Header Ads

ELIMU YA TANZANIA NA WALIMU WA WIKI NNE

(MAKALA)

Happiness Katabazi

SERIKALI ya awamu ya nne, imekuja na mkakati mpya wa kuinua elimu kwa kuimiza ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata kiasi kwamba, kwa sasa tumekuwa na shule za aina tatu. Aina hizo ni sekondari za kitaifa, kata na za binafsi.

Kwa hiyo, katika kila sekondari za kata, mhudumu mkubwa katika hizo shule ni halmashauri na manispaa. Serikali Kuu kwa upande wake itakuwa inatoa ruzuku katika shule hizo.

Hatua hiyo inalazimu kuongezeka kwa idadi ya walimu, vifaa vya kufundishia, mahabara na samani.

Katika kutatua tatizo la upungufu wa walimu, serikali ya awamu ya nne imekuja na mbinu ambayo wamejinadi kuwa ni dawa ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu, hasa ukichukulia wingi wa shule zilizojengwa.

Hatua hizo ni pamoja na kuwachukua walimu wote wenye diploma walio katika shule za msingi na kuwapeleka kufundisha sekondari za kata.

Hatua ya pili ni kuajiri wanataaluma wengine wasio walimu kujaza nafasi za walimu, na hatua ya tatu ni kuajiri walimu wa diploma na hatua ya mwisho ni kuajiri walimu wa leseni (crush programe), ambao kwa sasa huko mitaani wamepachikwa jina la ‘Voda Fasta’. Kwa hiyo, makala hii nitachambua nafasi ya walimu hawa wa leseni (Voda Fasta).

Tuangalie kwa sasa watoto wameandikishwa shule wakiwa na umri wa miaka 6 au 7. Kwahiyo tuchukulie mtoto ambaye ameanza shule na miaka 6, ina maana kidato cha sita atamaliza akiwa na umri wa miaka 19.

Sasa huyu mtoto mwenye umri wa miaka 19, tunafikiria hata masuala ya kubalehe hayajamtoka bado, hajui saikolojia ya malezi, hajafundishwa malezi na mbinu ya kufundishia.

Na wanafunzi hawa hawa, wanapohitimu kidato cha sita serikali inawachukua na kuwapeleka kwenye mafunzo ya wiki nne katika vyuo mbalimbali vya ualimu kwa kuwafundisha (mafunzo ya muda mfupi ya ualimu) na kuwaajiri kwa leseni, tayari kwa kutufundishia watoto wetu.

Watanzania tujiulize hawa walimu (Voda Fasta) wataweza kutekeleza majukumu ipasavyo ikiwa wenyewe bado ni watoto na walivyokuwa kidato cha tano na sita hawakufundishwa na walimu wao saikolojia na uongozi?

Na matokeo ambayo tumeishaanza kuyashuhudia ni mahusiano kati ya walimu na wanafunzi kwa lugha ya mitaani yanakuwa ya ‘kishikaji’, hakuna nidhamu, ufundishaji ni wa kukariri na vile vile kwa sababu walimu wengi hawa wa ‘Voda Fasta’ wanakuwa hawajatokwa vizuri na hali ya kubalehe, matokeo yake ni kutongoza wanafunzi na si muda mrefu tutashuhudia mimba nyingi mashuleni.

Isitoshe, shule nyingi ambazo voda fasta wamekwenda, kumeanza kutokea misuguano kati yao na wanajamii wanaoishi maeneo yanazozunguka shule na walimu wakongwe.

Tunavyosema msuguano katika jamii unatokana na kwamba, mwonekano wa voda fasta kama walimu, haupo kati ya walimu wakongwe wanaojua ualimu na maadili yake, wanakuwa wanakinzana sana na hawa Voda fasta na hivyo kuonekana kama wananyanyaswa kumbe ni kutokana na kutojua masharti na maadili ya kazi yao kama walimu, walezi na wazazi mbadala.

Kiutawala, hawa Voda fasta hawajui uongozi wa shule (School Administration) na kukabiliana na migogoro (crisis Management), mathalani migomo ya wanafunzi, matatizo ya kinidhamu na kisaikolojia, utendaji wa kiutawala. Mfano, majukumu ya mkuu wa shule, mwalimu wa taaluma, mwalimu wa malezi hata mwalimu anayesimamia miradi ya shule.

Hawa Voda fasta wamejikuta wakikabidhiwa madaraka ambayo hawajui miongozo na miiko yake na kulazimika kukabilina nayo ghafla bila kuwa na kiongozi au uzoefu kazini, hasa ukichukulia wakuu wengi wa shule mpya za kata ni walimu wenye diploma waliokuwa shule za misingi ambao nao pia hawana uzoefu au ujuzi wa uongozi kwa ngazi za sekondari.

Waliosomea diploma zao kama sehemu ya kujiendeleza tu kwa ajili ya kupandisha madaraja yao ya mishahara pasipo kuwa na nia ya ya kufundisha shule za sekondari.

Ili kuhakikisha malengo ya kila mtoto anapata elimu ya sekondari, serikali haina budi kuweka mikakati madhubuti ya kupata walimu wananaokidhi, si kupeleka bora walimu kufundisha watoto wetu hawa.

email:katabazihappy@yahoo.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis April 3,2007

No comments:

Powered by Blogger.