Header Ads

Kumbe Wanamageuzi ni wakombozi wa kweli wa taifa hili

Na Happiness Katabazi

WACHUNGUZI wa mambo ya siasa wanaoitazama Tanzania leo wataona kuwa mfumo wa Kidemokrasia unaojengeka na uchumi wa soko unaendelea kushamiri nchini ni mwendelezo wa sera za chama kimoja.

Mtizamo huo kwa hakika ni potofu kwakuwa sababu kubwa ya Tanzania kuondoka kwenye mfumo wa chama kimoja na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi ni kuzorota kwa uchumi uliyokuwa unatawaliwa na sekta ya umma.

Harakati za wanamageuzi kudai demokrasia vya vyama vingi zilizaliwa katika mchakato huo.Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere, alikiri ukweli huo na kukishinikiza Chama Cha Mapinduzi(CCM), kiridhie mabadiliko ya vyama vingi kuliko kingoje kung’olewa madarakani kwa shari.

Kwa mantiki ya Mwalimu Nyerere, moja wapo ya majukumu makubwa ya wanamageuzi ni kukiweka chama tawala macho ili kisinzie wala kubweteka.

Tukitazama Ilani za vyama vya Mageuzi tutaona kwamba mengi mazuri tunayoshuhudia leo hapa nchini kwetu, ni matokea ya juhudi za wana mageuzi, wanamageuzi ndani ya vyama visivyo madarakani na wanamageuzi nje ya vyama hivyo wameibua hoja nyingi nzuri za kulisaidia taifa letu ambalo zimewazindua wana CCM kwenye usingizi mnono na kuanza kuzitekeleza.

Tatizo ni kwamba walipoanza harakati zao wanamageuzi miaka ya 1980, walionekana kuwa wapinzani wa serikali na chama tawala,wahuni, vichaa,waroho wa madaraka na maadui,wanaharamu.

Mara nyingi viongozi wa CCM walitumia na wanaendelea nguvu za dola kuwahujumu na kuwadhibiti na alitumia baadhi ya vyombo vya habari kuwapaka matope ili waonekane kuwa ni wenye njaa kali, wasiro na sera na ambao wataleta vita endapo watachaguliwa kuongoza taifa hili.

Sambamba na mtizamo huo, viongozi wa CCM walijaribu kutoelewa hoja za wanamageuzi kwa kuzibeza kwa kujitapa kuwa CCM ni namba moja.

Lakini tukitizama basi baadhi ya sera au mambo muhimu ambayo wanamageuzi wamelitetea taifa, wanamageuzi walipinga ubinafsishaji holela wa Mashirika ya Umma na kutuambia kwa taifa sio nchi ya kwanza kubinafsisha sekta ya umma, hivyo hapana haja ya kukurupuka kufanya ubinafsishaji bila kujali maslahi ya taifa letu.

Wanamageuzi waliona kuwa ingekuwa vyema taifa livute pumzi na kupanga ratiba ya ubinafsishaji itakayowapa wananchi kipaumbelea katika umilikaji wa sehemu kubwa ya sekta ya sekta inatakayobinafsishwa badala ya kukabidhili hatamu wageni.

Je! tungewasikiliza wanamageuzi, tungeshuhudia Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) ingeuzwa kwa bei ya nazi sokoni?

Ebu tujiulize thamani ya Jengo la Millenium Tower ambalo limejengwa kwa bilioni 35, ni kubwa kuliko benki ya NBC iliyouzwa kwa bilioni 15?

Ebu tuangalie wanamageuzi kuhusu sekta ya madini, tukisoma sera na Ilani zaom wengi wao wanasema si halali wa Tanzania kuambulia mrahaba 3% kutokana na madini ya nchi wakati wageni wakiruhusiwa kuondoka na 97%.

Duniani kote utajiri wa nchi ni rasilimali zake za asili.Waarabu ni matajiri kwasababu wana mafuta,Makaburu wa Afrika Kusini ni matajari kwasababu wana dhahabu.

Iweje Tanzania ni nchi ya tatu kuzalisha dhahabu Barani Afrika na ni nchi pekee duniani kuwa na madini ya Tanzanite, iitwe nchi maskini?

Tunachokiona hapa ni kwamba CCM haijui itendalo,ingekuwa vyema chama hicho na serikali yake kingekuwa kinasikiliza wanamageuzi katika suala hilo.

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, amekiri upungufu wa sera ya madini na mikataba yake na ameaidi serikali yake itatazama upya mikataba hiyo nakuongeza kuwa serikali haitaruhusu kusainiwa mikatana mipya ya madini hadi hiyo iliyopo ipitiwe.

Lakini cha ajabu ambacho watanzania wamekishuhudia wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Kaskazi Kabwe Zitto, amewafungua maskio wananchi kupitia bunge, kuwa Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi, amesaini mkataba mpya licha mikataba ya zamani haijamalizwa kupitiwa.Wamesaini mkataba wa Buzwagi ,nchini London, Uingereza na kuliomba bunge liunde tume,na alichoambulia sote tunajua kwamba hoja yake ilitupiliwa mbali na kushughulikiwa kikamilifu na wabunge wa CCM na kusimamishwa kuudhulia vikao vya bunge hadi Januari mwaka 2008.

Ila kinachofurahisha ni kwamba Rais Kikwete, mwenyewe ni mhusika wa karibu na sera hizo na mikataba hiyo kwakuwa alikuwa Waziri wa Nishati na Madini,Waziri wa Mambo na nje na Kada mahiri wa chama tawala.

Suala ni kwamba ahadi za Rais Kikwete zitatekelezwa lini?Je ataruhusu serikali yake iendelee kuingia mikataba mipya na makampuni za madini kabla mikataba ya awali atujaalifiwa kama imeishamalizwa kupitiwa?

Kwahiyo tunasema wanamageuzi waendelee kuvuta kamba kwani hatujui nani ni nani katika mikataba ya madini bila shaka harakati na kelele za wana mageuzi zitalikomboa taifa.

Tukiangalia suala la umaskini, sera ya CCM ilikuwa ni ujamaa na kujitegema, sera hizo zilishindwa na wenyewe CCM walizitumbukiza baharini kule Zanzibar wakati Baba wa Taifa, aking’ali hai.

Sera za uchumi wa soko, ni sera za wanamageuzi sera hizo sasa zimetekwa na ccm ndizo rasmi sera zake.

Lakini tofauti ya wenye sera na waigaji wa sera ni kubwa,ccm imkumbayia sera za soko huria za Shirika la Fedha Duniani.

Hivyo CCM inazungumzia Mpango wa Taifa wa Kupunguza Umaskini ifikapo mwaka 2025(MKUKUTA).Wanamageuzi kwa upande wao wanazungumzia uchumi wa soko unaoendeshwa na kutawaliwa na wazawa hivyo kwa upande wao, suala si kupunguza umaskini bali ni kufuta umaskini haraka iwezekano.

Kwahiyo wanamageuzi kwa mujibu wa Ilani zao wanatoa kipaumbele katika kuwawezesha wazawa kwa makusudi.
Suala linajitokeza sasa ni kama ni sera hipi kati ya hizi mbili zitalikomboa taifa.

Tukitazama mifano hai ya nchi za Bara la Asia kama vile Marasia,Taiwan,Korea Kusini tunaona kwamba wenzetu wameamua kufuta umaskini badala ya kupunguza makali yake.

Tunatamani sana kama wanamageuzi wangevuta kamba na kushinikiza taifa likubali kufuta umaskini badala ya kupunguza.
Kinachoshangaza ni taifa kukubali kuuza taasisi za fedha.

Je ni busara gani kuuza benki ya Taifa ya Biashara kwa wageni na wakati huo huo kuanza kampeni ya kuanzisha Benki ya Wananchi?

Je ni busara gani kuanzisha Benki ya NMB kwa juhudi kubwa ya wananchi wenyewe bila mtaji wowote na mara ilipoanza kufanikiwa ikauzwa kwa wageni?

Je! Ni busara gani taifa kupoteza muda wake kuimiza na kuanzisha SACCOS wakati linakataa kuendesha benki ya Microfinance?Aina hii ya uchumi wa kundunduliza kamwe haiwezi kufuta umaskini.

Kwahiyo kilio cha wanamageuzi kutetea benki ya Microfinance isiuzwe ni kilio cha taifa na ndiyo mkombozi wa taifa kiuchumi.

Wanamageuzi walipambana kweli kweli na sera ya elimu ya ccm na serikali yake ,waheshimiwa wa ccm,waliamua kufuta masomo ya biashara,kilimo,uraia,michezo na wakaamua kuunganisha somoa Kemia na Fizikia bila mantiki yoyote.

Mantiki ya kufuta masomo hayo ni kuzalisha taifa la mambumbubu wasio na uwezo wa kukabaliana na utandawazi ili wakoloni waje kutatawala tena.

Hata taasisi zisizoza kiserikali zizilizo jaribu kupambana na aina hiyo ya elimu ,mfano,Haki Elimu, zilijikuta zikitishiwa kufungiwa.

Sera za mageuzi sio tu zilidai kurejeshwa kwa mtaala wa zamani ila pia zilidai kuboresga mtaala huo ili kumudu changamoto za utandawazi.

Wanamageuzi pia wamekuwa wakihoji wingi wa viajan wanaomaliza darasa la saba bila kupata nafasi ya kwenda sekondari.Ilani nyingi za vyama vya mageuzi zinaonyesha kwamba elimu ya msingi kwa mtanzania ingefaa ipandishwe kitado cha nne.

Nakiri mantiki na ubora wa nchi hii,kinachofurahisha ni kwamba tayari serikali ya ccm imekiri ubora wa hoja hiyo hii na kuanza kuitekeleza japo kwa 50%.
Tatizo ni kwamba CCM imekurupuka kuitekeleza hoja hii bila maandalizi ya kutosha.

Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba ccm sasa imeachana na sera zake na Ilani yake na inatekeleza kinyemelea sera na ilani za vyama vya mageuzi, tunaisifu CCM kwakuwa wepesi kukiri na kuiga kwani hiyo ina maana na faida ya kuwa na Vyama Vingi vya Siasa hapa nchini.

Tusibaguane kwa sera wala itikadi ila tujali maslahi ya taifa letu.Wazo bora la wanamageuzi,wanaharakati,wataalam,wanyonge na sisi wanahabari lichukuliwe na kufanyiwa kazi kwa umakini.

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu namba 0755 312 859 na barua pepe katabazihappy@yahoo.com na tovuti. www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Agosti 26,2007

4 comments:

Anonymous said...

Mimi ni mmojawapo wa wasomaji na wapenzi wa makala zako. Lakini nakerwa kiasi fulani na makosa madogo madogo hasa spelling na wakati mwingine kukosekana na nafasi kati ya neno na neno. Kiuandishi kasoro hizo zinapunguza ladha kwa msomaji. Nashauri uwe unaproof read preferably umpe mtu mwingine aproof read ndo utaondokana na makosa haya. Ukiacha kasoro hizi, nakupongeza kwa makala zako nzuri. Keep it up!

Anonymous said...

Huwa nafurahishwa sana na makala zako zinazoangalia matatizo yanayoikumba nchi yetu kwa sababu tu ya ubinafsi wa baadhi ya viongozi. Wengi wasipojirekebisha hasa katika sekta ya madini nchi yetu itaangamia. Hongera Happy

Anonymous said...

Pongezi rukuki kwa Makala yako!
Wanamageuzi wana fanya kazi nzuri sana...... tuwatie moyo, tuwakubali na tuwaunge mkono! Kila mmoja wetu kwa nafasi yake aonyeshe kuwakubali wanamageuzi pasipo kuongopa. Kwanini uogope, lolote la HAKI na mageuzi ya kweli hayaji kwa kuweka woga mbele....lazima kutamguliza ujasiri! Pongezi pia kwa CCM kuwakubali na wazidi kuwaiga wapinzani... ni jambo la heri, nina washukuru.

Mungu wabariki Watanzania, Wanamageuzi na CCM wazidi kuwakubali na kuwaiga wapinzani wao. Amen!

Anonymous said...

mbona dada hukutoa maoni yangu.
Muganyizi

Powered by Blogger.