Header Ads

Hatuna budi kuwabaini wadau wa ujambazi


IGP-Said Mwema

Na Happiness Katabazi

MWANZONI wa utawala wa serikali ya awamu ya nne, chini ya amiri jeshi mkuu Rais Jakaya Kikwete na mkuu mpya wa jeshi la polisi IGP Said Mwema, Watanzania tuliona mwanga wa matumaini katika ncha ya mwisho wa handaki lenye kiza kinene cha kushamiri kwa ujambazi hususan wa utumiaji wa silaha na mwingineo.

IGP mpya- mambo mapya, mathalani utumiaji wa helkopta kama teknolojia yenye tija katika kusaka majambazi na wahalifu kwa ujumla; heko ‘Njagu Mkuu’- Mwema.

Ama kweli kabla ya awamu ya nne matukio ya uporaji wa abiria wakiwa safarini, uvamizi wa mabenki, sehemu za starehe na majumba ya makazi pamoja na wizi wa magari yaligeuka kuwa ada siku hadi siku.

Katika kile kinachomaanisha kurejea kwa kasi mpya kwa uhalifu wa aina hiyo, mwaka huu matukio ya ujambazi yameshamiri upya kama ilivyoripotiwa na vyombo mbali mbali vya habari hususan mwezi Julai, 2007.

Ni katika mwezi huo wa Julai watalii wameporwa kule Mto wa Mbu, majambazi yaliiba nyumbani kwa mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, yakakwapua kwenye ATM mbalimbali, mengine yakakwapua kitita cha milioni ya shilingi katika benki ya NMB tawi la Mwanga,waliokuwa wanapata Tusker baridi baada ya kazi katika baa tatu za Changanyikeni nao yamewafika. Huko Geita nako nyumba ya wageni imevamiwa na wakora… loo, orodha ni ndefu kweli kweli!

Maswali kuhusu ujambazi huu ni mengi kuliko majibu. Miongoni mwa maswali hayo ni kwa nini ujambazi uongezeke na je majambazi wanamuduje kazi zao kwa msaada wa nani, ama nani hasa yuko nyuma yao akiwawezesha moja kwa moja ama kwa namna nyingine?

Wataalam kadhaa wa Sosholojia wanatwambia kuwa jambazi ni zao la jamii. Pengine ni kweli kwa kuwa majambazi nao wamezaliwa, yaani wana Baba na Mama, shangazi, wajomba, mahawala na wanandugu. Ama kwa hakika mtu hawi jambazi hivi hivi ila kwa sababu fulani fulani.

Wapo ambao wamekuwa majambazi kwa sababu walizaliwa na walikulia katika mazingira magumu, wakakosa mahitaji muhimu, wakakosa kufunzwa maadili, wakakosa kulindwa dhidi ya kujifunza tabia mbaya wakingali makinda.

Hivyo jamii yoyote iliyo makini haiwezi kupata usingizi endapo watoto yatima wanaongezeka, watoto wa mitaani wanarudufika idadi na wasioenda shule inashamiri.

Watoto wa jinsi hiyo ndio hugeuka kuwa vibaka na hatimaye majambazi kadri umri unavyoongezeka waongezekea na kadri matumbo yao yanavyozidi kuuma njaa.

Upo usemi wa kifalsafa kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Yafaa basi viongozi wetu na wanajamii sote kwa ujumla tuone haja ya kudhibiti ongezeko la watoto wa jinsi hii mitaani ili bomu walilobeba lisizidi kuongezeka petroli na utambi.

Basi linapozungumzwa suala la kusaidia yatima na watoto waishio katika mazingira magumu asiyejua umuhimu na maana yake afunguke macho sasa na asikie.

Kadhalika kisababishi kingine cha uwepo wa majambazi ni umaskini ambao unazidi kuota mizizi miongoni mwa wananchi tulio wengi. Hakika ni hatari kwa nchi tunapoendelea kushuhudia bila kuchukua hatua stahili za kudhibiti ongezeko la tofauti ya kipato kati ya wakwasi na mafukara.

Tofauti hiyo kubwa licha ya kuwa kichocheo cha tamaa ya mali kwa wale walio maskini ni chimbuko la chuki ya wasionacho dhidi ya walionacho. Maskini anapoendelea kuwa fukara ni rahisi sana kujiingiza katika ujambazi ili ajipatie cha kujaza tumbo lake.

Yamkini ujambazi mwingine ni vita vya chuki kati ya maskini wa kizazi hadi kizazi na tajiri wa enzi na enzi.

Hivyo, baadhi ya majambazi wanapoamua kubeba silaha wanaongeza kiwango cha kufyatua risasi wakiongozwa na chuki hii, na siombei mabaya ila tayari kuna kila dalili za kuzuka vita kati ya maskini na matajiri hapa nchini.

Baadhi ya mataifa makubwa duniani yameibaini chuki hii na wanajua wazi kwamba kadri dunia itakavyozidi kugawanyika kati ya wenye nacho na wasio nacho, ugaidi utaongezeka na uhalifu wa kimataifa utakomaa, na vita baina ya mataifa zitaongezeka.

Kwa kifupi ili tajiri ale kwa raha zake sharti ahakikishe maskini aketiye mlangoni pake naye kapata ukoko na makombo, vinginevyo kama wasemavyo waswahili pataendelea kuwa ‘hapatoshi/kujichimbika’, ujambazi utakuwa ni kila uchao tena kwa ari, nguvu na kasi ya chombo cha anga za mbali.

Ujumbe ni kwetu sote tunaofikiria kudhibiti ujambazi, imetupasa kutambua kuwa kadri tunavoendelea kuwa na sera zinazomtajirisha zaidi bepari (kwa mgongo wa ubinafsishaji na uwekezaji) ndivyo hivyo hivyo tunazalisha makabwela wasio na mbele wala nyuma.

Wenzetu wenye busara na akili timamu kama hayati Baba wa Taifa Julias Nyerere na Prof. Chachage wa Chachage waliutanabahisha kuwa nchi yetu sasa imetekwa na utandawizi ambao ni ubeberu katika lugha ya danganya jinga isemayo “utandawazi”. (Je ni kweli sisi watanzania ni mabwege hata kuliko yule Chifu Mangungo wa Msovero aliyeuza nchi kwa bei ya shanga na vipande vya nguo ya kaniki?).

Tujue wazi tunazidi kuongeza ‘makuruta’ katika jeshi hatari sana la ujambazi wa kujikwamua na kuelezea chuki iliyoko moyoni. Pengine lugha ya maneno ya kuwataka kubadilisha sera mbovu na mgawano mbaya wa keki ya taifa watawala wetu hamuielewi, eleweni basi lugha ya risasi za moto. Huko ndiko tunapoelekea sote, hata tukiachilia mbali hayo ya majambazi!

Chanzo kingine cha ujambazi kinachoshabihiana na niliyokwisha yataja, ni ukosefu wa ajira. Ni nani asiyejua kwamba matokeo ya mhitimu wa darasa la saba, kidato cha nne au cha sita na pengine chuo kikuu kukosa kazi ni kujiingiza katika vitendo vya uhalifu?.

Naam, asomaye na afahamu kwamba vita dhidi ya ujambazi haianzii katika kutisha wakazi wa ardhini kwa kurusha chombo cha usafiri kinachofanana na cha Mhe. Freeman Mbowe hewani, bali vita hii inaanzia katika kuwatafutia vijana ajira lakini kila mwaka shule zinapowaruhusu kuingia katika ulimwengu wa utafutaji.

Kwa ujumla jamii inao wajibu wa kudhibiti vyanzo hivi, na kwa maana hiyo jamii ni mdau katika suala zima la ujambazi.

Wengine ambao waweza kutajwa katika orodha ya wadau ni pamoja na vyombo vya dola, serikali na watu binafsi mmoja mmoja.

Udau huu uko katika namna ambayo wadau wengine wanao wajibu wa kutimiza ili kuiondolea jamii kero ya ujambazi, ilihali wadau wengine ni washirika wa majambazi. Ushirika wao umejikita katika kuwasaidia na kuwawezesha majambazi kuwepo na kufanya kazi zao.

Jambazi hawezi kutumia silaha hususan bunduki za kisasa, mabomu na silaha nyingine kali za kivita mpaka jambazi huyo awe amepata mafunzo mazuri ya kufanya hivyo.

Yawezekana majambazi wenyewe kwa wenyewe wanafundishana matumizi ya silaha katika makambi yao ya kificho, lakini hatuwezi kupuuza uwezekano kwamba majambazi wengine, yamkini walio wengi wana ujuzi wa matumizi ya silaha kutokana na mafunzo rasmi ya kijeshi.

Mara kadhaa matukio ya ujambazi yamebainika kuwahusisha moja kwa moja ama baadhi ya askari wa JWTZ au jeshi la polisi. Kwa upande mwingine, kitendo cha kufunzwa matumizi ya silaha kwa vijana wa kitanzania halafu wasipewe ajira yoyote iwe jeshini au kwingineko, ni cha hatari kabisa kwani ni mojawapo ya chimbuko la utaalam wa majambazi.

Kama nilivyosema mwanzo, ujambazi una uhusiano na ukosefu wa ajira na hivyo ni hatari zaidi kwa aliyefunzwa mbinu za kivita kukosa ajira.

Wakati umefika kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kufikiria upya kuhusu mafunzo ya kijeshi wanayoyatoa kwa vijana kwa kipindi cha miaka miwili huku wakipewa matumaini kwamba JWTZ itawachukua kwenda katika mafunzo zaidi (depo) na hatimaye waajiriwe katika jeshi hilo.

Inasikitisha kuona kwamba wanaofundishwa JKT ni wengi sana, na wanaochukuliwa na JWTZ na majeshi mengine ni wachache sana miongoni mwao. Yafaa JKT na taifa kwa ujumla tujiulize wanaobaki wanaingia katika sekta gani ya uhakika. Ya nini tujinase kwa tego letu sisi wenyewe. Nisikieni JKT; huo ndio udau wenu katika ujambazi.

Vile vile, jambazi hatumii silaha kali bila kuwa nayo. Swali la kujiuliza hapa ni je, majambazi wanapata wapi silaha. Baadhi ya majibu yako wazi kwani mara kadhaa majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha zinazomilikiwa na vyombo vyetu vya dola.

Na hiyo ndio sura nyingine ya udau wa vyombo hivi katika ujambazi. Jeshi la polisi linapoendelea kukaza buti katika kupambana na majambazi yafaa pia lijigeukie lenyewe na kuondoa kabisa ushirika wa baadhi yao katika kuwapatia majambazi silaha, kuwasindikiza majambazi kufanya uhalifu na kisha kuwatorosha.

Hatua za kuchukua ni pamoja na kuboresha maslahi ya askari wenyewe, ili isiwe kwao rahisi kushawishika kuchukua rushwa toka kwa majambazi na au kuwakodisha silaha wakafanyie uhalifu.

Kadhalika, jambazi hapati silaha na hatimaye kufanya uhalifu mpaka pawepo na udhaifu katika mfumo mzima wa uhifadhi silaha zenyewe na ulinzi thabiti wa maeneo tete. Enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa ni nadra sana mtu kukamatwa na risasi japo moja.

Lakini katika wakati tulionao mtu kukutwa na bunduki ,silaha na mabomu ni fasheni kana kwamba wahusika wanapata risasi kiurahisi kama vile kununua peremende kwenye kioski! Inakuwaje mambo haya…,maduka na maghala yetu yakuifadhia silaha na viambata vyake kwa nini yavuje kiurahisi namna hiyo?. Nitakuwa nimekosea wapi nikiwaorodhesha askari watunza maghala haya miongoni mwao ni wadau wa ujambazi nchini.

Suala la kwamba chanzo kingine cha majambazi na silaha wanazozitumia ni nchi jirani zetu. Lakini haitatosha kuwatupia lawama (japo za kweli) majirani hawa, maana laiti kama ulinzi wa mipaka yetu ungekuwa imara hao Wakenya wanaopora benki zetu huko Arusha, Mwanga na hata Dar es Salaam wasingefurukuta.

Wiki mbili zilizopita niliandika kwamba nchi yetu si salama japo tuna chombo kinaitwa Usalama wa Taifa na Idara ya Uhamiaji. Usalama wa Taifa kivipi ilihali mipaka yetu inapenyeka kiurahisi na majambazi kama maji yapenyavyo kwenye tenga la nyanya.

Na asante sana wasomaji wote mlionitumia pongezi kutokana na makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Twahitaji Usalama wa Taifa siyo Uhasama wa Taifa’.

Kumradhi walinzi wetu mipakani, udau wenu katika ujambazi ni udhaifu (pengine uzembe) huo katika kuifanyia doria thabiti mipaka yetu na kuwa makini katika vituo vya mipakani wanakopitia wageni kutoka na kuingia nchini.

Vile vile, jambazi mara nyingi havamii sehemu pasipokuwa na taarifa kwamba mahali fulani kipo anachokihitaji. Majambazi wanajua lini pesa zinasafirishwa, gari gani lina abiria wenye pesa, mahali gani wanalala watalii wenye vitu vya thamani, ni mfumo gani wa ulinzi uko mahali fulani.

Taarifa hizi wanazipata si kwa mzizi wala hirizi bali kutoka kwa wadau wao ambao pengine ni wafanyakazi wa taasisi itakayovamiwa au ni watu wa karibu wa wenye mali wanayoilenga majambazi.

Hapa ndipo udau wa mtu mmoja mmoja unapoingilia.Yafaa basi hatua za kudhibiti ujambazi zilenge pia kuwashughulikia wadau wa upashaji habari nyeti kwa majambazi.

Tochi itakayotumika hapa isikose kuwamulika wafanyakazi katika taasisi za fedha ambao uaminifu wao ni wa mashaka, walinzi ambao tabia zao ni walakini mtupu na wengineo.

Jambazi hafanyi shughuli zake bila kuwa na kambi/makao (base). Mara kadhaa imebainika majambazi ni wapangaji wa kawaida katika nyumba zinazomilikiwa na watu binafsi.

Tuwaulize wenye nyumba hizi, inakuwaje mtu usiyejua shughuli inayompatia riziki unaingia naye mkataba wa kupanga nyumba. Udau wa wamiliki wa nyumba katika ujambazi ndio huo. Lakini tuiulize pia serikali, mbona sheria ya ukaazi na ulazima wa mfumo wa wenye nyumba kuoanishwa na mfumo wa polisi hatujauibua?

Wenye nyumba jamani kuweni makini na watu mnao wapangisha, labda kama mnafanya mnachokijua endapo ninyi ni washirika wa majambazi.

Pia baadhi ya Madalali wa nyumba,vyumba nao kwa njia moja au nyingine ni wadau wa ujambazi kwani kupitia hiyo kazi yao ya udalali wamekuwa wakiwafahamu wahamiaji haramu na majambazi wanapoishi ila kwasababu wanazozijua wao wamekuwa hawataki kuisaidia polisi kuwafichua.

Nasema hivyo kwasababu mfano jambazi anaishi Kinondoni na akaona watu wameishaanza kujua nyendo zake anatafuta dalali anayemjua kisha anampa kazi ya kumtafutia nyumba katika maeneo mengine , ambapo katika eneo hilo atakuwa ni mgeni na hivyo itawachukua muda mrefu wananchi wa eneo hili kujua kazi anayoifanya.

Nasema hivi kwasababu mimi ni Mkazi wa Sinza C, na Kata ya Sinza ni eneo lilikuwa likisifika sana kwa kukaliwa na wahamiaji haramu na majambazi kuishi katika eneo hili,lakini mwaka jana Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya Sinza,ilikaa kikao pale Ukumbi Dulex, nami nilikuwa nimiongoni mwa wananchi walioudhulia kikao kile na ajenda kubwa ya kikao ilikuwa ni kupanga mikakati ya kutokomeza uhalifu na kuimarisha ulinzi Sinza.

Kama ilivyoada Polisi kituo cha Urafiki na Mabati, waliudhuria kikao hicho na kweli walishirikiana bega kwa bega na wananchi na ikatolewa azimio kwamba madalali nao washirikiane na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mitaa iliyopo Kata ya Sinza, na kweli baadhi ya Madalali kwa siri kubwa walishirikiana na kamati hizo ambao walitaja namba za nyumba wanazoishi wahamiaji haramu na watu waowashuku kuwa ni wahalifu na hatimaye Afisa Mtendaji wa Kata hiyo akishirikiana na Diwani wa Kata ya Sinza Salum Mwaking’inda, waliwasilisha orodha hiyo kwenye vituo hivyo vya polisi na kweli nilishuudia kwa macho yangu Defenda za polisi kila mara zilikuwa zikikatiza kwenye mitaa yetu nyakati za usiku na kuwakamata wahamiaji haramu kwenye nyumba walizokuwa wamepanga.

Hivi sasa wakazi wa ‘Sinza kwa wajanja’ tunaweza kusema idadi ya wahamiaji haramu na matukio ya uhalifu kwa kiasi fulani umepungua.heko polisi.

Wito kwa Manjagu wetu (Polisi), watumieni Madalali kupata taarifa za wahalifu wanapoishi na pia wahaamiaji haramu naamini mtafanikiwa.

Nisisitize hapa kwamba, kazi inayofanywa na jeshi la polisi kushughulikia majambazi kwa ufupi ni nzuri, kinachotakiwa ni utambuzi mpana wa wadau wa ujambazi na kuwashughulikia ipasavyo. Hatimaye wafikishwe mbele ya sheria, wakabidhiwe magerezani wakarekebishwe tabia (kama kweli Magereza yanafanya hivyo, na si kuwafunza wahalifu mbinu za nyongeza).

Naam, polisi dhibitini ujambazi wa kutumia silaha ila msisahau kwamba upo ujambazi mwingine unaozidi huu kwa mapana na makali yake, uko maofisini, unatendwa na wavaa kola nyeupe, suti na kubeba briefcase na, watu wenye haiba na staha mbele ya jamii. Kama waimbavyo wana bongo flava; ‘machoni kama watu moyoni hawana utu’, kina nani hawa… majambazi wanaotumia kalamu, na wadau wao.

Mwisho kabisa niiambie serikali kwamba hatuwezi kufanikiwa ikiwa tunaendesha mambo kishikaji. Tuanze kuthamini wataalamu wetu waliobobea katika taaluma husika kwenye taasisi binafsi na za umma hasa walio kwenye vyuo vya elimu ya juu. Pia tuwasikilize jeshi la polisi wanapoiomba serikali iwaongezee fungu ili iweze kufanyakazi yake kikamilifu kwani kitendo cha serikali kuendelea kuziba maskio na kutoa visingio kwamba serikali haina fedha huku serikali hiyo hiyo inaizinisha mamilioni ya hela kununulia mashangi ikome kuanzia sasa.

Watanzania tunataka tuishi kwa usalama katika nchi yetu, na polisi ndiyo wamekabidhiwa jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zetu hivyo hatuko radhi kuona ‘polisi njaa’ wanaotumia zana duni. Jeshi la polisi linapoiomba serikali itenge fedha za kutosha tunaomba wasikilizwe na kutekelezewa mara moja maombi yao.

Kwa kuwa sisi wananchi tumechoka kuona askari wetu wanaishi kwenye nyumba zisizoeleweka, sare zao zimepauka kama 'mashuka ya gesti', kuona askari wetu wamevalia ndani fulana ziliozoandikwa 'chagua ccm' badala ya kuvalishwa vikinga risasi 'bullet proof.

Umefiika wakati wa Jeshi la Polisi kutengeneza fulana zenye nembo ya Jeshi hilo ambazo zitavaliwa na askari wake wala moja kwa wiki kama ilivyo kwa askari wa JWTZ na JKT.Natumaini kwa uwelewa mkubwa alionao IGP Mwema na Makamishna wake swala hili watalifanyia kazi haraka.

Umefika wakati wa kuwa na jeshi dogo la polisi,bora na lenye vifaa vya kisasa vinavyowawezesha kufanyakazi katika mazingira yoyote yawe ya hatari au amani.

Pia umefika wakati nao polisi na makamanda wao kuungana pamoja kuikomalia serikali bila woga ili maslahi yao yaboreshwe kama ilivyo wafanyakazi wa majeshi mengine na sekta nyingine za serikali kwa kuwa askari wetu bila kuboreshewa maslahi yao ni wazi watavunjika moyo wa kulitumikia taifa hili. Hata hivyo napenda kumalizia kwa kuwaasa ndugu zetu kwenye jeshi la polisi wajihadhari sana na tabia ya kutumiwa na chama tawala hasa nyakati za uchaguzi.

Hivi mmeishawahi kujiuliza kama ninyi ni Umoja wa Vijana wa CCM au jeshi la usalama wa raia wa Tanzania? Tuhuma za nyie kutumika kuiba masanduku kura na kuwapiga raia wanapounga mkono wanamageuzi zitaisha lini? Hii kazi ya kuwabambikia kesi raia wanaounga mkono mageuzi amewapa nani na anawalipa nani kwa kazi hiyo? Hivi ninyi mnaona sisi raia hatujui wala hatuoni mnachokifanya? Basi endeleeni kuvaa vesti za “changua CCM” badala ya vesti za kukinga risasi tuone kama mtafika.

Sisi wananchi tunawapenda na kuwatetea kwa kuwa tunajua wajibu wa polisi kwa taifa lao lakini kwa tuhuma hizi, hatuwaungi mkono.

Mungu ibariki Afrika,Mungu inusuru Tanzania
0755312859; katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,Uk.7. Agosti 5,2007

4 comments:

Anonymous said...

Nam... kwa hakika Makala hii napenda kusema imekaa vizuri na imefika muda wake!

Heko mwandishi wa makala hii...H.K. Kazi unayo ifanya hatuna budi kuiunga mkono watanzania wote wenye uchungu na Maendeleo ya Taifa lao Tanzania. Napenda kukupongeza sana kwa umakini wako, utendendaji kazi wako pasipo kuegemea upande wowote kama wale wanao pewa vesti za "CC" Mungu akujaze na akuze zaidi juhudi na maarifa yako. Mungu inusuru Tanzania na watu wake!

Ombi; Kwako Mzalendo Mtanzania mahali popote ulipo acha tabia ya kukaa kimya pale unapoona mambo yanakwenda/yakienda ndivyo isivyo...! Sauti yako ni muhimu kusikika kwa Maendeleo ya Taifa hili ulimwengu waliita Fukara... ila mimi sikubali wala kuamini kuwa Tanzania ni masikini kiasi hicho kwa kile ninacho kiona viongozi wa Tanzania wakifanya katika maswala ya kupenda starehe, rushwa, ubadhilifu, kulindana, uanamtandao, serikali kuthamini chama tawala kuliko wananchi, kutowajika ama kuwajibishwa, kuunda tume ati za kuchunguza jambo au mambo pale yatokeapo.. "hili danganya totozi lengo ni kupoza sauti na kelele za wanao kuwa wanalalamika kwa wakati huo", kutunga sheria za kujilinda wao walioko madarakani na vibaraka wao, kukusanya mapato ya mabillioni ya fedha ya wavuja jasho na kuyafyeka hadi kupitiliza kwa njia wazijuazo wakiwaacha watanzania wakizidi kuandamwa na umasikini uliokithiri n.k.... Iko wapi siasa safi, uongozi bora, ndiyo.. watu tunao, ardhi tunayo vipi hayo mawili ya awali!? Kwa hayo machache tu yatosha kunithibitishia kuwa Tanzania ni Miongoni mwa Nchi Tajiri Duniani sema tu viongozi wa Siasa ndiyo kikwazo kwa Maendeleo ya Tanzania....Wameweka mbele siasa ya wizi na kujirimbikizia mali pasipo kutanguliza Utaifa! "Ama kwa hakika bora mara mia Mabepari weupe kuliko WEUSI"

Vyombo vya dola wanafanya kazi za siasa tofauti na zile zinazo wahusu ambazo ndizo walizo ajiliwa kwake. Sioni busara kurudia yote mwandishi aliyo yaandika, Makala imejieleza vilivyo...

Japo machache niliyo yaandika hapo juu nimejikuta machozi yakinitoka wakati natoa pongezi kwa Mwandishi wa makala hii muda mfupi baada ya kosoma makala hii. Ninako kwenda hata sijui kama nitafika siku ya kesho..... Eee... Mola niokoe katika ubepari huu mweusi!!! Kazi kwako pia mwanajamii. Kwa pamoja tutafika!

Anonymous said...

Makala hiii imenisisiua vya kutoshaa..nimetoka kujua blog hii kupitia kule kwa haki blog... kazana happy daima tupo nyuma yakoo maovu yotee weka wazi tuchangie

Anonymous said...

Unaongea kweli kabisa.. napenda kuwa wewe sio kama wale waandishi ambao wamefunga ndoa na CCM hivyo kuuza utu wao.
Josh

Anonymous said...

makala ni nzuri sana tatizo langu ni ulefu wa makala yenyewe kiasi inachosha.Ushauri wangu ...andika tu vile vya muhimu ukishambulia lengo halisi ili kumsaidia msomaji akimaliza kusoma awe anakumbuka alipoanzia, itapendeza sana.

Powered by Blogger.