Header Ads

VIGOGO TBA WAHUKUMIWA KWA KURUHUSU UJENZI JENGO LINALOCHUNGULIA IKULU


 Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu adhabu ya kwenda jela miaka tisa kila mmoja au kulipa faini ya Sh.Milioni 15 kila mmoja aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu  wa wakala wa majengo nchini (TBA,)Makumba Togolai Kimweri    na Richard Maliyaga waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya matumuzi mabaya ya madaraka ya kuruhusu ujenzi wa ongezeko wa maghorofa sita zaidi katika Jengo refu linalochungulia Ikulu Dar es Salaam.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambaye kwa sasa ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kilosa, alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa hati ya mashitaka ya kesi ina jumla ya makosa matano na   iliyofunguliwa chini ya Kifungu cha 31cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na RushwaNo 11 ya mwaka 2007.
Hakimu Fimbo alilijata kosa la kwanza lilikuwa ni la kuruhusu ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa 12 bila kufanya upembuzi endelevu na kosa la pili ,tatu, nne la  ni la kutoa kibali cha kujengwa kwa jengo hilo wakati hawakuwa na mmlaka ya kutoa kibali hicho ni Mamlaka ya Mipango Miji ya  Manispaa ya Ilala ndiyo ilikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha kufanyiwa marekebisho ya matumizi ya jengo hilo na kosa la tano ni la matumuzi mabaya ya madaraka ambao washitakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kwakuruhusu mabadiliko sakafu katika ujenzi huo ambao mabadiliko hayo yaliruhusu kinyume cha sheria  kuongeza idadi ya ujenzi zaidi wa ghorofa saba kwenda juu wakati jengo hilo lilistahili kujengwa ghorofa sita tu na hivyo kufanya jengo hilo sasa kuwa na jumla ya ghorofa 12.Mshitakiwa wa kwanza anakabiliwa na kosa la kwanza,pili na la tano wakati mshitakiwa wapili anakabiliwa na kosa la tatu,nne na tano.
Hakimu Fimbo alisema kwanza anashangwa hadi sasa Manispaa ya Ilala ilishindwa kuchukua hatua kuhusu ujenzi wa jengo hilo lilojengwa kinyume na sheria  ambalo lipo katika ukanda wa (security Zone),wakati Sheria inaipa mamlaka Manispaa ya Ilala kuchukua hatua na kwamba kutokana ushahidi uliotolewa mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona ghorofa la saba hadi 12 yalijengwa kinyume na sheria.
 “Ajabu sana kwani Manispaa ya Wilaya ya Ilala  ilikuwa na mamlaka ya kuchukua hatua za kisheria kuhusu ujenzi wa jengo hilo ambalo umekiuka sheria za nchi lakini ilishindwa kufanya hivyo…sasa nafikiri kupitia hukumu hii naona ni muda muafaka sasa kwa Manispaa hiyo kutekeleza yale hukumu hii ya mahakama kuhusu ujenzi wa jengo hilo ambalo haujakithi matakwa ya sheria za nchi”alisema Hakimu Fimbo.
Alisema anaukataa utetezi wa washitakiwa uliokuwa ukidai kuwa hawakuwa wakijua kumruhusu mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Royal Orchard Inn kujenga maghora zaidi juu kwani kuna vielelezo vilivyotolewa na wakili wa Takukuru, Leonard Swai kuwa kuna barua ya Katibu Mkuu Kiongozi iliyokuwa ikienda kwa kwashitakiwa hao ikiwaambia waombe kwanza kibari kwa mamlaka ya Mipango Miji  cha mabadiliko ya matumizi ya adhi katika Kitalu Na. 45 na 46 Mtaa wa Chimala ,lakini kwa maslahi yao binafsi walipuuza agizo la barua hiyo na kuamua kujitwisha madaraka ambayo hawana wakaamua kuruhusu ongezeko la ujenzi wa ghorofa za saba zaidi juu.
‘Kwa hiyo mahakama hii inakataa utetezi wao kuwa walikuwa hawana taarifa iliyowataka waombe kibali cha mabadiliko ya matumuzi ya ardhi hiyo ambayo ni eneo la Ukanda wa Usalama,…kama washitakiwa hao wasingevunja kifungu cha 32 cha Sheria ya Makazi No. 8 ya mwaka 2007 ni wazi mwekezaji ambaye ni kampuni ya Royal Orchard Inn Ltd asingeweza kunufaika  katika mkataba wa jengo hilo ambalo ni baina ya serikali na kampuni hiyo:
“Ni sahihi kabisa kama washitakiwa hao wasingevunja sheria , hakuna njia mwekezaji hiyo angeweza kupata uniti 19 ni kama amepangisha na anachukua kodi kila mwezi na kwamba kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 kinaonyesha washitakiwa walinufaika binafsi na ujenzi huo wa ghorofa hilo kinyume na sheria  na kwa maana hiyo mahakama upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka”alisema hakimu Fimbo.
 Baada ya kuwatia hatiani na kabla ya kutoa adhabu  aliwataka mawakili wa pande zote mbili kusema chochote kama wanacho ambapo wakili wa Takukuru, Leonard Swai alieleza kuwa hana rekodi za washitakiwa kuwa kama huko nyuma waliwai kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai ila akaiomba mahakama itoe adhabu kwa wengine ambao wamekuwa wakijijengea majengo bila kufuata sheria na hasa ukizingatia jengo hilo linapaka na Ikulu lina urefu wa ghorofa 12 wakati kisheria lilitakiwa liwe na urefu wa ghorofa sita lakini washitakiwa hao kwa maslahi yao binafsi wakavunja sheria na kuruhusu ujenzi zaidi wa ghorofa hilo ambalo ni refu nalipo security zone na linaatarisha usalama wa makazi ya Rais wa nchini(IKULU).
Kwa upande wa wakili wa washitakiwa Henri Masaba, Pascal Kamala aliomba mahakama hiyo itoe adhabu nyepesi kwasababu washitakiwa hao watendaji wa mara ya kwanza ya  mara ya kwanza na kwamba ni wagonjwa.
Hakimu Fimbo akitoa adhabu alisema kila kosa moja ni jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh.milioni tano kwa kila kosa.Hivyo kila mshitakiwa atakwenda jumla ya miaka tisa kwasababu kila mshitakiwa na akabiliwa na jumla ya makosa matatu au atalipa jumla ya Sh.milioni 15 .
Hata hivyo washitakiwa wote wameweza kulipa faini ya Sh.milioni 15 kwa kila mmoja mahakamani hapo na wameachiwa huru.
Akizungumza na waandishi wa habari za mahakamani nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo kutolewa, wakili wa Takukuru, Swai alisema kwanza amefurahishwa na hukumu hiyo nzuri na ambayo ni salamu kwa wale wote wanaojenga majengo kiholelaholela na pia ni sifa kwa PCCB kwani kesi hiyo iliendeshwa na PCCB, na kwamba kifungu cha 40 (1) na (2) cha Sheria ya PCCB, inaipa mamlaka PCCB ndani ya miezi sita kuanzia hukumu ilipotolewa na mahakama kuhusu kesi yoyote iliyoshitakiwa kwa sheria ya PCCB, kutaifisha mali husika na katika mazingira ya kesi hii, PCCB ndani ya muda huo ambao umewekwa kisheria unayo mamlaka ya kutaifisha ghorofa ya 7-12 ya jengo hilo ambalo mahakama imesema ghorofa hizo zilijengwa kinyume na sheria.
Julai mwaka 2013 washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka hayo waliyotiwa hatiani nayo jana ambapo ni jumla ya makosa matano.

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com; Februali 11 mwaka 2014.

No comments:

Powered by Blogger.