Header Ads

KINGUNGE,MARMO TUMECHOSHWA NA POROJO!


Na Happiness Katabazi

SEPTEMBA 15, mwaka huu, nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa hadhara viwanja vya Mwembe Yanga, Tandika, Dar es Salaam na kumshuhudia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, akitaja orodha ya vigogo 11 aliowaita mafisadi.

Baada ya Dk. Slaa kuanika majina ya vigogo hao, mapema wiki hii vyombo vya habari vilimkariri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Kingunge Ngombale – Mwiru, wakiwataka wapinzani kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwenye vyombo husika.

Mzee Kingunge aliwaambia waandishi wa habari Ikulu, Jumanne, kwamba tuhuma hizo ni za ‘uongo na uchochezi’ na kwamba wapinzani wanataka kuilazimisha serikali kuwakamata na aliwataka wananchi na umma uwapuuze wapinzani.

Binafsi nasema matamshi hayo ya viongozi hao wawili ni ya wanasiasa waliochoka.

Kwanza, wanasema viongozi wa upinzani wanapotosha wananchi kwa orodha ile ya vigogo 11. Sasa hatuoni ni jinsi gani usemi usio na mantiki unaweza kutolewa na kiongozi mwenye busara.

Hawa wana mageuzi wametaja vigogo na hawa wameeleza hilo hadharani kweupe. Hawa wametoa vigezo vya kisheria vya kumtaja kila mmoja kati yao.
Kuna waliotajwa kwa sababu walifanya vitendo vya kifisadi na kujineemesha na ufisadi huo. Kuna waliotajwa kutokana na maamuzi ya kifisadi waliyoyafanya.

Makundi haya yote mawili ni mafisadi. Mtu anayetaka kukanusha hilo, sharti athibitishe kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwa vigogo waliotajwa kuwa si mafisadi.

Lakini kitendo cha Kingunge kuamka na kusema kwamba habari hizo zimepotosha umma, ni kuamini kwamba umma ni ‘wapumbavu’ na hauna uwezo wa kufikiri.

Labda tuangalie asiye na uwezo wa kufikiri kati ya umma na Kingunge ni yupi. Lalamiko la huyu bingwa wa propaganda Kingunge ni kwamba wapinzani wangeviarifu vyombo vya dola, hivyo vyombo ni vipi?

Kingunge na Marmo watutajie chombo kimoja cha dola chenye uwezo kisheria kumchunguza Rais Jakaya Kikwete au Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Sheria inayounda (TAKUKURU) ya mwaka 2007 inampa uwezo rais wa nchi kumteua Mkurugenzi wa (TAKUKURU), hii ina maana kwamba mkurugenzi wa chombo hicho hawezi kufanya kazi dhidi ya rais, kwa sababu si tu kifungu hicho cha 6 (2), rais ana mamlaka ya kumteua, lakini kifungu cha 14 kinaweka masharti kwamba kila mwaka Machi 31, taasisi hiyo ya kupambana na rushwa itoe ripoti ya utendaji wake wa kazi kwa rais.

Kwa hiyo, kuwaambia wapinzani waende kulalamika (TAKUKURU) na kwenye vyombo vingine vya dola ni kudhania kwamba wananchi hawajui kwamba taasisi hiyo haina mamlaka ya kumchunguza rais.

Na kama Rais Kikwete ambaye naye ni miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha ile hatachunguzwa, basi na hao vigogo waliobaki hawatachunguzwa. Ikiwa madai kwamba kampuni ya Kagoda ilianzishwa na kupewa sh bilioni 30 na Benki Kuu (BoT) ili zitumike kama ‘rushwa’ wakati wa uchaguzi, usafi wa rais uko wapi?

Ikiwa rais mstaafu Mkapa tunaelezwa alijigeuza kuwa mjasiriamali na akaanza kufanya biashara badala ya kuongoza taifa, usafi wa mstaafu huyu tulioambiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere utakuwa wapi?

Ikiwa huyo Mkapa alipokuwa rais, familia yake pamoja na washirika wake wa karibu, wapinzani wanamtuhumu kwamba alijiuzia migodi ya machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira Coals Mines Ltd ili ajipatie mamilioni ya fedha kutoka TANESCO, usafi wa uongozi uko wapi?

Ikiwa BoT na gavana wake wanadaiwa kujiingiza katika makampuni yanayotajwa na wapinzani kuwa ni ya kitapeli ya Meremeta Ltd na Tangold Ltd, kwanini tusiamini wahusika wa makampuni haya ni mafisadi na matapeli wakubwa?.

Kampuni ya Meremeta kwa mujibu wa orodha ile inaonyesha ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa nje ya nchi kama kampuni ya wafanyabiashara wakwepa kodi. Je, wanaweza kutueleza Serikali ya Tanzania ilikuwa inakwepa kodi ya nchi gani, ya Tanzania, Mauritius au Afrika Kusini?

Je, huu ni uadilifu? Na mahesabu yaliyokaguliwa na Mkaguzi wa Serikali yako wapi? Na mbona imefilisika bila kufanya biashara yoyote licha ya kupewa mabilioni ya fedha na BoT?

Je, ni sahihi kuanzisha kampuni nje ya nchi, kuzipelekea mamilioni ya fedha nje ya nchi, kisha kuzifilisi na kuzipelekea tena fedha za walipa kodi kulipa madeni? Je, huu si ufisadi wa kupindukia?

Sasa wapinzani wanapotosha nini katika hili? Tunadhani kwamba serikali ina deni kubwa la kutoa maelezo sahihi kwa Watanzania badala ya viongozi wake kuropoka ovyo, ikifikiria bado wananchi wanaweza kurubuniwa kwa ombi lao la kutaka wananchi wawapuuze wapinzani?

Pia tunadhani watuhumiwa hao wa ufisadi nao wanapaswa wajitetee kwa umma.

Jambo li wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Kikwete imeweka rekodi katika awamu zote kwa kuingia katika kashfa kubwa ya ufisadi katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wake.

Hoja ya Kingunge ina maanisha kwamba wapinzani wana wajibu wa kufanya kazi za upelelezi badala ya taasisi za serikali. Taasisi hizo zenye wajibu wa kupeleleza rushwa, zipo na watumishi wake wanalipwa mishahara kwa kazi hiyo na hawana sababu ya kualala usingizi.

Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuingia madarakani alitangaza baraza lake la mawaziri na alinukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba baraza lake haliwezi kuwa na vijana peke yao kwakuwa bila wazee moto unaweza kuwaka, akimaanisha kwamba wazee ni ‘grisi’ inayoweza kulainisha mambo yanapokuwa magumu, akimaanisha kwamba amemteua Kingunge kwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika serikali na chama licha ana umri mkubwa.

Kutokana na matamshi ya Kingunge, Watanzania tujiulize hii ndiyo grisi tuliyoelezwa na rais wetu wakati akitangaza baraza lake la mawaziri?.

Sasa kwanini wangoje wapinzani wafanye kazi wawaletee ushaidi, kwani wapinzani wanalipwa kwa hiyo kazi? Huo ni uzembe wa serikali na hakika unawatia hasira walipa kodi.

Na kwa sababu ya uzembe huo, serikali haiwezi kuwatwisha mzigo wapinzani wa kuleta ushaidi. Kwa wajibu gani? Uwezeshwaji gani?
Hivi hizo taasisi za upelelezi zipo chini ya mamlaka ya wapinzani? Ieleweke wazi matamshi ya Marmo ya kutaka wapinzani wapeleke ushahidi na matamshi ya Kingunge kuwa tuhuma hizo ni za uongo na uchochezi na kwamba wapinzani wanataka kuilazimisha serikali kuwakamata na kuutaka umma upuuze tuhuma za wapinzani, ni matamshi yanayodhihirisha kukingia kifua ufisadi.

Na matamshi kama haya yaliyotolewa na viongozi hawa wa serikali, si mageni masikioni mwetu, kwani tulishawahi kuyasikia ya kitolewa na Rais mstaafu, Mkapa, enzi za uongozi wake, alipowaambia waandishi wa habari wathibitishe kuwa serikali yake ni ya wala rushwa na aliwanyoshea kidole waandishi kwamba hawaandiki rushwa ya wanahabari badala yake wanaandika rushwa ya viongozi wa serikali yake.

Aidha, lugha ya kutaka wananchi kuleta ushahidi kuhusu madai ya rushwa dhidi ya baadhi ya viongozi pia tumeishawahi kuyasikia sana kwa Mkapa.

Nasema tumechoka na porojo, tunataka kuona taasisi husika zinachukua hatua ili serikali iendelee kuaminiwa na kuheshimiwa ndani na nje ya nchi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0755 312 859; barua pepe;katabazihappy@yahoo.com; tovuti;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili la Septemba 23, 2007

8 comments:

Anonymous said...

Dada you are a legend in the making at such a young age! With this kind of writing nadhani utawawashia indiketa hata akina Lusekelo and Onyango-Obbo in the near future. Keep this up, our media needs strong talents like yours!

Anonymous said...

Huyu Babu amechoka na amefilisika sasa amebaki kama vile chombo cha kueneza porojo za CCM hivyo ni bora CCM wakamzuia kuzungumza badala ya kusema yote na kuonyesha udhaifu mkubwa sana. kama ndio Mshauri wa rais anakuwa hivi Basi tumekwisha kabisa.
Josh Michael
Colorado USA

Anonymous said...

Nimependezwa na maoni yako yaliyojaa ukweli mtupu. Endeleza mapambano haya ya kifikra usirudi nyuma.

M. M.

kitukosana said...

Safi sana kwa makala yako nzuri. Kuna jambo moja linanishangaza katika skendo hii. Waliotuhumiwa ni watu kama kuna na moja, na kila mmoja wao katuhumiwa kwa ufisadi tofauti yaani haulingana kwa aina wala muda alioufanya au kusaidia kuufanya. Jambo la ajabu kila aliyesimama kujitetea hajitetei yeye binafsi ila anapuuza hoja nzima kwanini? si kila mtu ajitetee kvyake kwa kuwa kashafa hazifanani? Kingunge anapobisha katika ujumla wake tumweleweje? Kwanza alipaswa atueleze alikuwa anaongea kwa niaba ya chama (CCM) au Serikali?
Nafikiri ni vema kila mtu ajitetea kivyake kwa sababu katuhumiwa mtu binafsi sio serikali, idara au chama.

Anonymous said...

Hakika Katabazi umetia fora!Binafsi sijawahi kuona mwandishi mwenye uchungu kiasi hiki, msema kweli, mzalendo, mwazi,…………

Ee mwenyezi ingia mioyoni mwa waandishi wote, watanzania sote , tuweze kupata ujasiri wa kuanika mambo hadharani bila kubakia kunung’unika tu pembeni huku tukiomba sauti zisisikike!

Hakika Taifa hili lingekuwa na akina Happy 170, leo hii UJINGA, UMASIKNI, MARADHI, RUSHWA (TAKRIMA) na aina yote ya UFISADI bye bye!

Kazi hii iliyo anzishwa na muungano wa vyama visivyo madarakani ina changamoto nyingi kwa watanzania!,.......wimbo.. Vijana msilaleeee lale laleeee....... moto huu tuuendeleze hadi mwisho tuwe wasafi wa ufisadi!

Mungu wabariki watanzania wabadilike, Eee Mora fanya miujiza hapa Tanzania!
JsM.
Ngara, Kagera.

Anonymous said...

CHA MSINGI MWOMBE JAAMAA WA HAKI-HAKINNGOWI.BLOGSPOT.COM AWEKE
LINK YAKO PALE KWAKEEE ILI KILA MARA TUWE TUNAKUTEMBELEA KUPITIA KWAKE KAMA ANAVYOTUPA HABARI KILA UNAPOTUMBUKIZA MAKALA MPYAA..
KAZIIII NZURI UNAFANYAAAA

Anonymous said...

Bsiiiiih(msonyo) imenitia hasira mimi,kumbe ndivyo mambo yalivyo hivi, I wish watanzania wengi wangekuwa na uwezo wa kuzisoma hizi makala zisizo na chembe ya udanganyifu wala hofu, lakini maskini ya Mungu hata hizo Tsh 300 za kununulia gazeti kwa mtanzania wa kawaida ni muujiza achilia mbali Tsh 4000 za kusafiri mpaka kwenye mji ulio karibu wenye umeme ila alipe Tsh 1000 za internet apate kuzisoma makala kama hizi, Anyway tutafika, Big up dada.

Anonymous said...

top [url=http://www.c-online-casino.co.uk/]free casino bonus[/url] check the latest [url=http://www.realcazinoz.com/]casino games[/url] autonomous no consign perk at the best [url=http://www.baywatchcasino.com/]www.baywatchcasino.com
[/url].

Powered by Blogger.