Header Ads

MAWAKILI:KESI YA ZOMBE MAJUNGU MATUPU

*Wadai wametolewa kafara na wakubwa wao
*Waeleza ushahidi haujajitosheleza, ni wa kuunga
*Wadai hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji hayo
Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa utetezi katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdalah Zombe na wenzake 12, wamedai kesi hiyo ni ya majungu na kwamba washtakiwa wametolewa kafara na wakubwa wao wa kazi.

Mawakili hao walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti katika Mahakama Kuu ya Tanzania wakati waliwasilisha hoja zao mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Masati, wakiiomba mahakama hiyo iwaachie huru washtakiwa hao.

Walidai washitakiwa hao wanapaswa kuachiwa huru kwa kuwa ushahidi wa mashahidi 37 wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo umeshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa washitakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Mawakili hao walidai ushahidi wa upande wa mashitaka ni wa kuambiwa, wa mazingira na baadhi ya mashahidi wanapingana katika ushahidi wao, kwani hakuna shahidi aliyeshuhudia tukio hilo la mauaji na kwamba ushahidi wao ni wa kuungaunga.

Aliyeanza kuwasilisha hoja hizo ni Wakili Majura Magafu, ambaye anawatetea washitakiwa wa tatu, nne, tano, sita, saba na 10, alidai ili mshtakiwa atiwe hatiani ni lazima mahakama iridhike na ushahidi wa upande wa mashtaka, ambao una jukumu la kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka yoyote na kueleza kuwa upande wa serikali umeshindwa kutimiza wajibu huo.

Magafu alidai ushahidi uliotolewa na mashahidi hao ni wa mazingira na wa kuungaunga na kwamba robo tatu ya ushahidi uliotolewa ni wa kuambiwa na kwamba hakuna shahidi yeyote aliyeshuhudia tukio hilo.

Alidai shahidi wa pili, sita na saba hawakuwa mashahidi wazuri, kwani waliieleza mahakama kuwa marehemu wote walikamatwa eneo la Sinza-Palestina, na pia mashahidi hao walishindwa kutaja idadi, majina na kuwatambua askari wanaodaiwa kuwaua marehemu hao.

“Suala la utambuzi ni muhimu na mashahidi walishindwa kuwatambua washtakiwa, mimi naamini mahakama bado ipo gizani kuhusu nani aliwaua marehemu.

“Kesi hii ilipelelezwa na maofisa wa polisi, lakini maofisa hao hawakuweza kuandaa gwaride la utambuzi…hii ni aibu kwa jeshi letu. Kwa ujumla katika ushahidi uliopo kwenye rekodi za mahakama hadi leo (jana) haijulikani ni idadi gani ya askari walihusika katika sakata hilo la mauji,” alidai Magafu.
Alidai kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na shahidi wa (36) ambaye alikuwa ni mkuu wa timu ya upelelezi wa kesi hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Sidyen Mkumbi, alieleza kushangazwa ni kwanini askari 13 ndio wameshitakiwa na kuongeza kuwa anachofahamu kulikuwa na askari zaidi ya 15 ambao nao walipaswa kufikishwa mahakamani katika kesi hiyo.
“Hao askari wengine wako wapi? Kwa sababu hiyo kwa nini tusiamini hao askari wengine walioachwa ni vigogo na hawa waliopo mahakamani wametolewa kafara na wakubwa wao wa kazi? Au kwa nini tusiamini kesi hii ni ya uzushi, yenye lengo la kuharibiana maisha na kunyang’anyana vyeo?” alihoji Magafu.
Alidai upande wa mashtaka baada ya kukosa ushahidi wa kuunganisha washtakiwa hao, uliamua kuwachukua mshitakiwa Rashid Lema na Koplo Rajabu ambao walieleza mauaji hayo yalifanyika kwenye msitu wa Pande na waliongozwa na mshtakiwa wa pili, Christopher Bageni.
“Katika Question Statement hakuna liloulizwa ni kwanini washtakiwa walikimbia. Je, haya yote hayawezi kuleta maswali kama ushahidi huo ni wa kupikwa?” alihoji.
Aidha, alihoji ni kwa nini shahidi Shabani Manyanya na Ramadhan Mbuta wasikamatwe kwa kuwa walidai walihusika na ujambazi wa duka la BIDCO lililopo Kariakoo.
“Nauliza kama mashahidi hao walifika mahakamani na kukiri hilo mbona hawajakamatwa? Je, hii si njama ya kusaidia upande wa serikali katika kesi hii?” alihoji Wakili Magafu.
“Ieleweke si jukumu la mshtakiwa kuithibitishia mahakama, ni upande wa serikali ndio wenye jukumu la kuthibitisha hilo na umeshindwa, ndiyo maana hadi leo kuna mashaka makubwa katika kesi hii.
“Ilidaiwa mauaji hayo yalifanywa na DC/Koplo Saadi, je, huyu Saadi mbona hayupo mahakamani? Na je, alikuwepo Sinza? Mbona upande wa mashtaka upo kimya katika hili? Sasa mnataka washtakiwa waeleze nini mahakamani?” alihoji wakili huyo.
Magafu alidai mahakama haiwezi kuhukumu watu kwa hisia, bali kwa ushahidi mzito na kueleza ushahidi wa timu ya upelelezi wa maofisa utabaki kuwa ni ushahidi wa kusikia.
Kutokana na hali hiyo, aliiomba mahakama itamke ushahidi wa upande wa mashtaka umejaa utata, wa kusikia na ushahidi wa kupika na washtakiwa wameletwa mahakamani kwa nia mbaya.
Kwa upande wa wakili Jarome Msemwa ambaye anamtetea Zombe, alidai hakuna shahidi hata mmoja aliyethibitisha kuwa Zombe aliua au alihusika katika mauaji hayo na kwamba kupitia kigezo hicho anaona hakuna kitu kinachofanya mshtakiwa huyo awe na kesi ya kujibu.
Msemwa ambaye alikuwa akitoa hoja huku Zombe akimpatia vikaratasi vya kusisitiza hoja zake, alidai mauaji ya watu hao yalitokea Januari 14 mwaka 2006 baada ya kutokea, tume ya Polisi iliyokuwa ikiongozwa na ACP-Mgawe iliundwa na ilimuona Zombe hana hatia.
Pia alidai tume ya Jaji Mussa Kipenka ambayo nayo ilichunguza mauaji hayo na kutoa mapendekezo kuwa washtakiwa wengine washtakiwe kwa mauaji isipokuwa Zombe aachiwe, kwani hana kesi ya kujibu mahakamani.
“Ndiyo maana naomba Zombe aachiriwe huru kwani hana kesi ya kujibu, licha ya kwamba si lazima mahakama hii ifuate uamuzi wa tume hizo,” alieleza Wakili Msemwa.
Hata hivyo, alidai baadhi ya mashahidi wakati wakitoa ushahidi wao walieleza kuwashangazwa na Zombe kushitakiwa kwa kesi ya mauaji akiwemo shahidi Mkumbi, ambaye alidai mshtakiwa huyo hajawahi kuhojiwa wala kuchukuliwa maelezo.
Msemwa alidai kwa mujibu wa shahidi wa 13, PC John toka kitengo cha mawasiliano (999), alidai siku hiyo hakusikia chochote kwamba Zombe alitoa amri watu hao wauawe na kueleza kuwa Mkumbi katika ushahidi wake alikiri hajui namba ya Zombe wala Bageni kama ilivyoelezwa awali kwamba washtakiwa hao siku hiyo walikuwa wakiwasiliana kuhusu kuwaua marehemu hao.
“Hadi hapo hakuna link yoyote inayoonyesha Zombe alikuwepo eneo la Pande au alipokuwa ofisini alitoa amri au rekodi za simu yake watu hao wauawe. Si siri upande wa serikali unategemea kuthibitisha kesi toka kwa mshitakiwa 11 na 12 (Rashidi Lema na Koplo Rajab) ambao wanashitakiwa na Zombe.
“Upande wa utetezi unategemea ushahidi wa washtakiwa hao badala ya sheria, na sheria hairuhusu na isitoshe washtakiwa hao hawakiri kosa linalowakabili na Lema alidai alisikia ‘afande’ akitoa amri kwamba marehemu wauawe, hivyo huo ni ushahidi wa kusikia na sheria inakataa kupokea ushahidi wa kusikia,” alidai.
Alidai maelezo ya Lema aliyoyatoa polisi hayakusema Zombe anahusika na mauaji na hata alipojisalimisha na kutoa maelezo yake kwa mlinzi wa amani, alidai Zombe anahusika katika mauaji na kudai kwa sababu hiyo, maelezo ya mshtakiwa huyo yana utata.
“Mheshimiwa jaji, kwahiyo Zombe ambaye yupo mahakamani hapa si mshtakiwa ni shahidi kwa sababu sheria na Katiba ya nchi inasema wazi mtu akikamatwa na polisi ni lazima ahojiwe na kuandika maelezo yake kabla ya kufikishwa mahakamani…sasa haki hizo zote Zombe hakupewa,” alidai Msemwa.
Alidai kubwa zaidi, Zombe hajawafahamu marehemu kabla na baada ya kufariki na kwamba hata miili yao hajawahi kuiona.
Aidha, Wakili Ishengoma ambaye anamtetea mshitakiwa Christopher Bageni, aliomba mahakama imuachie huru mteja wake kwa kuwa ushahidi uliotolewa haukumgusa.
Alidai chanzo cha mauaji ni fedha wakati mashahidi wengine walidai waliouawa walikuwa ni wahalifu na kueleza kwamba kutokana na utata huo mshitakiwa huyo anapswa aachiwe huru.
Alidai ushahidi unaomgusa Bageni ni wa shahidi 24, 27, 28 (Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Eliezer Feleshi), 30,31,32 na 36. Alidai ushahidi wa Feleshi unadai alipata taarifa kutoka kwa wakazi wa Sinza kwamba Bageni aliamuru marehemu wapigwe risasi.
“Naomba ushahidi wa DPP usitiliwe maanani na mahakama hii, kwani tunashindwa kuelewa ushahidi alioutoa ni wa ile tume ya rais au alitoa ushahidi wake unaotokana na wadhifa wake wa DPP.
“Ni DPP huyu huyu aliyeteua waendesha mashtaka katika kesi hii hadi kumteua Mwendesha Mashtaka, Mugaya Mtaki kuongoza waendesha mashtaka, hivyo ule ushahidi wote alioutoa kisheria, huwezi kuwa DPP kisha wakati huo huo uwe shahidi, hivyo ushahidi wake hauisaidii chochote mahakama hii,” alidai Ishengoma.
Hata hivyo, Wakili Longino Myovela ambaye anamtetea mshitakiwa wa nane na 13, alidai shahidi wa pili, sita na saba upande wa serikali ulikusudia kuonyesha marehemu walikamatwa kwa amani Sinza.
Aidha, kwa upande wa Wakili Denis Msafiri, ambaye anamtetea mshitakiwa wa 11 (Lema) ambaye jana hakuweza kufika mahakamani kutokana na afya yake kutokuwa nzuri na mshitakwia wa 12, alidai katika jitihada za upande mashtaka waliochukua maelezo ya washtakiwa waliyoyatoa kituo cha polisi na walinzi wa amani, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha washtakiwa hao walikiri kuua marehemu.
Msafiri alidai katika sheria za nchi hakuna kifungu cha sheria kinachosema mtu akiona uhalifu unatendeka akae kimya, achukuliwe hatua kama ametenda kosa.
“Kwa hiyo kitendo cha washtakiwa hawa kushuhudia mauaji ya watu hao wanne yakitendeka si kosa na kwa kuwa ilielezwa mahakamani hapo Koplo Saadi ndiye aliyeua na hadi leo hajakamatwa na kufikishwa mahakamani, yeye ndiye mwenye kesi ya kujibu hivyo naomba washtakiwa hawa waachiwe huru,” alidai Msafiri.
Mawakili hao walimaliza kuwasilisha hoja hizo saa 10:42 jioni, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mugaya Mutaki aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi leo, ili wapate muda wa kujipanga kuja kujibu hoja hizo zilizotolewa na mawakili wa utetezi.
Mbali na Zombe na Bageni, washtakiwa wengine ni Ahmed Makelle, Noel Leornad, Jane Andrew, Moris Nyangerela, Emmanuel Mabula na Felix Cedrick.
Wengine ni Koplo Michael, D. 2300 Abeneth, Koplo Rajabu, Rashid Lema na Festus Chenge.
Washtakiwa hao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006 katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Louis, nje ya Jiji la Dar es Salaam, waliwaua Ephrahim Chigumbi, nduguye Sabinus Chigumbi, Mathias Lukombe na Juma Ndugu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Februari 5 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.