Header Ads

JWTZ MSIPIGE RAIA

Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi katika nchi yoyote ile ni chombo maarufu na muhimu. Hakuna njia nyingine ya kumwelezea shujaa wa nchi isipokuwa kupitia taswira ya mwanajeshi.

Na ndiyo maana Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni chombo cha kujivunia kwa kuwa huliletea taifa sifa ya ukakamavu, nidhamu na uwezo mkubwa wa ulinzi wa mipaka ya nchi.
Panapotokea maafa, mara zote tegemeo kubwa la raia ni jeshi lao la ulinzi, kwa kuwa wanajeshi wa jeshi hilo ndio wenye sifa, maarifa, mbinu na vifaa vya kuokoa. Na kwa kawaida wanajeshi ni vipenzi wakubwa wa wananchi wao.

Kitendo kilichofanywa na askari wa JWTZ wiki iliyopita cha kuvamia ofisi za DAWASCO, kuwapiga na kuwanyanyasa watendaji wa shirika hilo na kupora kamera ya mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, ni kitendo cha aibu kwa jeshi hilo na hakiwezi kupita bila kujadiliwa.

Kwanza, raia si saizi ya wanajeshi katika makabiliano ya kivita na matumizi ya mitulinga (mabavu).

Kitendo kile ni sawa na kaka mkubwa kuvamia wadogo zake chekechea katika patashika ya kugombea chakula mezani, kwa vyovyote vile vitoto hivyo vya chekechea vitashindwa.

Lakini kitendo kile kinaonyesha jeshi letu bado lina wanajeshi wasio na nidhamu, kwa sababu hata kama wangekuwa wameudhiwa kwa kitendo cha kukatiwa maji, ufumbuzi wake usingekuwa kuvamia na kuwapiga watendaji wa Dawasco, bali kutuma mmoja wao kwenda na hundi ya malipo kwenye shirika hilo na kurejesha huduma ya maji.

Kuwapiga watendaji wa DAWASCO, hakuondoi ukweli kwamba JWTZ ni mdaiwa sugu. Kumbe ilikuwa ni upungufu wa busara uliopita kiasi kwa vijana wetu waliovaa sare za kivita wakiwa kwenye gari la kivita kufanya uvunjaji wa amani, kujeruhi na kunajisi sheria za nchi.

Labda JWTZ huheshimu tu Wazungu wanapoajiriwa kudai madeni kama ilivyokuwa kwa Net Group Solutions ya Afrika Kusini.

Kampuni hii ilidai madeni ya umeme yaliyokuwa yameshikiliwa na idara zote za serikali ikiwa ni pamoja na JWTZ na hatukuona akipigwa mtu! Kumbe mnyonge ni mmatumbi, Mzungu huogopwa kama simba!

Sasa hawa ndio mashujaa kweli wa nchi yetu? Labda suala zima la wanajeshi kutoka kambini na kuvamia raia kwa visingizio mbalimbali, kama vile kunyang’anyana ‘mabibi’ na raia vimekuwa vikilaaniwa mara kwa mara na taasisi za kutetea haki za binadamu nchini.

Kwa vyovyote vile tabia hii ina maanisha kuwa hatuheshimiani. Raia akienda kwenye kambi ya jeshi anatakiwa atii na kuheshimu sehemu ile kwa jinsi wanavyotaka wanajeshi. Lakini mwanajeshi akiingia uraiani na hata ofisini hataki kutii na kuheshimu ofisi za wengine. Hakika, kwa hali hii hatufiki!

Septemba 15,2007 , alipokula kiapo cha utii mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alishutumu na kulaani vikali tabia hiyo na kuahidi kwamba uongozi wake utaikomesha.

Kwa kuwa sasa hili limetokea, wananchi wana hamu sana kumsikia ana lipi la kuwaeleza kuhusu utovu wa nidhamu uliofanywa na wanajeshi wake wiki iliyopita katika ofisi za shirika linalomilikiwa na serikali la - Dawasco.

Ili wananchi waendelee kumheshimu, kumuamini na kutolinganisha kauli yake hiyo na porojo za kisiasa, tunamtaka Jenerali Mwamunyange atetee sasa heshima ya JWTZ.

Tunataka atuthibitishie kwamba wanajeshi wetu si genge la wahuni wanaochukua sheria mikononi mwao. Ikiwa atashindwa kufanya hivyo, raia watashindwa kumwamini na kuiheshimu JWTZ.

Na kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote wa JWTZ aliyekanusha kwamba waliofanya kitendo kile cha ovyo si wanajeshi, inatazamiwa jeshi litoe maelezo ya kuridhisha sambamba na kuwaomba radhi wananchi na litegemee pia kwamba uvamizi ule unaweza ukazua kesi kubwa ya madai ya fidia yanayoweza kuliletea taifa hasara kubwa.

Izingatiwe kwamba ule wakati ambapo raia walikuwa hawajui haki zao na ni waoga kutetea haki zao umekwisha. Serikali itajikuta ikidaiwa mabilioni ya fedha kwa kutozingatia kanuni za utawala bora.

Tuanelewa kwamba walioathirika katika kitendo kile ni pamoja na waandishi wa habari ambao mmoja alinyang’anywa kamera ili asiweze kutimiza wajibu wake. Hii ni mara ya pili kwa majeshi yetu kuwahujumu waandishi wa habari wakiwa kazini.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2005, askari wa Jeshi la Magereza waliwapiga waandishi wa habari na kuwajeruhi, eneo la Ukonga.

Wakati umefika sasa kuuliza kama majeshi yetu ni adui au rafiki wa haki za raia? Je, tuwatofautishe vipi waliotenda ushenzi ule na wale wahuni waliotumiwa kuwahujumu waandishi mahiri wa habari, Ndimara Tegambwage na Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi?

Kwa ujumla tunajua kama ilivyo ada ya taasisi za serikali zinapokutwa zimevunja haki za wananchi, kutakuwa na kulindana ili kuhakikisha kwamba waliofanya vitendo hivyo hawapatikani, hawakamatwi na hawachukuliwi hatua za kisheria.

Ikiwa hilo litaendelea, basi Tanzania itakuwa imejijengea utamaduni ambao majeshi yake ni ‘miungu watu’ wanaoweza kufanya udhalimu wa aina yoyote dhidi ya haki na uhai wa raia bila kukanywa wala kudhibitiwa.

Tutakuwa tunajijengea jehenamu ya aina yake na Tanzania haitakuwa tofauti na kambi za Al Ghareb, Iraq au Guantanamo Bay, Cuba.

Tukubali makosa, tukubali kusahihishwa na kama taifa tumrejee Mungu kama wimbo wetu wa
taifa unavyotuasa.

JWTZ itimize wajibu wake wa kulinda nchi na si kupiga raia. DAWASCO fanyeni kazi bila upendeleo na epukeni ufisadi. Hata hivyo kipigo mlichokipata kisiwakatishe tamaa, poleni na jengeni taifa lenu bila woga.

0755 312859katabazihappy@yahoo.com www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano la Februari 27,2008

No comments:

Powered by Blogger.