Header Ads

BINTI WA KARUME ARUSHA KOMBORA


*Adai Mahakama Kisutu inanuka rushwa
*Asema amewasilisha ushahidi Takukuru
*Asisitiza yu tayari kukabiliana na lolote

Na Happiness Katabazi

BINTI wa Rais, Amani Abeid Karume, ambaye ni wakili wa kujitegemea, Fatma Karume, anayedaiwa kufanya fujo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam juzi, ameibuka na kueleza kusikitishwa kwake na madai hayo huku yeye mwenyewe akitoa tuhuma nzito za rushwa dhidi ya mahakimu wa mahakama hiyo.

Fatma alitoa tuhuma hizo wakati alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na Tanzania Daima jana jioni wakati alipotakiwa kueleza kile kilichotokea katika mahakama hiyo juzi na uamuzi wake, baada ya Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) kutoa tamko la kusikitishwa na tukio hilo na kutaka uchunguzi ufanyike.

Wakili huyo, alisema baadhi ya mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wanajihusisha na vitendo vya rushwa, jambo aliloeleza kuwa alikuwa tayari ameshalitolea malalamiko yake rasmi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akizungumzia matokeo ya mzozo wake huo wa juzi, Fatma alisema alikuwa tayari kukabiliana na hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi yake kwa sababu tu ya kupigania haki anayoamini alidhulumiwa katika misingi isiyofaa.
“Niko tayari hata kufutwa uwakili. Natetea haki yangu ambayo naamini nilinyang’anywa, nimeingia kufanya kazi hii kwa sababu ya kutetea wananchi, hivyo siwezi kuona nikidhulumiwa nikanyamaza kimya. Enzi za utumwa zilishapitwa na wakati, ni bora nikalime nazi kuliko kupoteza haki yangu,” alisema Fatma kwa kujiamini.

Alisema hata kama yeye ni mtoto wa rais, bado anayo haki ya kudai kile anachodhani anadhulumiwa, kwani naye ni mtu kama walivyo watu wengine, na kimsingi akakataa suala lake kuhusishwa na urais wa baba yake.

Kuhusu kuwapo kwa rushwa, binti huyo wa Rais wa Zanzibar alisema anao ushahidi wa kutosha unaomuonyesha mmoja wa mahakimu waandamizi wa mahakama hiyo akiomba rushwa kutoka kwa mteja wake, Sadiq Walji.

“Ninao ushahidi wa uhakika hakimu (alimtaja jina), aliomba rushwa (akataja kiasi cha fedha zilizoombwa na hakimu huyo)…tena alimfuata mteja wangu katika Hoteli ya Sea Cliff Agosti 26 mwaka huu, na alimpatia fedha na akamrekodi bila ya yeye kujua ‘tape recorder’ (kinasa sauti). Hili ushahidi wa sauti yake tulishauwasilisha Takukuru na wamelifanyia uchunguzi kwa muda mrefu.

“Nasema hivi, Mahakama ya Kisutu inanuka rushwa. Inahusisha mahakimu na waendesha mashitaka. Rushwa imetawala pale, tena huyo hakimu kesho (leo) anapelekewa barua yake…mimi siyo mwehu hata kidogo, nasema hili kwa uhakika na serikali na watu wote wajue kuwa Mahakama ya Kisutu pana rushwa kila mahali,” alisisitiza wakili huyo wa kujitegemea.

Akizungumzia madai ya kufanya fujo ndani ya mahakama wakati kesi inaendelea, wakili Karume aliyefika kwa ajili ya kumuwakilisha Walji, kwenye kesi namba 60/2006 ya madai ya mtoto wa miaka miwili iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Addy Lyamuya, alisema hakimu huyo alimkosea, hali iliyosababisha malumbano.

Alisema, Hakimu Lyamuya alitaka kuipanga kesi hiyo tarehe za mbali bila sababu za msingi, jambo ambalo wakili Karume alipingana nalo kwa kuwa Hakimu Adolf Mahay, alikwishatoa uamuzi Agosti mwaka huu kuwa mtoto huyo wa mteja wake anayeishi kwa Saeeda Hassam , awe akiruhusiwa kila Ijumaa kwenda kwa baba yake na kurudishwa kwa mama yake Jumapili.

Fatma alisema licha ya uamuzi huo, mama wa mtoto huyo alikuwa akikaidi amri hiyo, hali ambayo ilimfanya yeye awasilishe ombi la kutaka mwanamke huyo achukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kuidharau amri halali ya mahakama hiyo.

“Licha ya kumuomba hakimu aipange leo, alikataa na kunijibu kwa ukali na akanionyeshea kwa ishara kwamba mimi ni mwendawazimu….nikamuuliza, madaraka hayo nani kampa ya kunionyeshea kwa ishara mimi ni mwendawazimu? Akaanza kuniambia nisimpangie kazi…nikashikwa na hasira na kutoka mahala nilipokuwa nimesimama na kumwambia zama za utumwa zilishapita katika nchi yetu, hivyo siwezi kukubali kuona navunjiwa heshima nikanyamaza kimya na nikamweleza kabisa nakwenda kumshitaki kwa wakubwa wake wa kazi.

Alisema baada ya kumweleza maneno hayo, hakimu alikwenda kumshitaki kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi na pia alikwenda kumshitaki kwa Jaji Kiongozi Amir Manento lakini hata hivyo alisema malalamiko yake hakuwa ameyapeleka kwa viongozi hao kwa maandishi.

“Licha ya kumweleza yote haya, hakimu hakutaka kunisikiliza na badala yake akanionyeshea kwa ishara kwamba, mimi ni mwendawazimu….ndipo nilipomweleza kwamba hawezi kazi na kwamba naenda kumshitaki kwa wakubwa wake wa kazi,” alisema Karume.

Fatma alisema pia kuwa, juzi asubuhi alikwenda kumshitaki Lyamuya kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi, pia alikwenda kumshitaki kwa Jaji Kiongozi, Amir Manento, lakini hata hivyo alisema malalamiko yake hakuwa ameyapeleka kwa viongozi hao kwa maandishi.

“Habari zilizoandikwa jana kwakweli zimeniumiza sana…kwani Lyamuya aliniita mimi mwendawazimu na mbaya zaidi, Mahayi anasema kwamba alijitoa kwenye kesi ninayoitetea kwa sababu nilimfokea. Haya mambo si ya kweli,” alisema Fatma katika mahojiano jana.

Katika tukio la juzi, Fatma alikuwa akituhumiwa kutoa maneno makali dhidi ya Hakimu Lyamuya, hali iliyodaiwa kusababisha hakimu huyo ajitoe kuendelea kusikiliza kesi inayomhusu mwanasheria huyo.

Tukio hilo la aina yake lilitokea katika chumba cha mahakama, wakati hakimu huyo alipotaka kuanza kusikiliza kesi ya madai namba 60/2006 ambayo ilianza kujadiliwa na hakimu huyo juzi hiyo kwa mara ya kwanza, tangu apewe jalada hilo.

Katika kesi hiyo, Fatma anamwakilisha Sadiq Walji, ambaye ni mdaiwa katika kesi hiyo ya madai ya mtoto. Mdai katika kesi hiyo namba 60/2006 ni Saeeda Hassam.

Kabla Hakimu Lyamuya kuanza kusikiliza kesi hiyo, Wakili Fatma, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi kesho, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo.

Kutokana na hali hiyo, hakimu alimtaka karani wake kuangalia kwenye kitabu cha kumbukumbu (diary) kama siku hiyo itafaa kusikilizwa kwa shauri hilo. Hata hivyo, karani alimweleza hakimu kuwa siku hiyo zimepangwa kesi nyingi za kusikilizwa, labda waipange Januari 13, mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa za juzi, Hakimu Lyamuya alikubaliana na maelezo ya karani wake na kumweleza wakili huyo kwamba kesi hiyo itasikilizwa tarehe hiyo.

Baada ya hakimu kupanga tarehe hiyo, Wakili Fatma anadaiwa kuwa alianza kufoka kwa sauti ya juu akitaka mahakama isikilize kesi hiyo jana jambo ambalo Hakimu Lyamuya alilikataa kwa kueleza kuwa hakuwa na nafasi.

Wakili huyo aliendelea kuomba mahakama kupanga kesi hiyo Januari 2 mwakani, ombi ambalo hakimu huyo alilikataa na kumweleza tarehe hiyo mahakimu watakuwa mapumziko, ndipo wakili huyo alipoanza kutoa kauli kali dhidi ya hakimu huyo.

“Kwanza wewe hujui kazi na ni mara yako ya kwanza kuniona mimi… hunijui ni nani, sasa nitakuonyesha… nitaandika barua kwa wakubwa wako wa kazi na kuwaeleza kwamba hujui kazi,” alidaiwa kusema Fatma hiyo juzi.

Kutokana na tafrani hiyo, mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza shauri hilo wala kulipangia tarehe na badala yake jalada la kesi lilirudishwa kwa uongozi wa mahakama hiyo, ili limpangie hakimu mwingine kusikiliza kesi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tafrani hiyo juzi, Hakimu Lyamuya, alisema ameshangazwa na vitendo vya utovu wa maadili vilivyoonyeshwa na wakili huyo na kueleza hajafikiria kuchukua uamuzi wa kumfungulia kesi.

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 23,2007








2 comments:

Anonymous said...

Mbona maswala ya rushwa yanaibuka baada ya yeye kuambiwa alileta fujo?

Anonymous said...

Nam!
Ni dhahili kwamba Karume aliamua kupaza sauti baada ya kutoa takrima ambao fadhila yake haikuzaa matunda. Wote wana kesi ya kujibu. Laiti TAKUKURU wangekuwa wanajua kazi yao haswaaa.... wangepata mengi kutoka ktk mzozo huu.

Shoka kwa nguruwe.... kwa binadamu balaa! Mh!

Powered by Blogger.