Header Ads

MIAKA MITATU YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE


RAIS KIKWETE AMESHINDWA KUTIMIZA NDOTO ZAKE
Na Happiness Katabazi
JUMAPILI iliyopita Rais Jakaya Kikwete ametimiza miaka mitatu tangu alivyoapishwa Desemba 21 mwaka 2005, kuwa rais wa awamu nne wa taifa letu.

Wakati rais Kikwete akiadhimisha miaka mitatu ya uongozi wake, pia mimi kesho Desemba 25 mwaka huu, naadhimisha siku yangu ya kuzaliwa ambapo nitakuwa natimiza miaka 30.Namshuruku mungu kwa kunipa uhai na afya njema.

Leo katika makala hii nitazungumzia mafanikio, mapungufu yaliyoonyeshwa na serikali ya awamu ya nne katika kipindi hiki cha miaka mitatu tangu alipoapishwa na Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta ,tarehe hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya asilimia 80 ya Watanzania kumpa ridhaa ya kuwaongoza katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2005.

Katika makala yangu hii nitataja sababu tano ambazo nitazianisha hapa chini ambazo zitatusaidia sote kutathimini utendaji kazi wa rais na serikali yake.

Majukumu ya rais kama yalivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.Moja ya kigezo cha kutathimini jinsi rais wetu anavyomudu majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hiyo.

Pili,kutathimini utendaji wa Kikwete jinsi hali ya nchi alivyoikuta wakati anakabidhiwa madaraka na hali ilivyo sasa baada ya miaka mitatu ya uongozi wake.

Tathimini yangu ya tatu; inaangalia yale ambayo Kikwete aliwahaidi Watanzania wakati anaomba kura endapo ameweza kuyatekeleza au ajayatekeleza bado au kashindwa kuyatekeleza.

Tathimini yangu ya nne;ninachoweza kutathimi akiwa yeye aliyechukua urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), utekelezaji wa Ilani ya chama chake.

Tathimini yangu ya tano;ni kumtathimini rais kulingana na matukio mbalimbali yaliyotokea chini ya utawala wake na jinsi alivyoweza kuyashughulikia.

Nianze na tathimini yangu ya kwanza;Ibara ya 33 ya Katiba ya nchi inatamka majukumu ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1984 Namba 15 ibara ndogo ya (9).Ibara ya 33(2)inasema rais atakuwa Mkuu wa nchi,kiongozi wa serikali na Amir Jeshi Mkuu.

Kikwete akiwa Amir Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ameweza kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo litakalo kumbukwa mno ni pale alipolituma jeshi lake la Ulinzi la Wananchi(JWTZ) kwenda kisiwa cha Anjoun-Komoro na lilifanikiwa kumng’oa muasi Kanali Mohamed Bacar.

Aidha Kikwete ameweza kusimika viongozi wa Majeshi yake, Mkuu wa (JWZT) Jenerali Davis Mwamunyange,Inspekta Jeneli wa Jeshi la Polisi(IGP)Said Mwema,Kamisnha Mkuu wa Jeshi la Magereza Agustino Nanyaro ambao utendaji wao una kwenda vizuri kwani nchi haijavamiwa na maadui, usalama wa mipaka yetu kwa kiasi kikubwa upo salama na hatujasikia wafungwa au mahabusu wamevunja magereza yetu na kutoroka.

Kwa upande wa Kiongozi wa Serikali; ukweli ni kwamba rais wetu kwa kipindi hiki cha miaka mitatu ameongoza serikali inayoteteleka.Ni serikali iliyokumbwa na kashfa nyingi kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu.

Na mfano mzuri katika hili ni kashfa ya mkataba wa kufua umme ambao ulimlazimisha kujiudhuru nyadhifa zao aliyekuwa waziri Mkuu Edwar Lowassa,waziri wa Nishati na Madini,Nazir Karamagi, Waziri Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Ibrahim Msabaha.Wakati aliyekuwa waziri wa Miundombinu Endrew Chenge naye alijiudhuru baada ya kukumbukwa na kashfa ya mkataba mbovu wa ununuzi wa Rada ambaye hata hivyo ianelezwa kwamba anaendelea kuchunguzwa.

Aliyekuwa waziri wake wa Fedha Zakhia Meghji aliwahi kukaririwa akisema kwamba alidanganywa na wasaidizi wake kuhusu kampuni ya Kagoda Agricultural ambayo kampuni hii inatajwa kuwa ni kampuni ya kifisadi na ilichota sh bilioni 40 katika Benki Kuu. Lakini kabla ya Meghji kusema hayo aliwahi kukaliliwa akijinasibu kwamba Kampuni ya Kagoda ilichota fedha hizo kwaajili ya kununulia vifaa vya usalama wa majeshi yetu.

Kashfa ya wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Jiko letu la Uchumi(Benki Kuu), kashfa ambalo ilimlazimu rais kuunda tume kuchunguza wizi huo na hatimaye tunaendelea kushuudia baadhi ya watuhumiwa wameanza kuburuzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Huu ni udhibitisho kwamba serikali anayoingoza rais wetu huyu ina viongozi na watendaji wasiyo makini,ingawa si wote.Vile vile katika kipindi chake cha uongozi , kina kuwa ni kipindi cha kupata historia nyingine ya kuwa na Baraza kubwa la mawaziri licha mapema Februari mwaka huu, alilazimika kulipunguza.

Ni serikali hii ilifanya kituko cha aina yake cha mawaziri wake kujimegea fedha za walipa kodi na kuanza kuzunguka mikoani kuwaelezea wananchi uzuri wa bajeti.Uamuzi ambao ulipingwa vikali na wananchi hadi kufikia mawaziri hao kukatisha ziara hizo kwani walikuwa wakikutana na wakati mgumo sambamba na kuzomewa na wananchi.

Hivyo wakati tukiazimisha miaka mitatu ya uongozi wa Kikwete nilazima tumweleze bayana kwamba uamuzi huu mawaziri wake kulandalanda mikoani kuelezea uzuri wa bajeti haukuwa sahihi kwani ulilenga kufuja fedha za walipa kodi.

Tathimini ya hali ailivyoikuta na hali ilivyo hivi sasa kijamii, kiuchumi na kisiasa;ukweli ni kwamba hali ya maisha imekuwa ngumu kuliko ilivyokuwa miaka mitatu nyuma kwani gharama za maisha zimepanda bei ya mafuta,vyakula ni ghali.Nikipindi ambacho tumeshuhudia kupanda kwa kasi bei za mafuta,ada za watoto mashuleni, ongezeko la uhalifu hususani uhalifu wa mtandao.Hali inazidi kuwa mbaya wakati rais aliwaaidi wananchi maisha bora.

Aliyoaidi wakati anagombea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, aliaidi wananchi mambo lukuki na miongoni aliyoyahaidi ni kushughulikia mpasukuko wa kisiasa Zanzibar ili kurejesha imani lakini hadi Jumapili miaka mitatu imetimia,jitihada zake za kumaliza mpasuko hazijazaa matunda.

Ahadi nyingine aliyowahadi wananchi , ni kujenga Vvyuo Vikuu vingi ili wananchi wake wapate elimu,ukweli ni kwamba hadi leo ameweza kutekeleza kwa kiasi fulani ahadi hiyo kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma.Hata akiondoka leo madarakani tutamkumbuka kwa kuanzisha chuo hicho.

Pamoja na hayo sera ya mtangulizi wake Benjamin Mkapa, ya Ubinafsishaji katika sekta mbalimbali ambayo imewezesha kuanzishwa Vyuo Vikuu kadhaa nchini.Kwa hiyo ukweli idadi ya wananchi wanaoingia vyuo ikuu imeongezeka.

Hata hivyo ubora wa elimu utolewao katika vyuo hivyo unaelekea kushuka zaidi kwasababu wakati idadi ya wanafunzi kujiunga vyuoni humo inaongezeka , idadi ya wahadhiri,miundombinu na vifaa vingine vya kujifunzia havijaongezeka. Mathalani uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Dodoma umethiri baadhi ya vyuo vingine kwani baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho wametolewa kwenye vyuo vikuu hivyo kuviacha vikiwa vimepwaya.

Kimsingi kuna kuwa hakuna mantiki ya kuanzisha utitiri wa vyuo wakati vyuo tulivyonavyo tumeshindwa kuviendesha na ubora wake unaporomoka.Mbaya zaidi ongezeko la vyuo hivi unatokea wakati ambapo kuna sera tata ya uchangiaji gharama wa elimu ya juu.

Sera ambayo inazidi kuathiri Elimu ya Juu na hadi naandika makala hii, vyuo zaidi ya vitano vimefungwa kutokana na wanafunzi kupinga sera hiyo ya uchangiaji mikopo.Bahati mbaya zaidi tatizo hili linagusa moja ya ahadi aliyoitoa Kikwete katika Ukumbi wa Dimond Jubilee mwaka jana, wakati akizungumza na wana vyuo, alisema hakuna mtoto wa maskini atakayefukuzwa chuo kwakukosa ada.Hii ni ahadi ya pili ya rais Kikwete ambayo ameshindwa kuitekeleza.

Katika kipindi hiki cha uongozi wake kumekuwa na chipuko mithili ya uyoga kwa shule za sekondari al maarufu “sekondari za Kata’.Hili ni ongezeko la kupigiwa mfano na pengine ukilitizama kwa juu juu ni la kujivunia lakini ukilitizama kinachoendelea ndani ya shule hizi ni aibu.

Badala ya kuwa na shule halisi,nyingi zina ripotiwa zimekuwa ni kambi ya za watoto wetu kwenda kukuza umri.Ni shule zilizoghubikwa na uhaba wa walimu na vifaa kiasi cha kutisha.Kwa ujumla kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa rais wetu kimekuwa ni kipindi cha kuporomoka kwa ubora wa elimu.

Rais Kikwete aliahidi kuleta usawa wa kijinsia katika uongozi kwa kuongeza nafasi za wanawake katika uongozi,kwa kiasi fulani ameweza kutekeleza ahadi hii na mifano ya hili ipo wazi kwani ameweza kuteua wanawake zaidi kuwa majaji wa Mahakama Kuu na Rufaa,wanawake 12 amewateua kuingia kwenye Baraza la Mawaziri, idadi ya wakuu wawilaya na wakuu wa mikoa ,wajumbe wa bodi mbalimbali imeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma na awamu zilizopita.

Ahadi yake nyingine ya kutoa ajira kwa vijana na maisha bora ,pamoja na jitihada alizozifanya hazijaweza kuzaa matunda yakutosha kwani hadi leo vijana wasiyo na ajira ni wengi na watanzania kwa ujumla hawawezi kuyaona maisha bora.

Kuhusu Ilani ya Chama chake, katika Ilani hiyo moja wapo ya mambo mazito ambayo CCM iliaidi yangeshughulikiwa na Kikwete, ni uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi;hadi hivi sasa ahadi hii imekuwa ni kaa la moto kwa rais wetu maana alijipatiwa ufumbuzi kama Ilani ya chama tawala ilivyotamka.

Na hadi hivi sasa ahadi hiyo inaedelea kuleta mtafaruku miongoni mwetu. Wakati baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wanaendelea kudai kwa nguvu wanataka mahakama ya Kadhi sasa na siyo kesho, Wakristo kupitia kwa viongozi wao wa kidini,hawataielewa serikali endapo itaridhia uanzishwaji wa mahakama hiyo.

(Hata hivyo ni maaskofu hawa hawa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 kupamba moto ,walibariki Ilani ya CCM na kusema Kikwete ni chaguo la mungu).

Hata hivyo nitakuwa sijatenda haki kama sitatoa pongezi kwamba katika utawala wake uhuru wa habari,uhuru wa wananchi kariba mbalimbali kutoa maoni yao bila kubughudhiwa unaendelea kukua kwa kasi ukilinganisha na tawala zilizopita.Tunamuomba mungu rais Kikwete aendelee kuwa na moyo huu wa kuwa mstahimilivu anapokosolewa.Licha kuna baadhi ya watendaji wake wachache ambao hawataki kubadilika wamekuwa wakijitahidi bila mafanikio kuzuia uhuru huo wa kutoa maoni.

Kuhusu tathimini yangu ya tano;kipindi cha uongozi wa Kikwete hali ya utulivu wa ndani umeteteleka na ishara ya kuteteleka kwake ni ongezeko la migomo watu wa kariba mbalimbali wakiwemo baadhi ya watumishi wa serikali,wanavyuo,madaktari , walimu kuiburuza mahakamani serikali na hata wanafunzi wa shule za msingi waliandamana kupinga ongezeko la nauli na mahabusu kugomea kula na kwenda mahakamani kusikiliza kesi zao.

Hii hali ya mitafaruku siyo ishara njema kwa taifa kwasababu inaweza kusababisha kujengeka kwa utamaduni mpya kwamba haki haipatikani hapa nchini hadi watu wagome.Huu ni udhaifu mwingine wa serikali hii kwamba watendaji wake hawapo tayari kutimiza wajibu wao mpaka washinikizwe kwa migomo na kubebewa mabango na kufungiwa maofisini.

Aidha kuhusu uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine; pengine rais katika kipindi hiki ameweza kuongeza uhusiano mwema na mataifa kwa manufaa ya taifa letu ingawa utaratibu alioutumia una lalamikiwa na wengi kwamba ni rais aliyevunja rekodi ya marais waliopata kuliongoza taifa hili aliyedhuru nchi za nje kwa muda mfupi mno hadi akapachikwa jina la msafiri maarufu wa karne ya 15 “Vasco Da Gamma’.

Watanzania tungependa kuona rais wetu akitulia ofisini au nchini na kushughulikia matatizo yanayowahusu wananchi moja kwa moja.

Pengine tukio jingine kubwa la kijamii linaloendelea katika utawala wa rais Kikwete ni ongezeko la vitendo na imani za kishirikina hususani mauaji ya wenzetu wenye ulemavu wa ngozi Albino.

Mauaji haya yamedhibitika kuwa na uhusiano wa watu kadhaa wanaotaka mali na utajiri wa chapchap.Tathimini ya utendaji wa serikali yake pia inaweza kufanywa kwa kuangalia ni jinsi gani imelishughulikia jambo hili la kikatili.

Ni wazi kwamba jitihada zilizofanywa hadi sasa hazijaweza kuikomesha aibu hii ya nchi ambayo pia inakwenda sambamba na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Laiti serikali ingekuwa na nguvu thabiti pengine ingeweza kuwaakikishia mara moja Albino wote nchini usalama wa maisha yao kwa kutengeza mpango wa dharula wa kuwalinda wenzetu hawa na siyo kuishia kulizungumzia suala hili majukwaani na kusubiri Albino wengine wauwawe ndipo Jeshi la Polisi lingilie kati.

Hivyo basi rais Kikwete hana budi kukaa pamoja na wasaidizi wake ili wayabaini mapungufu katika utendaji wao na kuyarekebisha mara moja kwa maslahi ya taifa letu.Akumbuke pia kwamba kadri utendaji wa serikali yake utakavyoendelea kutowaridhisha Watanzania ndivyo wananchi watakavyopoteza imani naye na pengine watafikia hatua yakunyima ridhaa ya kuwaongoza wananchi katika kipindi kijacho.

Tunampongeza rais wetu katika yale yote ambayo ameweza kuyatekeleza yenye alama za kuonekana na yasiyoonekana kwa Watanzania walio wengi ambao wapo nje ya mfumo wa utendaji wa serikali ya awamu ya nne.Mwisho nawatakieni wasomaji wote sikuu njema ya Christmas na Mwaka mpya.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Desemba 24 mwaka 2008




No comments:

Powered by Blogger.