Header Ads

Twahitaji Usalama wa Taifa si Uhasama wa Taifa

Na Happiness Katabazi

KISWAHILI kama zilivyo lugha nyingine, kina maneno kadhaa ambayo ama yana maana ya kitu kimoja au maana yake inashabihiana.

Mfano wa maneno haya ni hili ‘taifa’ waweza kulifananisha na neno ‘nchi’ na pengine neno ‘dola’. Taifa au dola kama inavyojulikana ni jumuiya ya watu wanaolikalia pande la ardhi yenye mipaka inayotambulika rasmi kwa mataifa au dola nyingine.

Hivyo taifa au dola hufanya mambo yake ndani ya mipaka yake na hutumia vyombo kadhaa kuendesha shughuli hizo na kulinda masilahi ya wanataifa dhidi ya maadui wa ndani na nje.

Wataalamu wanatanabaisha kwamba dola/taifa lina mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama), wengine huongeza mhimili wa nne, yaani vyombo vya habari. Mhimili wa Serikali ndiyo wa kiutendaji na hivyo husimamia vyombo kadhaa katika utendaji huo. Hivi huitwa vyombo vya dola, ambavyo ni pamoja na majeshi ya ulinzi na usalama.

Hapa Tanzania tunalo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linalohusika sana katika kulinda nchi yetu na mipaka yetu dhidi ya maadui wa nje na pale inapobidi kuingia vitani kulinda nchi.

Katika hili twaweza kutoa mfano jinsi JWTZ walivyofanya kazi ya barabara mnamo mwaka 1978/1979 dhidi ya majeshi ya adui Idd Amini Dada wa Uganda (sasa marehemu).

JWTZ katika vita iliyopiganwa mwaka huo walifanya kazi iliyotukuka, kiasi kwamba sitarajii itakuja kusahaulika miongoni mwa Watanzania na katika historia ya nchi hii.

Naam! JWTZ walitimiza wajibu nyeti ambao si mwingine, bali kulihakikishia taifa letu usalama.

Tunalo jeshi jingine, Polisi, hawa tunaambiwa siku zote wako kwa ajili ya usalama wetu sisi raia na usalama wa mali zetu tulizojaliwa kuzimiliki.

Nao kazi yao si haba. Mara kadhaa wametuweka salama dhidi ya vibaka wakwapuaji, majambazi wa kutumia silaha, wavunja sheria za nchi na wengineo.

Hata hivyo pamoja na jitihada zao nzuri, matukio ya uhalifu bado yapo nchini na pengine wanashindwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, mathalani vifaa duni na mengineyo.
Lakini hatuwezi kusita kusema kwamba, vitendo vya baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi si tu ni kero bali vinaondoa maana ya dhana nzima ya wao kuwa chombo cha usalama wa raia na mali.

Kwa muda mrefu baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Traffic) wameendelea kuwanyanyasa wenye magari kwa rushwa.

Aidha, udhaifu mwingine wa Jeshi la Polisi umejikita katika namna ambavyo watu fulani wenye mamlaka huamua kukitumia chombo hiki ndivyo sivyo, mathalani, katika matukio kadhaa badala ya polisi kuwalinda raia walitumiwa kuwatesa raia.

Asiyeelewa hili awaulize vijana wa vyuo vikuu walivyotandikwa mara kadhaa na FFU, au wamuulize Profesa Ibrahim Lipumba kisa cha kujeruhiwa mkono wake na askari waliopaswa wamlinde.

Kama hilo halitoshi, kumbukumbu ziwapeleke huko Zanzibar ambako askari polisi
walitumika kuwamwagia maji ya ‘washawasha’ raia wema. Polisi wasinielewe vibaya, kazi yao ni nzuri sana ila kasoro za ufisadi na unyanyasaji ni mbaya. Isije ikawa mnatimiza lile neno lililonenwa na nabii akisema ‘chachu kidogo inachachua donge zima’.

Naam!, kwa ujumla twaweza kusema, mipaka yetu ni salama (heko JWTZ), raia tuko salama kiasi chake (asante polisi). Lakini je, kama tutatumia usalama katika maana yake kamili, taifa letu Tanzania liko salama? Na hili si swali la kipima joto hata lijibiwe kwa kusema tu ndiyo, hapana au sijui. Jibu linahitaji fikra pana.

Tangu tukingali watoto wadogo tumekuwa tukisikia uwepo wa chombo kiitwacho Usalama wa Taifa.

Wengi tunaweza kuwa tunafahamu majukumu ya chombo hiki kinadharia tu, maana shughuli kinazozifanya hazionekani moja kwa moja hadharani mara zote.

Yamkini kazi za wanausalama wa taifa hufanyika kwa usiri mkubwa. Ndiyo maana inakuwa hata si rahisi kujua nani mwajiriwa katika chombo hiki. Watu wanaishia kutuhumiana tu, mara utasikia ‘ooh, fulani ni usalama wa taifa na fulani naye…’ lakini hakuna uthibitisho, ni siri kwelikweli.

Hawa wanaodhaniwa kuwa ni wanausalama wa taifa wako katika vyama vya siasa, taasisi kama vile vyuo vikuu na kwingineko, ambako kama pasipochungwa huenda patahatarisha masilahi ya vigogo.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba inakuwaje mtu wa usalama wa taifa afanye kazi ya kudhibiti jitihada za chama fulani kisiweze kushika madaraka ya dola kihalali?

Inakuwaje mtu wa usalama wa taifa atumiwe kudhibiti midomo ya wasomi katika vyuo vikuu wasiseme ukweli, wasiwe na uhuru wa fikra bali wahubiri tu na kukariri yale yaliyo matakwa ya vigogo?

Inakuwaje usalama wa taifa kufanya kazi ya kudhibiti vyombo vya habari ili viandike yale tu ambayo wakubwa wanataka na si vinginevyo!

Inakuwaje usalama wa taifa uone kwamba kazi inayotakiwa ni kuwadhibiti waandishi wa habari wasifanye kazi yao, kama ilivyotokea wiki mbili zilizopita pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kati ya wapiga picha hadi Rais Jakaya Kikwete, akaingilia kati!

Katika hili, sina budi kumsifu Rais Kikwete. Ama kwa hakika kitendo chake cha kuwakataza walinzi wasiwazuie waandishi kufanya kazi zao ni cha upeo wa hali ya juu wa uelewa na ni funzo kwa wanausalama ambao wanasahau majukumu yao ya msingi na kujishughulisha na vitu ambavyo wala si hatari kwa usalama wa taifa.

Kudhibiti vyombo vya habari, wasomi na wanasiasa wa kambi ya upinzani, wanausalama wetu mfahamu fika kwamba uko si kulinda usalama wa taifa bali ni kujenga uhasama wa kitaifa.

Usalama wa taifa mkitambua hilo, rejeeni katika shughuli za kimsingi mnazopaswa kuzifanya hususan zama hizi ambapo usalama wa taifa letu na wa wakati ujao unazidi kuwa shakani.

Hamisheni nyenzo zenu pale Chuo Kikuu Mlimani mzielekeze kwenye maofisi ambako wizi wa kalamu unazidi kushamiri, ufisadi unaoota vitambi na uzandiki unastawi kupitia mikataba ya kishenzi inayosainiwa kati ya wezi wa ughaibuni na wenzetu wachache wanaokosa hata lepe la uzalendo, wanaiuza nchi hii kila uchao mchana kweupe na nyie mpo eti usalama wa taifa…usalama upi?

Tuseme hamjasikia hayo yanayotokea katika Benki Kuu ya nchi hii, kwanza mlikuwa wapi hata msiyadhibiti yasitokee? Au mlikuwa Tanzania Daima na MwanaHalisi mkiangalia nani anawaandikia wananchi ukweli ili ashughulikiwe?

Mmelala usingizi upi mpaka madini ya nchi hii na rasilimani nyinginezo vinachotwa na wageni kwa ‘raha zao’. Yamkini mlikuwa kwenye lecture rooms pale Mzumbe au SUA mkidhibiti wahadhiri wasitoe mihadhara ya takwimu za uporaji huo.

Mlikuwa wapi wakati hao wezi wakifanya mambo yanayowahusisha na kashfa nzito pengine kuliko zote nchini (ya BoT, Meremeta Gold Company, Kampuni ya Alex Stewarts, Akaunti ya madeni ya nje, Bank-M na kwingineko?).

Au mlikuwa kwenye mikutano ya hadhara ya ushirikiano wa vyama vya upinzani ili kukusanya ni hoja gani za nguvu wamezijenga mkawaripoti kwa vigogo watafute namna ya kuwajibu?
Ni usalama wa taifa upi mnaoshughulika nao ndani ya nchi ambayo wengi wanazidi kufukarika wachache wananeemeka kwa kasi ya roketi?

Ama hamjui kwamba hapana usalama palipo na wingi wa fukara, maana wajapokata tamaa amani itayeyuka kama barafu wakati wa jua kali.

Yatosha mliojishughulisha na masilahi ya wachache wala nchi, oneni uchungu, rejeeni maadili ya taaluma yenu, liokoeni taifa lenu, watumikieni wananchi, turejesheeni usalama wa taifa.

Watanzania tunautamani usalama wa taifa unaomlenga kila mmoja wetu, unaolenga uhifadhi wa rasilimali zetu na unaolinda haki ya kila mmoja wetu, awe raia huru au raia anayetumikia kifungo (pengine kwa kuvunja sheria au kubambikiziwa, au kushindwa kutoa rushwa kwa hakimu na karani mahakamani).

Katika hilo mawazo yananirejesha kukitazama chombo kingine cha dola, Jeshi la Magereza. Chombo hiki nacho kilipewa jukumu zuri, kuwahifadhi wahalifu wanapotumikia vifungo vyao na kuwafanya warejee katika tabia njema zinazofaa katika jamii (re-socialization). Jukumu hili nalo lililenga usalama wa jamii.

Cha ajabu ni kwamba, wafungwa kadhaa wanapomaliza kutumikia vifungo vyao badala ya kurejea uraiani wakiwa watu wema waliobadilika, wazingativu wa maadili ndiyo kwanza huja na mbinu kali zaidi za uhalifu.

Msomaji usishangae bali tushirikiane kuliambia Jeshi la Magereza litufafanulie; bangi na pengine dawa za kulevya zinapenyaje na ulinzi wenu mkali na kuwafikia wafungwa? Au baadhi yenu mna masilahi katika hiyo miradi?

Inakuwaje huko magereza wafungwa ‘wanashikishana ukuta’ (wanaingiliana kinyume cha maumbile), au kwenu ninyi hiyo ni haki ya mfungwa?

Hao chawa wataisha lini kwenye virago wanavyolalia wafungwa, wataacha lini kulala mzungu wa pili na kwa msongamano katika vyumba vidogo.

Au hamjui kwamba kwa kuwaweka wafungwa katika mazingira ya kinyama namna hiyo ndiyo kwanza mnawajengea moyo wa ‘kihayawani’ na kikatili badala ya kuwarejesha katika uadilifu.

Mtueleze wazi mnakuwa wapi hadi wafungwa wa kike wanapachikwa mimba wakiwa magerezani?

Jeshi la Magereza, ebu jiulizeni leo hao wafungwa mnaowahifadhi wakimaliza vifungo vyao usalama wa taifa utakuwa katika hali gani?

Mama yetu Tanzania, leo wewe si taifa salama, waambie wanao (wananchi) wajue hali uliyonayo, washiriki kilio chako ili tumbo lako lisizidi kuwa shimo tupu lililotolewa utumbo wote (mali asili) kwa manufaa ya wageni; lisiendelee kupata uchungu wa kuzaa wana mafisadi na wahalifu, mwite mwanao serikali akishtue chombo chake Usalama wa Taifa kisiendelee kubweteka ilhali usalama wako unazidi kutokewa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0755 312 859 au barua pepe; katabazihappy@yahoo.com. Au www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,Uk 6, Juali 22, 2007

4 comments:

Innocent Kasyate said...

Kweli Uhasama wa Taifa ndio ugonjwa mbaya kabisa kuliko hata ukimwi.Hongera, kaza buti nakuombea Mungu sana akulinde manake maadui ni wengi sana shauri ya akili kidogo na njaa sana.
Tanzania itakombolewa na mawazo kama haya.
Pasua zaidi.

Anonymous said...

Huu ni ukweli mtupu!
Hongeleni sana waandishi wenye kujali masilahi na Mstakabali wa Taifa, usiokumbatia mfumo wa ulimbukeni katika kupenda Takrima ili muandike ya kuwasifia Wakubwa!

Mwenyezi atawalinda na atatulinda! Hawa jamaa si ajabu kuwaona, kuwasikia wakifanya kazi ambazo hawakuajiliwa kwazo. Kama hawana kazi ya kufanya waende kijijini waongeze tija, wakalime kuliko KUSALITI maadili ya kazi walizo ajiliwa!
Huu ni uhuni, ujima kama si umbeya. Kirusi hiki kimeenea katika ofisi na idara zote za Serikali na hata maeneo mengine.... toba! Kwa nini usifanye kazi yako kama ulivyo apa kutekeleza na kulinda!
Hii ndiyo inayo pelekea Maofisa wote kufanya shughuli nyingi zisizo wahusu, kufanya kazi zao chini ya viwango na tija.
Acheni kufanya kazi za siasa ambazo hamziwezi kamwe.... ndiyo kwani si kazi zenu hizi haziwahusu hata kidogo!
Kwanini mnapenda kufanya kazi za wengine...!!? Acha walio ajiliwa kama siyo kuchaguliwa ama kuteuliwa wafanye kazi zao....zenu zipo.... zitekelezenni mletee Taifa Tija na Maendeleo ya mabosi wenu sisi wanachi...
Mashairi na nyimbo za siasa mnazo imbishwa waachie wanasiasa wenyewe! Kwa leo Inatosha! Kaza kamba dada H.K na waandishi wa habari wengine igeni utamaduni na UJASIRI huu, mabadiliko ni hatua, zingatieni uwazi na ukweli acheni kupenda hongo/Takrima, JsMvunamaboko.

Anonymous said...

Mh asante we. Maanake kwa kweli mimi nimeshakata tamaa na Tanzania kabisa sio utani. Hongera sana ndugu na I hope somebody will do something about it, though it doesn't look that way any time soon. Sasa naona kihoro cha vigogo wa Tz ni kuuza hiyo petroleum, kwa nguvu, wasione hiyo Nigeria yenyewe inauza mafuta dunia nzima lakini wananchi ni maskini kuliko wote duniani.SHAME ON THEIR FACES! Najua hayajali lakini iko siku tu mola atatutizamia.

Anonymous said...

Ninamshukuru sana Dk dawn acuna, aliandika uchawi wa mapenzi ambao ulimrudisha mpenzi wangu wa zamani katika masaa 48, shukrani kwake, ikiwa una hali kama hiyo.
*Ukitaka kumrudisha mpenzi wako.
*Kama unataka kupata mimba.
*Ukitaka kuacha kuharibika kwa mimba.
Ikiwa unataka kuponya aina yoyote ya ugonjwa. Ikiwa unataka kujiunga na illuminati, na wengine,
Wasiliana naye yeye ndiye mtu sahihi wa kutatua tatizo hili.
Barua pepe: { dawnacuna314@gmail.com }
Whatsapp: +2348032246310

Powered by Blogger.