Header Ads

LOWASSA AMENICHANGANYA


Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere aliwai kusema ili nchi iendelee yahitaji mambo manne, nayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Wahaya na sisi Wanyambo tuna msemo: “Omukama ainduka anketo tainduka alulimi.” Kwa Kiswahili: “Mfalme hujigeuza kitini, si katika ulimi (kauli).”

Kwa kawaida kiongozi anatakiwa kuwa na kauli thabiti na msimamo katika ayasemayo.
Uchumi unapaa ni kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu Edward Lowassa aliyoitoa kabla na wakati wa kufunga kikao cha Bunge la bajeti, la mwaka wa fedha 2007/2008, mjini Dodoma.

Waziri Mkuu Lowassa, akisoma hotuba yake ya kufunga kikao cha Bunge, alilalamika kuwa kuna baadhi ya waandishi wa habari, wachora katuni na wanaharakati wamekuwa wakipinga hilo.

Alisisitiza tena kuwa uchumi unapaa, kutoa vigezo na kuwataka wanaopinga hoja hiyo pia kuleta vigezo vya kupingana na hali hiyo.

Lakini mwishoni mwa wiki akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, akijibu swali la wananchi wa Sengerema waliotaka kujua ni kwanini mfumko wa bei umeshika kasi katika kipindi kifupi tangu Rais Benjamin Mkapa aondoke madarakani.

Pia walitaka kujua ni lini ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania itatimizwa.
Lowassa akijibu swali hilo alisema mfumuko wa bei unaoendelea hivi sasa umesababishwa na uchumi wa nchi kutokuwa mzuri. Na kuhusu ahadi ya maisha bora itatimizwa lini, aliwajibu kuwa maisha bora hayaji kwa wananchi wake kutofanya kazi kikamilifu katika sehemu zao za kazi.

Hapa waziri mkuu amenichanganya, kwani ni yeye aliyeuambia umma kupitia Bunge kuwa uchumi wa nchi unapaa kwa kasi ya ndege, lakini mwishoni mwa wiki iliyopita anawaambia wananchi wa Sengerema walipodai awaonjeshe huo uchumi unao paa, anasema vinginevyo.

Hivi waziri mkuu tukuelewe vipi? Ni mtu yuleyule uliyezungumza bungeni ndiye uliyezungumza Sengerema mwishoni mwa wiki?

Tuambizane ukweli kwamba wataalamu wako walilidanganya taifa kwa kukupa taarifa zisizo sahihi na hali halisi ya uchumi.

Kumbuka wakati wa kampeni jinsi CCM walivyoliimbia taifa ngonjera ambazo kiutekelezaji ni sawa na ndoto za Abunuasi. kwani hazitekelezeki.

Kwa jinsi hali ya mambo inavyokwenda, unaweza kuona kabisa uwezekano wa serikali kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Mfano, nia njema ya kujenga shule lazima iendane na taaluma ya elimu katika kujenga shule. Shule ni walimu wanafunzi, majengo, madawati, mahabara, vitabu n.k.
Sasa kila kimoja kwa nafasi yake. Tukijenga darasa, tukaweka wanafunzi ndani bila kupata walimu, tukae tukijua tunajenga genge la wahuni.

Na hizo ndizo shule zako Lowassa tunazoambiwa kwamba hazina walimu wa kutosha, hao ni wale walimu wako wa wiki nne. Tuambizane ukweli la sivyo taifa hili tutalipeleka pabaya.

Hao Watanzania wenzetu wanaojazwa upumbavu katika shule za kata bila walimu, watalipeleka taifa hili kuzimu.

Shule bila vitabu, madaftari, karamu, chaki, na vifaa vya maabara, si shule, hawa wanafunzi ni kiwango gani cha elimu ambacho wanapata?

Twende kwenye vyuo vikuu, serikali ina vyuo vikuu vinne, Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sokoine na Chuo Kikuu Uhuria. Hivyo vyuo vikuu kwanza ni vidogo na serikali haifanyi juhudi ya kupanua ili viweze kupokea wanafunzi wengi.

Uwezo wa vyuo vikuu hivyo kuvipanua ni mkubwa na unahitaji ongezeko la walimu, mishahara waboreshewe, inahitaji vifaa vya elimu ya juu, kompyuta na maabara za kisayansi.

Badala ya kulifanya hili, serikali inakurupuka na kuanzisha chuo kikuu kipya cha Dodoma. Ili kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma, serikali imelazimika kuchukua baadhi ya wahadhiri kutoka kwenye vyuo vikuu hivyo vine, ingawa vyuo vyenyewe havina walimu wa kutosha.

Je, hayo maendeleo yako wapi kama una bomoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sokoine, Mzumbe na Chuo Kikuu Huria ili ujenge Chuo Kikuu cha Dodoma maana yake nini? Au tunataka utitiri wa vyuo vikuu usio na viwango?

Twende kwenye sekta ya afya, huko vijijini tunaowajua ni waganga wa kienyeji na wakunga wa jadi, si madaktari ambao serikali inawasomesha kwenye vyuo vikuu na ndio wanaozalisha kina mama huko vijijini.

Badala hata ya kuwasaidia wakatoe huduma bora zaidi, mnakimbilia kujenga majengo ya zahanati bila kuweka wataalamu wa kutosha na dawa.

Wenzetu wa Kenya wanatengeneza dawa za mitishamba, tena wakati mwingine miti hiyo wanaivuna hapa kwetu na kwenda kutengeneza dawa hizo nchini mwao na kisha wanakuja kutuuzia hapa, na katika hili tukae tukijua tunapoteza na kukosa teknolojia.

Miti tunayo, waganga wa jadi na wakunga tunao, kitengo cha miti shamba kipo lakini akipewi fedha za kutosha badala yake fedha za walipa kodi zinanunulia mashangingi na kuishia kwenye ziara za viongozi.

Viongozi wakipata ajali wanapelekwa kutibiwa Afika Kusini, kwa matibabu ambayo waganga wetu wa hapa kupitia kitengo hicho cha tiba asilia kitengo cha MOI, kinaweza kutoa matibabu hayo.

Mheshimiwa Lowassa, wewe unawaambia wananchi wa Sengerema kwamba serikali ina mikakati ya kuboresha maisha yao, mikakati hiyo ni ipi tusiyoijua?
Au unataka kuzungumzia MKUKUTA, MKURABITA na mabilioni ya Kikwete? Kweli hiyo mikakati itatutoa kwenye umaskini?

MKURABITA ni mkakati wa walionacho na wanarasimisha mali walizonazo, kwa maana kama hauna mali, MKURABITA haukufikii.

MKUKUTA ni mpango wa kupunguza makali ya umaskini lakini umaskini una baki pale pale, hautuhakikishii kama tutaondoka kwenye umaskini kwa mikopo ya sh 50,000 au sh 100,000. Serikali itaondoaje umaskini kwa mikopo hiyo midogo?

Mabilioni ya Rais Kikwete hayawezi kutokomeza umaskini kwa sababu mikopo hii inatolewa kwa masharti na maskini hawezi kutekeleza masharti hayo, na si kila anayeomba anapata kutokana na masharti ya kibenki.Hata fedha hizo zingetolewa bila masharti, pia hazitoshi.

Kwa hiyo sisi tunachokusii Lowassa, usijalibu kupotosha wananchi kwasababu tayari wameishagundua siri ya sifuri.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Jumatano Septemba 26 mwaka 2007

6 comments:

Anonymous said...

Dadangu,
Nakusifu sana kwa kuliona hili kwani viongozi wetu walio wengi porojo ndo zimejaa mdomoni. Hii inatokana na kutokuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri mambo na kutokuwa na utaalamu dhidi ya masuala mbalimbali wanayoyaongelea. Na suala jingine tena la msingi ni kujisahau na kusahau walipotoka. Si shangai kwa kiongozi wa juu serikalini hususani Tanzania kusema ya kuwa uchumi umepanda, maana ni mara chache sana kujua hata bajeti zao binafsi wanazozitumia kila siku kwani kila kitu kimepangwa na kinafanywa na mtu mwingine. Usishangae leo ukimuuliza mheshimiwa waziri mkuu kuwa anatumia shilingi ngapi kwa siku na akashindwa kukupatia jibu sahihi. Maana hajui lolote. Hawa watu wanaishi kama miungu wadogo. Hawa hawatofautiani sana na enzi za utawala wa Warumi wa akina Kaizari hususani akina Nero. Leo hii huwezi ukasema kila mtazania ataishi maisha bora pasipo kumuandalia mazingira ya kufanya hivyo. Ukiona kiongozi anaanza kutoa majibu ya mkato jua mambo ni magumu na ahadi hazikelezeki tena. Anyway tutazidi kuomba sana ili Mungu aibariki Tanzania na watanzania wake. Lakini kila chozi analolitoa mwananchi wa kawaida mlalahoi ambaye hajui kesho atakula nini hakika litalipwa.

sinaapfle@yahoo.com

Anonymous said...

Cha kuuma ni jinsi mvi zake zinavyoleta mandhari ya busara, lakini yanayotoka mdomoni ni kujikakamua tu na kuropoka majidudu tu ya ajabu yasiyokuwa hata na vivuli!! Hebu fikiria, PM mzima anatoa mfano wa kugawana sungura... ni aibu kwa kweli.

SteveD.

Anonymous said...

Huo ndio usanii wa Viongozi wengi wa Tanzania sio wasema Ukweli na pia Ujue kwamba Kukubali kwa Lowassa Kusema uchumi ni mbovu na Mfumuko wa bia ni mkubwa ni Kukubali kuwa Sera zao zimekwama sasa wanashindwa waseme nini.. Then huyu wakati mwigine anakuwa kama ana Kurupuka vile katika kauli zake. yeye alisema kuwa Uchumi unakua sasa inakuaje?? je huo sio Kusema ukweli katika Bunge?? je nani msema Ukweli. Wameshindwa sasa. Then Kujenga chuo cha DODOMA wanateka Sera ya CHADEMA> UNAKUMBUKA WAKATI WA KAMPENI MBOWE ALISEMA KUWA ATAFANYA MAJENGO YA DODOMA KUWA CHUO KIKUU YALE YA CHIWAGA. SASA WAO WAMEFANYA NINI?? WAMESHINDWA NA WAMECHOKA SASA . SASA ZIMEBAKI MAJUNGU NA USANII TU.
JOSH MICHAEL
COLORADO MAREKANI

Anonymous said...

DADA HAPPY ASANTE KWA MAONI YAKO.BINAFSI NAWALAUMU SANA WATANZANIA KWA KUJIFANYA WANA IMANI,IKO WAPI KAMA MATIBAU MAZURI NI KWA VIONGOZI NA WATOTO WAO TU.UKIFIKA WAKATI WA UCHAGUZI WANADANGANYWA NA PEREMENDE TU LOWASSA UNAANDAA KUWEKA MISINGI YA KUONGOZA WATU WASIO NA ELIMU SIKU ZIJAZO HATA UKIJENGA SHULE MPAKA KWA MJUMBE WA NYUMBA KUMIKUMI.NINACHOKIONA MIMI UONGOZI WENU NI WA UONGO NA AFADHARI YA KINGUNGE ASIYEAMINI MUNGU TUTAMUELEWA KWANI YEYE BINADAMU KWAKE NI KAMA WANYAMA TU.LOWASA KANISANI NA MISIKITINI MNAFUATA NINI KAMA ZILE KANUNI ZA MSINGI MPO KINYUME NAZO,USISE UONGO HAPO WAONGO NI NYINYI NAMBA WANI,USIIBE KAMA KUNA MAJIZI KAMA NYINYI WALE VIBAKA WA KEKO NA UKONGA WAACHIWE HURU MASKINI USITAMANI MALI YA MTU MWINGINI KAMA KUNA TAMAA MBAYA KULIKO YENU MUNGU ANIHUKUMU LEO MNATAMANI MALI NA HAKI YA MASIKINI WASIO NA CHOCHOTE KWA KUWABAMBIKIA WAWEKEZAJI HEWA ILI MGAWANE MAFAO YA MTANZANIA.MUNGU IEPUSHE TANZANIA MIKONNI MWA HAWA WADANGANYIFU WANAJIITA WAADILIFU.BROTHER MUGA

Rashid Mkwinda said...

Watafika mahali hawa watu wataanza kuogopa kimvuli chao lakini time will Tell, watu wameamka wanajua mbivu na mbichi, mchele na Chuya, wakati ukifikia naamini kila mmoja atajua wapi anakwenda na kutafakari wapi alikotokea, jambo la muhimu ni kutumia kalamu zetu kwa maslahi ya watanzania na kuepuka kutumika kama wapambe wa wanasiasa, wanapenda sana kutumia kalamu zetu kuwapandisha daraja wanafika mahali kalamu zilizotumika kuwafikisha walipo wanaanza kuziogopa.

Wametumima viatu mwaka huu....baada ya miaka mitano wanakuja na kutuuliza hivi mlikuwa mnataka viatu aina ganii??????

Bg up Dadaa
Alamsiki !!!!!

Anonymous said...

Nimefurahia mandhari ya kijiwe chako. Tuko pamoja dada, na endelea na ujasiri huo huo. Ni vyema kupiga kelele maana ipo siku watasikia.

- http://nilichokiona.blogspot.com
- http://uchambuzi.wordpress.com

Powered by Blogger.