Header Ads

ZAMU YA MGONJA KEKO

*Apanda kizimbani kwa mashtaka manane
*Akabiliwa na tuhuma za Mramba na Yona
*Mtuhumiwa wa 21 EPA apanda kizimbani

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi ambaye yuko kwenye likizo ya kustaafu, Gray Mgonja, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka manane ya matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia taifa hasara ya sh. 11,752,350,148
Mgonja, alifikishwa mahakamani hapo jana majira ya saa 7:20 mchana, chini ya ulinzi mkali wa makachero wa polisi, waliokuwa wakiongozwa na Msaidizi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kati, Inspekta Gewe Ninga.
Mgonja ambaye aliwahi kutajwa na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (Chadema), kwenye orodha ya watu 11 wanaodaiwa kuhusishwa na tuhuma za ufisadi, alitinga mahakamani hapo kwa gari aina ya Toyota, Rav 4, yenye namba za usajili T123 ATW kuingizwa moja kwa moja kwenye mahabusu ya mahakama hiyo.
Kabla ya kufikishwa kwa Mgonja mahakamani hapo, makachero wa polisi, wale wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), askari wa Kikosi cha Mbwa cha Kilwa Road, walikuwa wametanda kila pembe ya mahalama kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kuwa tayari kukabiliana na hali yoyote ya vurugu kama ingelitokea.
Ulinzi huo uliimarishwa ili kuzuia kile kilichowahi kutokea wakati Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba, na Waziri wa Nishati na Madini Serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, walipofikishwa mahakamani hapo Novemba 25 mwaka huu, wakikabiliwa na mashtaka kama ya Mgonja.
Ilipofika majira ya saa 7:52, Mgonja aliingizwa kwenye ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo, tayari kwa kusomewa mashtaka yake.
Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, ambaye alikuwa akisaidiana na mwanasheria wa Takukuru, Joseph Ole, mbele ya hakimu Henzron Mwankenja, alidai kuwa, mshtakiwa huyo, anakabiliwa na mashtaka manane ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisabababishia serikali ya Jamhuri ya Muungano hasara ya sh 11,752,350,148.
Manyanda alidai kuwa Oktoba 10 mwaka 2003, katika ofisi ya Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa mtumishi wa serikali na wadhifa wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuipatia msamaha wa kodi kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers), Government Bussiness Corporation, kinyume na maelekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA).
Alidai kuwa kati Desemba 18-19 mwaka 2003, katika wizara hiyo na wadhifa huo, mtuhumiwa alitumia madaraka ya ofisi ya umma vibaya kwa kutoa notisi ya serikali yenye namba 423 ya mwaka 2003 ya kusamehe kodi kampuni hiyo ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation, kinyume na mapendekezo ya TRA ambayo yalikataza kampuni hiyo isipewe msamaha wa kodi.
Katika shitaka la tatu, alidai kuwa, Desemba 19 mwaka 2003, mshitakiwa huyo akiwa na wadhifa huo, alitoa notisi ya serikali yenye namba 424 ya mwaka 2003 ambayo ilitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, kinyume na TRA.
Aidha alidai kuwa, katika shtaka la nne, Oktoba 15 mwaka 2004, alitoa notisi ya serikali yenye namba 497 ya mwaka 2004 kwa kampuni hiyo na katika shtaka la tano, wakili Manyanda alidai kuwa, Oktoba 14-15 mwaka 2004, akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, alitoa alitoa notisi ya serikali yenye namba 4198 cha 2004 ya kusamehe kodi kampuni hiyo.
Aliendelea kudai kuwa, Novemba 15 mwaka 2005, mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma, alitoa notisi ya serikali yenye namba 377 ya mwaka 2005, iliyotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, kinyume na mapendekezo ya TRA.
Mwanasheria wa Takukuru, Joseph Ole, ambaye alisoma maelezo ya shtaka la saba na nane, alidai kuwa Novemba 15 mwaka 2005, katika Wizara ya Fedha, mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alitoa notisi ya serikali namba 378, yenye kuisamehe kodi kampuni hiyo hiyo.
Aidha katika shtaka la nane, Ole alidai kwamba kati ya mwaka 2003-2007, katika Wizara ya Fedha, mshitakiwa huyo akiwa mwajiriwa wa serikali, kwa makusudi au kwa kushindwa kuchukua tahadhari katika utendaji wake, aliidhinisha notisi za serikali namba 423/2003 na 424/2003, 497/2004 na 498/2004, 377/2005 na 378/2005 ya kuisamehe kodi kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation na kuisababishia serikali hasara ya jumla ya sh 11,752,350,148.
Hata hivyo upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.
Mshtakiwa huyo ambaye anatetewa na jopo la mawakili wa kujitegemea, Profesa Leonard Shaidi, Dk. Alex Nguluwe, Pius Kisarika na Silvanus Mlola, alikana mashtaka yote.
Kiongozi wa jopo hilo la mawakili wa Mgonja, Profesa Shaidi, alidai mahakamani hapo kuwa kesi ya mteja wake inafanana na kesi ya jinai namba 1,200 ya mwaka huu, inayomkabili Mramba na Yona, hivyo anaomba masharti ya dhamana yaliyotolewa kwa washtakiwa hao yatolewe kwa mteja wake (Mgonja).
Hata hivyo Hakimu Mwankenja alimuuliza swali wakili wa serikali Manyanda kwa nini Mgonja asingeunganishwa katika kesi ya Mramba na Yona kwa sababu mashtaka anayokabiliwa nayo, yanafanana na yanayowakabili mawaziri hao wastaafu.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Manyanda alidai kuwa upelelezi wa kesi ya Mramba na Yona haujakamilika na endapo utakamilika, wanaweza kuunganishwa kwenye kesi moja itakayojumuisha washtakiwa wote watatu.
Baada ya kusikiliza hoja za pande hizo mbili, Hakimu Mwankenja, aliahirisha kesi hiyo kwa dakika 15 ili aende akaandike uamuzi wa dhamana na alirejea mahakamani hapo majira ya saa 8:52.
Hakimu huyo, alisema kuwa dhamana kwa mshtakiwa huyo ipo wazi na anatakiwa adhaminiwe kwa fedha taslimu sh bilioni 5.9 au hati ya mali yenye thamani hiyo.
Mwankenja alisema amefikia uamuzi wa kumtaka mshtakiwa apate dhamana kwa kiasi hicho cha sh bilioni 5.9 kwa sababu yupo peke yake kwenye kesi hiyo na kuongeza kwamba, endapo kesi ya kina Mramba na Yona ikivunjwa na kuundwa kesi moja, dhamana hiyo itapungua.
Katika sharti la pili alimtaka mshtakiwa kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi aombe kibali cha mahakama na kwamba awe na wadhamini wawili wa kuaminika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo walijitokeza wadhamini wawili waliojitambulishwa kwa majina ya Ramadhani Mlinga na Devina Mlaki ambao walidai kwamba wanafanya kazi pamoja na mshtakiwa.
Hata hivyo Mgonja alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo kufanya apelekwe rumande katika Gereza la Keko ; aliondoka mahakamani hapo majira ya saa 10:08, huku akiwa amepandishwa kwenye gari alilokuja nalo asubuhi.
Katika safari ya Keko, Mgonja alisindikizwa na Land Rover Defender mbili za polisi, zenye namba za usajili T220 AMV na PT 0940 ambalo lilikuwa limebeba mbwa watatu, ikiwa ni mara ya kwanza kuletwa tangu kuanza kwa kesi zinazohusiana na tuhuma za ufisadi.
Mngonja anakuwa kiongozi wa tatu mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kufikishwa mahakamani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Wakati huo huo mshitakiwa mwingine wa kesi ya wizi wa EPA, Mfanyabiashara, Jonathas Munisi alifikishwa mahakamani hapo jana, akikabiliwa na mashtaka ya wizi na kujipatia ingizo kwenye akaunti lenye thamani ya sh bilioni 2.6, mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mwanasheria Kiongozi wa Serikali, Staslaus Boniface, alidai mbele ya hakimu, Addy Lyamuya kwamba, Julai 25 mwaka 2005, mshtakiwa huyo alijipatia ingizo la kiasi hicho cha fedha kwa madai kwamba Kampuni ya Njake Enterprises, ilipewa kibali cha kurithi deni la Kampuni ya Elton ya Japan. Hata hivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo.
Lyamuya alisema ili mshtakiwa apate dhamana, lazima atoe nusu ya fedha anazotuhumiwa kuiba, yaani sh bilioni 1.3 au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani sawa na kiasi hicho, sharti ambalo alishindwa kulitimiza, kesi hiyo kuahirishwa hadi Desemba 30 mwaka huu.
Kufikishwa kwa mtuhumiwa huyo kunafanya idadi ya watuhumiwa wa wizi wa EPA, kufikia 21.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Jumanne ya Desemba 16 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.