Header Ads

KWANINI MAWAZIRI WANAZOMEWA?

Na Happiness Katabazi

MTAJI Mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake ni uoga na ukondoo wa Watanzania. CCM imekuwa ikidumisha ukondoo huo ili wananchi wabaki mbumbumbu wasio na uwezo wa kuona ukweli wa mambo na kuweza kukosoa sera, sheria na vitendo viovu wanavyofanyiwa na serikali.

Ningependa kuwapongeza Watanzania kwamba wameweza kuthibitisha katika wiki mbili hizi kwamba wamepevuka, si mbumbu tena kama baadhi ya viongozi walivyofikiria.
Wananchi wa Tanzania wameweza kuelewa hoja ya ufisadi iliyotolewa na Watanzania wenzao ambao nao wanaipenda nchi yao.

Pili, Watanzania wameweza kuwaadhibu viongozi wa serikali na CCM waliokwenda mikoani kubeza hoja ya wapinzani kwa kuwazomea adharani. Nawapongeza sana wananchi hasa wa Mkoa wa Mbeya.

Viongozi wa serikali wamekuwa wakitisha na kusema kwamba wapinzani ni wachochezi na hata vyombo vya habari vilivyoandika habari za ufisadi vimeitwa kuwa ni vya uchochezi.

Hii inamaanisha kwamba serikali ya CCM ina amini kwamba wenye haki ya kuwaambia Watanzania ukweli ni wao pekee.

Kwa hiyo, mtu mwingine yeyote akienda kuwaeleza wananchi taarifa zozote zile anaitwa mchochezi, mzushi, hana kazi za kufanya, asiye na hoja.

Lakini upo usemi unaosema kwamba unaweza kuwadanganya watu wote kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote, kwani ukweli unaposimama, uongo hujitenga.

Sisi Watanzania tuna uwezo sasa wa kuchambua mchele na pumba, si mahala pake sasa kulishwa kasumba na propaganda za CCM wakati fedha zetu zinaporwa, mali na rasilimali zetu zinafujwa na nchi inakwenda mrama na gharama za maisha zimepanda.

Jambo la kusikitisha ni kwamba serikali inawasikia wageni au wafadhili, lakini haiwasikilizi wananchi wake. Kwa hiyo serikali imeanza kuzijibu hoja za wapinzani kijuujuu baada ya wafadhili kuchachamaa.

Hii inamaanisha kwamba wafadhili wasingechachamaa, hoja za wapinzani zingepuuzwa, ukweli ungefichwa na ufisadi ungeendelea.

Kipimo cha heshima ya serikali yoyote duniani na viongozi wake, ni jinsi wananchi wanavyowapokea na kuwa tayari kuwasikiliza. Wimbi la zomeazomea ni ‘tsunami’ inayoizengea CCM na serikali yake.

Ipo hatari serikali hii ikasombwa na tsunami hiyo, kwani wananchi wanapokosa imani nayo, hawaiheshimu tena na wala viongozi wake hawaonekani kuwa viongozi wenye heshima.

Ukiangalia uendeshaji wa dola, mihimili mikuu ya dola imepoteza sifa. Mhimili wa kwanza ni Bunge, limepoteza umaarufu na sifa yake baada ya kujigeuza kuwa kama kamati tendaji ya CCM.

Matukio kadhaa ya hivi karibuni, yamedhihirisha kuwa Bunge letu kwa kiasi fulani halisikilizi hoja wala kufuata kanuni, kwa kuwa CCM ina vita ya kuangamiza wapinzani.

Kumbe fursa ya sauti ya wanyonge kusikika bungeni imepotea na mfano halisi ni jinsi Bunge lilivyojadili hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kuhusu utata wa mkataba wa Buzwagi.

Mbunge huyu kijana alifikisha hoja bungeni akimtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alivyotia saini mkataba huo hotelini nchini Uingereza.

Basi, hata kama Bunge lingeona hakuna haja ya kuunda tume huru ya uchunguzi wa mkataba ule, basi hoja hii isingesababisha Zitto kuadhibiwa, maana hakuwa amemdhalilisha mtu.

Mhimili wa pili ni serikali, nao umepoteza sifa kwa kujiingiza kwenye kashfa nyingi za kiutendaji, kashfa za namna hiyo zinaashiria ufisadi mkubwa ndani ya serikali yetu.

Mhimili huu una kashfa nyingi, ikiwemo kashfa ya IPTL ambayo hadi sasa tunaendelea kuilipa kampuni hiyo dola 100,000 kila siku, kwa mradi wa ovyo, na hatujui ni lini kashfa ya Richmond itachunguzwa ili wananchi waambiwe ukweli.

Kwa mtazamo wangu, hata chombo cha kukabiliana na rushwa kimekuwa chombo cha kusafisha na kupaka rangi ufisadi, kama kilivyofanya kwenye Richmond, baada ya Watanzania kuteseka sana kwa kukosa umeme na fedha nyingi kulipwa kwenye makampuni yasiyo na uwezo wa kuzalisha umeme.

Na hata hatujaambiwa nani amewajibishwa, tulichoambiwa ni kwamba hapakuwepo na rushwa. Hivi nani anaamini maelezo hayo?

Takukuru sasa inachunguza kashfa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na mkataba wa Buzwagi. Hivi Takukuru ina ubavu wa kuchunguza kashfa hizo? Watanzania tungoje tu kuambiwa Buzwagi na BOT hapakuwa na vitendo vya rushwa wala ufisadi.

Sasa matokeo ya aina hii ya utendaji wa dola ndiyo yanayopelekea wananchi kukosa imani na serikali, CCM na viongozi wake na kuamua kuwazomea na kuwapiga mawe.

Kama viongozi wetu wa serikali wasipobadili tabia na wakashirikiana na wananchi kutokomeza ufisadi na kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, nasisitiza tena viongozi wa CCM na serikali wasije kushaanga wakicharazwa bakora mitaani.

Wananchi wamechoshwa na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi, wamechoka na uroho wao wa mali usio na kipimo. Na hakika nasema, wakiacha kuzomea, watabeba bakora na kuanza kuwacharaza viongozi wetu, hatua ambayo sitaki tuifikie.

Mungu Ibariki Afrika,Inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Alhamis ya Oktoba 11,2007

9 comments:

Anonymous said...

Dada wewe Chadema sana, acha uongo wako, pia fanya mazoezi kupunguza umbo hilo. Hapa Ulaya siyo deal tena kuwa na li mwili kama hilo.
John

Rashid Mkwinda said...

Wamekataa Utanzania na kuthamini mambo ya kigeni,Tunawaita malimbukeni,hawajithamini, hawathamini kilicho chao kwa kudhani kuwa cha wenzao ndicho chao,bali wanaliwa wao,na kushibisha matumbo ya wenzao, wengi tunao wa aina yao, wapo tunakula nao tunacheka nao tunaandika nao, wala hakuna wabishao.

Hata hivyo Dadaa unajua jamaa wa aina hii hupenda kupania watu ambao si hirimu yao na hawawajui ni wa aina gani na wana mtazamo gani katika maendeleo ya nchi yetu lakini kikubwa nijuacho hawa jamaa ni katika wale walio wengi ambao tunawafahamu ni wa aina gani na wana mtazamo gani ambao ni maadui wa maendeleo ya nchi yetu.

Hivi suala kupunguza umbo hapa linakujaje na Ulaya na Tanzania wapi na wapi, kwani Ulaya ni mbinguni watu wengine xxxxxssssssfyuuuuuu!!!!!!

Rashid Mkwinda said...

Mwenda mbio angaa agana na Nyonga ungaa agana na Nyonga wewe!!!!haya ni maneno ya kifasihi katika wimbo mashuhuri ulioimbwa na Mrisho Mpoto katika utunzi wa Irene Sanga.

Ni mtazamo wa msanii lakini ujumbe wake unashabihiana na yanayojiri kwa zama tulizonazo.

Mbio za Awamu ya NNE ni Kasi Mpya , Nguvu mpya na Ari Mpya, lakini kasi hii haina mustakabali mzuri kwani kwa bahati mbaya sana mwenda kasi hizo hajaagana na watendaji wake, yaani ni Kasi mpya Nguvu Mpya, Ari mpya bila fikra mpya.

Tukae chini tutafakari enyi wananchi mpingao ukweli uliopo, hivi kwanini watu hawataki kuzinduka?kalamu zetu zitafanya kazi hadi bahari zote zikauke kwa kuandiaka ukweli na naamini bahari zitakapo kauka na ndio utakuwa mwisho wa dunia hakuna kitakachoandikwa tena zaidi ya wale waliohujumu na kufisidi mali za Wadanganyika watakaposimamishwa mbele ya Muumba kujibu Ufisadi waliokuwa wakiufanya duniani.

Kalamu zitaandika,midomo itasema,Tv zitatangaza na magazeti yatachapisha uozo unaofanywa chini ya jua linalowamulika Wadanganyika.

Tunasema imefika wakati wa walio nyamaza kunena, waliolala kuamka, waliosimama wakatembea, wanaotembea kukimbia na wanaokimbia kupaa angani kupaza sauti juu ya hujuma, dhuluma na ufisadi uliokithiri ndani ya jamii ya Wadaanganyika.

Alamsiki Dadaangu nakutakia kila la kheri Mungu akupe utambuzi zaidi na kutoa kile unachoona kinafaa katika jamii ye2.

Wakatabahu
RASHID

Anonymous said...

Kaka Rashid napoongelea mwili naongelea juu ya matitizo mengi sana, mojawapo ni la afya bwana. Dada zetu Bongo wanadhani unene ni deal, lakini kwa ujumla siyo hivyo, mimi nilikuwa nasema afanye mazoezi au aingie kwenye diet kidogo kuliko kula lunch hizo chips za kwenye bars etc.
John

Anonymous said...

Mimi Nakubaliana na wewe kabisa huyu anasema kuwa wewe Chadema ni Mpuuzi maana hata wazazi wake na ndugu zake wa kamalubanga kule hawana hata maisha bora hivyo CCM wamechoka na Imefika mwisho wa kufikiria Kama Kikwete hataweza kusikiliza Atashangaa mwaka 2010 anapata kura asilimia 20 ya kura. Watu wechoka na Porojo hizo za CCM Hawana Jipya bali ni Porojo tu. Hivyo Kuna Haja ja CCM kuona kuwa ushindi wa asilimia 80 sio Uthibitisho kuwa wanapendwa sana. hata Kidogo hivyo Wasijifanye wao Ndio Vingunge wa Nchi hivyo kwanza waseme mali zao. Na nyingi wananchi msiwape kura hata kidogo
Joshua Michael
Colorado Marekani

Anonymous said...

Kaka wa Colorado, nimependa sana usemi wako juu ya porojo za CCM, your very right, nadhani wabongo wengi wemechoka sana na siasa za CCM. Sina matatizo na wapinzani, but kitu kimoja wapinzani wa bongo hawana msimamo kabisa, maybe 2010, tungoje tutaona. Pia huyu kaka anayeongelea unene, yeye yanamuhusu nini mambo ya unene? Dada Happy tulete news bwana, achana na hao mabwana ambao wamekimbia bongo na wala hawana visas huko wanakoishi.

Anonymous said...

Dada Happy we peperusha habari kama kawaida bila kujali upuuzi wa huyu John,na nadhani hana akili timamu na kama anazo basi hakugusa shule kabisaa,Unene na uchadema vimekujaje kwenye hii mada,na kama Ulaya hauna dili wala Happy haishi huko na mawaziri wanaokosolewa ni wa Tanzania sio wa Ulaya.
Sio kweli kuwa watu wanene wote ni wagonjwa,mimi nijuavyo dalili za magonjwa mengi ni wembamba,John fahamu kuwa Mungu huwa hampi binadamu kila kitu,atakupa hiki na atakunyima kingine na hata wewe hapo haujakamilika lazima una kasoro ambayo huwezi kuiona kwa macho ila mimi nimeishaifahamu mojawapo kama nilivyokuelezea mwanzo na pengine unazo nyingine nyingi tu ila haujifahamu.
Benny.

Anonymous said...

kama wewe ni john nina mashaka hatuzungumzii umbile hapa ni maoni hapa hatupo kwenye miss tz kama huna hoja kaa kimya awe chadema,cuf ubaya uko wapo anazungumzia hali halizi ya bongo nakusihi(john)kama unavyojiita urudi darasani uweze kujifunza kutenganisha mada dada Happy wembe ni ule ule katika jumuia yoyote wajinga lazima tuwe nao god bless you, brother Muga. London

Anonymous said...

Anon October 10, 2007 8:02 PM, Mtoa Maoni:- Anonymous
Mtu asiye na hoja ni rahisi kupayuka matusi. Hii ni dalili yako ya kutoelewa mambo. Nenda shule.

Powered by Blogger.