Header Ads

RAIS KIKWETE JIHADHARI NA UDANGANYIFU, HUTOAMINIKA



Na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete amewaahidi Watanzania kuwa serikali yake iko vitani dhidi ya ufisadi. Amesisitiza taifa limpe fursa kuifanya kazi hiyo kwa umakini na umahiri unaostahili.

Ili kuonyesha azima yake hiyo, aliviagiza vyombo vyake vya utendaji, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuunda timu ya pamoja kushughulikia ufisadi uliojitokeza BoT, hasa ule wa akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA).

Katika utekelezaji wao, kamati hiyo hivi karibuni imezungumza na wahariri wa vyombo vya habari kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na IGP Said Mwema, wakisema kwamba kazi wanayoifanya ni nzuri, imeanza kuzaa matunda na fedha zimeanza kurejeshwa, wanahitaji muda na usiri mkubwa.

Kwa wananchi wa kawaida tatizo si usiri wala muda, hayo tunajua ni mahitaji ya lazima ili kazi yao iweze kufanyika vizuri. Tatizo kubwa ni kwamba Rais Kikwete hakuvisafisha vyombo hivi vikawa safi ili kuviwezesha kupambana na ufisadi.

Tunajua kwamba ni kesi ya ngedere amelekewa nyani.Kama vyombo hivi vyenyewe vinatuhumiwa kushiriki kwenye ufisadi kama ambavyo kamati ya uchunguzi wa mkataba wa kufua umeme wa Richmond iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ilieleza Bunge, vitakuwa na uhalali gani wa kusimama na kuwanyooshea kidole mafisadi wenzao?

Tatizo la pili ni ufisadi wenyewe: Ni nani wa kuaminika aliye kwenye kamati hiyo inayoendesha mahojiano na mafisadi, anayeweza kuaminiwa na Watanzania hata kuthibitisha kwamba fedha zimerejeshwa?

Huu ni mchezo wa nyani kula kula mahindi mabichi. Kusingizia fedha zimetoka mfuko huu kuziingiza kwenye mfuko wa pili bila kujua huu mfuko wa kwanza ulipataje hizo fedha.

Watanzania tumechoka na viinimacho vya baadhi ya viongozi kuleta fedha chafu za mihadarati au za ufisadi mwingine na kuwagawia washirika wao kwa siri, ili waje kuzitoa kwenye harambee wanazozisimamia.

Vivyo hivyo, fedha chafu zinaweza kusafishwa kwa kurejeshwa serikalini kupitia dirisha hilo la kashfa ya EPA. Kama Rais angependa tumuamini angelazimika kuweka wajumbe wenye sifa za kutukuka na ambao ni huru wanaoweza kuaminika na wananchi.

Lakini ilivyo hivi sasa hata tungeambiwa sh billion 133 zote zimerejeshwa, haitaondoa shaka kuwa fedha hizo zimepatikana kutoka kwenye fedha chafu ama za mihadarati au za uharamia mwingine.

Tunamwomba Rais Kikwete asilifumbie macho hili kwa sababu linakera na kuwaletea wananchi kichefuchefu na likiendelea hivi litamchafua.
Ifike mahala Watanzania tujiulize; hizi fedha zinazorejeshwa na hawa mafisadi, tena kwa kipindi kifupi, zilikuwa wapi?

Hawa mafisadi katika kipindi hiki kifupi wamefanya biashara gani iliyowaingizia fedha hizi?

Na hii ndiyo maana tunasema ni vizuri wananchi waelezwe kosa la jinai lilitendwa, mtu aliyetenda ili hata kama ikiamriwa asifikishwe mahakamani tujue kwamba huyu ni fisadi.

Kwa vyovyote vile, hakuna chombo cha kuwasafisha hawa isipokuwa mahakama. Hatutaki tuambiwe utaratibu wa utendaji wa BoT ni wa kizembe kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kujichotea mamilioni ya fedha kutoka benki hiyo. Na hili ndilo Rais analokwepa kuwaeleza Watanzania.

Yawezekana kabisa kwamba vigogo ndani ya CCM na serikali ‘walikatiwa pochi’ ya fedha za EPA na inawezekana pia kuwa hiyo ndiyo sababu ya kukwepa kutaja majina ya mafisadi.

Yawezekana pia fedha za EPA zilitumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kuiweka Serikali ya Awamu ya Nne madarakani.

Lakini hayo ndiyo maswali magumu na machungu ambayo ni lazima taifa liambiwe, ili kesho na keshokutwa vyama vya upinzani vinapolalamika kuhusu gharama za uchaguzi, tuweze kuvielewa kwa sura mpya.

Lazima Watanzania waelewe CCM hailalamikii gharama za uchaguzi kwa sababu zina njia za kifisadi za kuchofa fedha.

Tusipoyasema haya taifa hili halitashinda vita ya ufisadi kwa sababu ufisadi umefungamana na siasa za CCM na jinsi chama hicho kinavyoendesha nchi.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 26 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.