MFAHAMU KWA UNDANI JAJI AUGUSTINO RAMADHAN
HONGERA JAJI AUGUSTINO RAMADHAN
Na Happiness Katabazi
JUNI 17 Mwaka 2015 ,Jaji wa Mahakama ya Afrika Ya Haki za Binadamu ,Agustino Ramadhani alichukua fomu ya Kugombea nafasi ya rais kupitia Chama cha Mapinduzi .
SEPTEMBA 9 mwaka 2014, vyombo habari nchini vilichapisha habari kuwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imemteua Jaji mkuu mstaafu wa Tanzania Agustino Ramadhan kuwa rais wa mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka miwili uteuzi na kwamba uteuzi huo unaanza mara moja baada ya aliyekuwa rais wa mahakama hiyo Sophia Akuffo wa Ghana kumaliza muda wake.
Jaji Ramadhani Mtanzania wa kwanza kushikilia kiti hicho tangia kuanzishwa kwa mahakama hiyo baada ya kupata kura 7 kwa kura nne dhidi ya mpinzania wake katika nafasi hiyo ya rais wa mahakama hiyo huku nafasi ya makamu wake ikichukuliwa na jaji Eisie Thompson kutoka nchi ya Nigeria.
Katika nafasi hiyo ya makamu walikuwepo majaji watatu waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na baada ya upigaji wa kura mara ya kwanza wawili walifungana kwa kura 4 na mmoja kupata kura tatu ndipo uchaguzi ulirudiwa na jaji Thompson kuibuka mshindi kwa kupata kura 6 dhidi ya tano za mpinzani wake.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya uteuzi huo jaji Ramadhan alisema kuwa ni heshima kwa Taifa la Tanzania kwani ndio mara yake ya kwanza kupata nafasi hiyo huku akisema kuwa nafasi hiyo ni heshima kwake na kwa taifa lake.
“Kesi yeyote inayohusu nchi yangu mimi sitakuwepo kutokana na sheria zetu za mahakama hii na kuwa tayari watanzania watano wamefungua kesi kwenye mahakama hii na kesi mbili zimetolewa hukumu ya mchungaji mtikila na Zongo”alisema jaji Ramadhan
Alisema kuwa mpaka sasa ni kesi tano zimefunguliwa katika mahakama hiyo na mbili teyari zimetolewa ikiwemo dhidi ya serekali ya Tanzania kesi iliyofunguliwa na mchungaji Christopher Mtikila iliyohusu mgombea Binafsi huku akisema kuwa kuchukuwa hatua kwa utekelezaji wa hukumu kunategemea na serekali kama imejiunga na mikataba ya kimataifa.
Jaji Agustino alisema kutokana na sheria za mahakama hiyo wakati wa usikilizaji wa kesi zinazoihusu Tanzania yeye hawezi kuisikiliza na kuwa atajitoa kuisikiliza kama Sheria inavyomtaka Kuwa huwezi Kuwa Jaji Katika Kesi inayokuhusu na Kusema Kuwa Mahakama hiyo inaundwa na majaji 11 kutoka nchi tofauti za bara hili .
Aidha mahakama hiyo iliwaapisha majaji watatu wa mahakama hiyo kabla ya kuanza mchakato wa upigaji kura kumteuwa jaji wa mahakama hiyo huku ripoti ya mahakama hiyo kila mwaka ikipelekwa kwa Umoja wa Nchi za Afrika.
Uchaguzi huo huwa ni vipindi vya miaka miwili miwili na iwapo ukimaliza muhula wa kwanza kama utateuliwa tena kushika nafasi hiyo utakuwa ndio kipindi chako ya mwisho kushikilia nafasi hiyo.
Binafsi Nampongeza Mzee wangu Jaji Ramadhan kwa kushinda nafasi hiyo ambayo ushindi huo ni Tanzania pia Kwani ushindi huo umeandika historia mpya wa Tanzania Kwa Mtanzania Huyo Ramadhan kuwa Mtanzania wa kwanza kushika wadhifa huo.
Nilipokuwa Mwandishi wa Habari za mahakamani nimekuwa nikiripoti Kesi mbalimbali ikiwemo baadhi ya Kesi zilizokuwa zikisikilizwa na Jaji Ramadhan ikiwemo Kesi yakihistoria ya Rufaa iliyokuwa imekatwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mchungaji Christophe Mtikila , ambapo jopo la Majaji Saba wa Mahakama ya Rufaa iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Ramadhan ambapo mwisho wa siku jopo Hilo lilikubaliama na hoja za Mwomba rufaa (AG) Aliyekuwa akiwasilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali George Masaju, Kuzuia kuwepo Kwa mgombea binafsi.
Katika Utawala wa Jaji Ramadhan wa Ujaji Mkuu na ' mpiganaji wake' Msajili wa Mahakama ya Rufaa alikuwa ni Jaji Francis Mutungi ambaye Kwasasa ni Msajili wa Vya Vya Siasa nchini, binafsi nilikuwa nikifanya nao Kazi Kwa karibu na alikuwa wakinipa ushirikiano wa kikazi na nasaha mbalimbali.
Jaji Ramadhan ana vitu viwili ambavyo navipenda sana kutoka kwake .Moja ,Ramadhan ni mtu anayependa Kusema ukweli na ukweli huo upenda kuweka adharani.
Pili; Jaji Ramadhan ni miongoni mwa Majaji wakuu wachache ambao ni nimewaona ambao wanaingilika kirahisi pindi mwanahabari unapotaka kufanya mahojiano naye kuhusu mambo mbalimbali na ushahidi wa Hilo ni hizo makala zangu mbili niliyofanya nae mahojiano wakati alipoteuliwa Kuwa Jaji Mkuu na alipostaafu wadhifa huo.
Hivyo nakuombea Afya njema ,Mungu akutangulie Katika wadhifa wako huo mpya wa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, Kwani ni Miezi michache tu ulimaliza kutumikia wadhifa wako wa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba
Chanzo: Facebook: Happy Katabazi
Blog: www.katabazihappy.blogspot.com
0716 774494
Septemba 10 Mwaka 2014
(Makala hiyo hapo chini , nilifanya mahojiano na Jaji Ramadhan muda mfupi baada ya kustaafu Utumishi wa umma kwa mujibu wa Sheria)
DISEMBA 2013
JAJI RAMADHANI AWA MCHUNGAJI
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani ametawazwa kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi Zanzibar.
JAJI RAMADHANI AWA MAKAMU MWENYEKITI TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
APRILI 7 Mwaka 2012, Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo alikuwa Jaji Augustino Ramadhani.
AUGUSTINO RAMADHAN: KESI YA MGOMBEA BINAFSI SITAISAHAU
Na Happiness Katabazi
“KESHOKUTWA,yaani Desemba 28 Mwaka 2010 nitakuwa nikikumbuka siku yangu ya kuzaliwa na nitakuwa ninatimiza umri wa miaka 65, siku hiyo pia itakuwa ya kihistoria kwangu kwani ndiyo nitakuwa nastaafu kazi ya utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Nchi.”
Hii ni nukuu ya maneno ya Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan, alipoanza kuzungumza na jahazi Jumapili kuhusu maisha yake na kazi
Anasema kuwa katika kipindi chote cha utawala wake amefanya kazi kwa ushirikino mkubwa na watendaji wa serikali pamoja na wale wa mahakama.
Anabinisha kuwa anajivunia kuwa katika uongozi wake aliheshimu sheria na Katiba na hata watendaji wenzake kwa kiasi kikubwa walijitahidi kufuata mambo hayo Yafuatayo ni mahojiano ya Jaji Ramadhani na Jahazi Jumapili.
Swali: Ulijisikiaje wakati ukiteuliwa kuwa jaji mkuu mwaka 2007 na changamoto zipi ulizozikuta?
Jibu: Nilifarijika kuteuliwa kushika wadhifa huo wa kuongoza mhimili wa mahakama kwa sababu ni nadra kupata nafasi kuu kama hii.
Changamoto kubwa niliyoikuta ni uhaba wa watendaji, ambapo majaji wa Mahakama Kuu na Rufaa kwa wakati huo walikuwa 11 na hivi sasa tuko 16.
Katika Mahakama Kuu, Rais Kikwete, aliteua majaji 30 kuanzia mwaka 2008 hadi sasa ambapo ni wastani wa majaji 10 kila mwaka.
Mahakimu wa mahakama za mwanzo wapatao 100 wameajiriwa kuongoza mahakama hizo jambo ambalo kwa kiasi fulani limeharakisha usikilizaji wa kesi.
Hivi sasa Mahakama Kuu ina Kanda 13 na kanda hizo zina majaji wawili wawili isipokuwa Kanda ya Tabora, Mwanza majaji wanne, Arusha watatu.
Changamoto nyingine ni uhaba wa vitendea kazi na teknolojia za kizamani za kurekodi mashauri lakini nashukuru Desemba 6 mwaka huu, tulizindua mfumo wa kidigitali wa kurekodia mwenendo wa kesi pamoja na tovuti ya mahakama.
Teknolojia hiyo ya kidijitali imeishafungwa inatumika kwenye Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na vitengo vyake vya Kazi, Ardhi na Biashara.
Swali: Ushirikiano wa mahakama na mhimili mingine ulikuwaje Jibu: Kimsingi wakati nikiingia mambo yalikuwa si mazuri, watendaji wa mahakama tulikuwa tukilalamikiwa na wabunge, wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa serikali.
Jibu: Tatizo hilo nililitatua kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na Rais Jakaya Kikwete pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kwenye shehere zetu mbalimbali.
Nami pia nilikuwa nikihudhuria sherehe za kiserikali pamoja na vikao vya Bunge hasa vile vya bajeti.
Kupitia ushirikiano huo mpya tuliweza kuhabarishana changamoto zinazotukabili na namna ya kuzitatua kulingana na uwezo tuliokuwa nao.
Swali: Kwa nini mahakama huchelewesha usikilizaji wa kesi?
Jibu: Kuna aina mbili za ucheweshwaji wa kesi, mosi mahakama pili ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ofisi ya Mwanasheria, polisi na mawakili wa kujitegemea.
Wakati mwingine hakimu au jaji anakuwa yuko tayari kusikiliza kesi lakini upande wa mashtaka unadai haujakamilisha upelelezi au unashindwa kuleta mashahidi kwa wakati.
Sababu nyingine ni baadhi ya mawakili wa kujitegemea wanakuwa hawajajiandaa kuendesha kesi husika sasa kwa sababu hizo ndiyo maana kesi zinashindwa kumalizika mapema.
Wananchi wengi hawatambui mchakato wa uendeshaji wa kesi ndiyo maana mwisho wa siku huishia kuitupia lawama mahakama kuwa inachelewesha kesi.
Lakini pia mhimili wa mahakama umeweza kusimamia sheria na Katiba. Pia mfumo wenyewe na baadhi ya sheria kwani tumeweza kubadilisha kanuni za uendeshaji wa kesi za Mahakama ya Rufani.
Kanuni za awali zilizotungwa mwaka 1979 zikafutwa na kanuni hizo mpya zilizopitishwa mwaka 2009 zimeanza kutumika Februari mwaka huu.
Swali: Wazee wa baraza wa mahakama wamekuwa wakilalamika kutolipwa posho kwa nini hali hiyo inajitokeza?
Jibu: Ni kweli kulikuwa na malalamiko hayo na wazee wa baraza walikuwa wanapata posho ya sh 1,500. Ila kuanzia Julai mwaka huu posho yao imeongezeka wanapata posho ya sh 5,000.
Wakati mwingine wazee hao walikuwa wanakopwa na mahakama wanakwenda kusikiliza kesi, hili lilikuwa linasababishwa na ufinyu wa bajeti ya mahakama.
Swali: una maana gani unaposema uongozi wako mahakama ilizingatia sheria na Katiba?
Jibu: Aah! Namaanisha kwamba mahakama imeangalia Katiba kwa mtizamo mpya unaopaswa uwe, ibara za Katiba zinazohusu majaji na ajira zao.
Huko nyuma majaji wa mahakama kuu walikuwa wanastaafu kwa mujibu wa sheria wakiwa na umri wa miaka 60 na wale wa mahakama ya rufaa miaka 65, halafu wanapewa mafao yao na kisha wanaweza kurejeshwa kufanya kazi hiyo kwa mkataba.
Hivi sasa hivi Rais wa nchi anaweza kuongeza umri wa kustaafu wa jaji anayekaribia kustaafu, Mfano Jaji wa Mahakama Kuu ana miaka 59;
Rais anaruhusiwa kumuongezea hata miaka mitatu mbele ya utumishi kabla ya umri wa miaka 60 kustaafu na akishastaafu katika umri huo alioongezewa na rais ndiyo anatapewa mafao yake yote.
Swali: Serikali imefanya jambo gani kwa mahakama mbalo utalikumbuka?
Jibu: Kubwa zaidi ni kukubali ombi letu la kutaka tuwe na mfuko wa mahakama ambao tunaamini utatusaidia kutatua matatizo yetu yanayokwamishwa na uhaba wa fedha.
Kilio chetu kikubwa kilikuwa ni kuiomba serikali ituwekee angalau asilimia mbili ya bajeti ya seriakli katika mfuko huo, sasa hivi mahakama inapewa asilimia 0.4 ya bajeti ya serikali.
Kiwango hiki ni kidogo sana kwani hata mikoa ya Lindi na Mtwara bajeti yake ni kubwa kuliko bajeti ya mahakama ambayo ina ofisi katika kata, wilaya na mkoa.
Pia naishukuru serikali kwa kutujengea mahakama za mwanzo mbili za kisasa zilizopo Kerege na Lugoba mkoani Pwani ambazo zimezinduliwa mapema wiki hii na ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh milioni 600.
Swali: Kipi unajivunia katika utawala wako?
Jibu: Ni kuanzisha mchakato wa mahakama kupata mfuko wake na ninaamini hadi kufikia Julai mwakani mwakani mfuko huo utapatikana.
Jibu: Ikumbukwe kwamba licha ya kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, mimi ni Jaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu na za watu ya Afrika yenye makao makuu yake jijini Arusha.
Katika mahakama hiyo tuko majaji 11. Ila majaji wa mahakama hiyo hatufanyi kazi muda wote, tunakutana mara nne kwa mwaka na kwa siku 10.
Kwa hiyo nafasi hiyo ya ujaji wa mahakama hiyo ya Afrika nayo itaniwezesha kuniingizia kipato. Pia nitakuwa nikilipwa pesheni za kustaafu na serikali yetu.
Nakusudia kuwa mhadhiri wa sheria (Visiting Lecturer), katika baadhi ya vyuo vikuu na ninakusudia kuandika vitabu.
Swali: Ni kesi gani ulishiriki kuisikiliza na kuitolea maamuzi ambayo hutoisahau?
Jibu: Ni kesi ya Kikatiba ambayo mwanasheria mkuu wa serikali alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa, dhidi ya Mchungaji Christopher Mtikila, kwamba mahakama inaweza kutamka kwamba ibara ya Katiba inaweza kuvunja ibara nyingine ya Katiba?
Nitaikumbuka kesi hiyo kwa sababu ni mara ya kwanza kwa mahakama ya rufani nchini kuketi majaji saba kusikiliza rufaa moja , pia ni mara ya kwanza kwa mahakama ya rufaa kuwaita marafiki wa mahakama-Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramaganda Kabudi.
Alikuwapo pia aliyekuwa mhadhiri mwandamizi wa sheria wa UDSM, marehemu Profesa Jwani Mwaikusa na Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar (DPP), Masoud Othman Masoud.
Sababu hasa inayonifanya niikumbuke kesi hiyo ambayo mimi nilikuwa kiongozi wa jopo hilo la majaji ni muda niliotumia kufanya utafiti na hatimaye tukafikia uamuzi wa kutoa hukumu; kesi ile ambayo wananchi wengi hupenda kuita kesi ya mgombea binafsi.
Ila mimi siiti kesi ya mgombea binafsi bali naiita kesi ya Kikatiba.
Swali: Wosia gani unautoa kwa majaji na mahakimu?
Jibu: Ninawaasa waendelee kuzingatia sheria na Katiba ya nchi katika utendaji wao wa kila siku kwani wakumbuke wao ndiyo kimbilio la wananchi wenye kudhulumiwa au kuminywa haki zao.
Ni vema wakaendelea kuilinda heshima ya mahakama kwa kutoa haki bila upendeleo wowote.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Desemba 26 mwaka 2010
(Makala hii hapa chini ,nilifanya mahojiano na Jaji Ramadhani ikiwa ni siku Chache tu tangu ateuliwe na Rais Kikwete kushika wadhifa wa Jaji Mkuu )
HUYU NDIYE AGUSTINO RAMADHAN: JAJI MKUU MTEULE TANZANIA
Na Happiness Katabazi
Mapema wiki hii Rais Jakaya Kikwete, alimteua aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Augustino Ramadhani (62) kuwa Jaji Mkuu mpya, Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, alifanya mahojiano maalumu na Jaji Mkuu huyo mteule na katika makala hii amezungumzia historia ya maisha yake kwa mapana na masuala mengine mbalimbali yanayohusu Mahakama ambayo ni mhimili mahususi.
Swali: Umepokeaje uteuzi wa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania?
Jibu: Nimepokea uteuzi huu kwa furaha. Na nimechukulia kwamba Rais Kikwete ana imani nami na pia ameridhishwa na utendaji kazi wangu na kabla ameamini kuwa mimi nitaendeleza yaliyofanywa na watangulizi wangu yaani Jaji Augustino Saidi, Jaji Francis Nyalali na Jaji Barnabas Samatta.
Sikutazamia, uteuzi umenijia ghafla. Hivyo nataka nipate muda wa kujipanga ili siku za usoni aliyeniteua asione alichagua mtu asiyestahili kushika wadhifa huu.
Swali: Watanzania wangependa kusikia kauli yako kwamba ni mambo yapi umejipanga kuyafanya katika uongozi wako?
Jibu: Ni mapema mno kusema nimejipanga kuanza kukabiliana na jambo gani maana nafasi hii ni ya kuteuliwa, labda kama nafasi hii ingekuwa ya kisiasa ningeweza kutamka mapema namna hii kwamba nimejipanga kufanya nini.
Sipendi kuwadanganya Watanzania kwamba ooh, nitafanya ili na lile, kwakuwa mimi ni mwanasheria mwandamizi, hivyo leo hii nikurupuke na kusema kitu ambacho sijakifanyia utafiti, nitakuwa nadhalilisha taaluma ya sheria na Mahakama kwa ujumla.
Nitakapoingia ofisi mpya nakuona ofisi hiyo mambo yanaendeshwaje, kuna ‘miba gani’, na kushirikisha wenzangu hapo ninaweza kutoa kauli ya nini tumejipanga kukifanya.
Ila ninachoweza kuwahakikishia wananchi ni kwamba, nimelenga kusimamia mambo matatu. Moja nitahakikisha haki inapatikana haraka iwezekanavyo, maana imekuwa ni tatizo linalolalamikiwa na watu wengi wanapotafuta haki katika vyombo vya sheria.
Nitahakikisha pia haki inapatikana bila rushwa na kwamba nitajipanga na watendaji wenzangu kuona ni jinsi gani tutakabiliana na tatizo hilo.
Pia nitahakikisha haki inapatikana kwa gharama nafuu, maana haki imekuwa ikipatikana kwa gharama kubwa hasa inapokuja gharama za kuwalipa mawakili, lakini nitaweka mipango na wenzangu na kuandaa mazingira ya kupatikana haki kwa gharama nafuu.
Swali: Kuna malalamiko mengi ya ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?
Jibu: Maoni yangu. Si ucheleweshwaji wa kesi za mauaji tu, bali kesi zote zinacheleweshwa. Kwa upande wa kesi za jinai, kuna sababu tatu ninaweza kuzitaja kuwa zinachangia ucheleweshwaji wa kusikiliza, upande wa kwanza ni serikali ambao waendesha mashitaka huwa wanasema upelelezi kwa kesi fulani bado haujakamilika.
Na sisi kama Mahakama ni vigumu kujua ni matatizo gani yanawakabili katika upelelezi, kwa kweli hili ni tatizo kubwa na kila kukicha limekuwa likipigiwa kelele.
Upande wa pili ni mshitakiwa mwenyewe, wakati mwingine unachelewesha kuleta mashahidi mahakamani ila hali hiyo katika upende huu wa mshitakiwa hutokea mara chache mno.
Upande wa tatu ni Mahakama yenyewe, sasa kwenye Mahakama yenyewe kuna mambo ambayo yanasababisha kesi kuchelewa kusikilizwa. Uchache wa vyumba vya kuendeshea kesi na mfano halisi pale Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ina vyumba vinne tu vya kuendeshea kesi, hapa Mahakama ya Rufani ina vyumba viwili vya kuendeshea kesi. Sasa majaji ina wabidi wasubiriane kuendesha kesi na kesi nyingine zinachukua muda mrefu wakati zikiendeshwa.
Jingine linalochangia ucheleweshwaji wa kusikiliza kesi ni uhaba wa majaji na mahakimu, hili ni tatizo na hata kama unao mahakimu na majaji wengi, lakini vyumba vya kuendeshea kesi ni vichache kama ilivyo sasa hapa nchini, bado tatizo kesi kuchelewa kusikilizwa litakuwa pale pale.
Tatizo jingine la ucheleweshwaji ni uhaba wa nyenzo, leo hii hapa majaji na mahakimu kurekodi mienendo ya kesi kwa mkono badala ya kutumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti kama ilivyo kwa mahakama za nje. Kwa hiyo muda mwingi sisi majaji na mahakimu kuandika. Mfano Mahakama ya Afrika Mashariki, majaji wake wanatumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti.
Halafu pia katika hili la nyenzo, kutokuwepo kwa mfumo wa kompyuta ‘computerization’, unakuta jaji anaandika hukumu kwa mkono kisha hukumu hiyo inapelekwa kuchapwa kwa mchapaji sasa unakuta hukumu moja inaandikwa mara mbili.
Kwa hiyo hayo matatizo niliyoyataja hapo juu yanachukua muda mwingi na si siri yanachangia ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi kwa wakati.
Swali: Mahakama yako ina majaji, mahakimu na wataalamu wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?
Jibu: Majaji, mahakimu na watalaamu katika mhimili wa Mahakama hawatoshi na kuna haja waongezwe kwa kuwa uchache wao nao ni sababu moja wapo inayopelekea ucheleweshwaji wa kesi.
Swali: Unazungumziaje madai kwamba kuna mahakimu hawana ujuzi wa kutosha na kwamba mishahara midogo wanayopata inawafanya baadhi yao wajihusishe na vitendo vya rushwa?
Jibu: Wakisema mahakimu hawana uzoefu wa kutosha nitawaelewa, siyo hawana uzoefu, hili nakataa kwakuwa mahakimu wote wamehudhuria kozi katika vyuo husika na kozi zao zinatofautiana kwa muda, kwani mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya kozi zao huwa ni za muda mfupi tofauti na mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi, kwakuwa hao ni wanasheria kamili, ila nasema hivi kinachotakiwa hapa ni kwa mahakimu hao kupenda kujifunza zaidi kila mara bila kuchoka kwa kuwa elimu haina mwisho na mtu au kiongozi yeyote anayependa kujifunza mara kwa mara anapata fursa ya kujua vitu vingi na uzoefu wake unaongezeka na ninatoa changamoto kwa watendaji wote wa mahakama kupenda kujisomea na kuifunza.
Kweli mishahara ni midogo kama ilivyo sekta nyingi nyingine, lakini mishahara kuwa midogo siyo sababu ya mfanyakazi wa Mahakama kuchukua rushwa kwa sababu kuna wanaopata mishahara minono na kila kukicha wanapokea na kudai rushwa. Binafsi yangu nasema hivi rushwa ni urafi wa mtu binafsi.
Swali: Unaridhika na mfumo wa Mahakama ya Tanzania?
Jibu: Hadi sasa mfumo wa Mahakama hapa nchini unaridhisha ila nitahakikisha ninakaa na wenzangu kuona ni jinsi gani tunaweza kuuboresha zaidi.
Swali: Ni tukio gani unalikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?
Jibu: Tukio ambalo sitalisahau lilikuwa ni kule kufiwa na baba yangu mzazi, Mathew Douglas Ramadhani, Machi mosi mwaka 1962, nilikuwa na umri wa mika 15, tukio hili lilinishtua sana na siwezi kulisahau kwa sababu nilikuwa bado mtoto mdogo, nilikuwa nikiwaza nani angenisomeshwa.
Tukio lililonifurahisha ni siku nilipomuoa mke wangu kipenzi Luteni Kanali Saada Mbarouk, ambaye anafanya kazi Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Nilifunga naye ndoa Novemba mosi mwaka 1975.
Swali: Ni kitu gani kilikutuma kujiunga na fani ya sheria?
Jibu: Nilipenda kusoma sheria kwanza pale Tabora Sekondari (Tabora School) nilipokuwa nasoma kuliwa na mwalimu akiitwa Butterworth, alikuwa akitufundisha somo la historia tangu kidato cha kwanza hadi cha sita, yeye alikuwa mwanasheria, sasa huyu vile alivyokuwa anazungumza ni tofauti na walimu wengine kwa namna alivyokuwa anabishana na kuchukulia mambo tofauti na walimu wengine.
Basi tangu hapo alinivutia na zaidi ya hapo marehemu baba yangu alisomea somo la sheria, alichukua shahada ya BA na moja ya masomo ya hiyo digrii ilikuwa ni sheria na nyumbani kulikuwa na vitabu vya sheria na katika maktaba ya nyumbani.
Lakini si hivyo tu baba yangu mzaa mama, Masoud Than, alikuwa mkalimani wa mahakama na babu alimlea mama Justine Dodo naye alikuwa mkalimani wa jaji enzi za ukoloni na kutembea naye miji mingi hapa Tanganyika. Sasa haya yote nalazimika kusema yalifanya nipende sheria na hadi nikaenda kuisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Swali: Unafikiri idadi ya wanawake waliobahatika kuchaguliwa kuwa mahakimu na kuteuliwa kuwa majaji wanatosha na kama hawatoshi nini kifanyike?
Jibu: Majaji na mahakimu wanawake hawatoshi na chakufanya Mahakama iwezeshe wanawake ili waweze kufikia vigezo vinavyotakiwa ili siku moja wateuliwe kuwa majaji au wachaguliwe kuwa mahakimu.
Nasema kuwa idadi ya majaji wanawake ni ndogo, kwa mifano hai, mfano mmoja wapo unapatikana hapa Mahakama ya Rufani, mahakama hii ina jumla ya majaji 13 na watatu kati yao ni wanawake waliosalia ni majaji wanaume. Sasa hii ni tofauti kubwa sana.
Hapo awali Mahakama ya Rufaa ilikuwa na jaji mwanamke mmoja tu ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kuwa hakimu hapa nchini anaitwa Eusebio Mnuo, na Rais Jakaya Kikwete alivyoingia madarakani akateua majaji wawili katika mahakama hii nao ni Jaji Natalia Kimaro na Engela Kileo.
Swali: Ni changamoto zipi zinaikabili Mahakama ya Tanzania?
Jibu: Changamoto ni nyingi, moja ya changamoto kubwa inayotukabili ni kutoa haki zote katika mashauri ya jinai na madai haraka, kupiga vita rushwa na suala la rushwa nalitazama katika sehemu mbili ya kwanza ni rushwa ya kweli na ya pili rushwa ya kudhaniwa.
Hivyo watendaji wa Mahakama wanatakiwa waweke juhudi kwamba kusiwepo na mazingira ya rushwa ya kweli na ya kudhaniwa. Na changamoto ya tatu inayoikabili mhimili mahususi wa Mahakama ni kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wengi kwakuwa haki ina gharimu hasa inapokuja suala la mawakili, sasa tuhakikishe haki inapatikana kwa wote wenye madai yao mahakamani.
Swali: Hivi sasa kuna mchakato wa waumini na taasisi ya dini ya Kiislamu wanataka irejeshwe Mahakama ya Kadhi, nini msimamo wako na kama ikija itakaaje katika mtiririko wa mahakama?
Jibu: Kwa kweli kuhusu hili la Mahakama ya Kadhi siwezi kulizungumzia kwakuwa ninavyofahamu mimi suala hili lipo kwenye mchakato katika ngazi husika hata hivyo sina taarifa rasmi kama utekelezaji wa suala hilo umefikia wapi, hivyo binafsi siwezi kuzungumzia jambo kama sina taarifa za uhakika.
Swali: Huoni wakati umefika wa shughuli za Mahakama ya Tanzania kuendeshwa kwa Kiswahili ili wananchi waridhike na maamuzi yanayotolewa, kwakuwa hivi sasa mahakama zinaendeshwa kwa lugha ya Kiingereza na wananchi wengi wanaona hawatendewi haki na hasa unapofikwa wakati wa mawakili wa pande mbili wanapobishana kisheria wawapo mahakamani?
Jibu: Nakubali kwamba ipo haja ya kuendesha shughuli za mahakama kwa lugha ya Kiswahili. Na kwakweli tayari limefanyika hilo la kuendesha mahakama kwa kutumia lugha ya taifa, sasa hivi mahakama za mwanzo zinaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na sehemu kubwa ya Mahakama za Wilaya.
Lakini hata Mahakama ya Rufani tunaendesha Kiswahili inapobidi kuwa kanuni za Mahakama ya Rufani zinaruhusu kuendesha mashauri kwa Kiswahili au Kiingereza ila kumbukumbu lazima ziandikwe kwa lugha ya Kiingereza.
Na ninaamini ikitumika lugha ya Kiswahili mahakamani itaondoa manung’uniko ya wananchi na itasaidia watu waone haki inavyotendeka.
Swali: Huoni wakati umefika sheria zote za nchi ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili kama ilivyo Katiba ya Tanzania ambayo ndiyo pekee imeandikwa kwa lugha ya taifa?
Jibu: Katika hili siwezi kusema wakati umefika kwa sababu hadi sasa hakuna maneno ya Kiswahili yaliyowekwa katika lugha ya kitaaluma ya sheria (many legal technical terms yet produced) yakipatikana hapo tunaweza kusema wakati umefika sheria za nchi ziandikwe katika lugha ya Kiswahili.
Swali: Wadhifa huu mpya wa ujaji mkuu, huoni kwamba unaweza kukuzuia usiendelee kupiga kinanda kanisani?
Jibu: Kwanza kabisa kupiga kinanda nachukulia kama ibada, yaani kama vile ninavyokuwa na uhuru wa kwenda kusali hivyo ninao uhuru wa kuingia kanisani na kupiga kinanda.
Kwahiyo ieleweke uteuzi huu hautanizuia kupiga kinanda kwani hata nilivyokuwa Jaji Mkuu Zanzibar nilikuwa nahudhuria ibada na kupiga kinanda hata Jumapili ijayo (leo) nitakwenda kanisani St. Albano kusali na kisha nitapiga kinanda kama kawaida.
Enzi nasoma Tabora School ndipo nilipojifunza kupiga kinanda na mwanangu aitwaye Francis ndiye anayeonyesha kufuata nyayo zangu katika upigaji kinanda.
Licha ya kupendelea kupiga kinanda pia napenda kucheza mpira wa kikapu, na nimeanza kucheza mchezo huu tangu nasoma hadi nilivyokuwa ndani ya JWTZ niliupenda sana mchezo huu hadi nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Basketball Association (TABA, sasa BFT baada ya kuwa shirikisho) na mimi na wanamichezo wengine akiwemo Ofisa Habari na ofisa Utamaduni Manispaa ya Kinondoni Iddi Chaulembo, mwaka 1972 tulifufua chama hicho mkoani Iringa kitaifa.
Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana?
Jibu: Nimezaliwa Desemba 28, mwaka 1945 Zanzibar mjini nikiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane, wa kike wanne na wanaume wanne. Ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana.
Nimesoma shule mbalimbali za msingi Mpwapwa mkoani Dodoma 1952 -1953 nikaenda Town School-Tabora nikasoma darasa la tatu hadi la nne mwaka 1954-1956 na darasa la sita na saba nilisoma Kazel Hill sasa inatwa Shule ya Msingi Itetemia mwaka 1957-1958. Na darasa la nane tu mwaka 1959 nikarudi kusoma Mpwawa.
Mwaka 1960-1965 nilijiunga na Tabora School kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwakuwa nilifaulu nilichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966, na nilisoma shahada yangu ya Sheria na ilipofika Machi 1970 nilihitimu masomo.
Na mwishoni mwa Machi mwaka huo huo wa 1970 nikajiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), niliingia jeshini kama mwanasheria raia mpaka kipindi cha mafunzo ya kijeshi nikaenda kwenye mafunzo na kisha nikarudi kuitumikia JWTZ.
Ilipofika mwaka 1971 nikapewa kamisheni kambi ya Mgulani nikawa Luteni (nyota mbili). Nikaendelea na jeshi hadi mwaka 1977, nikahamishiwa Brigedi ya Faru-Tabora nikiwa na cheo cha Meja.
Sasa mwaka 1978, wewe mwandishi ulikuwa hujazaliwa, ndiyo mzee Aboud Jumbe Mwinyi, wakati huo akiwa ni rais akaniita Zanzibar na kuniteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na kipindi hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.
Aidha Oktoba 1978 niliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Na ilipofika Machi 1979 nilirudishwa JWTZ na baada ya muda mfupi nikapelekwa kwenye vita ya Uganda , nikiwa na cheo cha Luteni Kanali na kwenye vita hiyo nilikuwa naendesha mahakama za kijeshi.
Vita ilipokwisha nikarudi Zanzibar. Januari 8 mwaka 1980 nikaapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati huo nikiwa na cheo cha Luteni Kanali. Nikaendelea na Ujaji Mkuu Zanzibar hadi Septemba 1989 alipoapishwa Jaji Mkuu Zanzibar Hamid Mahamod Hamid.
Hata hivyo Juni 23 mwaka 1989 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania hadi mapema wiki hii nilivyoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Nilipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa Bara ndiyo sababu ya kuacha ujaji Mkuu Zanzibar.
Januari 1993 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na niliendelea na nafasi hiyo hadi Januari 2003 na Oktoba 2002 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambapo kipindi changu cha miaka mitano katika tume ZEC kinamalizika Oktoba mwaka huu.
Mwaka 1997 nilistaafu JWTZ nikiwa na cheo cha Brigedia, na niliagwa kwa heshima zote za kijeshi licha sikupewa mafao yangu kwakuwa mafao hayo yameunganishwa kwenye kazi yangu ya ujaji hivyo mafao yangu yote nitalipwa wakati nikistaafu kazi hii ya Ujaji Mkuu, kama mungu atanipa uzima.
Novemba 2001, niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki nafasi ambayo natakiwa nimalize kipindi changu cha miaka sita Novemba mwaka huu.
Nina mke mmoja ambaye Mungu ametujalia tumebahatika kupata watoto wanne, wawili ni wasichana na wawili ni wavulana.
Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Francis (30) huyu ni mwanasheria na anafanyakazi ya uwakili Manchester, Uingereza, Brigeth, huyu ana shahada ya Uandishi wa Habari na anafanyakazi ICAP hapa nchini, Marina ni mfamasia, yuko Liverpool, Uingereza na Mathew naye ni mfamasia, anafanya kazi Liverpool.”
Blog: www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 22,2007.
Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook: Happy Katabazi
0716 774494
Juni 18 Mwaka 2015.
MFAHAMU KWA UNDANI JAJI AUGUSTINO RAMADHANI

Juni 1Mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment