Header Ads

NECTA PAMECHAFUKA,PASAFISHWE

Na Happiness Katabazi

IMEANZA kuwa mila na desturi kwamba kila mwaka kipindi cha mitihani ya taifa ya kidato cha nne, zinakuwepo taarifa za kuvuja kwa mitihani hiyo.

Inapovuja, wanaotiwa nguvuni ni watahiniwa wanaodaiwa kukutwa na majibu.

Hata siku moja, Jeshi la Polisi lenye makachero wengi halielezi limewakamata wanaodaiwa kuvujisha mitihani. Nikirifikiria, napata mashaka juu ya utendaji wa makachero wa jeshi hilo.

Mapema Oktoba mwaka huu, wanafunzi wa kidato cha nne kote nchini walianza kufanya mtihani wa taifa. Siku tatu kabla, vyombo vya habari viliwakariri baadhi ya watahiniwa hao wakisema mitihani imevuja.

Kama ilivyo ada ya watawala kupinga hata mambo ya wazi, walikubali kwa shingo upande kwamba mtihani wa hisabati umevuja na kujinasibu, mitihani mingine haijavuja.

Hivyo, Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), walilazimika kuahirisha mtihani wa hisabati hadi Oktoba 27. Wanaoitakia mema nchi yao waliendelea kusema wazi kwamba mitihani yote imevuja.

Lakini, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe na Mkurugenzi Mtendaji wa NECTA, Joyce Ndelichako, walishupaza shingo zao na kubuni mbinu mpya ya kuwakimbia wanahabari.

Tukio la mwaka huu, ni tofauti na miaka mingine ambapo ilivuja kwa kuipora, ilipokuwa ikisafirishwa kwenda mashuleni. Kwa mtazamo wangu, safari hii, imevuja ndani ya ofisi za NECTA iliyokabidhiwa jukumu la kitaifa.

Nafahamu, mtihani unapima kiwango cha uelewa wa mwanafunzi kwa aliyofundishwa katika kipindi cha miaka minne. Kuvuja kwa mitihani kunaharibu dhumuni lake.

Mwanafunzi anayepata mitihani iliyovuja, anajijengea msingi wa kushindwa kuelimika, anakuja kufanya kazi ya kitaalamu bila uelewa, mwisho wa siku analeta madhara kwa taifa. Nalazimika kuamini yaliyotokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ulipofanyika upasuaji tata, ni mtiririko wa wataalamu feki.

Ni dhahiri kwamba mchezo wa kuvujisha mitihani unaimarika, ndiyo maana Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Idara ya Usalama wa Taifa, haliwagusi tatizo hili linalohatarisha usalama wa taifa letu.

Niliamini, baada ya taarifa za awali, wahusika wangeingia mtaani kuchunguza mtihani umevuja kwa kiwango gani, badala yake NECTA inajichunguza yenyewe.

Kwa kuwa Mungu amfichi mnafiki, amewafunulia Watanzania ‘uozo’ wa kufunga mwaka, unaofanyika ndani ya ofisi za NECTA. Mwanzoni mwa wiki hii, imeripotiwa kwamba baraza hilo limesambaza vyeti bandia vya matokeo ya kidato cha nne mwaka jana (result slip) kwenye shule mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa habari hiyo, wanafunzi walioathirika ni waliohitimu kidato cha nne mwaka jana. Baadhi yao wamepata misukosuko ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa maidai ya kughushi.

Mmoja wa waathirika hao ni Alexander Gundula (22) aliyekuwa mahabusu mjini Mbeya, kwa kosa la kupatikana na cheti feki, lililofanywa na NECTA.

Huyu alikuwa miongoni mwa askari wanafunzi wa Chuo cha Magereza Kiwira. NECTA imekiri udhaifu na kumwomba radhi kijana huyo kwa maandishi.

Katika hili, nampa pole Alexander kwa msukosuko na kulipongeza Jeshi la Magereza na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Azania, kwa sababu wametimiza wajibu wao kikamilifu.

Wakati nikitoa pole na pongezi kwa makundi hayo, walaaniwe baadhi ya watumishi wa NECTA walioshiriki kutengeneza ‘result slip’ feki ya kijana huyu na wengine. Nawalaani kwa sababu watu hao wanacheza na maisha ya watoto ambao wazazi wao walijinyima ili kuwapeleka shule.

Nalazimika kuamini kwamba, mchezo huo haujaanza leo, kwa sababu Azania ni shule iliyopo jijini Dar es Salaam, kama wameweza kufanya hivyo hapo, kwenye sekondari za vijijini hali itakuwa mbaya zaidi.

Kwa tukio hili, kila aliyemaliza kidato cha nne hapa nchini asijiamini kwamba cheti alichonacho si halisi, ni cha kughushi, hivyo kila mtu kwa wakati wake analazimika kufika NECTA ili kukihakiki.

Tukio hili lisipodhibitiwa, ni dhahiri kwamba wananchi watajenga chuki kwa serikali yao kwa sababu ya dhuluma kama hii kutoka kwa watumishi wake ambao mishahara yao inatokana na kodi za wananchi.

Vijana wataona hakuna umuhimu wa kusoma, badala yake watatafuta fedha za kuwahonga baadhi ya watendaji wa NECTA ili wauziwe vyeti. Tusifikishwe huko.

Nalazimika kuamini kwamba NECTA imeoza, hivyo inahitaji kupanguliwa. Haiingii akilini kuwa ofisi hii ya umma inakumbwa na kashfa halafu kiongozi wake hataki kujiuzulu, wala hatusikii watumishi wake wakifikishwa mahakamani.

NECTA inapokumbwa na uozo wa namna hii, naamini serikali na vyombo vyake vimeshindwa kazi, vimepania kuliteketeza taifa letu.

Wananchi tumeipa dhamana serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ituongoze, ikitokea baadhi ya vyombo vyake vya utendaji vikashindwa kutimiza wajibu na hatuoni viongozi kushtuka, maamini umefika wakati wa kuiwajibisha serikali.

Migomo ya kudai haki, ubadhirifu wa fedha za umma ni matukio yaliyotamalaki na hakuna jitihada zozote za serikali kuwashughulikia watuhumiwa.

Nalazimika kukubali kwamba nchi inaelekea pabaya, moyo wa kizalendo kwa wananchi na taifa umetoweka na baadhi ya watawala ni wachumia tumbo. Wakati umefika kila Mtanzania kwa nafasi yake kubadili tabia.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0755 312 859
katabazihappy@yahoo.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania la Alhamisi, Oktoba 30 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.