Header Ads

DK.MVUNGI:TULICHAGUA BORA VIONGOZI 2005

.Asisitiza Bunge linahitaji wanamageuzi wengi
.Amsifu Zitto Kabwe kwa ushujaa bungeni

Dk. Edmund Sengondo Mvungi, ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye pia alikuwa ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, anazungumzia kwa mapana mustakabali wa mageuzi nchini.Ungana na Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, aliyefanya mahojiano maalum na msomi huyo ofisini kwake hivi karibuni.

Swali: Miaka miwili imepita tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambao wewe uligombea urais wa Tanzania na wewe na wagombea wenzako wa vyama vya mageuzi mlishindwa vibaya katika uchaguzi huo. Kwa nini umekuwa kimya kuhusu mambo mengi yanayotokea nchini?

Jibu: Sijui kama tulishindwa katika uchaguzi ule. Kama ni kushindwa, basi Watanzania tulishindwa vibaya katika uchaguzi ule. Tulishindwa kuchagua viongozi bora tukachagua bora viongozi, tulishindwa kuchagua sera bora za kutuletea mageuzi na maendeleo ya haraka kwa walio wengi tukachagua chama kilichochoka na ambacho hakina sera bora.

Kama kura asilimia 8o za mshindani wangu ni za kweli, basi tujionee wenyewe maana halisi ya kura zile katika utekelezaji wa yale aliyoahidi kwa kila Mtanzania. Maisha bora kwa kila Mtanzania! Bila shaka ukweli unajidhihirisha sasa, maisha bora kwa wawekezaji kutoka nje, kulia na kusaga meno kwa Mtanzania mlalahoi!

Ni kweli nimekuwa kimya kwa kuwa nimerejea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo nafundisha sheria. Mwajiri wangu amenipatia somo jipya la 'Maadili ya Taaluma ya Sheria" juu ya lile la "Sheria ya Katiba", hivyo kazi imeongezeka maradufu. Nautumia muda wangu mwingi kuandaa
mihadhara kwa ajili ya wanafunzi wangu.

Swali: Unataka kutuambia umeachana sasa na siasa za mageuzi?

Jibu: La hasha! Sijaacha siasa, kwani binadamu aliyeachana na siasa ni yule aliyekwisha
kufa. Binadamu ni mwanasiasa kwa asili na hulka yake. Kila jambo tunalotenda ni siasa.
Viongozi wa siasa ni aina moja tu ya wanasiasa tulionao. Mimi bado ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama changu na mshauri wa sheria na haki za binadamu wa chama changu
cha NCCR-Mageuzi. Nashiriki katika michakato mbalimbali ya mageuzi inayofanywa na
wanamageuzi nchini pamoja na ile inayofanywa na wanaharakati katika asasi zisizo za
kiserikali.

Swali: Unasemaje sasa kuhusu ukimya wako kuhusu mambo kadha wa kadha yanayotokea katika nchi yetu yenye mguso wa kisiasa?

Jibu: Kimya kinaweza pia kuwa jibu. Ni vyema kujipa muda kukaa kimya na kusikiliza wengine
wanasema nini. Hiyo inawapa wananchi fursa ya kushirikiana na serikali kutekeleza yale
waliyoahidiwa. Pale utekelezaji unapokinzana na misingi ya demokrasia tunayojenga,
najitokeza kuelezea msimamo wangu, kwa mfano suala la muswada wa sheria ya haki ya kupata
habari na sheria ya huduma ya vyombo vya habari ulioletwa na serikali. Sikukaa kimya,
nilijitokeza kuzungumza na kushiriki katika harakati ya kuweka mambo sawa kwa mujibu wa
misingi ya taaluma ya sheria, haki za binadamu na maslahi ya wadau wa habari.

Swali: Unaonaje mwenendo wa mageuzi, tunapiga hatua au tunarudi nyuma, hasa ukitizama
kusimamishwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto bungeni hivi karibuni?

Jibu: Swali lako kubwa kweli. Mimi binafsi naona tunapiga hatua kwenda mbele. Hakuna
nafasi kwa jamii kurudi nyuma, kwani kila hatua inayopigwa hata kama itaonekana ni mbaya
na yenye kuwaumiza wananchi, bado ni hatua yenye mafunzo mema au mabaya kwetu. Kwa mfano
naona jamii imekomaa zaidi, kwa kuwa imejionea yenyewe ukweli na uongo, haki na dhuluma
vikitendwa na serikali yao mbele ya macho yao na vikigusa maisha yao. Sihitaji kuendesha
darasa la haki za binadamu kwa ndugu zangu Wabarabaig kule Hanang kwa wao kujua kuwa
serikali imevunja haki yao ya kumiliki ardhi walimozaliwa na ambamo wamekuwa wakifugia
mifugo yao kwa zaidi ya karne moja.

Wabarbaig kule Hanang wamejionea wenyewe kuwa serikali ilithamini zaidi uwekezaji katika
kilimo cha ngano ni bora kuliko haki yao ya kuishi, kujenga utamaduni wao na kujipatia
riziki yao kwa kufuga. Sihitaji kuwakumbusha jinsi serikali ilivyotwaa ardhi yao kwa
mabavu kwa kuwachomea nyumba zao, kuharibu mali na mifugo yao. Wabarbaig wanajua kuwa hata
baada ya serikali kushindwa kuendelea kulima ngano haikuwarejeshea ardhi yao bali
ilitafuta wawekezaji wauziwe ardhi ile. Mashamba yale sasa yatauzwa kwa wawekezaji na
mawili yatagawiwa kwa wafugaji na wakulima ambao si wale walionyang'anywa ardhi mradi wa
ngano ulipoanzishwa. Hiyo ndiyo busara ya serikali yetu!

Vivyo hivyo sihitaji nguvu kubwa kuwaeleza wananchi wa Kijiji cha Nyamuma kule mkoani Mara
kuwa serikali yao ilifanya kitendo cha kifisadi kuwavamia na kuwachomea nyumba zao,
kuharibu mali zao na kuumiza wengine katika zoezi la kupanua mipaka ya hifadhi ya
Serengeti. Kule serikali iliona kuwa haki ya wanyama kuishi ni muhimu kuliko ile ya
wananchi wake. Wananchi wa Nyamuma wanajua kuwa serikali yao haiwathamini kwani hata baada
ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuamua kesi yao na kuamuru serikali iwalipe
fidia ya jumla ya shilingi milioni 850, serikali imegoma kulipa.

Mimi ninayo mifano mingi tu ya kuonyesha kuwa somo kuhusu ufisadi, kutoheshimu sheria, ubadhirifu wa kodi na rasilimali za umma vinavyofanywa na serikali linaanza kueleweka sasa kwa matukio halisi
yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Haya si mambo ya kuzua au ya kubuni. Mageuzi si
usanii bali ni mchakato halisi wa kupigania haki na maendeleo ya watu. Mimi naona mpaka
hapo tulipofikia ni hatua kubwa katika mageuzi ya nchi. Hapo zamani za kale, tulikuwa
tumegubikwa na ukiritimba wa chama kimoja na hatukuwa na haki ya kusema wala kujua. Sasa
tunayo haki ya kujua na kusema. Hapo kesho tutajinyakulia haki ya kujiamulia mambo yetu
sisi wenyewe. Haki hii itatuwezesha kuwaondoa madarakani hao Miungu Watu wanaovunja haki
zetu za msingi kwa kutumia nguvu za dola.

Kuhusu kufukuzwa kwa mbunge Kabwe Zitto, hilo ni tukio la kusikitisha, lakini
linaloelezeka. Tuko vitani kuleta mageuzi na Zitto kaumizwa na risasi ya adui vitani. Ni
shujaa wa vita hivi na tumpe moyo wa kuendelea kupambana. Waliomjeruhi wanadhania
wameshinda, la hasha! Kitendo chao kimewaamsha wananchi kujua ukweli wa demokrasia tuliyo
nayo kuwa haitoshi. Kumbe haitoshi kuchagua wanamageuzi wachache kutetea haki zetu kule
bungeni. Kumbe Bunge la Jamhuri halipo, badala yake tunalo Bunge la Chama Cha Mapinduzi!
Wanakutana kama kamati ya chama na kuamua kulindana na kisha wanaingia bungeni kulindana.
Tungelisema hili bila mfano huu halisi wa kusimamishwa vikao vya Bunge kwa Zitto ambao
wananchi wamejionea wenyewe kwenye luninga wangesema sisi ni wazushi! Sasa kila mmoja
amejua kuwa katiba, sheria na kanuni za Bunge vyote vina dosari nyingi za msingi.

Kumbe katiba, sheria na kanuni za Bunge vimeunda Miungu Watu ambao haipaswi wasemwe! Upo
msemo unaosema kwamba anayemsema mfalme kuwa yuko uchi, hata kama kweli mfalme yuko uchi
wa mnyama, ajue shingo yake ni halali ya mfalme. Ataitwa mzushi, asiye na adabu na kisha
ataadhibiwa kwa kukatwa shingo. Hicho ndicho alichofanya Kabwe Zitto. Alimshuku Waziri
Karamagi kuwa ni mla rushwa kwenye mkataba ule wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi na kwa kuwa
huyo ni Mungu Mtu, hata kama tuhuma za rushwa dhidi yake ni za kweli, Bunge la Jamhuri
limeona hakuna haja kuchunguza tuhuma hizo ila ni busara zaidi kumwadhibu aliyetoa tuhuma
hizo.

Tukio hilo ni moja tu katika matukio mengi yatakayotokea siku za usoni. Wamesema kuwa hizo
ni rasharasha tu. Inamaanisha nini tamko hilo? Mimi naona wamejipanga kulihujumu kabisa
taifa hili.

Waswahili wanasema "wamekaa mkao wa kula". Ile hoja ya Mbunge wa Karatu (CHADEMA) Dk.
Willbrod Slaa kuhusu ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inatisha. Angepata fursa
ya kuiwasilisha bila shaka vichwa vingepukutika! Kumbe Watanzania tutajionea mengi,
mabilioni ya fedha za umma kutafunwa bila maelezo, kodi za wananchi kutafunwa hivyo kwa
kisingizio cha kutoa mikopo ya kupunguza umasikini, mikataba mingi ya kufilisi rasilimali
za asili kuwekwa saini kwa siri ili umma using'amue na kuhoji. Tutajionea wenyewe vituko
na kashfa nyingi za kushangaza kama vile viongozi kupora mali za umma au kutumia nafasi
zao kujitajirisha, unyang'au na kila uchafu unaoendana na ubeberu! Baba wa Taifa
alitufundisha wakati ule wa uhai wake kuwa ubepari ni unyama, na hakuna ubepari mbaya kama
ubepari uchwara unaojegwa katika enzi za utandawazi.

Wale uwadhaniao kuwa siyo utagundua kuwa ndio. Waliokuwa wahubiri wa ujamaa na uadilifu
utagundua kuwa ndiyo mabepari wa leo wanaoshiriki katika kila namna ya umafia. Haya mambo
ni ya kweli, yapo na tusidhani ni uzushi au hadithi ya "Elfu lela ulela"!

Swali: Dk. Mvungi hayo unayosema yanatisha. Sasa wanamageuzi mmejipanga vipi kukabiliana na hayo uliyoyaelezea?

Jibu: Ni vyema kwanza kujiweka sawa kuyafichua maovu haya wananchi wayajue. Kulijua tatizo
ni hatua ya kwanza katika kulipatia jambo hilo ufumbuzi. Mimi siamini kuwa kule CCM kila
kiongozi au kila mwanachama ni fisadi. Wapo wenye nia njema kule ambao pia wanaumia
wakiona ufisadi huu. Kumbuka ufisadi ni uovu wa kupindukia na hauna itikadi. Hiyo ni sura
moja ya kukuonesha kuwa tatizo tulilonalo ni la kitaifa na linahitaji ufumbuzi wa kitaifa
siyo wa chama kimoja au vyama vya upinzani peke yake.

Tunahitaji sasa uhuru wa pili. Tunahitaji kuanzisha mchakato wa kulikomboa taifa kutoka
kwenye ufisadi unaojijenga hivi sasa. Hatunaye Baba wa Taifa kutuongoza na kutuonyesha
jinsi ya kulitekeleza hili. Lazima tukae chini tutafakari mambo haya ili kwa pamoja tuvute
kamba kuzuia maangamizi ya taifa letu. Mimi kweli naona wenzetu hawa hawana aibu kabisa
kufanya maovu haya. Tunazo rasilimali nyingi mno kiasi kwamba tunaweza kusema Tanzania ni
Bustani ya Eden. Lakini kumezuka waroho na mafisadi wakubwa wanaotumia nguvu za dola
kuruhusu uporwaji wake na wageni kwa kisingizio cha "uwekezaji". Tusipogundua kuwa lugha
ya "uwekezaji" ni lugha ya utandawazi inayohalalisha ubeberu, hatutagundua ukweli kuwa
"uwekezaji" ndio ufunguo wa umasikini wa mataifa ya dunia ya tatu. Sijui kama viongozi
wetu wa leo wanatofautiana sana na Sultani Mangungo wa Msovero. Afrika imefilisika
kiuongozi na tunahitaji sasa mapambano ya uhuru wa pili kuikomboa Afrika kutoka kwenye
ubeberu huu unaojiita utandawazi.

Kumbuka uhuru wa pili ni dhana kubwa na nzito kifalsafa. Tutakuwa tunajipanga kupambana na
Watanzania wenzetu ambao wamesimama upande mmoja na ubeberu. Hawa wanao ndugu, jamaa na
marafiki wa ndani na nje ya nchi. Hawa wameshikilia hatamu za dola. Hawa wamejilimbikizia
mabilioni ya fedha kuweza kumrubuni kila mtu mwenye roho nyepesi nyepesi. Kwa pamoja hawa
wanaunda tabaka la kinyonyaji na kifisadi linaloangamiza taifa. Tabaka hili halina aibu,
huruma wala uzalendo.

Linajali matumbo yao tu na likishapora huhifadhi fedha na rasilimali hizo nje ya nchi.
Hili ni tabaka hatari kabisa. Hivyo usiniulize kama wanamageuzi tumejipanga vipi, jiulize
wewe uko upande gani katika harakati hizi, na uko tayari kufanya nini kwa ajili ya nchi
yako. Mimi nikuulize: Je, kuna kabila la Watanzania linaloitwa "wanamageuzi"? Kama hakuna
kwa nini mwanamageuzi awe mimi, asiwe wewe?

Swali: Je, unadhani ushirikiano wa vyama vya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi ni jambo makini na litakalofanikiwa?

Jibu: Mimi naona ushirikiano huo ni jambo zuri na la kuungwa mkono. Tuwape moyo waimarishe
ushirikiano ule, labda utazaa mafanikio kama tutapata chama kimoja kikubwa cha upinzani
nchini.

Swali: Je, wataacha ubinafsi na kuweka mgombea mmoja wa urais?

Jibu:
Suala la mgombea mmoja wa urais si zito wala gumu kama kukubali kuunda chama kimoja.
Tunachopigania ni kuwa na upinzani unaoleta maana, unaoweza kuiondoa CCM madarakani au
kuligawa Bunge na serikali za mitaa ili chama kimoja kisiwe na ukiritimba wa siasa na
maamuzi nchini. Hatutaki kuwa na Bunge la chama kimoja ambapo wanakutana kama kamati ya
chama na kufanya maamuzi kisha wakaingia bungeni na kupiga muhuri maamuzi yao.

Swali: Kuna baadhi ya Watanzania wanasema wanaotaka katiba mpya wanataka kugawana vyeo, wewe unasemaje?

Jibu: Ah! Hayo ni mawazo yao kama wanasema hivyo na ninayaheshimu. Mimi nataka katiba mpya
na sina lengo la kugawiwa cheo chochote. Nataka katiba mpya kwa kuwa katika katiba ya sasa
misingi ya demokrasia ni finyu sana. Lazima tuwe na katiba ya taifa huru la kidemokrasia
ambapo kila raia ana haki sawa na fursa sawa. Nataka katiba inayoweka misingi ya
demokrasia ya umma hivyo kwamba umma uwe na nafasi ya kuidhibiti serikali badala ya
serikali kuudhibiti umma. Nataka katiba inayounda tume huru ya uchaguzi badala ya hii ya
sasa ambapo uchaguzi unaendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Swali: Kwani ni kweli kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ndiyo inaendesha uchaguzi?

Jibu:
Sijui ni lipi zuri, kujua ukweli na ukaishi kwa taabu na mahangaiko au kutojua
chochote na ukaishi kwa amani mustarehe. Kamati ya Ulinzi na Usalama haina mamlaka ya
kuendesha shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na katiba ya nchi. Lakini
katika utendaji, kamati hiyo ndiyo inapanga kila kitu na kutekeleza mikakati yote ya nani
ashinde na nani ashindwe. Wananchi hupiga kura, lakini kamati hii huchagua nani awe
kiongozi.

Swali: Rais Kikwete amesema tayari mikataba ya madini inadurusiwa. Tutapata sasa asilimia
30 kupitia kodi na mrahaba. Je, huoni hiyo ni hatua nzuri?

Jibu: Mimi namsifu Rais Kikwete kwa kutambua ukweli kuwa mikataba ile na sheria ya madini
ina kasoro. Hilo ni jema kabisa. Sikubaliani naye kuwa asilimia 30 inatosha! Mimi nadhani
tungepata asilimia sabini wawekezaji wakachukua thelathini. Sasa mwenye rasilimali ni
nani, sisi au wawekezaji? Tatizo hapa ni woga tulionao kuwa wawekezaji hawatapatikana.
Hiyo si kweli. Ramani ya madini ipo, wao hawaji hata kutafuta madini hayo, wanakuja
kuchimba tu!

Nchi zenye sheria nzuri za madini huhakikisha kuwa migodi ni mali ya raia wake, hivyo hata
ukitoza asilimia 30 kodi na hata usipotoza mrahaba hupotezi kitu kwani rasilimali iko
mikononi mwa raia wako. Tatiz o hapa ni kuwa tunatoa bure rasilimali ya Watanzania kwa
wageni, jambo ambalo si la busara wala halali. Lakini kule migodini hatuna udhibiti kwa
kujua kiasi gani cha madini kimepatikana. Wanachimba na kumimina dhahabu na kuondoka nayo
bila sisi kujua wamepata kiasi gani. Wanachotuambia wamepata ndicho chetu. Watanzania
tunayo tanzanite, dhahabu, almasi, na sasa tunayo pia mafuta. Kwa nini sisi ni masikini
kuliko mataifa ambayo hayana kabisa rasilimali asili kama hizo? Kama mtu ataniambia kuwa
tunao uongozi bora, sasa tumwombe Mungu atupe nini zaidi?

Swali: Unasemaje kuhusu ubinafsishaji wa sekta ya umma, huoni kama sasa uchumi wa nchi
unapaa ukilinganisha na hapo zamani tulipokuwa tunafuata ujamaa?

Jibu: Wengi wanaozungumzia kushindwa kwa ujamaa hawaujui hata huo ujamaa ni kitu gani.
Hebu nieleze hao wanaotetea ubinafsishaji wanaweza kuonesha mradi gani mpya waliojenga
ukiacha hizo mali zetu walizogawiana bure kwa kisingizio cha ubinafsishaji? Mimi naona
ubinafsishaji ungeandaliwa vizuri ungetusaidia kwa maana kwamba rasilimali zile
tungeziweka mikononi mwa wazawa au kuzibakiza mikononi mwa umma, lakini tukaruhusu wageni
kuwekeza kama wabia. Tusingekubali kabisa kuwapatia rasilimali zile kwa asilimia zaidi ya
hamsini. Kwa kufanya vile tulijikata miguu ya kuingilia kwenye ubepari sasa tumekuwa
viwete kiuchumi kwenye nchi yetu wenyewe.

Si kweli kuwa uchumi unapaa. Uchumi unaopaa ni wa nani? Labda ule wa wageni tuliowapatia
rasilimali zetu bure. Kwa mfano serikali iliuza benki nzima ya Biashara ya Taifa kwa
shilingi bilioni 15 tu, thamani ambayo hailingani na hata lile jengo yalimo hivi sasa
makao makuu ya benki hiyo. Mara baada ya kukabidhi benki kwa wanunuzi, tuliwalipa wanunuzi
hao bilioni 15 kama fedha za huduma za kibenki kutoka benki ya NMB. Sasa tuliuza benki
hiyo kwa bei gani? Lakini pia tuliwapatia akaunti yetu ya dhamana za fedha za kigeni yenye
dola milioni 80 hivi, kule Marekani. Unaweza kusema sisi ni wafanyabiashara wazuri kwa
kufanikisha uuzwaji huo wa benki yetu? Naweza kuchukua mfano wowote wa ubinafsishaji na
nitakuonesha kuwa tulifanya madudu.

Swali: Hivi karibuni serikali imetangaza kuwa itapeleka shilingi bilioni 22 kila mkoa
katika mchakato wake wa kupunguza umasikini, hili nalo walionaje?

Jibu:
Ah, ndugu yangu acha tu wapeleke, hazitakosa walaji hizo. Mimi siamini kuwa kila mtu
anaweza kujiajiri au kuwa mwekezaji. Kuamini kuwa mtu ambaye hajawahi kufanya biashara na
ambaye hana hata uzoefu wa biashara ataandika andishi la mradi na kufaulu kuanzisha
biashara au mradi wa uzalishaji mali ni hatari. Ubepari haujengwi kiholela hivyo. Ubepari
ni mfumo wa kisayansi kabisa wa uchumi. Ukiuendea kichwa kichwa utapoteza rasilimali za
walipa kodi bure. Kumbe kwa kudra ya Mungu wako watakaoweza na pia wako wengi
watakoshindwa. Tusishangae hayo yote mawili yakitokea kwa kuwa kweli hakuna maandalizi ya
kutosha yamefanywa kwa mchakato huo.

Swali: Maandalizi gani hayo unadhani yangefanywa?

Jibu:
Kila jambo litafanyika vizuri kama watendaji au wadau wake wataandaliwa kwanza
kielimu. Mimi naona silaha dhidi ya umaskini ni elimu bora na afya bora. Mengine yanaweza
kuja kama ziada. Taifa ambalo linaweza kuamua kuwa vijana wake walioko nje ya nchi
kujitafutia elimu hawana haki ya kusaidiwa wanapokwama kama wale waliokwama kule Ukraine
bado halijajiweka sawa kupambana na umasikini. Tuko tayari kuchangia harusi, vifo, michezo
na kadhalika, lakini tunasita kutoa fedha za kodi zetu kuwasomesha vijana wachache tu
ambao wamekwama kule Ukraine.

Mimi sioni mfungamano wa kisera wa malengo yetu. Iko wapi mipango ya elimu ya ujasiriamali
kwa hao watakaokopesha mabilioni hayo? Je, ni kitu gani shilingi milioni moja katika
biashara au mradi wa kukimu familia ya kawaida yenye watu wanne hivi? Zipo nchi zinayo
miradi ya kujikimu kwa raia wake. Lakini nchi kama hizo hazitoi mikopo holela kwa kila
mtu. Zinatoa mikopo kwa watu waliokwishahitimu kiwango fulani cha elimu na pia utaalamu wa
mradi unaoombewa fedha. Kisha wameunda taasisi ya kifedha yenye wataalamu wa kusimamia
mafunzo ya miradi, uendeshaji wa miradi na usimamizi wa miradi kwa wanaokopeshwa hadi
miradi yao iweze kujiendesha. Hili si jambo dogo la kukurupuka.

Swali: Eleza mtazamo wako wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo imebakiza miezi michache itimize miaka miwili tangu iingie madarakani.

Jibu:
Mimi naona wamewaahidi Watanzania mbingu, lakini tulichopata ni jehenamu. Maisha
yetu sasa ni hoi bin taabani. Wakubwa uchumi wao binafsi unapaa, sisi walalahoi tumechoka!
Kiutendaji inaonekana katika kila jambo kuna 'usanii' mwingi, lakini tunachokipata ni duni
kabisa. Sipendi kubeza wala kudanganya. Je, walimu bila elimu ni jambo jema kwa elimu ya
taifa? Mimi naona ni kujidanganya tu kudahili wanafunzi na kuwajaza kwenye madarasa bila
walimu. Si kila mtu anaweza kuwa mwalimu, hiyo kazi ni wito, lakini pia ni taaluma.

Unaweza kusifiwa kwa kuanzisha chuo kikuu kipya, lakini chuo hicho kina wahadhiri? Na je,
hivyo vyuo vikuu vilivyopo umevifikisha wapi? Mimi naona tumekwama hapo, vyuo vikuu
tulivyonavyo hatuna uwezo kuviendeleza, ila tunajenga vingine! Kwa nini hatuoni kwamba
kuendeleza na kupanua vyuo vilivyopo ni bora kuliko kujenga vipya? Sasa naona elimu ya juu
imevamiwa kimamluki. Wale binafsi wanatoa tu vyeti bila kujali viwango vya elimu kwani
akifeli mwanachuo watakula wapi? Mimi naona hayo si mambo mazuri kwa taifa letu. Maendeleo
ya taifa hutegemea elimu, na tukichezea elimu tunachezea uwepo wa taifa letu. Tutakuwa na
watu wenye vyeti, lakini wasio na elimu. Tutashindwa katika kila jambo tutakalotaka
kulifanya kwa kuwa hakuna jambo linaloweza kufanywa na mbumbumbu.

Mimi naona utendaji wa papara katika kila jambo, lakini kwa kweli hakuna serikali
inayoweza kufanya kila kitu. Wangechagua mambo machache wakayafanya vizuri badala ya
kupapasa kila kitu na kukifanya vibaya. Naona uchungu kabisa kuona jinsi wanavyoachia
rasilimali asili kuporwa na wageni. Hilo nina uchungu nalo na sioni woga kulisema. Sheria
ya madini ni bomu na viongozi wa awamu ya tatu na ya nne walaumiwe kwa hilo. Naona pia
uchungu kwa ubinafsishaji holela wa rasilimali zetu. Tulijiuza rahisi mno, hilo ni jambo
ambalo sioni cha kujivunia. Naona pia kuwa ufisadi umekithiri na umegubika serikali nzima.
Hii kashfa aliyoibua Zitto na ile anayoizungumzia Dk. Slaa ni ishara mbaya kwa taifa.
Wakubwa wengi wanadanganya na kulihujumu taifa. Mimi naona hayo yanatosha, hakuna haja ya
kuzungumza mengi kwani yanatia uchungu. Watanzania wawe tu na juhudi na ushujaa wa
kukabiliana na hayo, wasikate tamaa. Sisi wanamageuzi tutaendelea kueleza kasoro hizi,
siyo kwa nia mbaya ila kwa kuwa bila ukweli, hakuna haki na bila haki taifa huangamia.

Swali: Sasa ni jambo gani la kuwatia moyo Watanzania unaweza kulisema?

Jibu: Kwa Watanzania wenzangu sote tunajua hali tuliyofikia. Wengi hatuna chakula, mavazi,
tiba na watoto wao hawapati elimu. Hatuhitaji nguvu nyingi kuelezea hali mbaya tuliyomo
kijamii na kiuchumi. Lakini hali hii isitukatishe tamaa kwani hakuna shida isiyo na mwisho
na penye nia pana njia. Najua kila mwananchi sasa ni mwanamageuzi. Tulipoanza tulikuwa
wachache. Sasa kila mmoja ni mwanamageuzi. Hili halina rangi za vyama kwani umasikini
hauna chama. Lazima tujifunze sasa na kwa haraka jinsi gani ya kubadili hali zetu kwa
kujikomboa wenyewe badala ya kungojea ukombozi uletwe na serikali. Nadhani kwa hili tuko
mbioni kufikia hatua ya mgeuko kote nchini.

Lazima mbinu za mageuzi zibadilike haraka. Hatuwezi kufunzwa mbinu za mageuzi na walio
madarakani. Inawezekana sasa tukaamua kubadili kabisa mchakato wa mageuzi kwa jinsi ambayo
italeta tija na kupunguza hasara ya upotevu wa muda na rasilimali. Kwa kuwa wenzetu walio
madarakani wamejikita katika ufisadi, wizi wa kura, matumizi ya dola kubaki madarakani na
kila jitihada ya kuleta mageuzi kwa amani wanazipiga vita, inawezekana tukaziacha mbinu za
sasa na kuona jinsi nyingine ya kuleta mabadiliko. Sijui tutachagua njia ipi, lakini
wakati ukifika njia itapatikana. Hakuna linaloshindikana wananchi wakiamua.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0755 312 859; barua pepe;
katabazihappy@yahoo.com na tovuti; www.katabazihappy.blogspot.com.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Novemba 11,2007

2 comments:

Anonymous said...

Dada Happy, I was waiting to hear if you were going to writen anything concerning "Mahakama ya Kadhi" lakini kimya, wewe na mambo yako ya Chadema and NCCR tu? unaogopa watu wa Bakwata watakupiga mawe....andika tu....Mtikila ndiye mwenye msimamo, ngojeni muone mahakama itaanza muda siyo mrefu, by February, andika basi kuhusu mahakama ya Kadhi,
John

Anonymous said...

Wewe John vipi, umerudi tena? sasa wewe kila mara dada huyu akiweka mada mpya wewe ni kwanza kukosoa...tuambie blog yako ni hipi hili na sisi tutembelee? ofcourse ningependa mjadala wa mahakama ya kadhi uwe huru kwa wote.

Powered by Blogger.