Header Ads

Heri kuleta timu za taifa kuliko Real Madrid


Real Madrid ni wageni wa rais Kikwete binafsi au rais wa Tanzania?
.Ujio wake ni gharamazaidi kuliko faida
.Ni fahari ya kisiasa kuliko uchumi,kisoka
.Mamilioni yangewekezwa kwa soka la vijana

Na Happiness Katabazi

Kwani Klabu ya Real Madrid ina kuja Tanzania kama mgeni wa nani?
Ni mgeni wa Rais Jakaya Kikwete binafsi au wa rais wa Tanzania, kwa hiyo kwa gharama za nani? gharama ya mlipa kodi?
Kwa hiyo sisi Watanzania tunaishi kwa ufahari na pesa nyingi za kutupa kwa kuwalipa wachezaji nyota ambao baadhi yao wanalipwa Sh Milioni 200 kwa wiki.
Sasa hawa wachezaji wanakuja hapa nchini watatusaidia nini hata kama watacheza na timu yetu ya Taifa.
Real Madrid ni klabu wala siyo timu ya taifa fulani, sasa mimi sioni faida yake kwa kuwa hata timu yetu ikiifunga licha ni ndoto za mchana, haitaonyesha kama imeifunga timu ya taifa fulani. Sasa inakuja hapa kwa misingi gani?
Mimi nafikiri kila kitu lazima kiendane na uwezo, kwa hiyo hata kama Watanzania tungependa klabu hiyo ije icheze hapa, ni ndoto ambazo zikiingizwa kwenye mfuko wa mlipa kodi zitatupeleka pabaya.
Kwa sababu taifa lina mambo mengine ya kipaumbele kuliko kujiingiza kwenye anasa za michezo kama hii.
Kwa sababu kama ni suala la kukuza vipaji, basi fedha zitakazotumika kuwa ‘kirimu’ Real Madrid, zingetumika kuibua vipaji na kuendeleza michezo katika shule nyingi hapa nchini.
Lazima tuwe na maono ya mbali na kuweza kutofautisha michezo kama anasa na michezo kama elimu na uwezeshwaji wa wananchi.
Michezo inapokuwa kwenye ngazi ya klabu ni vyema tuiachie sekta binafsi ya michezo (klabu ikaalika klabu yenzake kwa kuwa itajua vema ni jinsi gani itagharamia hiyo lakini mlipa kodi halazimiki kuchangia).
Rais wetu Jakaya Halfan Mrisho Kikwete,, anaposafiri nje ya nchi, ajitambue ni kiongozi wa wananchi na wananchi wake wanaishi kwenye lindi la umaskini uliotukuka.
Ambao hawana chakula,tiba,umeme wa uhakika, barabara,maji safi na salama ya kunywa na hivyo,wanafunzi wamerejeshwa majumbani kwa kukosa mikopo, asijione yeye ni sawa na Mfalme wa Saudi Arabia, anayeongoza kutoa mialiko bila kujali athari zake kiuchumi kwa watu wake.
Kwa sera,mtindo huu wa Rais Kikwete, maskini wa Tanzania watapasuka mapafu.Anatupeleka kwa ari,kasi na nguvu ya kutuua kabisa.
Natoa mfano halisi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanafunzi hawana maji ya uhakika, vyoo vinanuka,hawana madarasa ya kusomea,mabweni hayatoshi wanapanga uraiani ,wahadhiri wanalalamika kwamba mishahara wanayopewa ni midogo na aikidhi mahitaji ,wanafunzi hawana mikopo,lakini rais wa watu hawa yupo tayari kumlipa star ya Real Madrid Sh.Milion 200 kwa wiki . Hakika hii ni busara isiyo na busara.
Mwishoni mwa mwaka jana, Soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya, liliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni na wafanyabiashara wa soko hilo wengi ni raia wa kawaida wa kima cha chini.
Serikali ya awamu ya nne haijawajibika kwa namna yoyote ile. Na kama serikali inaweza kuchangisha wafanyabiashara wakubwa wawape fedha za bure klabu ya Real Madrid, kwa nini serikali hiyo isiwachangishe wafanyabiashara hao wakubwa wawasaidie wafanyabishara wa Soko la Mwanjelwa?
Tembelea hospital yaTemeke,Mwananyamala, utaona wakina mama wajawazito wanavyojifungua katika hali duni.
Hutaona wagonjwa wanavyoishi katika hali duni,utaona mitambo ya kawaida kama X-Ray haipo lakini Rais wetu, ndoto zake zipo kwenye starehe ya Real Madrid. Je huyu ni rais wa walala hoi?
Upo umaarufu wa bure wa kusikika kwamba wewe ndiye rais pekee uliyeleta timu hiyo na watoto wa kijiweni watakusifia kweli kweli bila kujali kwamba hata hiyo fedha ya kuingia langoni kuwaona mastar wa real Madrid wakilisakata kabubumbu hawatakuwa nayo.
Kwa hiyo JK kakosea, kama yeye alikuwa na akiba yake binafsi hivyo anaileta timu hiyo kwa gharama zake hiyo ni sawa, hatuna ubishi.
Lakini haiwezekani, hatutaki na tunakemea Rais wetu kualika klabu hiyo ya nje na kutumia wadhifa wa Urais kutoa maelekezo ya kuchangisha gharama za klabu hiyo.
Hilo hatulitaki kwa sababu ni kudhalilisha nafsi hiyo ya urais wa Tanzania.Kumbe rais wetu sasa ni wakala wa kawaida wa klabu za michezo za Ulaya?
Rais hakutakiwa kabisa kujiingiza katika biashara ya klabu za mpira,yeye kama raia angeweza akafanya mipango ya kualika timu za Mataifa mfano timu ya taifa ya Nigeria, Hispania, Italia, Afrika Kusini, Ujerumani, England na kadhalika.
Na hizo timu ingekuja hapa nchini,itakuja kama sehemu ya ushirikiano wa Utamaduni kati ya nchi yetu na nchi hiyo na isingekuwa na gharama za kibiashara kama hizi kwakuwa taifa ya timu yake ingechangia gharama na sisi taifa letu lingechagia gharama ukitofautisha na ujio wa Real Madrid, wananchi na makampuni ya hapa yataigharimia kwa asilimia mia moja.
Hivyo fikra hizi za kualika nyota wa klabu ya Real Madrid, kuja hapa nchini kupora kile kidogo kilichosalia mifukoni mwa

Watanzania, tunazipinga kwakuwa hazituakikishii maisha bora kwa kila Mtanzania, badala yake ina mwakikishia Mtanzania wa kawaida atakuwa maskini maradufu.

Mungu ibariki Afrika!
Mungu inusuru Tanzania.
katabazihappy@yahoo.com

No comments:

Powered by Blogger.