Header Ads

ANDREW CHENGE ACHA WANAHABARI

Na Happiness Katabazi

MARA zote mama yangu mzazi Oliva Ndimugeita, amekuwa akiwaambia ndugu, jamaa na sisi watoto wake kwamba tukimuona au kumsikia binadamu awaye yeyote anadai heshima kwa nguvu, tujue binadamu huyo ana matatizo.

Jumamosi iliyopita nyakati za asubuhi baada ya kumaliza kusoma habari kubwa kwenye moja ya gazeti la kila siku (si Tanzania Daima) iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Chenge ageuka Mbogo’, niliamini maneno ya mama yangu kuwa yamejaa ukweli na hekima.

Ndani ya habari hiyo Andrew Chenge, amenukuliwa aking’aka kwamba wandishi wa habari siku hizi hawamheshimu, lakini ipo siku atawafunza adabu.

Kwa mujibu wa habari ile, Chenge alionekana mwenye hasira, alipotoa kauli hiyo baada ya kuulizwa juu ya maoni yaliyotolewa na wananchi, asasi za kijamii na wanasiasa kwamba hakustahili kuwepo katika timu ya kurekebisha kasoro kadhaa kwenye mradi wa Jengo la UVCCM.

Maoni hayo yanatokana na ukweli kwamba, Chenge anakabiliwa na tuhuma za ufisadi ambazo hadi sasa zinachunguzwa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai(SFO) ya Uingereza.

“Kwa nini waandishi wa habari hamniheshimu? Naomba tafadhali mniheshimu. Siku hizi hamniheshimu kabisa, lakini kuna siku nitawafunza adabu,” alisema.

Kwanza nataka ieleweke wazi kwamba matamshi haya ya Chenge, kusema ipo siku atawafunza adabu waandishi wa habari ni matusi na vitisho, anapaswa atuombe radhi. Pia ni kauli ya kitisho ili wanahabari wasiwe na ujasiri, waingiwe woga wasiandike maovu yake.

Chenge anaposema atawafunza adabu waandishi wa habari ni dhahiri shairi kwamba waandishi wa habari wa kada zote hawana adabu!.

Leo hii Watanzania wa makundi mbalimbali wanapolalamikia serikali imeingia mikataba ya kihuni na mibovu ambayo inawanufaisha wawekezaji wa kigeni kuliko raia wa nchi hii, ni lazima tumtaje Chenge, Baraza la Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tatu na rais Benjamin Mkapa.

Tunamtaja na tutaendelea kumtaja kwa sababu Chenge ndiye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi chote cha awamu ya tatu hivyo alikuwa mshauri mkuu wa masuala ya sheria kwa serikali.

Mikataba yote ya ‘kihuni’ ambayo leo hii inaigharimu serikali na wananchi wake imesababishwa na viongozi wenzake na yeye akiwemo.

Katika hili, hana ujanja kwani yeye ni mwanasheria kitaaluma alipaswa kuifahamu kwa undani mikataba hiyo kuwa ni mibovu kabla haijaingiwa na serikali.

Chenge lazima atambue kuwa tutaendelea kumwandika, wananchi wanateseka na gharama za maisha kwa sababu ya fedha za walipa kodi ambazo serikali ilikuwa ikizilipa kwa kampuni ya IPTL. Fedha hizo zingewekwa kwenye sekta ya afya bila shaka wananchi tungepata huduma bora katika hospitali zetu.

Lakini, Chenge na wataalam wengine wa serikali aidha kwa kukosa uzalendo katika taifa lenu au kwa uzembe mkaliingiza taifa kwenye mikataba ya kinyonyaji yenye harufu ya rushwa kama IPTL, Netgroup Solution na mingine ambayo inawanufaisha wawekezaji wa kigeni.

Najiuliza ni kwa nini Chenge hana huruma na waandishi wa habari hadi atake tena kuwafunza adabu kwani wanahabari ni wananchi ambao nao wanasulubika katika mikataba hiyo ambayo nalazimika kusema mbunge huyu mbaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya awamu ya nne na wenzake walishawashikisha adabu wananchi kwa kuiliingiza taifa kwenye mikataba hiyo.

Wakati umefika sasa wanahabari tumhoji Chenge ni adabu ipi nyingine anataka kutufunza? Kwa mtazamo wangu kauli ya yake inamrudi kwa sababu alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini alishindwa kuishauri vema isiingie mikataba dhalimu.

Hivyo Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), aelewe wazi wanahabari hawana chuki nae anaandikwa kwa mazuri na mabaya yake na siku zote za maisha atambue kwamba tunapolalamikia mikataba mibovu, lazima tuihusishe serikali ya awamu aliyokuwa Mwanasheria wake Mkuu.

Wananchi wa kada mbalimbali waliojitokeza kupinga uteuzi wake wa kuwa mjumbe wa timu ya kurekebisha kasoro kadhaa za jengo la UVCCM, wanayo haki ya kuhoji uteuzi wake kwa sababu alishindwa kuona ubovu wa mikataba ya IPTL, Netgroup Solution, Rada na mingine.

Leo, baada ya kujitoka kwenye uwaziri kutokana na kashfa ya ufisadi wa ununuzi wa rada ndiyo anaweza kuona kasoro katika mkataba wa mradi wa jengo la UVCCM?

Hivyo kutokana na mlolongo wa tuhuma nilizoziorodhesha zinamhusisha Chenge, ndizo zinazosababisha adai heshima kwa nguvu na hapo ndipo maneno ya mama yangu mzazi yanapotimilika kwamba ‘binadamu yeyote anayedai heshima kwa nguvu ana matatizo’.

Hivyo naomba uwe mstahimilivu na ungetaka mabaya yako yasiandikwe basi tangu mwanzo katika utendaji wa kulitumikia taifa hili, usingejiingiza kwenye kashfa ambazo leo tuhuma hizo zinakutafuna kila kukicha.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0755312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

CHANZO.Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 17, 2008

No comments:

Powered by Blogger.