Header Ads

MADABIDA KIZIMBANI KWA ARVs FEKI
Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi amemfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano kwa makosa mbalimbali likiwemo kosa la kusambaza dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi 'ARVs' ambazo zimeisha muda wa matumizi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba, wakili wa Serikali Shadrack Kimaro alidai kuwa mbali na Madabida, washitakiwa wengine ni Seif Salum Shamte ,Simon Msoffe, Fatma Shango ,Sadiki Materu na Evance Mwemezi na kwamba hati ya mashitaka ina jumla ya mashitaka matano.

Wakili Kimaro alilitaja kosa la kwanza ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza, pili, tatu , nne ni la kusambaza dawa za ARVs zilizokwisha muda wa matumizi kinyume na kifungu cha 76(1) cha Sheria ya Taifa ya Vyakula, Madawa na Vipodozi ya mwaka 2003.

Alidai kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 5 mwaka 2011 Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa na wadhifa wa Afisa Mtendaji Mkuu, Mkurugenzi wa Oparesheni, Meneja wa Masoko na Mhasibu Msaidizi wa Tanzania Pharmacetical Industries Ltd, kwa makusudi ,walisambaza dawa hizo kwa Bohari Kuu ya Madawa(MSD), Tinis 7776 ya dawa hizo wakionyesha zina 30mg + nevirapine 200mg +Lamivudine 150mg ikiwa na No.OC 01.85 zinazoonyesha zimetengenezwa Machi 2011 na zinamalizika muda wake matumuzi Februali 2013 wakijaribu kuonyesha dawa hizo ni hali kumbe siyo kweli.

Kosa la pili alidai ni kusambaza dawa hizo kinyume na sheria hiyo ambapo Aprili 11 mwaka 2011,washitakiwa walisambaza tena kiasi hicho cha dawa za ARV feki kwa Bohari Kuu ya Madawa(MSD) ambazo zilikuwa zinaonyesha zimetengenezwa MAchi 2011 na zitamaliza muda wake wa matumuzi Februali 2013, wakionyesha kuwa dawa hizo ni halisi kumbe sikweli.

Wakili Kimaro alilitaja kosa la tatu kuwa ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa kati ya Aprili 12 na 29 mwaka 2011 Dar es Salaam, kwania ya kudanganya wote kwa pamoja walijipatia Dola za Kimarekani 98,506.08 sawa na Sh. 148,350,156.48 toka kwa MSD wakionyesha malipo hayo waliyolipwa yanatokana na wao kuipatia MCD kiasi kile cha dawa za ARVs.

Aidha alilitaja kosa la nne ni la kushindwa kuzuia kutendeka kwa makosa hayo kinyume na kifungu cha 382 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 linalomkabili (Materu na Mwemezi), kuwa Aprili 13 mwaka 2011 washitakiwa hao ambao ni waajiliwa wa MSD wenye wadhifa wa Meneja uhakiki wa ubora wa madawa wakijua wanatenda kosa walishindwa kutumia njia zinazowezekana kuzuia kosa hilo la MSD kukubali kununua ARVs feki zisinunuliwe.

Shitaka la tano ni la kuisababisha hasara kinyume na kifungu cha 57(1) na 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002, kuwa kati ya Aprili 5 na Aprili 30 mwaka 2011 washitakiwa wote kwa makusudi walishindwa kutimiza wajibu wao na kusababishia MSD hasara ya Sh.148,350,156.48 kwa kuiuzia ARV feki.

Washitakiwa walikana mashitaka yote na wakili Kimaro alidai upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Mwaseba alisema kila mshitakiwa apate dhamana ni lazima atoe fedha taslimu au kusalimisha hati isiyoamishika yenye thamani Sh. 13.5.

Ni Madabida na Sedekia peke yao ndio hadi jana saa nane mchana waliweza kutumiza masharti hayo ya dhamana na mahakama iliwapatia dhamana na washitakiwa wengine waliosalia walishindwa kutimiza masharti hayo na hivyo hakimu akaamuru wapelekwe gerezani na akaiarisha kesi hiyo hadi Februalia 24 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 11 mwaka 2014

No comments:

Powered by Blogger.