Header Ads

TUNASUBIRI MAAFA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ina umaarufu wa pekee nchini. Ina sifa nzuri na mbaya ambazo mara kadhaa zimeripotiwa katika vyombo vya habari.
Baadhi ya hukumu zilizowahi kutolewa na mahakama hiyo dhidi ya viongozi wa taasisi mbalimbali au watu maarufu kwenye jamii yetu, ni moja ya sababu zinazoipa umaarufu mkubwa mahakama hiyo.
Ushahidi wa hili ni hukumu za kwenda jela za watu wa aina ya Rafiki Baghdad, mfanyabiashara maarufu, aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Aden Rage, Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mlandizi, Sixtus Kimaro, mwanamuziki Babu Seya na wanawe na kadhalika.
Ni katika mahakama hii ambako kesi ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi katika serikali ya Awamu ya Tatu, Nalaila Kiula, kesi ya wanajeshi wawili wa Uingereza waliokuwa wakituhumiwa kumbaka msichana Mtanzania baharini hadi kufa, zilizosikilizwa.
Ni Kisutu hapo hapo ambako kesi zinazowakabili vigogo za wizi wa mabilioni ya fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili mawaziri mawili waandamizi wa serikali ya Awamu ya Tatu - Basil Mramba na Daniel Yona - zinapoendeshwa.
Mlolongo wa matukio yanayoijengea umaarufu wa pekee mahakama hii ni mrefu, ikiwa ni pamoja na kesi ya mauaji ya watu wanne inayomkabili aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe.
Na kama alivyoahidi Mkuregenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP), Eliezer Feleshi, kuwa bado anashughulikia mafaili ya watuhumiwa wa EPA, haina shaka akikamilisha kazi hiyo tunazidi kushuhudia watuhumiwa zaidi wakiwamo vigogo wakifishwa mahakamani hapo.
Zaidi ni kwamba inasifika kwa utoaji hukumu kwa umakini katika baadhi ya kesi ambazo hazina umaarufu, hususan kesi za mirathi na migogoro ya ndoa, ingawa baadhi ya hukumu zimekuwa zikitenguliwa na Mahakama Kuu.
Lakini pia mahakama hii ina sifa mbaya ikiwa ni pamoja na tuhuma za watumishi wake kugubikwa na rushwa, uchafu wa vyoo, uchakavu wa majengo ya mahakama hiyo, ucheleweshwaji wa kutoa maamuzi katika mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani hapo, usalama hafifu na mahakama hiyo kukosa uzio unaoleweka.
Baada ya kuainisha sifa za Mahakama ya Kisutu, nieleze sasa lengo la makala hii. Lengo la makala hii ni kujulisha mamlaka husika changamoto zinazoikabili mahakama hii na mahakama zetu nyingine.
Kwa waandishi wa habari za mahakama mimi ambao sehemu kubwa ya saa za kazi huzitumia tukiwa mahakamani, sina shaka tutakubaliana kwamba chumba Namba 2 cha Mahakama ya Kisutu kina hewa chafu ya mikojo inayotokea katika baadhi ya vyoo vya mahakama hiyo, hali inayosababisha wananchi wanaohudhuria kesi mbalimbali katika chumba hicho kupata usumbufu mkubwa.
Chumba hiki ni doa kwa mahakamani hii, mapangaboi yake ni machakafu, paa lake limevamiwa na ndege walioligeuza kuwa maskani yao, lakini ni ndani ya chumba hicho hicho ambao utakuwata mawakili na waendesha mashitaka, wasomi waliovalia nadhifu, bila kuwasahau waandishi wa habari wakifanya shughuli zao.
Usalama mahakamani hapo nao hauridhishi ingawa kwa kipindi cha hivi karibuni Jeshi la Polisi limejitahidi kumwaga makachero wake katika mahakama hiyo, baada ya kesi za EPA na ukiukwaji wa maadili kuanza kusikilizwa.
Kazi kubwa wanayoifanya makachero hawa ni kunusanusa huku na kule kinachosemwa na kinachotokea wakati kesi hizi zikisikilizwa. Hawa hawako kwa ajili ya kuweka ulinzi wa kudumu.
Ukifika mahakamani hapo utashuhudia ulinzi wa kizamani, watu wa aina tofauti wanaingia na kutoka pasipo kuulizwa wala kupekuliwa. Kwa mtu mwenye kufikiri vizuri, hali hiyo itampa picha ya hatari hasa kwa jinsi mahakama hiyo ilivyo na wateja wengi wakubwa na maarufu ambao ni lazima wana maadui ambao si ajabu siku moja wakaamua kuwadhuru hadharani.
Ushahidi wa hili ni tukio la hivi karibuni la wananchi kuwazonga na kuwazomea Mramba na Yona wakati wakiondoka mahakamani hapo, baada ya kupewa dhamana. Kwa jinsi hali ilivyokuwa, kama kuna kikundi cha watu waliokuwa wamedhamiria kuwadhuru watu hao wangeweza kufanikisha dhamira yao kirahisi.
Hii ndiyo hali halisi, tukifikiria sababu ya wananchi kufanya mahakamani kitendo ambacho hakiruhusiwi kikatiba kwa sababu Yona na Mramba ni watuhumiwa tu, hawajatiwa hatiani na mahakama. Hivyo, kwa wananchi kufikia hatua ya kuwazonga kiasi kile ni wazi kwamba uwezo wa kudhurika kwao (Mramba na Yona) ni mkubwa kwa sababu moja tu, uvumilivu wao umefikia kikomo.
Hapa nieleweke kuwa sitetei watuhumiwa au wahalifu, ninazungumzia sheria tulizojiwekea na tukakubali kuzitii. Kama Mramba na Yona wangechanwa hata na wembe katika mshikemshike huo, halafu baadaye mahakama ikaja kuwaona hawana hatia au DPP akaamua kutumia kifungu cha 91 sura ya 20 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kuondoa kesi zao mahakamani, ingekuwaje?
Mbali na tukio hilo, matukio ya watuhumiwa kutoroka wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, baada ya kujipaka kinyesi au lile la mwaka jana lililotokea mahakamani hapo la mtuhumiwa mmoja wa kesi za wizi wa kutumia silaha katika benki za NMB, NBC na katika duka la kubadilisha fedha la Namanga, kujirusha kutoka ghorofani, yanaonyesha umuhimu wa kuimarisha ulinzi mahakamani hapo.
Kinachohitajika kwa serikali ni kuhakikisha inaongeza bajeti ya mahakama ya Tanzania ili iweze chombo hicho kiweze kufanya kazi katika mazingira yanayokubalika. Serikali inapaswa kuachana na kasumba ya kupeleka fedha nyingi katika masuala ya kisiasa kuliko mahakama na sekta nyingine muhimu.
Hii iwe changamoto kwa serikali, ilichukulie hili kama jambo la dharura kwa sababu ni wazi kuwa uwezo wa kuboresha mahakama zetu upo. Nasema upo kwa sababu sijawahi kusikia vikao vya Bunge au semina elekezi kwa makatibu wa kuu wa wizara, mawaziri na wakuu wa mikoa vinashindwa kufanyika kwa sababu ya uhaba wa fedha.
Lakini ni jambo la kawaida kwa Mahakama Kuu kuendesha vikao vichache au kesi chache kwa sababu ya uhaba wa fedha. Tatizo la msongamano wa mahabusu magerezani, linachangiwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa fedha, wakati Watanzania wanashuhudia kila kukicha ongozeko la magari ya kifahari yakitolewa kwa viongozi.
Serikali ina kila sababu ya kufanya jitihada za makusudi kama ilizofanya katika kuboresha maslahi ya vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Desemba 17 mwaka 2008

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Uchambuzi mwanana Da Happy. Asante sana kwa changamoto na uelimishaji huu

Powered by Blogger.