Header Ads

MWALIMU NYERERE NATAMANI UONE TUNAVYOKUENZI



Na Happiness Katabazi

MWALIMU Julias Nyerere Baba wa Taifa letu,jana tumeadhimisha miaka tisa tangu ulipotutoka Oktoba 14,1999, na tukakupumzisha kwa amani katika Kijiji ulichozaliwa cha Mwitongo-Butiama mkoani Mara.Tunaendelea kukuenzi baba japo kwa mitindo mbalimbali.Tukikuita baba kwa sababu wewe ni mwasisi wa taifa letu la Tanzania.

Baba,ulikuwa Mwalimu wetu na hata leo hii unaendelea kutufundisha katika yale yote uliyotuusia.Kuondoka kwako kulituachia majonzi mazito ambayo uzito wake haujapungua hadi leo.

Tunazidi kukukumbuka baba na tunaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi yetu ya kukuenzi milele na milele.

Baba katika wingi wetu wapo wanaokuenzi au tupo tunaokuenzi kikweli kweli na wapo wanaokuenzi kinakfi.
Kwa sababu hiyo na kwa mara nyingine tunakusii uchungulie duniani na ujisomee na kujionea mwenyewe yale yanayojiri katika harakati za kukuenzi siku hadi siku.

Baba, si unakumbuka kile chama ulichokiasisi mwenyewe,mapema mwaka huu kilikuenzi wazi wazi pale kilipoamua kufanya kikao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) katika kijiji ulichozaliwa Butiama ambako mwili wako ilipopumzishwa ukingojea parapanda ya mwisho.

Katika kikao hicho vigogo wa chama chako cha CCM, walikuenzi kwa kuibuka na Azimio la Butiama ambalo lilitutoa machozi tukikukumbuka kwa kuwa lilielekea kupingana na kile ulichokiamini pale waliposhindwa kuamua kukataa kuridhia makubaliano yao na CUF kuhusu Mwafaka wa kisiasa Zanzibar, badala yake wakapiga kalenda mwafaka huo kwa kusingizia suala hilo likapigiwe kura na wananchi.

Mbaya zaidi baba, wakaibuka miongoni mwetu wakaamua kuuenzi Muungano uliouasisi wewe na Mzee Abeid Aman Karume, kwa mabishano makali juu ya ‘Zanzibar ni nchi au laa’.

Usishangae baba hivi ndivyo tunavyolienzi onyo lako kwamba tusithubutu kubaguana maana dhambi ya ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu.

Vilevile baba wakiwa kule Butiama waliamua kukuenzi kwakukumbatia wahujumu uchumi lakini usishangae siku hizi wahujumu uchumi tunawaita ‘mafisadi’, badala ya kuwatimua uanachama kama ambavyo ungependa iwe lakini walitetewa, kuchekewa na kupakatwa.

Baba, kile chama ulichokiasisi si kimoja tena ila ni chama ambacho kimeamua kukuenzi kwa kuunda makundi na mitandao yenye kuasimiana na kuhujumia .Ipo mitandao mingi baba, kuna kundi la mtandao halisi, mtandao maslahi na mtandao majeruhi ambayo utendaji wake unatia shaka na wasiwasi juu ua jinsi gani watakavyokuenzi ifikapo uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kukuenzi kwetu baba kupo pia kwenye Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), samahani baba hata huko kuna mkataba feki umeingia.

Tunakuenzi kwa kumkemea na kumshughulikia kwa hira mjukuu wako jasiri, Nape Moses Nnauye ambaye alilalamikia wazi wazi uchafu wa mkataba wa mradi wa jengo la UVCCM kwa kumfukuza uanachama wa jumuiya hiyo.

Kwa ujumla baba nchi inakuenzi kwa kukosa viongozi bora.Hivi sasa tunaviongozi ambao ni mahiri wa kuendesha ‘Fund Rising’,Viongozi wetu walio wengi ni mahiri kuheshimu hotuba na nukuu zako ila matendo yao yako mbali na kile wanachokisema.

Wapo waliodiriki kukuenzi kwa kutumia majukwaa ya kidini ili wajitakase ufisadi wao.Wengine wanakuenzi kwakusema uongo mchana kweupe.Wapo wanaoamini fedha ni msingi wa maendeleo hata wanajilimbikizia ‘vijisenti’ ughaibuni.

Kukuenzi kwao ni kukudharau wewe baba yetu uliyekufa maskini bila kuliibia taifa.

Tunakuenzi baba kwa kuendeleza mapokezi ya kishindo kwa viongozi wetu.Utakumbuka baba ,watanzania walivyokupokea wakati unatoka Umoja wa Mataifa kwa kukuimbia ‘baba kabwela,baba kabwela’.

Tunaendeleza wimbo huu hususani majimboni kwa kuwaimbia ‘baba kabwela’ viongozi wanaokumbwa na kashfa nzito za ufisadi ambazo zimewaladhimu kujiudhuru nyadhifa zao za serikalini.Wana CCM wenzio wanakuenzi kwa kuwafanyia sherehe kubwa kana kwamba makosa yao ni mambo ya kujivunia.

Yule mwanafunzi wako katika medani ya siasa Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye sasa amezeeka kiumri na amechoka kimawazo ameamua kukuenzi kwa kuwatishia vijana wako wa ccm wanaokemea maovu ndani ya chama na serikali kwamba hakuna mtu maarufu kushinda chama.

Baba ,viongozi wetu inabidi wakumbuke maneno ya Yesu Kristo aliyowaambia watu wa taifa la Uyahudi,kwamba “Hamjui kwamba mnaye baba mwingine,ninyi si watoto wa Ibrahim,ninyi ni watoto wa ibilisi,kwa kuwa ibilisi amekuwa mwongo na mnafiki tangu mwanzo,nanyi mnayatenda hayo hayo kama baba yenu”.Sasa baba ,wanao tunapojivunia ubaba wako,baadhi ya yetu wanaye baba mwingine ambaye si wewe!Baba yao ni beberu(bepari aliyekomaa),kwani bepari amekuwa mnyonyaji,tangu mwanzo hata leo hii,angali akinyonya kwa kutumia utandawazi,ubinafsishaji na kuendekeza masilahi binafsi.Viongozi wetu wa leo mnamuenzi baba yupi?

Baba tunaendelea kushangaa na kujiuliza hasa tunaposoma andiko lako la “Uongozi wetu na hatima ya Tanzania”.Baba utakumbuka mwanafunzi wako uliyetuachia na ukatudhibitishia ni msafi, aliamua kukuenzi kwa kuigeuza Ikulu kuwa pahala pa ujasiliamali.

Akuishia hapo baba alijimegea pande la nchi hii na kulifanya mali yake binafsi katika harakati za kudhibitisha usafi alionao.

Amekuenzi kwa kuwa mwanafunzi wako mzuri maana kama ulivyosema unang’atuka naye mwezi uliopita ametangaza kung’atuka katika shughuli zote za kisiasa, sasa anaelekeza ujasiriamali wake katika dini.

Samahani baba, imekuwa ndiyo tabia yetu sasa kwamba mhujumu uchumi asikamatwe wala kushitakiwa bali abembelezwe kulipa kidogo kidogo kile alicholiibia taifa.

Si unakumbuka baba ulituambia kwamba ulimchukulia hatua yule raia wa kigeni aliyesema serikali yetu ipo mfukoni mwake,hukungoja ushaidi wala kupoteza muda wala kuunda tume .Sisi baba tumeamua kukuenzi kwakufanya kinyume.

Baba tunakuenzi hata kwakuizalilisha nafasi yako ya kwanza kabisa ya Uongozi wa kiserikali uliyoishika muda mfupi baada ya nchi kupata uhuru .Baba siunamkumbuka yule kijana wako uliyemshangaa mwaka 1995 kwamba utajiri wa chapchap ameupata wapi; amekuenzi kwa kutumia nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu vibaya kiasi cha kuliingiza taifa hasara kubwa pale aliposhinikiza nchi iingie mkataba na kampuni ya kihuni ya Richmond .

Baba kwa mara ya kwanza katika historia, kijana huyu na vijana wenzake Nazir Karamagi ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Ibrahim Msabaha, iliwalazimu kukuenzi kwa kujiuzulu.

Tunaendelea kukuenzi baba kwa kupuuza mafunzo yako ya kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuheshimiwa utu wake badala yake baba tunakuenzi kwa kuzuliana kashfa, vifo na uongo kila kukicha.

Kwa mfano baba tumefikia hatua ya kusemana adharani kwamba kiongozi huyu ndiye kamuua kiongozi yule ama anataka kumuua.Kashfa hizi baba zinakaribia kutuingiza kwenye uvunjifu wa amani uliyotuachia.Sasa tumeanza kuenzi amani hiyo kwa kutwangana mawe, kuzomeana kwenye mikutano ya ardhara ya vyama vya siasa.

Baba tumezidi kukuenzi kupitia ile sera uliyoacha tumeianzisha ya ubinafsishaji.Utakumbuka baba hukupenda tuuze au tubinafsishe benki zetu wala rasilimali zetu.

Samahani baba hatukukusikiliza tukaziuza benki hizo ikiwemo Benki ya Makabwela(NMB).

Tulidhani baba tukiuza benki hii tunafanya jambo la maana kumbe tunasababisha matatizo makubwa ambayo hivi juzi ilisababisha wafanyakazi wa benki hiyo nchi nzima wakagoma kwa siku mbili mfululizo.

Na hivi leo tunavyokuenzi bado tunaugulia maumivu yaliyotokana na mgomo huo.Mbali na hilo baba tumekuenzi kwa kuuza lilokuwa Shirika la Reli(TRC).Samahani mwekezaji tuliomuuzia hana fedha kiasi kwamba kila siku anakwenda serikalini kulialia ili serikali imsaidie kulipa mishahara wafanyakazi.

Hatuna uhakika kama kilio chake hiki ni cha kweli au ana lake jambo na hao walimpigia chapuo la kuendesha Shirika hilo na wale wanaoidhinisha asaidiwe fedha za kuwalipa mishahara wafanyakazi.

Baba, tumekuenzi kwa kuvunja rekodi ya ziara ulizozifanya kwa kutembele nchi mbalimbali ulimwenguni.

Utakumbuka baba yule kijana wako ambaye wakati anaondoka duniani alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa , sasa hivi ndiye mkuu wa Kaya yako ameamua kukuenzi kikwelikweli kwa kujizolea sifa mbalimbali, moja wapo ya sifa alizonazo ni uwezo mkubwa wa kulimudu vyema somo la Giografia hususani matumizi ya Atlas.

Ni umahiri huo ambao unamuwesha kuvunja rekodi kwa rais wa taifa uliloliasisi aliyetembelea nchi nyingi kwa muda mfupi.

Baba, nitakuwa natenda dhambi kama sitakueleza hili kwamba uendelee kumuombea mkuu wetu wa Kaya Rais Jakaya Kikwete, aendelee na moyo wake wa kuruhusu uhuru wa watu kutoa maoni kwani katika hili binafsi nampongeza.

Huko ulipo baba, uendelee kumuombea kwa mungu ili asibadilishe msimamo wake wa kuturuhusu sisi wananchi wake kutoa maoni.

Katika hili baba nampongeza Kikwete kwani hivi sasa baba ruksa kuikosoa serikali na viongozi wake licha kuna baadhi ya watendaji wake wanakosa uvumilivu.

Tunakuenzi baba kwa kudumisha demokrasia ya vyama vingi.Na utakumbuka ulishauri vyama vingi viwepo na vikawepo ila ukaonya visiwe utitiri.

Utuwie radhi baba kwani kadri muda unavyozidi kwenda vyama vingi vilivyoanzishwa nchini vinazidi kuwa dhaifu.

Sababu ni nyingi za udhaifu huo miongoni mwa udhaifu huo ni kuama ama kwa vijana wako walioamua kukuenzi kwa kuendekeza uchu wa madaraka na binafsi.

Leo hii wakikosa madaraka hapa kesho wakikosa ruzuku pale wanaamua kukimbilia kwingine.

Baba vipo pia vyama vilivyoamua kuenzi mtizamo wako wa umoja na mshikamano kwakuanzisha ushirikiano miongoni mwao japo mara kadhaa vyenyewe kwa vyenyewe vinafanya mambo yanayoashiria kutokuwa na nia ya dhati ya kushirikiana.

Samahani baba demokrasia uliyotuachia tumeshindwa kuifanya ikomae.Baba ulipenda uhuru wa vyombo bila unafki licha katika utawala wako vyombo vya habari vilikuwa ni vichache na uliwapenda pia waandishi wa habari , ni bahati mbaya tumeamua kukuenzi kwa kuuminya uhuru huo na kuwafanyia matendo ya hiana baadhi ya wanahabari.

Mathalani wapo waliokuenzi kwa kuwamwagia tindikali na kuwatishi kuwaua au kwapeleka mahakamani waandishi wa habari, na kuvinyima baadhi ya vyombo matangazo ya kiserikali ili kuvidhoofisha.

Kwa upande mwingine baba, wapo wanaandishi wa habari wenzetu ambao kwa makusudi wameamua kujigeuza ‘disposable tissue’ za wanasiasa manyang’au ambao wanabaka uchumi wa taifa kwa kuwaandikia habari na makala za kuwasafisha ili jamii iwaone ni wanasiasa wema.

Aidha, baba tunakuenzi kwa mifumuko ya migomo na maandamano ya kila kukicha.Hata leo walimu nchi nzima wanatarajia kuanza mgomo usiyonakikomo ili kushinikiza serikali iwalipe haki zao.

Wanafunzi wa Shule za msingi na sekondari nao pia hivi karibuni waliandamana wakipinga ongezeko la nauli.Haijawahi kutokea tangu taifa lipate uhuru.

Huko kwenye Vyuo Vikuu ndiyo usiseme migome imekuwa ni jadi.Pia baba hata mahabusu nao mwaka huu waligoma kushuka kwenye makarandika na wengine waligoma kula wakishinikiza kesi zao zisikilizwe haraka kama zilivyo za mahabusu wengine ambao wanaujaama na vigogo au walikuwa watumushi wa ngazi za juu serikalini.

Baba katika utawala wako elimu ilikuwa ikitolewa bila ubagudhi na kusema watoto wa wakulima na wafanyakazi lazima wapate elimu, lakini hivi sasa tunakuenzi baba kwa kutoa elimu kwa madaraja katika vyuo vikuu.

Baba nao wana Tarime juzi waliamua kukuenzi kwa kukiadhibu vikali chama chako na badala yake wakakipigia kula za ndiyo chama CHADEMA ambacho ulivyokuwa hai uliwai kusema chama hicho cha upinzani kina sera nzuri.

Siyo tu walikitosa chama chako bali wana Tarime waliakikisha wanakula sahani moja na chama chako ambacho hivi sasa kinaonekana kuishiwa sera katika chaguzi zake na badala yake kimekuwa kikitumia hira za kila aina kupata ushindi lakini Mungu amfichi mnafiki,mbinu hizo za hira zimeweza kutokomezwa na wana Tarime.

Nikuume sikio baba, katika uchaguzi huo ulifanyika Jumapili iliyopita, vyama viwili vya CHADEMA na CCM ,baadhi ya wafuasi wake walikuwa wakiudhuria mikutano ya kampeni na silaha za jadi na ikafikia mahala wafuasi hao kujeruhiana kwa silaha za jadi ikiwemo mapanga.

Licha ya Katibu Mkuu wa chama Yusuf Makamba, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Waziri Kilimo,Chakula na Ushirika Steven Wassira,Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi John Chiligati, Kaimu Katibu wa Kitendo cha Propaganda Tambwe Hiza, ambaye huyu utakumbuka alikuwa ni yule kijana alikuwa CUF na akawa anakisakama sana chama chako lakini hivi sasa amesalimu amri amejiunga na chama chako na kupewa cheo chapchap,chama ulichokiadidi hazikufua dafu mbele ya Chadema.

Jitihada zao za kuwepo kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Tarime hazikuza matunda.Ama kwa hakika jopo hili la viongozi wa chama na serikali uwepo wao katika kampeni za uchaguzi mdogo halafu uwepo wao ukashindwa kukiletea chama chako ushindi,nadiriki kutamka kumemeendeleza wimbi la kukipaka matope chama chako na kuonyesha ishara mbaya chama chako kwenye chaguzi zijazo.

Sikufichi baba, katika uchaguzi huo mdogo chama chako nacho kiliamua kukuenzi kwa kutumia ‘mijihela’ mingi kiasi cha Sh bilioni moja kwaajili ya kampeni, kukodisha Helkopta ili kuwaamasishe wananchi wa Tarime wakipe kura.

Lakini wananchi hao waliwepa pamba masikioni na kuichagua CHADEMA ambacho pia nacho tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 hadi uchaguzi mdogo wa Tarime,kimeamua kimeamua kukuenzi kikamilifu kwa kutumia Helkopta katika kampeni zake.

Kwa kifupi, baba ile CCM safi ulizikwa nayo pale Mwintongo na CCM chafu ndiyo imebaki na inendelea kututawala.

Hata hivyo baba kampeni za uchaguzi mdogo wa Tarime kutokana na kampeni zake zilitawaliwa na uwamgaji damu wa hapa na pale ikiwemo kukatana mapanga hali iliyosababisha masikio na macho ya watanzania wote kuelekeza kwenye uchaguzi huo;kumewafundisha Watanzania kitu kimoja kwamba siku zote vyama vya upinzani vikitaka kuishinda CCM, lazima vipambane kufa na kupona.

Tunakuenzi baba kwa kuliingiza taifa kwenye aibu iliyopitiliza kule bungeni Dodoma katika bunge la bajeti mwaka huu, tumeamua kukuenzi kwa stahili ya aina yake ya kukumbatia ushirikina.

Mara hii kwa kufanya vitendo vinavyoashiria ushirikina mchana kweupe.Tumekuenzi baba kwa kutuhumiana kwamba tunalogana kwa kunyunyiza unga mweupe ili tusisemane na kukosoana pale kunapokosea.

Baba ushirikina wetu auishii hapo tumeamua kukuenzi kwa kuwachinja Malbino na kunyofoa baadhi ya viuongo vyao0, kwa kuwafanya kafara za kutafutia mali,utajiri na vyeo.Samahani baba kwakukuenzi kwa stahili hii ya kutenda maovu, tunaomba utuombee msamaha kwa mungu kama ulivyoaidi ukisema unajua tutalia lakini utatuombea kwa mungu.

Baba Mungu alikuumba na ukaisha kuifanya kazi yake hapa kwetu duniani,akakutwaa.Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahali pema peponi.Amina.

0755 312859
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano ,Oktoba 15 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.