Header Ads

KAMATI YA MADINI NI 'MAZINGAOMBWE' YA KIKWETE!


Na Happiness Katabazi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, asitake kuwadanganya wananchi kwa kuwa ndiye aliyeahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini katika siku za hivi karibuni ameonekana kuwa na ‘ndimi mbili’.

Anajaribu sasa kukwepa ahadi zake. Siku chache zilizopita alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari wa nchi za nje kwamba hafahamu ni kwanini Tanzania inakuwa maskini.
Huyu ni rais wa nchi ambayo bajeti yake ni tegemezi kwa fedha za wafadhili kwa asilimia 46! Huyu ni rais wa nchi ambayo haina uwezo wa kuwapatia elimu bora watu wake.
Hata vijana 27 waliokwama kule nchini Ukraine, serikali yake ilishindwa kuwaokoa, wakalazimika kukatisha masomo na kurudi nchini kwa nauli za kubahatisha.
Huyu ni rais wa serikali ambayo inaendesha hospitali zisizo na dawa za kutosha, madaktari na manesi wanaishi kwa mishahara isiyokidhi mahitaji.
Huyu ni rais ambaye mvua ikinyesha siku moja nchi nzima anayoiongoza inaogelea kwenye mafuriko na mijini magari na watu wanatembea kwa tabu. Lakini rais huyu hajui ni kwanini Tanzania ni maskini.Tanzania ina madini.
Tanzania ina rasilimali za wanyama na misitu, vyote hivyo Bunge limevitungia sheria ambazo zinawaruhusu wawekezaji wa nje ‘kupora’ mali hizo kupeleka nje bila kulipa kodi na kusamehewa kodi.
Lakini rais wetu ambaye amekuwa waziri kwa muda mrefu, hajui ni kwanini ni nchi yetu ni maskini. Rais Kikwete amesikika akisema kwamba wawekezaji katika sekta ya madini wakitulipa kodi kwa asilimia 30 na mrahaba wa asilimia tatu, inatutosha.Ebu tumuulize rais wetu, inamtosha nani hiyo kodi na huo mrabaha?

Kama inamtosha yeye, sawa, lakini kama taifa, hicho sicho tunachokitaka, sisi kama wananchi wa taifa hili tunataka ubia wa asilimia 51 na asilimia 49 zibaki kwa wakezaji na bado walipe kodi serikalini.
Hilo ndilo dai kuu la Watanzania, ingawa bado halijawekwa kwenye sheria na sera za nchi.
Sasa kama rais wetu anataka kucheza, acheze anavyotaka, lakini sisi tunataka tumiliki migodi kwa asilimia 51, na wawekezaji walipe kodi na ieleweke wazi, hatuna mjadala katika hilo.
Nasema kwamba, bila wazalendo kushirikishwa kwenye migodi na wakajenga hisa zao kwenye thamani ya madini yenyewe, hatutaweza kujikomboa na kujitoa hapa tulipo.
Pili, tunataka haki ya kutawala shughuli za migodi na kujua kiasi gani kinachimbwa na kupatikana, kinatokana na umiliki wa hisa. Sasa sisi tukiendelea kujikita kwenye kusubiri kupewa kodi kama anavyodai sasa rais wetu, tukae tukijua tumeliwa.
Ninachokiona ni kwamba, Rais anataka kukwepa mjadala huu na badala yake wiki iliyopita ameunda kamati ya kupitia mikataba ya madini, sijui kama wananchi wengi wanafahamu kwamba kamati hiyo haina mamlaka ya kubadilisha vipengele vya sheria vilivyopo kuhusu madini. Sasa kamati teule ya rais inaenda kuchunguza kitu gani?
Hapa ndipo busara ya baadhi ya wananchi wanapomnunia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) kukubali kujiunga na kamati hiyo, inapojionyesha.
Kwa sababu wananchi wanajua sheria ya madini ipo na ni mbaya na haijabadilishwa. Wananchi wanajua sera ya CCM kuhusu madini ipo na ni mbaya na haijabadilishwa hadi sasa.
Kwa hiyo, mikataba yoyote itakayotiwa saini na iliyokwishatiwa saini inatokana na vitu wiwili, navyo ni sera za CCM kuhusu madini na sheria ya nchi inayohusu madini.
Kwa hiyo sasa kupitia kamati hiyo tutapata nini? Hatutapata kitu, tumeingizwa kwenye ‘mazingaombwe na longolongo’ na anayefikiria tutapata kitu na aseme.
Hata kama hao wajumbe wote wa kamati teule ya rais ni maadui wa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, bado hawataweza kuthibitisha kwamba waziri huyo na wenzake waliomtangulia waliingia mikataba kwa makosa kwa sababu atasema alifuata sheria za nchi ambazo wananchi tunasema ni mbaya kusaini mikataba hiyo. Lakini hoja hii haitusaidii kitu.
Hoja kuu ni kuhusu sheria ya madini ibadilishwe, Watanzania wawe wabia kwenye migodi kwa asilimia 51 na wawekezaji wabakie na asilimia 49 na walipe kodi, hivyo kama hatuwezi kupatiwa haya, rais na chama chake kinachounda serikali, itafika wakati tutawaita nao ni mafisadi.

Kwa mantiki hiyo, kama kamati yako hii ya kuchunguza mikataba ya madini haitaleta hilo, tutawashitaki kwa Mungu na yeye ndiye atajua cha kuwafanya, kwani tumekuwa tukilia kuhusu hili kila mara, lakini tunapuuzwa.
Kwakuwa tumepata taarifa kuwa kamati nne zilishaundwa kwa ajili ya kuchunguza sekta ya madini, tunataka serikali iweke wazi ripoti za kamati za kazi zilizotangulia ili tujue zilipendekeza nini na serikali yetu ilishindwa kutekeleza lipi katika hizo kamati ili kamati hii mpya isirudierudie kufanya yaliyokwishafanywa na kamati zilizotangulia.
Nasisitiza tena, rais cheza unavyotaka, lakini sisi wananchi tunataka kuona hiyo hoja kuu niliyokwisha itaja hapo juu inatekelezwa kwa vitendo.
Wewe ndiye rais wetu, tumekuamini kuwa unafaa kutuongoza, funga bao kwa kichwa, mkono, kifua na hata mguu, lakini hakikisha hoja hii kuu inatekelezwa na tena hatuna subira katika hili, tunataka kuona ukilitekeleza kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,uk.21.Novemba 25 mwaka 2007.

6 comments:

Anonymous said...

Katabazi....
Kama kawa, unaendelea kunena. Bahati mbaya sana Nchi hii Tanzania tuna viongozi wasio ona, kusikia ama kusikiliza hata kubadilika.... kinyume chake Rais na timu zake walikuwa wamepata jibu Makini hata kabla ya kuendelea kumnyonya mlala tabani, mlipa kodi kwa kumbebesha mizigo ya vijikamati hivi vya kila kuchwao visivyo na macho wala masikio!
One day Yes!

Anonymous said...

Naungana na wewe Dada yangu kwa asilimia 200 maana tatizo sio kupitia mikataba ya madini tatizo ni sera mbovuuu za CCCM na viongozi wake walisaini mikatba hiyo. then ni kuwa capital flow ni kubwa sana toka huko Tanzania na kwenda nje kwenye rasilimiali za madini na hivyo kuathili mfumo mzima wa sekta ya madini. then Tazama watu wa kwenye madini madhala yake kwa mazingira na kusema kama vile CCM hawajui vile. Sitaki kusikia Rais wa Kulipuka kama Jk!! Hivyo sisi tunaongozwa na Ilani ipi?? Je Mkukuta, Ilani ya CCM< Je Mkutabita hapo ndipo unapopata shida sana au Busara za Mwenyeketi. Then Watu kwa kwenye Migodi walipwe fidia na kuwa na hisa kwenye migodi hiyo kuona pato kubwa linbaki huko Tanzania. Kuunda tume sio kitu then ni kubalisha sheria then kwa sasa huwezi kubadili sheria maana wanaweza kukupeleka mahakamani ya London na kukudai fidia kubwa kama vile IPTL. Watu na wananchi wa Tanzania wanabidi kujua kuwa Sera za CCM na Viongozi wake ndio wabovu na Mafisadi wa Madini na rasilimali nyingine . Umefika wakati wa kuwaweka kando na kuwapumzisha viongozi wa CCM na serikali yake.
Josh Michael
Colorado USA

Anonymous said...

Tatizo ni Sheria na Sera Mbovu za CCM na viongozi wake kuhusu Madini, then CCM wamelewa na uwingi wa rasilimali za huko Tanzania. then Capital flow ni kubwa sana kutoka huko Tanzania na kuja hukju Ughaibuni kwenye sekta ya madini, then kam ndio hvyo tatizo ni kubadili sheria za madini na taratibu zetu zote na kuona watu na Nchi inapata faida kubwa sana katika madini, Sitaki Rais wa Kuripuka kama JK maana naona siku hizi ni mtindo wake wake huo kwa kupoza mambo na kuwarubuni watu. hakuna mifumo mzuri wa uchumi huko Tanzania. Yote ni Matunda ya CCM hayo ni sera zao. Kujisifia tu kuwa na madini na Amani ni Upuuzi na kuona tupo Katika Umaskini mkubwa kam nini. CCM wapewe likizo ndio jibu kubwa.
Josh Michael
Colorado Marekani

Anonymous said...

Happiness, nakupongeza kwa makala zako, ambazo huwa zina nifanya nisome gazeti la tanzania daima mtandaoni.

Nimesoma hii makala yako na nimeona mapungufu ya hali ya juu, yaani sikutarajia mwandishi makini kama wewe ungeweza kuandika makala yenye serious short comings kama hii.

Sasa wee unataka serikali iwe na hisa 51% na foreign investors 49% wakati wawekezaji wanawekezi mtaji 100% kweli hii inaleta maana? Yaani wewe uwekeze mtaji 100% and then you get 49% profit????? Isitoshe hawa jamaa wameleta management skills na technology, na ndio wanapata dhahabu lakini nayo kama wawekezaji lazima wawe na uhakika wakurudisha mitaji yao, ambayo imetoka kwa wanahisa wao.

Wasiwasi wao unatokana na historia ya serikali ya ccm ya kutaifisha mali za wawekezaji...na kuwa mujibu wa makala hii ambayo imejaribu kurepresent public opinion, muelekeo wake ni ule na utaifishaji!

Chamsingi ni jamaa walipe kodi that is it, ila mambo ya capital structure, happpiness tusiende huko maana serikali haina mitaji na techonologia ya kuwekeza kwenye madini.

Halafu nchi rasilimali nyingi tu zaidi ya madini ya kuweza kutuletea maendeleo na maendeleo yatakuja pale tu wananchi watakapo amua kutumia elimu, nguvu na ufahamu wao kuzalisha, na kutumia rasilimali kujinasua na umasikini. Rais anashindwa kuelewa kwanini wananchi bado hawajafikia uamuzi huo.

Anonymous said...

Dada Happy nyie ndiye mtakaeikomboa taifa letu kwa kalamu. Endelea kuelisha umma. MUNGU akubariki. AMEN.

Rashid Mkwinda said...

Yeeeah wasomaji wa Happy mwajua kwamba siku chache zijazo ndani ya mwezi huu anazaliwa?anatimiza miaka kadhaa? okay cku ikikaribia nitawajulisha mie kuna m2 kanihabarisha juu ya uzawa wake subirini siku c nyingi,tutamvisha nepi na kumuogesha

Powered by Blogger.