Header Ads

Taaluma ya Habari:Inaandaliwa Kitanzi!



Taaluma ya Habari: inaandaliwa kitanzi!

Na Happiness Katabazi

DEMOKRASIA ni msingi wa utawala bora na utawala bora ni kutawala kwa misingi ya uwazi, ukweli na kuwashirikisha wananchi.
Uwazi katika Serikali ni nini? Uwazi katika uendeshaji wa serikali yoyote ile unamaanisha kwamba, shughuli zote za serikali ziwekwe wazi kwa wananchi.
Taasisi/mhimili unapojihusisha na kuhabarisha wanajamii ni vyombo vya habari. Kwa hiyo, serikali iwe tayari kutoa habari kwa waandishi wa habari wazifikishe kwa wananchi.
Sasa kilichotokea kwenye Rasimu ya Muswada wa Uhuru wa Habari wa mwaka 2006 nchini ni kwamba, habari zote zinazohusu uundwaji wa sera za nchi ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha rasimu yenyewe.
Habari zote zinazowasilishwa na kujadiliwa ndani ya baraza la mawaziri na maamuzi ya baraza la mawaziri ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha rasimu hiyo.
Habari zote zinazohusu usalama wa Taifa, Ulinzi wa Taifa, Ushirikiano wa Kimataifa ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha rasimu hiyo.
Habari zote ambazo zimelindwa na sheria, kanuni au mila za usiri wa shughuli za usiri wa serikali ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha rasimu. Pia habari zote zinazohusu siri za biashara na biashara ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 33.
Habari zote zinazogusa maslahi ya uchumi wa nchi ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 34. Habari zote zitokanazo na utafiti kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha rasimu ni siri. Habari zote zilizopatikana kwa ahadi kwamba zitabaki siri nazo pia ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 36.
Habari zote ambazo uchapishwaji wake unaweza ukaathiri maslahi ya Taifa, jamii ni siri kwa mujibu wa kifungu cha 38. Na Waziri husika anapewa mamlaka ya kutangaza habari fulani ni siri na isitolewe na vyombo vya habari kwa kuwa itaathiri maslahi ya taifa kwa mujibu wa kifungu cha 42 cha rasimu hiyo.
Wanahabari wenzangu na jamii kwa ujumla ukijumlisha vipengele vyote hivi na ukizingatia kwamba kwa mujibu wa sheria ya Uhifadhi wa Nyaraka za Taifa , muda wa usiri ni miaka thelathini.
Je, huo uwazi wa serikali yetu katika misingi ya utawala bora uko wapi? Kwanini serikali yetu inapenda ngonjera hata kwenye maswala nyeti kama haya?
Hebu viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza, tuelezeni kwa fikra zenu uwazi katika shughuli za serikali ni kitu gani?
Au sasa tuseme mawaziri na viongozi wa serikali wanapofanya harusi kubwa za watoto wao, birthday ya Taifa, safari za Rais na Waziri Mkuu nje ya nchi ndiyo habari za kuwaambia wananchi?
Tuachane na hilo, rasimu ya mwasada huu ni mbaya pia kwasababu unaweka vipengele vitakavyounda baraza la habari la serikali, hilo limeitwa Media Standard Board kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha rasimu hiyo.
Sasa baraza hili linaundwa ili kutawala na kudhibiti taaluma ya habari nchini kwa hiyo baraza hili ndilo litakuwa na uwezo wa kubuni maadili,kuyaweka na kuwadhibiti wanahabari kulingana na maadili hayo.
Baraza pia litakuwa na uwezo wa kutoa leseni za uandishi wa habari kulingana na masharti yatakayowekwa na baraza.
Mwenyekiti wa baraza hili atateuliwa na rais na litakuwa ni taasisi ya serikali. Pia baraza hili litakuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya wanajamii dhidi ya wahandishi wa habari.
Taasisi ya Uandishi wa habari ni muhimili usio rasmi wa dola ambao ni vyema ukibaki huru bila kuingiliwa na dola.
Kwa rasimu hii kwa mara ya kwanza, muhimili huu una rasimishwa kwa mithili ya kutawaliwa na kufungwa minyororo badala ya kulindwa na kupewa uhuru kwa kutekeleza kazi zake.
Baraza la habari lililopo limeundwa na wadau wa habari baada ya serikali kushindwa kuunda baraza hilo mwaka 1993, kutokana na harakati za wadau kupinga kuundiwa habari na serikali.
Leo hii wanahabari tuna baraza letu tunalolitii na kulithamini ambalo utendaji wake ni wakusifika.
Baraza la habari la Tanzania lina ufanisi wa asilimia 97, kwamba mashauri yote yaliyoamriwa na baraza yametekelezwa kwa ufanisi huo.
Sasa kwanini serikali inataka kuiondolea jamii taasisi inayojiendesha yenyewe, inayofanyakazi kwa ufanisi ili kutuundia baraza la kikilitimba la serikali?
Shime wanahabari, tushike kalamu na Note Book, tujitome kwenye vyombo vyote vya habari kuhakikisha tunaandika makala na habari kwa mapana zaidi kuhusu hii rasimu ili wanajamii ambao nao wanaitaji kupata habari wajue serikali imedhamiria kuichinja chinja taaluma ya habari.
Nanimalizie makala hii kwakumwoma Rais Kikwete, aisome rasimu vilivyo aone vipengele vilivyowekwa ambavyo vinachinja taaluma ya uandishi wa habari wa hapa nchini kwake na kisha arejee maagizo na ahadi zake ambazo amekuwa akizitoa alipoingia madarakani kuwa serikali yake itashirikiana kwa karibu na vyombo vya habari na pia alikuwa akiwataka watendaji wake kutowakimbia na kutowanyima habari waandishi wa habari.
Binafsi naamini maagizo na ahadi zake hizo alikuwa akizotoa kwa moyo mmoja ila kama alikuwa akizitoa kwa malengo ya kufurahisha umma basi ukweli utadhihirika pale atakapo kubali rasimu hii iwe sheria na pia ndipo tutakapo amini msemo maarufu usemwao “hakuna urafiki wa kudumu baina ya wanasiasa na wanahabari’.
Mungu Ibariki Tanzania
0755-312859:katabazihappy@yahoo.com
mwisho

No comments:

Powered by Blogger.