hicho  ambapo wafuasi wa wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, katika hali ya uvunjifu wa amani walivamia  kiwanja hicho  wakiongozwa na Ponda na mshitakiwa wa tano(Mukadamu).

Wakili Kweka alidai baada ya washtakiwa hao kuvamia kiwanja hicho  walikaa kwenye kiwanja hicho kuanzia Oktoba 12-16 mwaka huu hado Oktoba 16 mwaka huu na wakaaribu msingi uliokuwa umeanza kujengwa na kampuni hiyo  na malighafi zilizokuwa zimeifadhiwa kwenye kiwanja hicho kwaajili ya ujenzi na katika uhalifu huo washitakiwa hao walikuwa wakiongozwa na Ponda na Mukadamu na kwamba tukio lilipotiwa polisi  Oktoba 16  na washtakiwa walikamatwa na polisi wakiwa katika eneo hilo  ambapo Oktoba 18 mwaka huu, walifunguliwa kesi mahakamani hapo.

Akipangua maelezo hayo ya awali, wakili wa washitakiwa Mansoor alianza kwa kudai kuwa wateja wake wanakanusha maelezo kuwa BAKWATA ni taasisi inayotambuliwa na serikali na ipo kwaajili ya kuwawakilishwa waislamu wote na pia wanakanusha kuwa Mukadamu hakufikishwa mahakamani hapo Oktoba 18 mwaka huu, Mukadamu alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 8 mwaka huu na kwamba anaomuombe Mukadamu dhamana kwasababu makosa anayokabiliwa nayo leo yana dhamana.

Wakili Mansoor pia aliomba upande wa jamhuri uzingatie haki za msingi za Ponda kwani wanazifunja haki za kiongozi huyo wa kiroho ambapo wanamfunga pingu hadi anapomuingiza ndani ya chumba cha mahakama na kwamba wanaomba upande wa jamhuri uwapatie maelezo ya mlalamikaji na orodha ya majina ya mashahidi watakaowaleta kutoa ushahidi.

Akipangua hoja hizo kwa vielelezo wakili wa serikali Kweka alieleza kuwa kuhusu ombi la kuwapatia upande wa utetezi majina ya mashahidi na vielezo tutakavyotumia katika kesi hizo haliwezekani kwasababu tayari kuna maamuzi mbalimbali yaliyokwisha tolewa na Mahakama ya Rufaa nchi ambayo yameeleza wazi kuwa upande wa jamhuri haulazimiki kuwapatia upande wa utetezi majina ya mashahidi wake na vielelezo vyake na kuongeza kuwa kifungu cha 192 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 , haielezi kuwa upande wa jamhuri unapomaliza kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa ni lazima uwapatie majina washitakiwa majina ya mashahidi na vielelezo.

Aidha kuhusu hoja iliyoomba Mukadamu apatiwedhamana leo ,wakili Kweka alidai Mukadamu alifunguliwa kesi Novemba 8 mwaka huu na siku hiyo DPP aliwasilisha hati ya kufunga dhamana yake chini ya kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, na kwamba DPP bado hajaiondoa hati hiyo na kwamba jamhuri ni sikivu sana na kwamba wameipokea hoja ya wakili Mansoor kuhusu kutotaka Ponda afungwe pingu mikononi hadi akiwa anaingizwa ndani ya chumba cha mahakama.

Kwa upande wake Hakimu Nongwa alieleza kuwa DPP bado hajaondoa hati ya kufunga dhamana ya Mukadamu aliyoiwasilisha Novemba 8 mwaka huu,na kwamba hati hiyo bado ipo kwenye kumbukumbu za mahakama  na ndiyo masharti ya dhamana hayajabadilika na kwamba hivi sasa Ponda na Mukadamu katika kesi hiyo ndiyo wataendelea kusota rumande kwasababu DPP bado ameendelea kufunga dhamana yake na kuongeza kuwa maofisa usalama watumie njia nyingine za kumlinda Ponda siyo kumfunga Pingu mkono Ponda hadi wanapomuingiza ndani ya chumba cha mahakama.

Aidha hakimu Nongwa aliushauri upande wa Jamhuri ulete idadi ya jumla ya mashahidi  wanaokusudia kuwaleta kutoa ushahidi katika kesi hiyo na kuarisha shauri hilo hadi Novemba 29 mwaka huu, itakapokuja kwaajili shahidi wa kwanza wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 16 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.