Header Ads

TUHUMA ZA KOMBA NZITO,ASHITAKIWE

Na Happiness Katabazi
“KAPTENI John Komba akipita njiani watu wote wanalia yooo,tupatie pesa….”hiki kibwagizo kinapatikana kwenye wimbo wa Dakika tisa uliopigwa na Bendi ya TOT Respect, ambao hivi sasa wimbo huo unatamba kwenye vituo mbalimbali vya redio na Televisheni.

Kwa tafsiri nyepesi kigwazo hicho kinadhiirisha Komba ni Mtanzania mwenye fedha nyingi.Lakini kwa upande mwingine kibwagizo hicho kinachosema ‘Kapten Komba akipita njiani watu wote wanalia yoooo’ kinadhiirisha wanamuziki wa kundi hilo ndiyo haswa wanalia baada ya kulizwa mishahara yao ya miezi 14 na nguli huyo wa sanaa ya muziku nchini .

Nasema wanalia kwasababu wanamuzi wa kundi hilo wamekuwa wakitumia taaluma yao ya sanaa kwa kuimba, kunengua katika bendi hiyo .Na wengine wanaolia ni washabiki,wanachama,wakereketwa wa CCM na wananchi ambao wanachangia fedha chama hicho na wanachi kukatwa kodi na serikali ambazo ugawanya na CCM kupewa ruzuku kutoka na idadi kubwa ya wabunge waliyokuwa nao.

Jumatatu ya wiki iliyopita Tanzania Daima ndilo lilikuwa gazeti pekee liloandika habari kwamba Mkurugenzi wa Kikundi cha Sanaa cha Tanzania One Theatre(TOT), Kapteni John Komba , anakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha katika kikundi hicho kinachomilikiwa na chama tawala CCM.

Tuhuma hizo zimeibuliwa katika taarifa ya ukaguzi maalum, uliofanywa na kitengo cha ukaguzi cha CCM, kwa maagizo ya Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, kutokana na tuhuma zilizowasilishwa kwake dhidi ya Kapteni Komba.

Ukaguzi huo, ulifanyika kuanzia Machi 3 hadi 16, mwaka huu na baadaye April mosi hadi 6, na taarifa yake kuwasilishwa rasmi kwa Makamba April 22. Taarifa hiyo ya Uchunguzi ambayo hadi leo Tanzania Daima ina nakala yake Komba anadaiwa kutafuna sh milioni 30 za mishahara ya wafanyakazi miezi 14.

Uchunguzi huo ambao umepata baraka za chama, unadai kuwa CCM ilitoa sh 37,442,923 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya miezi 14 kuanzia Juai 2006 hadi Agosti 2007 kwa awamu, lakini ni sh milioni sita tu, ndizo zilizolipwa kwa wafanyakazi kwa mishahara ya miezi miwili.Pia anatuhumiwa kuwapunja wafanyakazi wa TOT kwa kuwalipa posho ya sh 20,000 kwa siku wanapokuwa nje ya Dar es Salaam badala y ash 40,000 zinazotolewa na chama.

Pia Komba na kiongozi mwenzake ndani ya kundi hilo, wanahusishwa na udanganyifu wa kulipa warithi wa marehemu wasio waasisi wa chama jumla y ash 27.3 milioni, lakini baadhi ya waliotajwa kwenye orodha ya malipo, wamekana kupewa fedha zozote.Mbali na tuhuma hizo hizo pia anatuhumiwa kusajili gari la CCM kwa jina la asasi yake isiyo ya kiserikali inayojulikana kwa jina la Educare Girls.

Kwanza kabisa nitoe shukrani zangu za dhati kwa vyanzo vya habari viadilifu toka ndani ya CCM ambavyo kwa siri kubwa walifanikiwa kulipatia gazeti hili nakala hiyo ya ukaguzi ambayo imebaini ufisadi unaodaiwa kufanywa na Komba ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi.

Ni ukweli ulio wazi kwamba vyanzo hivyo visingejitoa muhanga na kulipatia gazeti hili na magazeti mengine nakala hiyo, jamii yote isingejua kwamba Komba ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kuwa anakabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Tungeendelea kumuona Komba ni mwema, Kada mwaminifu wa CCM asiye na mawaa.Lakini kwa kupitia nakala hiyo ya ukaguzi sasa tumeanza kukubaliana na minong’ong’ono iliyokuwa ikilindima chini kwa chini kuwa kiongozi huyo alikuwa akitafuna fedha la kundi hilo, licha ushaidi wa hayo ulikuwa ni mgumu kupatikana.

Sishangai Komba kutuhumiwa na ufisadi kwani kuna viongozi wakubwa wa chama hicho wanaandamwa na tuhuma za ufisadi.Ila kwa wenye tuhuma za ufisadi wa wazi ambao pia wananguvu na uswahiba na kundi la wanamtandao wamekuwa wakilindwa ila wale wanachama ambao wanatuhuma za ufisadi kama aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Abiud Malegesi alishughulikiwa kikamilifu kwasababu hakuwa mwanamtandao.

Hakuna ubishi kwamba CCM safi alizikwa nayo Baba wa Taifa Julias Nyerere na CCM chafu ndiyo imebaki na kwasasa inaongozwa na Mwenyekiti rais Jakaya Kikwete.Kila kukicha makada wake wanakumbwa na tuhuma za nzito za ufisadi unahoujumu uchumi wa taifa hili.

Hii siyo picha nzuri na ishara njema kwa mustakabali wa taifa kwa baadhi ya makada wa chama tawala kuhusishwa na ufisadi.Na kibaya zaidi wanapotuhumiwa na tuhuma hizo wanalindwa bila kufikishwa mahakamani kwa kisingizio kuwa huyu ni ‘mwenzetu’.

Kasumba hiyo ya ‘mwenzetu’ndiyo inayoiangamiza CCM .Komba anajadilika kwani yeye ni mbunge na MNEC ambaye ambako huko jimboni anaongoza Watanzania wenzetu ambao kwakumuamini waliamua kumchagua , sasa anapokumbwa na kashfa kama hii ama kwa hakika hana budi kujiudhuru ili apishe makada wasafi washike nafasi yake.

Kama ameweza kutafuna mishahara ya wafanyakazi wa TOT, hatashindwaje kutotimiza ahadi alizowaaidi wananchi wake wa mchague kwenye uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2005?
Kama ameweza kutapeli magari ya chama kwanini Watanzania tusiamini kwamba nyimbo anazoimba za kuisifu CCM kuwa chama hicho ni kiziru ni kisima cha viongozi, kuwa ni uongo mtupu?

Kwanini Watanzania tusiamini kuwa Komba yupo CCM kwaajili ya kuchumia tumbo?Nasema ni mchumia tumbo kwasababu kama angekuwa ana mapenzi ya dhati ya chama chake asingefanya ubadhilifu huu ambao umeainishwa kwenye ripoti ya wakaguzi wa CCM.

Komba kama kweli anaipenda CCM asingekubali kuvunja maadili ya CCM ambayo yanamtaka mwanachama wake kuwa mwaminifu na asiyesema uongo na asiyebagua.

Sasa ninalazimika kuamini kwamba tuhuma hizi za ubadhirifu wa fedha zinazomkabili, alizitarajia zimkabili tangu miaka ya 1990, nguli huyu alipoamua kuipa kisogo kazi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuingia uraini kuanzisha kundi la TOT kwaajili ya kujiongezea kipato zaidi.

Kitendo kilichofanywa na Komba kinakwenda kinyume na haki za binadamu kwani kila mtu anastahili kulipwa ujira wake kutokana na kazi anayofanya.Na kamwe kitendo hiki hakivumiliki.

Misho nimalizie kwa kumtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI) Robert Manumba, aueleze umma kuwa ameishachukua hatua gani dhidi ya Komba kwani kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi imebainisha kwamba komba alitenda jinai kwa kughushi.

Sitaki kumsikia DCI Manumba akijitetea kwamba tuhuma hizo hazijafika mezani kwake, kuna wananchi wanatuhumiwa kufanyamakosa kama hayo na wala yanakuwa hajafikishwa mezani kwake lakini anatuma ‘nusanusa au makachero wake ’wake wanaenda kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.

Sasa tunataka kuona DCI akionyesha makucha yake kwa kutuma ‘nusanusa’ wake wakamhoji na kumchukulia hatua Komba kwakuwa Komba ni Mtanzania kama walivyo watanzania wengine,
Ambao wanapotuhumiwa kutenda jinai ushitakiwa na Jamhuri ya Muungano na sivinginevyo.

Huu ni mtihani wako wa mwisho DCI, bado tunakumbuka mwaka jana Jeshi la Polisi ambalo hivi sasa limeanza kurejesha imani kwa wananchi, lilisema limebaini Mbunge wa Buchosa(CCM) ,Samwel Chitalilo amegushi cheti cha elimu , lakini katika hali ya kustaajabisha serikali ikashindwa kumshitaki.

Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumamosi, Septemba 27 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.