Header Ads

MSHIKEMSHIKE WA WANYAMBO KIJIJI CHA MAKUMBUSHO LEO

Na Happiness Katabazi

WENYEJI wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera ambao ni Wanyambo,leo wanatarajiwa kuanza tamasha la siku tatu la kuenzi utamaduni wao ikiwa ni katika kunadi mila na desturi zao.

Asili ya jina la kabila hilo limetokana na maana kuwa Mnyambo ni mtu mwenye asili ya eneo la Maziwa Makuu.Pia asili ya jina la kabila hilo limetokana na aina moja wapo ya ndizi inayofahamika kwa jina la Enyambo.

Aidha neno nyambo linamaanisha mtu au kitu au mmea asilia pia yupo ng’ombe wa asili wilayani Karagwe ambaye anajulikana kwa jina la Enyambo linalofahamika katika nchi za Uganda na Rwanda.

Maneno hayo yanatamkwa na Mwenyekiti wa Tamasha la Wanyambo, Revelians Tuluhungwa alipofanya mahojiano na Tanzania Daima mapema wiki hii, kuhusu uzinduzi wa tamasha la Wanyambo litakalo zinduliwa leo na kumalizika Jumapili wiki hii na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Mohamed Ghalib Bilal katika kijiji cha Makumbusho,Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Anasema jumla ya wanyambo 200 kutoka Karagwe wamekuja kuungana na wanyambo waishio hapa jijini kusherehekea tamasha hilo la kuenzi utamaduni wao.

Anasema Wanyambo wamejiandaa kuonyesha na kueleza mila na desturi za kabila hilo hasa nyumba ya asili, makazi ya Mnyambo iliyojengwa kijijini hapo hivi karibuni ambayo imegharimu zaidi ya Sh. milioni nne, vyakula na vinywaji vyao vya asili, mavazi, nyimbo ,ngoma,kazi za mikono, misemo, majigambo na malezi ya watoto.

Katika makala hii Tuluhungwa anaelezea mazingira ya himaya ya Karagwe na wanyambo kutukuka na kufahamika duniani miaka katika kipindi cha miaka 150 iliyopita na kutofahamika katika Tanzania ya leo sambamba na kupanda na kushuka kwa umaarufu wa kabila hilo.

Tuluhungwa anaeleza historia ya Karagwe kwa kusema himaya ya mfalme wa Karagwe ilikuwa ndiyo utawala mkubwa katika maeneo ya maziwa makuu kwa miaka kama 500 na Bweranyange Mji Mkuu wa Mfalme wa Karagwe ndipo alikaa mfalme Ruhinda wa kwanza, mwanzilishi wa himaya za Kihinda.

Anasema Ruhinda alitawala eneo lote la Karagwe, Ankole, Kihanja, Ihangiro Biharamulo Bushubi na Bugufi Kaskazini ,Akipakana na Bunyoro na mto Mwiruzi Kusini ya Biharamulo na Mkoa wa Kigoma.

Tulungwa ambaye ni mtumishi wa miaka mingi wa Shirila Umoja wa Mataifa la UNICEF, anasema maeneo yote aliyoyataja hapo juu yalitawaliwa na watoto wa Mukama wa Karagwe ambao muda ulipopita walijitenga na kuanzisha tawala huru.Himaya ya mfalme wa Karagwe hiyo ilitukuka na kuandikwa kwenye magazeti ya ulimwengu wakati wa wavumbuzi hususani Uingereza zaidi ya miaka 160.

“Karagwe ilikuwa ndiyo njia pekee ya kufikia utawala wa Buganda kwa wageni wote toka Pwani na Zanzibar .Kati ya Novemba 1861 na Februari 1862 John Hannington Speke na James Grant walikaa miezi mitatu Kafuro jirani na Bweranyange na wakaandika kwa kirefu juu ya mila na desturi za Karagwe chini ya mfalme Rumanyika Orugundu Rzinga Mchuchu wa Nkwanzi ambalo ni jina la utani lenye maana ya shujaa mfuga nywele ndefu mwana wa Nkwanzi. Na kwamba kwa hivi sasa kuna hifadhi ya wanyama ya rumanyika Orugundu kuenzi mtawala huyo ambayo kwa mashariki yake katika kijiji cha Ibamba kunapatikana mto wenye maji moto ya Mutagata”anasema Tuluhungwa.

Kupungua umaarufu wa Karagwe
Tuluhuhungwa anasema kufikia miaka ya 1880 na 1890 wakati wababe duniani wakishindwa kugawana Afrika huko Berlin 1884 na baadaye wakati Zanzibar na Buganda zilikuwa tawala zinazolindwa na mfamle wa Uingereza , Karagwe iliangukiwa na nuksi ambazo zilifika tawala nyingine zote kubwa katika historia kama za Alexander mkubwa utawala wa Kirumi.Ilipungua umaarufu mpaka wakoloni wa kijerumani hawakuitamani na Wamisionari pia waliipita kando na kuongeza kuwa visa vya kuipunguza Karagwe umaarufu vimeandikwa kwa kirefu na marehemu Profesa Katoke katika kitabu chake cha ‘The Making of The karagwe Kingdom’

Anasema awali ilikuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilikuwa vimeanza wakati Speke na Grant wakiwa Karagwe Novemba 1861 mpaka Desemba 1862 Matokeo yake ilikuwa kupungua kwa amani na kuihama Karagwe upande ulioshindwa na kupunguza wingi wa watu.

Pili ugunduzi wa njia fupi toka Mombasa kwenda Uganda kulitoa Karagwe kwenye njia Kuu ya biashara ya kimataifa na kupunguza umaarufu wake.

Magonjwa ya mifugo kama ng’ombe sotoka ilishambulia mifugo ya wakazi wa karagwe katika kipindi hiki na kupunguza utajiri wa Karagwe.Wakoloni walikuwa hawavutiwi na nchi maskini.

Sababu za kisiasa na utawala; Karagwe ilipita kipindi ambacho wafalme walikufa wakiwa wadogo bila kuacha warithi walioishafikia umri wa kutawala ,ikalazimu kutawala kwa kutumia viongozi wa muda kama vile Kakoko waliotawala kwa ukatili na kuharibu himaya.

Matokeo ya kupungua umaarufu
Ni kutopewa kipaumbele katika mipango ya wakoloni wa Kijerumani kulifanya Wamisionari kutovutiwa kuweka vituo vyao Karagwe.

Kwahiyo wamisionari wa Kikatoliki wao walianzisha vituo vyao Kashozi 1892, Bunena 1905, Kagondo na Rubya 1904,Katoke Biharamulo na kuanzisha shule sehemu zote hizo.Misheni ya kwanza Karagwe ilianzishwa 1934 baada ya miaka 40 baada ya kumpata Padri wa kwanza mwafrika wa kwanza Oscar aliyepadrishwa Bukoba 1917.Wa kwanza Karagwe Padri Rwakiboine alipandrishwa 1943 miaka 26 baadaye na shule na hospitali zilifata misheni.

Kupoteza umaarufu
Kama watu wote waliotawaliwa na wageni na kunyanyaswa, kutawaliwa na wageni wa Kihanja chini ya Wajerumani kuliwaathiri kujiheshimu, nakujitambua kama wanyambo.
Kujifunza elimu na dini kwa njia ya kuhemea katika lugha zaidi ya Kinyambo kiliathiri sana Kinyambo,Waumini na wanafunzi walizoea kusikia makatekista na walimu wakifundisha kinyambo kibovu kilichoathiriwa na lafudhi na misemo ya kabila la wahaya.

Bila kutaka wasomi walijikuta wakiathiri matumizi ya lugha yao ya kinyambo kwa jeuri kutokana na wingi wa mashule ya dini, serikali.Jumla ya yote ni kwamba kuanguka umaarufu wa Karagwe ghafla wakati wa kuja kwa ukoloni, kulitekeleza mazingira ya kuathiri kinyambo mpaka wanyambo wenyewe wakawa kama wamemezwa na Wahaya ,kabila ambalo hakukuwepo kabla ya ukoloni.
Leo hii tunapoaadhimisha tamasha la wanyambo, tunasimama kwa ujasiri wao kufanya tamasha hili la siku tatu kuanzia leo na kurudisha mchango wa wanyambo wanaojiamini katika kujenga taifa la Tanzania.

Wanyambo kabila lisilojulikana
Tuluhungwa anasema athari za kutotambulika wanyambo ni nyingi na zinazeondelea kuathiri watanzania wa kinyambo wengi.Taarifa zinajitokeza kila siku wanyambo kubughudhiwa Idara ya Uhamiaji kwa sababu baadhi ya Maofisa wake hawajui kwamba kabila hilo lipo.Ni maombi ya wanyambo kupitia tamasha hili kwamba kubughudhiwa wanyambo kwa kutowajua au kudhihaki wao kama kwamba kabila la wanyambo suyo raia halali nchini ni unyanyasaji usiokubalika na ukomeshwe mara moja.

Kabila la wanyambo ni miongoni mwa makabila makubwa Mkoani Kagera mengine ni Wanyambo wenyewe, wasubi, washubi,wahangaza,wazinga na wahaya.

Wanyambo wengi hawajitambui
Anasema inatia hofu kwamba hata wanyambo wenyewe hasa waishio nje ya Karagwe hawana ufahamu kama wao ni wanyambo au ni wahaya kwa sababu baadhi yao hujitambulisha kama ni wahaya na wanajaribu hata kuigiza lugha yao.

Historia ya Wanyambo haijatafitiwa kwa kina na hivyo hakuna machapisho ya kutosha yanayoelezea historia ya Wanyambo.Yapo machapisho machache sana hasa ya Profesa Katoke na hadithi za wapelelezi kana Hans Mayer ambayo hayako sokoni tena na yaliyopo hayatoshelezi mahitaji.

Anasema mila na desturi za Wanyambo zilizo nje ziko hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, nyimbo ,misemo ,majigambo,hadithi na taratibu za maisha nyingi zimetoweka na zilizobaki ziko hatarini kupotea kabisa.

Mfano mzuri ni ngoma ya Amakondere ambayo imebaki ikichezwa na kundi moja tu la wazee waishio Rwanyango ambazo hazijarekodiwa ambapo itakuwa vigumu kuruthishwa kizazi kimoja hadi kingine.

Aidha uwepo wa ngoma ile unategemea sana uhai wa wazee hao hata ala za muziki wa ngoma hizo (Amakondere) hazilimwi tena na huenda mmea huu umeshatoweka kabisa.Kwa upande wa lugha ya wanyambo (Orunyambo) imeanza kupoteza uhalisia wake kutokana na mwingiliano na kutozungumzwa mara kwa mara hivyo huenda ikapotea kabisa.

“Kwa ujumla wanyambwa wanapata usumbufu katika kujitambulisha hasa wanapohitaji baadhi ya huduma katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu hudhaniwa jamii ya wanyambo ni wakimbizi kutoka nchi jirani za Burundi na Rwanda”.

Historia ya Wanyambo
Wanyambo ni kabila lilokuwa miongoni mwa makabila makubwa na yenye nguvu za kivita na kiuchumi.Watu wa kabila hili la wanyambo walikuwa na ufalme ulioongozwa na wafalme Abakama 14 kwa nyakati tofauti.Watu wake ni wakulima na wafugaji.

Historia ya kabila hili ilifahamika ukanda wote wa Ziwa Magharibi Victoria pamoja na nchi za Rwanda na Burundi.Kutokana na uhunzi wa mapambo mengi ya kifalme yalitengenezwa na kuhifadhiwa kwenye ngome ya mfalme.Mapambo hayo yalipendwa na mengine yalichukuliwa na Wajerumani ,walipewa zawadi na Omukama Rumanyika. Kwa ujumla ni kabila lililoheshimika hivyo wanyambo walijivunia Unyambo wao hali iliyoibua misemo kama, Ndyu Munyambo akala nakalenje, Omunyambo agamba echabweine.

Aidha anasema siku ya utamaduni wa Mtanzania ni utaratibu uliobuniwa na Bodi ya Makumbusho ya Taifa chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni mwaka 1994 kabla Makumbusho ya taifa haijahamishwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama ilivyo sasa ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali hapa nchini kuonyesha tamaduni zao katika Kijiji cha Makumbusho ,Kijitonyama,Dar es Salaam.

Malengo ya kuwa na siku ya Utamaduni wa Mtanzania
Ni kutoa nafasi kwa jamii moja baada ya nyingine kati ya jamii nyingine tulizonazo kuonyesha mila, desturi na mienendo yao mbalimbali ya jadi ili jamii nyingine ziweze kuelewa na kuthamini utamaduni wa watanzania wenzao.

Kujifunza na kufahamu aina mbali mbali za mila na desturi zinazofaa kudumishwa, kuboreshwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama utamaduni wa Taifa.

Kufanya Kijiji cha Makumbusho kuwa kielelezo halisi cha maisha ya Watanzania.

Malengo ya kufanya Tamasha la Wanyambo
Kuonyesha mila, desturi na mienendo yao mbalimbali ili Wanyambo wenyewe na jamii nyingine ziweze kuelewa ,kuheshimu na kuthamini Utamaduni wa wanyambo hivyo kukuza uelewano wa kitaifa.
Wanyambo na jamii nyingine zitaweza kujifunza aina mbalimbali za mila na desturi za Wanyambo zinazofaa kudumishwa, kuboreshwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hali hii itaondoa utata na kupunguza usumbufu pale wanapokuwa wanahitaji huduma muhimu kama vyeti vya kuzaliwa , hati za kusafiria,viza, vitambulisho vya kupiga kura pamoja na nyaraka nyingine muhimu kwani wamekuwa wakipata shida kwa sababu ya kutojulikana kwa kabila lao.

Kuweka mikakati ya kufanya utafiti ili kubaini mila, desturi na tamaduni za Wanyambo zilizo njema na kuzihifadhi kwa njia ya maandishi ili ziweze kurithishwa kizazi hadi kizazi na zitumike kwa manufaa ya jamii nzima.Kila la Kheri Wanyambo.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 21 mwaka 2011

1 comment:

Bakorea said...

Katabazi, nimeipenda atikali hii,
ila naamani wanyambo na wahaya wako kitu kimoja..na nimefika hapa kwasababu nimewahi kuambiwa na wazee wangu kuwa Omukama Kibi wa Kiziba alikuwa mdogo wa Rumanyika. sasa angalia tovuti hii..http://kiziba.com/
jamaa anasema wanyambo ni ufalme mmoja wapo wa wahaya, kama ilivyo kihanja, Iangiyo, kyamutwala nk..
Msalimie Ngurumo

Powered by Blogger.