Header Ads

SPIKA SAMUEL SITTA AMEKWENDA HATORUDI

Na Happiness Katabazi KWELI udongo auvimbiwi. Utammeza pia mpendwa wetu,Wakili msomi na mwanasiasa machachari Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano WA Tanzania, Samuel Sitta ambaye amefariki Alfajiri ya Leo 7/11/2016 katika Hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa amelazwa kwaajili ya matibabu. Mwanasiasa huyu nilimpenda licha kuna kipindi alivyokuwa spika wa bunge alikuwa Anatoka nje ya mstari na niliwahi kumuonya kupitia makala yenye kichwa cha habari kisemacho: " SPIKA SAMUEL SITTA NI FISADI PIA?". Sitta alichukuia dhuruma, ubadhilifu wa mali za Umma. Enzi akiwa spika, bunge Lake ndiyo liliunda kamati ya kuchunguza mkataba wa kampuni ya Richmond ambayo kamati ya Bunge Februali 2008 iliyokuwa inaongozwa na Mbunge Wa Kyela ambaye sasa ni Waziri, Dk.. Harrison Mwakyembe kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Msabaha kujiudhuru nyadhifa zao. Nitamkumbuka Sitta kwa kauli yake hii aliyowahi kumjibu aliyewahi kuwa Mbunge Wa Mkuranga, Adam Malima ulipotokeaga mzozo bungeni Sitta akiwa Spika. Mzozo huo ulimhusu mmiliki wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi Kuwa anatumia vibaya vyombo vyake Malima akalalamika. Spika Sitta alitoa kauli hii "Malima apuuzwe'. Malima aliendelea kulalamika Sitta akajibu hivi " Akashtaki hata kwa Shetani". Kila nikikumbuka majibu hayo ya Sitta nacheka Sana. Sitta nitamkumbuka na msemo wake wa Mafisadi. Naweza kusema Sitta alikuwa mwanasiasa jasiri, mwenye historia ya kupanda na kushuka katika ulingo wa Siasa. Mara ya kwanza kukukutana na Sitta ilikuwa January 2007 ,sebuleni kwake Masaki, Dar es Salaam, nikiwa Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima., nilienda kufanya naye mahojiano kuhusu mchakato wa Kamati Richmond umefikia wapi. Tulizungumza Mambo mengi sana na akanitazama akasema Huku akinitazama usoni akasema "Amebaini mimi ni mwanamke jasiri".Na akanitaka nisibadilke. Sikumuelewa Sitta kwa kauli yake hiyo lakini kadri siku zinavyosonga mbele pia kuna watu wazima na wenye madaraka na wasiyo na madaraka kwa nyakati tofauti wamekuwa wakinitamkia hivyo Kama alivyonitamkia Mzee Sitta Kuwa Mimi Happiness Katabazi ni jasiri Sana. HISTORIA YA MAREHEMU SPIKA SAMUEL SITTA Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko wilayani Urambo Mkoa wa Tabora. Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”. Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V – VI. Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (L LB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971. Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa? Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi miwili baadaye akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao. Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (sasa marehemu) na wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu”. Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. Miezi kumi baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7 walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni. Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. Hii ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971. Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala. Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976. Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta amekuwa kiongozi wa juu wa CCM na serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na waziri katika nyakati tofauti na ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi. Sitta amemuoa Margareth Simwanza Sitta na wana familia imara. Mbio za ubunge Enzi za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta amekuwa mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria. Mwaka 1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR. Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta. Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu na aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa NCCR na Wilson George Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660 (72.3%) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio na changamoto nyingi. Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). Baada ya ushindi huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; utendaji wake wa kuiuma serikali na wakati mwingine kuipuliza kwenye Bunge la Tisa ulimfanya achukiwe na serikali. Ilipoonekana ana nguvu akatengenezewa “chui wa karatasi” (mshindani), Andrew Chenge. Chenge naye akachukua fomu ya uspika ghafla, likatengenezwa ‘zengwe’ kuwa wagombea wote wana nguvu, hapo CCM ikapata mwanya wa kutamka kuwa haiwataki wote ili kuondoa mvutano. Sitta akapoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda. Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri, wadhifa aliodumu nao hadi mwaka jana mwanzoni alipobadilishwa na kupelekwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi. Mbio za urais Samuel John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010). Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa nchi, akiwemo yeye. Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa, mara kwa mara, juu ya urais alionyesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa, alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi. Mungu aiweke roho ya Marehemu Spika Sitta mahali panapostahili. Chanzo:Facebook.Happy Katabazi Blog. www. katabazihappy.blogspot.com 7/11/2016. 0716 774494

No comments:

Powered by Blogger.