Header Ads

Hoja ya Zitto Kabwe:Bunge limesigina demokrasia!

Na Happiness Katabazi

JUMANNE ya wiki hii, tulishuhudia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likimwadhibu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), kwa kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Januari 2008 baada ya kumtia hatiani na kosa la kulidanganya Bunge.

Hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge huyo kijana kuliko wote kutoka katika majimbo ya uchaguzi, ya kuliomba Bunge liunde kamati teule kuchunguza uharaka uliosababisha Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Mustafa Karamagi, kusaini mkataba wa madini nje ya nchi, siku hiyo iligeuzwa na wabunge wa CCM na kuwa jambia kali kwa mbunge huyo kijana machachari, ambaye anajiamini na kusimamia yale anayoyaamini.

Katika hoja yake, Zitto alihoji sababu za Karamagi kusaini mkataba mpya wa madini wa mgodi huo London, Uingereza na kwa nini mkataba huo ulisainiwa wakati serikali ikiendelea kudurusu mikataba kama ilivyoagizwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Hoja ya Zitto kusimamishwa ubunge, ilijengwa na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir na Bunge likalazimika kuongeza muda wake ili kutekeleza adhabu hiyo, ambayo Zitto mwenyewe alipotakiwa kujitetea alisema yuko tayari kwa lolote.
Awali Zitto wakati akiwasilisha hoja hiyo, alitaka kujua sababu za kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusu asilimia 15 bila ya kibali cha Bunge.

Wapenzi wasomaji, tukumbuke sakata la Mbunge wa Mkuranga, Adam Kighoma Ali Malima na mfanyabiashara Reginald Abraham Mengi ambalo lilikuwa ni la kibinafsi na halikuwa na maslahi ya taifa, liliundiwa Kamati ya Bunge kuchunguza ukweli kwa sababu tu suala hilo lilisemwa bungeni na likaligharimu serikali zaidi ya sh milioni 100, ukweli ukabainika.

Tulitegemea Bunge lingemwadhibu aidha Mengi au Malima, lakini suala hilo liliishia kusemwa na Spika Samuel John Sitta kwamba, imetumika busara na mjadala ukafungwa.

Inakuwaje suala la Zitto Kabwe ambaye hoja yake ni ya msingi, ina maslahi kwa taifa, Bunge hilo hilo likamwadhibu, tena katika kipindi kifupi bila kuunda kamati ya kuchunguza wala kumpa nafasi ya kujitetea kwa sababu tu ya kutoa hoja bungeni?

Hata kama aliambiwa ajitetee wakati huohuo alipomaliza kutoa hoja, muda aliopewa haukutosha kwa yeye kujiandaa kutoa utetezi wake dhidi ya hoja ya Mudhihir, kwani kanuni za utoaji haki zinahitaji mtu kupewa mashitaka au tuhuma zake, ili azisome na kuzielewa, na hatimaye apewe muda wa kutosha kutoa majibu yake dhidi ya tuhuma hizo. Bila shaka hizi ni sheria za mwituni, za mbabe ndiye mwenye haki, ndizo zilizotumika.

Naamini Zitto alitumia uhuru wake wa kutoa maoni yake juu ya suala hilo kwa mujibu wa ibara ya 18 ya katiba inayohusu uhuru wa maoni na ibara ya 100 ya uhuru wa majadiliano bungeni kama ibara hizo zilivyoainishwa kwenye katiba ya nchi ya kuibua mambo yaliyokuwa yamejificha na yenye utata.

Kumwadhibu Zitto kwa hoja ya mbunge aliyetaka aadhibiwe, bila kuwa na kikao chochote cha kutoa maamuzi hayo kisheria, ni kukiuka kanuni za msingi za utoaji hoja.

Kwamba mtu aadhibiwe, asihukumiwe bila kupewa nafasi ya kujitetea na hilo Spika Sitta analijua, lakini kalipuuzia na kutengeneza kosa jipya linaloitwa 'kutoa hoja binafsi bungeni' ikipingwa mtoaji ana kosa anastahili adhabu na kila anayeshitaki na kushindwa kesi anastahili adhabu.

Mheshimiwa Sitta ni mwanasheria, tena ni wakili wa kujitegemea na aliyeahidi kuliendesha Bunge kwa ‘standards and speed’, na kwamba atawabana sana mawaziri watakaotoa majibu mepesi kwa maswali magumu.

Je, anataka Watanzania tuamini kwamba hafahamu kanuni za msingi za utoaji haki (rules of natural justice)? Je, anataka kuweka historia (precedent) kwamba mtu yeyote au wakili atakayeshitaki mahakamani na kushindwa kesi kwa hoja, ni muongo na anapaswa kwenda jela? Hata kidogo siamini kama hii ndiyo tafsiri ya sheria, naungana na Wakili wa kujitegemea, Sambwe Shitambala kwamba, ingekuwa hivyo, mawakili wote wanaoshindwa kesi kwa sasa wangekuwa ndani.

Mimi ninajiuliza, kuna ubaya gani kwa mtu kutoa hoja? (what’s wrong with putting up an argument?).

Ninaamini kwamba Spika anapokuwa anaendesha Bunge, yeye si wakili wala hakimu au jaji, hivyo basi maoni ya kina Mudhirhir kuwa Mhe. Zitto asimamishwe, hayawezi kuchukuliwa moja kwa moja kuwa ni uamuzi pasipo kuangalia ushahidi wa pande zote mbili, kwani hata Mungu mwenyewe katika bustani ya Eden hakuwaadhibu Adam na Eva bila kuwasikiliza, kila mmoja alipewa mashitaka yake akajitetea na mwishowe akapitisha adhabu.

Vivyo hivyo, wananchi, tulitegemea Bunge lingeunda kamati kuchunguza aliyoyasema Kabwe, kuona kama ni uongo ama kweli na baadaye kumwadhibu au kumwachia. Pia kitendo cha kumwadhibu Kabwe kinakwenda kinyume cha kanuni za haki za binadamu, zinazotaka usawa mbele ya sheria na kuondoa ubaguzi. Hivi inakuwaje kwa kosa hilohilo la kusema uongo, Malima hakuadhibiwa, lakini Zitto akaadhibiwa? Hata pale alipoambiwa amwombe msamaha Spika akakataa, na spika kujifanya kutumia busara kumaliza mgogoro?

Hivi tuseme kwamba kwa sababu Mhe. Malima hakuwa kambi ya upinzani ndiyo maana hakustahili adhabu hata ilipothibitika kuwa amedanganya? Ziko wapi standards and speed za Spika Sitta.

Zaidi ya hayo, wananchi tunajiuliza kuwa, hivi Bunge letu halina adhabu nyingine ya kuwapa wabunge zaidi ya hiyo ya kuwasimamisha kwa muda? Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004 zinaeleza wazi utaratibu utakaotumika pindi mbunge anapotuhumiwa kusema uongo na adhabu zake. Sasa ilikuwaje kumsimamisha Zitto bila kufuata utaratibu huo ambao Bunge limejiwekea lenyewe?

Je, Bunge halioni kwamba kwa kumsimamisha mbunge ni kuwaadhibu wananchi wasio na hatia, kwani matatizo yao na mapendekezo yao yatakosa uwakilishi? Poleni wananchi wa Kigoma, poleni Watanzania wenzangu, poleni vijana.

Hakika hii inatuonyesha kwamba wananchi tuna thamani wakati wa uchaguzi tu, na si baada ya hapo kwani bungeni anaguswa mbunge kama mbunge na si wananchi wake.

Imefika wakati sasa kwa Bunge kurekebisha kanuni zake ili kutofautisha adhabu zinazoweza kutolewa kwa mbunge kama mbunge kwa utovu wa nidhamu aliounyesha bungeni au uongo na adhabu ya mbunge na wananchi wake.

Hivi ni kweli Bunge limeshindwa kutofautisha maana ya uongo na maana ya kosa kwa maana ya ‘error’ au kupitiwa, au kuchanganya vitu viwili tofauti?

Kwa uelewa wangu mdogo, uongo ni hali ya kusema jambo unaloamini kuwa si la kweli au kusema jambo la kubuni kwa lengo la kuwaaminisha wengine ili kuwapotosha ‘knowingly misrepresenting facts’.

Lakini kuchanganya ni hali ya kutaja kitu kimoja kinachofanana na kingine kama vile ndiyo kile ulichokitaja ‘citing wrong provision’, ni vitu vya kawaida sana katika maisha ya binadamu. Tatizo hapa si nani mkweli nani mwongo, suala ni utaratibu mbovu usio wa kibinadamu uliotumika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari, Jumatano wiki hii, zilitueleza kwamba kitendo cha Zitto kuchanganya sheria ya madini, vipengele vya sheria ya kodi hali akiamini anayoyasema ya kweli, hiyo si tafsiri nyingine ya uongo, labda angetaja kitu ambacho hakipo kabisa katika ukweli na uhalisia wake.

Tatizo kubwa hapa lilikuwa ni kusainiwa haraka kwa mkataba; (a) nje ya nchi, (b) kwa kutofuata taratibu zilizowekwa, (c) kinyume cha kauli ya Rais Kikwete na aliyekuwa Waziri wa Nishati Dk. Ibrahim Msabaha, ambao waliwahi kusema kwamba serikali haitasaini mikataba mingine ya madini hadi mikataba ya madini iliyopo itakapomaliza kupitiwa, kauli ambazo hazijafutwa hadi leo, na hivyo tunaamini kauli hizo bado ni hai.

Ingekuwa ni busara kwa Bunge kuchunguza mambo hayo matatu kwa kuzingatia hoja zilizotolewa na Zitto na majibu ya hoja yaliyotolewa na Karamagi, kwani Mhe. Karamagi alikiri kusaini mkataba nje ya nchi na kitendo hicho ni kweli kilikuwa kinyume chaa kauli za rais na aliyekuwa Waziri wa Madini wakati huo.

Jambo lililokuwa limebaki hapa, ni kuthibitisha tu endapo utaratibu ulifuatwa ama haukufuatwa, na kama ingeonekana ulifuatwa, huo ndiyo ungekuwa mwisho wa jambo, kwani Mhe. Zitto angekuwa ametoshelezwa majibu kwa wasiwasi aliokuwa nao.

Tofauti na tulivyotarajia, umechukuliwa uamuzi wa haraka bila kuzingatia mambo tuliyotaja hapo juu, kwa maslahi ambayo tunaamini si maslahi ya taifa, bali ni maslahi ya ki-CCM zaidi.

Dhahama hili lililomkumba Zitto, litasababisha wabunge wetu wengi kuwa mabubu wanapokuwa bungeni au kuishia kuunga mkono hoja, hata iwe dhaifu kwa hofu ya kwamba akiuliza sana uenda akazikosa posho bungeni.

Tunafikiri kwamba hali hii ni kinyume cha nia ya ibara ya 100 ya katiba ya nchi, inayotoa haki ya uhuru wa majadiliano bungeni.

Endapo kungekuwa na chombo kingine cha kukata rufaa, tunaamini maamuzi ya namna hii yangetenguliwa. Lakini kwa kuwa Bunge lina mamlaka makubwa sana, tunaobaki kuumia ni sisi wananchi, hasa sisi walalahoi.

Uamuzi huu wa Zitto kusimamishwa hautufurahishi, si siri, haujawafurahisha Watanzania wengi, kwani hoja iliyokuwepo mezani haikuwa na maslahi kwa CHADEMA, CUF, CCM, TLP na vyama vingine, ni taifa zima.

Na kumwadhibu mbunge huyo hakujaweza kuondoa ukweli kwamba kuna mikataba ya kishenzi inayoingiwa na serikali na suala la Buzwagi ni mfano tu kati ya mikataba mingi mibovu iliyoingiwa, hasa ya madini.

Si siri tena, wabunge wengi wanaonyesha kuwa hawana utashi wa kulinda maslahi ya wananchi, na ndiyo maana wakakataa kuunda kamati kujadili suala lile muhimu. Na kwa jinsi Mhe. Mudhihir alivyoanza kutoa hoja ya kusimamishwa Zitto, na baadaye kuchangiwa na wabunge wengine, akiwemo Mheshimiwa John Samuel Malecela, inaonyesha kuwa mpango wa kumuondoa Zitto ulikuwa umepangwa mapema kabisa, tangu Zitto alipoanza kudadisi hotuba ya Karamagi.

Ikumbukwe kuzimwa kwa jambo lile bungeni si tiba, na wala kumuadhibu Zitto kwa kuonyesha uzalendo wake, kwani hakusaidii kuziba tatizo, bali kilichofanyika ni kudhihirisha tu kwamba Bunge limetumika kusigina demokrasia na uhuru wa majadiliano bungeni.

Tukubaliane kimsingi maswali ya Zitto hayajajibiwa, kwani jibu la kuwa kulikuwa na ulazima wa kuharakisha mkataba si jibu lenye mantiki hata kidogo, kwani sote tunaelewa kwamba hizo dola milioni 800 si za kwetu na kwamba sisi tunanufaika na asilimia tatu tu ya mapato ya madini.

Bei za mafuta zinavyopanda, mikataba ya kishenzi kama ya IPTL, ununuzi wa rada na kadhalika, haiwaumizi wanachama wa vyama vya upinzani tu, bali inamgusa na kumuumiza kila Mtanzania, hata wanachama wa CCM inayotawala nchi.

Hivyo, binafsi naamini kwamba hata wale wanachama wa CCM wanaoafiki kuondolewa kwa Zitto, ni kwa sababu ya unafiki tu, si kwamba hawajui ukweli, na baadhi wanaojua ukweli wamebaki kukaa kimya ama kuteta kwa chinichini tu, wakiogopa kama wataonwa watafukuzwa uanachama au majina yao kutopitishwa kugombea uongozi msimu ujao.

Ifike wakati kuwa, kunapokuwa na hoja yenye maslahi ya taifa, wabunge wote na wananchi tuweke itikadi zetu pembeni, tutetee hoja hizo au kupinga kama hazina maslahi kwetu.

Namaliza kwa kusema kwamba, kanuni za Bunge zinatumika au kutafsiriwa vibaya na baadhi ya wabunge. Sidhani kama Bunge la Kenya au Uganda, wanasimamishana ovyo, licha ya kwamba Bunge la Kenya limekuwa likisifika kwamba wabunge wake hata hufikia kupigana pindi wanapotofautiana katika hoja yenye masilahi ya taifa, lakini hatujasikia wakisimamishana kwa mtindo kama uliotumiwa na Bunge letu wiki hii.

Je, uhuru wa majadiliano bungeni na demokrasia ni mkubwa Kenya kuliko Tanzania?
Watanzania ebu tuamke usingizini, tuache itikadi zetu na woga tutetee maswala yanayohusu maslahi ya taifa zima na si vyama vyetu.

Wosia wangu kwa shujaa Zitto, sasa arudi jimboni kwake akaongee kwa ukaribu na wananchi waliomtuma bungeni, akawaeleze sababu zilizosababisha Bunge limsimamishe ubunge kwa kuwa wao ndio watakaomuhukumu, kwamba ndiyo waliyomtuma au amekiuka maagizo yao.

Aidha, atumie nafasi hii kuzungumza na wapiga kura wake na kupumzika na kuhimiza maendeleo ndani ya jimbo analoliongoza. Na asisahau kunusanusa na kupeleleza ufisadi unaofanywa chini chini kisha auanike bungeni atakaporudi.

Na uamuzi huu wa kusimamishwa naomba umtie nguvu zaidi na arudi na moto mkubwa panapo majaliwa Januari mwaka 2008, kwa maslahi ya wapiga kura wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Watanzania kwa ujumla. Tunakuombea Mungu akupe afya njema ili uweze kulitetea taifa hili kwa ujasiri ule ule. Tupo nyuma yake.
Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Mwandishi wa wa makala hii anapatikana kwa simu; 0755 312 859; baruapepe: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihapppy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 19,2007

5 comments:

Anonymous said...

Hello habari mimi ni Mtanzania naishi Hapa Tokyo. na Ni Mfanya biashara , Kuna swali nataka ulifanyie kazi ikiwezekana tutalipa hata nauli ya ndege uje Japan kuangalia malalamiko yetu. ni kuhusu Ukaguzi wa Magari yanayotoka hapa Kuja Tanzania, Hoja yetu ni kwa nini magari haya yasikaguliwe hapo Tanzania. kwa anayetumia. na sio huku? Cha ajabu nasikia magari yakifika hapo Tanzania yanakaguliwa tena. sina Uhakika na hilo hebu lifanyie kazi tafadhali
Willy
Wilna international
Tel; 81-90-7218-7118
http://members.jcom.home.nejp/wilna

Anonymous said...

Aisee Uchambuzii yakinifu
unajitaidi tunatarajia mengi
zaidi kutoka kwako..

anthony said...

Habari,
kwa kweli nimesikitishwa sana na kinachoendelea nchini Tanzania katika suala zima la siasa,hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyowachanga na wenye fikra siziso na mlengo wa mabadiliko katika suala zima la siasa na demokrasia japo tayari nchi yetu imefikisha miaka arobaini tangu ipate uhuru wake..kwa kifupi nachotaka kusema nchi yetu ina mapungufu makubwa sana ya kisheria hayo yameonekana wazi wazi kabisa ambapo kila mtu amekuwa mahakama na kujichukulia maamuzi yake mwenye ya utoaji wa hukumu pasipo kufuata haki na sheria husika hilo suala lililotokea bungeni si la ajabu sana kwa nchi yetu kulinganisha na mambo mengi tunayoyashuhudia kila kukicha mfano mzuri tunaweza kuuona kwa hawa polisi wetu , utakuta polisi kamkamata mtu ,basi pale pale anaanza kumpiga,sasa kama ikatokea mtu kapigwa na kisha kwa bahati mbaya katolewa jicho au kudhuriwa na badaye atakapofikishwa mahakamani kuoneka kumbe hakuwa na hatia...JE ni nani wakulaumia ,je ni fidia gani anayoweza kulipwa mtu kama huyu..HAKUNA!sheria ya Tanzania imekuwa wazi kabisa ambapo inaeleza kuwa ni mahakama pekee tu ndiyo inayoweza kuthibitisha kuwa mtu fulani anamakosa au la na siyo mtu yoyote kutoa hukumu,hiyo ni katiba iliyoandika ..kwa hivyo basi nilichokuwa nataka kusema kuwa katiba kama katiba tumekuwa nayo tangu nchi yetu ilipopata uhuru, lakini mpaka kesho imekuwa kama pambo kwani hakuna anayetaka kuifuata,hakuna anayeona umuhimu wake,hakuna msisitizo wa serikali kwa wanachi juu ya kuifahamu katiba yao,leo hii katika jamii zetu kati ya familiya mia moja utakuwa familiya moja ina katiba ndani au hakuna kabisa hali inayopelekea wanachi kutojua nini haki zao za msingi wanazopaswa kupewa na serikali ,Watu wamekuwa wakificha madhambi yao na kila mtu amaekuwa akiitumia vibaya .Adhabu aliyopewa bwana Zito Kabwe kwa kifupi ilikuwa kinyume na matakwa ya sheria na ya kikatiba pia kwani spika wala kamati ya nidhamu ya bunge haina haki ya kutoa adhabu kama hiyo ila mwenye haki ya kutoa adhabu kama hiyo ni mahakama inayoshughulia matatizo ya katiba au kwa nchi nyingine inaitwa (constutition court) hiyo ni mahakama pekee tu ambayo ingeweza kulitazama suala la zito Kabwa na hatimaye kutoa hukumu ambayo ambayo ingekubaliwa kwa pande zote mbili kulingana na uzito wa kosa na wala si vinginevyo.


anthony alnashir
russia

Anonymous said...

hebu mtafut huyoo waziri aliyeleta
balaa la maandamano juu ya zitto kabwe atueleze ukwelii.Tumechoka

Anonymous said...

Kwanza nimpongeze mwandishi wa Makala hii.
Pili ninawapongeza watu wote tulio guswa na swala zima la maamuzi mabovu ya baadhi ya wabunge wa 'CC' na kiburi na jeuri alivyo navyo 6! kwa masilahi ya Watanzania wote!

Hakika tukiendelea hivi kukataa na kupinga kwa nguvu zetu zote maovu yote watutendewayo na wanyama-watu hawa, ni dhahili tunaelekea pazuri kwani siku zinaweza kuanza kuhesabika za hawa wanao jifanya miungu watu, wasio kosea, wasio taka kukosolewa wala kushauriwa, kuambiwa ukweli, n.k. Wanazidi kutuharibia Siasa, waitumia kama mchezo usio na minzani! Demokrasia itakuwa iwapo tutawatolea uvivu wabadhilifu hawa, wasio penda umma kuelewa na kupiga hatua ktk kupata mandeleo kwa kutumia vizuri rasilimali zao!
Ukimya na umbumbu huu LAZIMA ufike kikomo!

Wapenzi wote tunaotaka kuona kuwa Demokrasia na siasa safi vinashamili hapa Tanzania hatuna budi kuanza harakati za kujikomboa na dhuruma hii. Kundi la watu wanaona nchi kama ya kwao, maamuzi mengi kwa faida yao wachache, Uroho wa kushibisha matumbo yao na kuweka kando Umma wa watanzania, wao wateule!? Hawakumbuki hata wale masikini walio wapa kura!

Hakika elimu ya uraia na siasa haina budi kufundishwa kwa watanzania wengi hasa walioko vijijini. Maovu haya tutaweza kuyadhibiti ipasavyo pale tu watu wengi hususani vijijini watakapo jua umuhimu na nafasi ya vyama visivyo tawala (Upinzani). Hata mwamuko tunao anza kuona leo hii ni pamoja na juhudi ya vyombo vya habari kujuza na kuelimisha umma (kwani wapo baadhi tunaofahamu umuhimu wa vyombo vya habari) kwa maendeleo ya Nchi, vyama visivyo tawala, watu wenye elimu (baadi yao wameanza kutumia Usomi wao kufanya maamuzi sahihi).

Ikumbukwe pia kwamba bado wananchi wengi wana imani potofu inayo endelea kujengwa na chama tawala kuwa Upinzani ni kupalilia chuki, machafuko (kuondoa amani) n.k vitu amabvyo si sahihi kwani wao wanapenda kuona kwa maisha yao yote kuwa wanchi wanazidi kulala usingizi fofofo na umasikini wa kupindukia!
Tanzania haipaswi kuitwa Nchi masikini hata chembe! Umasikini huu ni wakujitakia. Mambo kama; Siasa mbovu, ELIMU duni kwa wanachi walio wengi vijijini na TAKRIMA, kutowajibika na kutoadhibiwa kwa watendaji wa serikali na viongozi wa juu wa siasa, uroho wa madalaka na kutopenda kujiuzuru, kupenda rushwa ni baadhi ya mifano michache inayo changia Umasikini huu wa kujikadilia!

Lazima tuamke katika umbumbu huu. ELIMU KWA WAPIGA KURA ni nyenzo na jambo la kuvalia njuga kwa nguvu zetu sote wapenda demokrasia na Siasa safi. Wakati ni huu japo tulichelewa lakini tutafika!
Kila mmoja kwa nafasi na uwezo aliokuwa nao!
Eee.. Mungu utubariki....

Powered by Blogger.