Header Ads

IDARA YA USALAMA WA TAIFA NI SEHEMU YA UFISADI?

Na Happiness Katabazi

BAADHI ya Watanzania wakiwemo viongozi mbalimbali wastaafu na wale wa vyama vya upinzani,wamekuwa wakiliambia taifa kwamba limepungukiwa na viongozi waadilifu na wakaona kwamba umaskini unaolikabili taifa letu ni wa kujitakia.

Kwakuwa licha ya rasilimali kubwa tulizonazo hatuna viongozi wenye upeo wa kutuonyesha njia ya kuzitumia vyema ili tupate maendeleo.

Badala yake tunaona kuwa tunao viongozi wasiyo waadilifu,mafisadi,wazandiki na wababaishaji wa kutupwa.

Uongozi wa taifa una mfumo wa kitaasisi ambao wengi wanaita ‘system’.Kwa lugha ya kawaida system inamaanisha mfumo wa Idara ya Usalama wa Taifa katika kuchagua na kudhibiti ubora wa viongozi na mwenendo wao.
Moja ya wajibu mkubwa wa Idara ya hiyo ni kulipatia taifa viongozi bora,wazalendo na waliofundwa vya kutosha kutumia madaraka yao kutetea maslahi ya taifa.Lakini wimbi la ufisadi lililojitokeza nchini ni ishara kwamba idara yetu ya usalama wa taifa imeshindwa kazi.

Moja,idara hiyo imegeuka kuwa ni sehemu ya CCM kwahiyo badala ya kutekeleza wajibu wake tulioujata kulingana na Katiba na sheria za nchi, ikiangalia vyama vyote,taasisi zote za kijamii nk.

Baadhi yao wamejifanya ni watendaji wa CCM na wanapotenda hivyo kazi yao kubwa inakuwa ni kuhujumu viongozi walio kwenye vyama shindani kana kwamba hawa si watanzania na ila ni maadui wa nchi.

Pili,kuzuka kwa kundi la wanamtandao ambalo linadaiwa kumuweka madarakani rais Kikwete kunaashiria ushiriki mkubwa wa idara hiyo kupanga mtandao kuhusisha sekta zote za jamii na kuhusisha watendaji muhimu serikali ili wote kwa pamoja watekeleze azimima ya CCM kubaki madarakani.

Inasemakana kwamba nyuma ya ufisadi unafichuliwa yapo makampuni ya kifisadi ambayo hayumkini yalioanzishwa na idara ya usalama wa taifa kukusanya mabilioni ya fedha yaliyotumika na wanamtandao na CCM kwenye uchaguzi wa 2005.

Hakika yeyote anayependa kusema ukweli atakiri kwamba mabilioni ya fedha yaliyotumika kwenye mchakato ndani ya CCM na mabilioni ya fedha yaliyotumika na ccm katika uchaguzi uliopita hayana maelezo au chanzo kingine kama si makampuni hayo ya kifisadi ya kupora fedha za umma.

Sasa tujiulize taasisi hii ina uadilifu kiasi gani na Je aijashiriki katika ufisadi kwa namna yoyote ile?. Ikiwa watetezi wa usalama wa taifa watasema inatenda kazi zake kwa mujibu Katiba na sheria za nchi Je walilala wapi BOT ilipohujumiwa?

Je ilikuwa wapi maslahi ya nchi katika uzalishaji wa umeme yalipohujumiwa katika mradi wa IPTL na Richmond?

Je walikuwepo wapi maslahi ya nchi yalipohujumiwa katika ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara,TTCL, na makampuni mengine mbalimbali ya umma?

Tunachokiona sisi Idara ya Usalama wa taifa isiyojua wajibu wake na ambayo ufisadi ni sehemu kuu ya kazi yake. Pia tunachokiona sisi ni idara hii isiyojua kutetea maslahi ya ya nchi ambayo ipo tayari kuona rasilimali za nchi zikihujumuiwa ili mradi wanafanya hivyo ni marafiki zao.

Kazi kubwa ni kulindana, kupeana vyeo bila kuwa na sifa na pia kuwapiga vita wale wanaojitokeza kupingana na mwenendo wa kifisadi.

Tumefikishana mahala watu sasa wanamwagiwa tindikali,wanahushishwa kwenye ajali za kupangwa na bila shaka siku si nyingi tutashuhudia mauaji ya watu kwa mtindo wa kijambazi unaotumika na Mafia.

Inapotokea kwamba viongozi wa taifa ama serikali wanapata nyadhifa au kuajiliwa kazini kwa sifa za ubabaishaji au kughushi na hilo likafumbiwa macho,basi hakuna usalama wa taifa.

Kwa maana kwamba ikiwa uongozi utawekwa mikononi mwa matapeli walioghushi sifa za elimu basi hatima ya taifa itakuwa hatarini.

Je viongozi wa aina hii wataelewa nini kinachoendelea kuhusiana na mikataba ya biashara ya madini au mikataba ya umma? Kwa hiyo tusishangae serikali yetu inaendeshwa sawa kama viongozi hawajaenda shule kwani siyo kila anayejiita Daktari ni Daktari wa kweli.

Mfano ilikuwaje kampuni ya kihuni ya Richmond kupewa mkataba wa mabilioni ya fedha kununua majenereta ya umeme bila usalama wa taifa kujua?

Je kukosekana kwa umeme Je si jambo nyeti na hatari kwa usalama wa taifa?Au labda idara hii inaona Watanzania wamelala usingizi na wako tayari kufanyiwa vitendo viovu na wako tayari kulipishwa kodi na kubebeshwa gharama kubwa za maisha bila kulalamika au hata kufanya maandamano?

Labda Watanzania wamekuwa wapole mno katika kutetea haki zao.Bila shaka usalama wa taifa utaona ugumu wa maisha wanaopata wananchi pale tutakapokuwa tayari kuandamana na kuwatoa maofisini na kuwafukuza kwa bakora hao mafisadi?

Kwa ujumla , vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tulivyonavyo, chombo ambacho akijatufanyia haki ni Idara hii ya usalama wa taifa.Hawa wamelala usingizi wa pono nchi ina hujumiwa,wananchi tunapata taabu .JWTZ,Magereza,JKT na Polisi wanafanyakazi nzuri, tunawapongeza, licha ya kwamba wamekuwa wakilalamika bajeti za wizara zao ni finyu kuliko bajeti ya Idara ya usalama wa Taifa.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) chini ya Jenerali Davis Mwamunyange, wanafanyakazi nzuri na ndiyo maana hadi sasa nchi yetu haijavamiwa na maadui.

Polisi chini ya IGP-Said Mwema,nao wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la uhalifu.

Magereza chini Kamishna Mkuu, Agustino Nanyaro nao wamejitahidi, kwani hadi sasa hatujasikia wafungwa wamevunja magereza na kutoraka. JKT na wanajitaidi kuwalea vijana na kuzalisha mali.

Wakati umefika sasa watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa wawajibike kikamilifu bila kumuonea haya kiongozi yeyote, ama sivyo itabidi idara hii ivunjwe tuunde jipya na hilo linawezekana kama tuna uchungu wa kweli na Tanzania yetu.

Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania

katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Februari 13 mwaka 2008

3 comments:

Anonymous said...

Napenda kuchukua furusa hii kukupongeza wewe mwandishi wa makala hii nyeti kwa usalama wetu!

Ni ukweli usio kifani kwamba idara hii ni nyeti na inahitaji watu makini siyo hawa Wazandiki wanao fuata maelekezo na matakwa ya chama tawala hata wao kujiita CC!

Ina uma sana kwa chombo muhimu kama hiki kuwa bubu na kutumikia chama na kuweka pembeni katiba waliyo iapa kuifuata, kuilinda na kuitetea.

Pamoja na kuandika makala hii, nakuomba pia ujikite zaidi na makala kadhaa zinazo husu idara hii muhimu ili wahusika waweze kuamuka katika dibwi hili la usingizi fofofo.

Mungu akuzidishie heri, fanaka na Neema tele. Mungu wabariki waandishi wa Tanzania Daima. Amen

Anonymous said...

Poa sana.

Anonymous said...

Saaafi sana.

Powered by Blogger.