Header Ads

WANA MTANDAO NA MAFISADI NI KUNDI MOJA

Na Happiness Katabazi

KATIKA uwanja wa siasa Tanzania, yamezuka maneno ‘mtandao’ na ‘ufisadi’. Hapa kuna jukumu la kutosha kuoanisha dhana zinazobebwa na maneno haya mawili.

Neno mtandao lilizuka kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, likikusanya watu katika nyanja mbalimbali, wakiwemo wasomi, wafanyabaishara, wanahabari, wafanyakazi serikalini na matapeli ambao walikuwa na tamaa ya kupindua wazee katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutumia chama hicho kuingia Ikulu.

Kwa asilimia 95, kundi hili lilifaulu kuiteka CCM kwa kuwapiga bakora wazee na kuwagaragaza katika chaguzi za ndani za chama na kushika madaraka serikalini.

Ujana ulioanishwa na kundi hili na itikadi yake ikawa ni Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya. Na kwa itikadi hii kundi hili likaingia Ikulu.

Kitu ambacho Watanzania hawakujiuliza ni wapi vijana hawa walipata mabilioni ya fedha walizokuwa wakizitumia kwenye kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama na katika uchaguzi mkuu uliopita.

Zilizuka tetesi kuwa kundi hili lilikusanya fedha nyingi toka nje ya nchi, hasa kutoka Iran na Libya.

Watanzania hawakubaini kwamba kundi hili lilikuwa limejijenga ndani ya nchi katika taasisi nyeti za fedha na Benki Kuu (BoT).

Imewachukua Watanzania miaka miwili ya utawala wa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya kugundua kwamba kundi hili ni la kifisadi au limetenda ufisadi mkubwa ndani ya nchi yetu.

Mikataba ya serikali na kampuni hewa iliwezesha kundi hili kuchukua mabilioni ya fedha kutoka bajeti ya serikali. Ikumbukwe kwamba kundi hili lilikamata viongozi wakuu wa serikali katika kila sekta na lilifanya kazi kwa kusaidiwa kwa karibu na baadhi ya maofisa toka vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Inadaiwa mikataba ya serikali kwenye sekta ya maliasili iliwezesha kundi hili kupata mabilioni ya fedha kwenye asilimia 10 walizokuwa wanapewa na kampuni hizo, lakini pia katika michango waliyochangiwa na kampuni hizo kwa visingizio mbalimbali.

Tulishuhudia wagombea wa CCM wakichangiwa kwenye mikoa mbalimbali ya nchi mamilioni ya fedha. Jambo la kushangaza ni pale ilipogundulika mifuko ya pensheni imetumika kuchangia kampeni za CCM na mauzo ya majengo yalifanywa kwa kutumia taasisi ya ubinafsishaji na taasisi za umma kupitia mifuko hiyo kuwaneemesha wafanyabiashara makuadi ambao kazi yao ilikuwa kulikusanyia fedha kundi la mtandao.

Kana kwamba hiyo haitoshi, imedhiirika sasa miradi ya majengo mbalimbali kama vile minara pacha ya BoT ilitumika pia kuiba mabilioni ya fedha kupitia kandarasi.

Mfano jengo ambalo lilipangwa kugharimu sh bilioni 83, sasa limegharimu sh bilioni 523. Hilo halijachunguzwa na hakuna anayethubutu kulichunguza kwa sababu haiyumkini hizo ndizo baadhi ya fedha zilizoiingiza serikali ya awamu ya nne madarakani.

Hivi sasa mtandao umekamilika kwa kuwa wamegawana vyeo vyote serikalini kama walivyoahidiana kwenye kampeni. Aliyeahidiwa u-DC, u-RC alipata na hilo tulilithibitisha tulivyokuwa na baraza kubwa la mawaziri mithili ya darasa la chekechea.

Tatizo kubwa linaloukabili mtandao leo hii ni vyeo vimekwisha kwenye chama na serikali, ambaye hakupata analia na kusaga meno na anashauriwa asubiri mwaka 2010.

Lakini upo pia msambaratiko utokanao na wale wanamtandao wanaotaka kula sasa na si kungoja 2010.

Matokeo yake wanalaumiana, kuchomeana nguru na kusalitiana, hasa pale ambapo mwanamtandao aliyekabidhiwa madaraka amefanya kosa au kashfa.

Hilo tumeliona wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyejiuzulu, alipojitetea bungeni kwamba kuna wanaotaka cheo chake. Kumbe uwaziri mkuu ulikuwa ni wake lije jua ije mvua, akosee asikosee! Jambo hili linasikitisha sana.

Hivi sasa katika vyombo vya habari inaonekana wazi kwamba upo mgawanyiko kati ya vyombo vya habari vinavyounga mkono kundi moja la mtandao dhidi ya jingine.

Swali ni kwamba, kwani wanamtandao ni watu wema? Mbona inadhihirika wazi kwa vitendo vyao kwamba hakuna tofauti kati ya mtandao na ufisadi?

Je, mafisadi wanapogombana kundi moja likisema kwamba kundi jingine ni fisadi zaidi sisi Watanzania tunafaidika nini?

Tunachosema ni kwamba, mtandao ni ufisadi na yeyote aliyeshiriki kwenye kundi hili la mtandao kwa namna yoyote ile ajue wazi ameshiriki kikamilifu kujenga na kuimarisha ufisadi hapa nchini.

Kila mmoja ajichunguze alishiriki vipi kusaidia kundi hili kuingia Ikulu. Tunaweza kulaumiana bila sababu, tukubaliane kwamba kundi la mtandao halikuwa jema ndani ya CCM na si jambo jema ndani ya Tanzania kwani ni mwanzo wa mwisho wa CCM.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Machi 19 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.