Header Ads

BILA KAZI YA ZIADA,HADHI YA MAHAKAMA YA TANZANIA INAKWISHA!

Na Happiness Katabazi

JULAI mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alimteua Jaji Augustine Ramadhani(62) kuwa Jaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Jaji Mkuu, Barnabas Samatta, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Na ni kwa mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mahakama iliongezewa nguvu na kubadilishwa jina kutoka kuwa Idara tu ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria na kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mabadiliko haya yalikuwa na maana kwamba sasa mahakama inatambilika rasmi kama muhimili wa dola. Muhimili ambao kwa muda mrefu ulikuwa umegandamizwa na serikali(executive) kwani mahakama ilikuwa inapangiwa kila kitu ikiwemo bajeti yake.

Pamoja na dhana ya uhuru wa mahakama lakini bado katika mazingira ya utendaji wake isingeweza kujidadavua na kufanya mambo yake kama inavyotaka.

Kwa hali ilivyo sasa mahakama yetu ya Tanzania ina kazi kubwa sana ya kufanya. Zipo changamoto nyingi ambazo inabidi izitatue ili kufikia uhuru wa kweli wa mahakama na utaoaji wa haki kwa haraka na pasipo malalamiko.

Ni miaka 28 sasa tangu Mahakama ya Rufani ilipoanzishwa lakini hadi sasa bado hakuna mabadiliko makubwa. Mh.Jaji Mkuu; mahakama nyingi za mwanzo huko vijijini zinatisha ukiyaangalia majengo yake, ukiachilia mbali samani zilizomo humo ndani.

Hakuna sehemu za kuweka mafaili, vitendea kazi hakuna,nyumba za mahakimu n.k. ambapo hakimu anatembea umbali mrefu kufika kazini na mara nyingine hakimu anapoendelea na kesi kunyeshewa na mvua au upepo.

Hali hii imetokea pia huko Biharamulo ambako pia wakati mwingine mahakama hufanyika kwenye wodi la zamani la hospitali ya Biharamulo. Haya yote yanafanya mahakama zetu zikose uhuru wake na ukiachia hayo mahakimu wengi kutoripoti vituo vya kazi walivyopangiwa au kuhama hasa kipindi hiki ambacho mahakimu wengi wanaoenda huko ni wale wenye Stashahada.

Ifike wakati sasa mahakama hizi za mwanzo ziangaliwe na kwa kuwa pesa za serikali kuu hazitoshi basi nashauri iendeshwe harambee na Mahakama Kuu kuwahamasisha wananchi kujenga mahakama kama inavyokuwa kwa vituo vya polisi ili wajijengee mahakama zao wenyewe.

Aidha, katika mahakama zetu za chini kuna ukosefu mkubwa wa samani,vitendea kazi kama vile karatasi,n.k na upungufu wa majengo ambao unafanya mahakimu na wengine kukosa mahali pa kukaa, mifumo ya maji taka ni mibovu, vyoo vinatia kinyaa.

Ukienda mathalani pale Kisutu utakuta mahakimu wawili wanakaa chumba kimoja, hakimu mwingine hata kiti anachokalia utamwonea huruma aidha hata chumba cha kukaa mawakili nacho hakitoshi, hali inayofanya utendaji kazi kuwa mgumu sana.

Katika mahakama nyingine kama huko Kigoma Hakimu Mfawidhi anawajibika kutembea umbali mrefu na saa nyingine kupanda treni wakati anapokwenda kukagua mahakama za mwanzo. Mambo haya yote yanaathiri sana uhuru wa mahakama.

Kutokana na kukosekana mazingira mazuri ya kufanyia kazi unakuta mahakimu wengi wanaamua kutokwenda wanakopangiwa kazi au kuwa wavivu au saa nyingine kupewa lifti na wadaiwa katika kesi, au kufadhiliwa mahitaji muhimu kitu ambacho kinaathiri utoaji haki.

Unategemea nini hakimu ambaye anatoka Bunju na kuja kuendesha mahakama ya Kisutu huku akitumia usafiri wa daladala?

Humo humo kwenye daladala wamepanda watuhumiwa au wadaiwa ambapo saa nyingine anajikuta amelipiwa nauli au mwenye nyumba wake. Naam! yaweza kuwa ni ukarimu lakini kwa nini uwe kwa hakimu?

Je unategemea mwenye nyumba huyu au mtu aliyemlipia nauli ya daladala hakimu mara atakapopatwa na kosa kuhukumiwa kwa haki?

Hali hii ndivyo ilivyo hata kwa makarani wetu ambao mishahara yao ni midogo, wakati kazi wanayofanya ni kubwa sana. Kila kukicha wanacheza na mafaili ambayo pamoja na vumbi wanalolipata hawapati hata ‘allowance’ ya maziwa.

Hali hiyo inapelekea kuanza kuwaomba wateja pesa, mara nyingine kwa nia njema tu si kwa lengo la rushwa. Mara nyingi hata rushwa zinazolalamikiwa mahakamani si za mahakimu kama mahakimu ni bali nyingi zinapokelewa na makarani kwa kisingizio kwamba mahakimu wanataka chochote ili wateja washinde kesi zao.

Mara nyingine makarani wamekuwa wakituhumiwa kwa makusudi kuwa wanaficha majalada ya wateja ili tu kulazimisha rushwa kwani mteja akisumbuka sana mwisho huamua kutoa chochote.
Mara nyingi rushwa hizi ni za kati ya Sh. mia tano, elfu moja, elfu mbili hadi elfu tano.Inasikitisha sana kuona kwamba hukumu imetolewa lakini inachukua miezi mitano hadi sita kupata hukumu yake, na bado hukumu ikishachapwa kule kukabidhiwa tu na karani utasugua viatu weeeee mpaka uchoke.

Baadhi ya Makarani hata imefikia wanathubutu kuwaacha wateja na kwenda kunywa chai au kupiga soga tu na ndugu zao kwa zaidi ya masaa mawili huku wananchi wakisota tu kwenye korido za mahakama.

Kisingizio kompyuta mbovu mara mafaili mengi n.k.Yupo rafiki yangu mmoja ambaye alifungua kesi yake katika mahakama ya Kisutu hapa Dar-es-salaam, ilichukua zaidi ya mwezi kupata tu wito wa mahakama(summons) kila siku anaambiwa njoo mchana mara njoo asubuhi.Cha ajabu kesi hii ilikuwa kwa Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi kabisa,lakini utendaji wa makarani wake ukaongoza kuwa mbovu. Watumishi wa mahakama hawajali kabisa.

Wengine wamefikia hatua kuomba rushwa mchana kweupe pee hata kwa kulazimisha kana kwamba ni halali. Tatizo kubwa linalotokea hapa ni kwamba hakuna hata mfumo mzuri wa kupeleka malalamiko katika mahakama zetu.

Ukiachilia malalamiko ya rushwa hakuna mfumo mzuri wa kiutendaji wa kupeleka malamiko yanayohusu utendaji wa watumishi wa mahakama,na hata kama upo basi au haujulikani au walio na wajibu hawataki kufanya wajibu wao, kwani utakuta baadhi ya wakuu wa makarani wenyewe ndiyo wanaongoza kwa kupokea rushwa au kulalamikiwa kwa utendaji mbovu.

Ukichunguza sana utakuta kama vile makarani hawawajibiki kwa mahakimu na hivyo wanakuwa hawawaheshimu. Kwa ufupi makarani wanaharibu sifa ya mahakama kuliko mahakimu wenyewe hasa wanapokuwa na ujuzi kidogo wa sheria basi hapo hujifanya mahakimu au majaji wenyewe.Ukimkuta karani mzuri basi ni yule aliye chini ya hakimu aliyemakini na mkali sana,vinginevyo karani atakuchezea anavyoweza.

Unakuta hadi saa nyingine wanashindana na wanasheria kwa kukosoa hati zao mbalimbali wanazoziwasilisha mahakamani kana kwamba wao ndio wataalamu wa sheria.

Kundi jingine linaliochangia kuipaka matope na kuharibu uhuru wa mahakama ni Waendesha Mashitaka (PP)ambao ni watumishi wa Jeshi la Polisi chini ya IGP-Said Mwema, lakini wanafanya kazi za ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini inayoongozwa na Eliezer Feleshi,chini ya utaratibu wan chi uliopo.

Yaani baadhi ya Waendesha Mashitaka Mahakamani wanaongoza katika kuomba na kuporushwa mahakamani toka kwa ndugu na jamaa wa washtakiwa.

Hali hii hujitokeza sana pale ambapo Hakimu ametoa dhamana tena ya wazi na bure kabisa lakini mara akiachiwa tu anapokwenda kusaini na kukamilisha taratibu nyingine za polisi kama kutaka waandikiwe amri ya kutolewa gerezani, baadhi ya Waendesha Mashtaka(PP) na ndiyo huchukua nafasi yao wakishirikiana na karani husika kuwazungushazungusha na kuweka urasimu kibao na hata mara nyingine kuwatishia ndugu kwamba karandinga linakuja ili tu ndugu watoe chochote.

Pia Baadhi ya Waendesha Mashitaka wamekuwa wakituhumiwa kuaribu ushaidi katika kesi mbalimbali pindi wanapopewa rushwa na washitakwa, nasijawai kusikia wakikanusha hili, hakika ili ni tatizo na viongozi wao hawana budi kulikemea hili ili lisiendelee kuichafua mahakama zetu.

Mahakama zetu zinahitaji mabadiliko makubwa ili kukabiliana na changamoto hizi.

Ofisi za Mahakimu Wafawidhi zinapaswa kuwa wazi ili kukaribisha malalamiko ya watu na kupewa uwezo wa kudhibiti makarani wasio waaminifu katika kazi zao.

Na siyo ofisi za mahakama za Wafawidhi tu bali kuanzia ngazi zote za mahakama ziwe wazi kupokea malalamiko pia mahakama zote zitengeneze masanduku ya maoni ambayo yatawezesha raia kutumbukiza maoni na malalamiko kuhusu watumishi mbalimbali wa mahakama.

Na kuwe na tume au kamati ya utumishi wa mahakama ambayo itachukua maoni hayo na kuyafanyiakazi kama alivyokuwa kuwa akifanya Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jaji Laurian Kalegeya, alipokuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mfawidhi wa Mahakama za Dar es Salaam.

Jaji Kalegeya enzi akiwa Jaji Mfawidhi alisaidia sana kuleta nidhamu mahakamani kwa kuzitembelea mahakama mara kwa mara hasa za mwanzo,kuongea na watumishi na kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya watumishi wake wasiyowaaminifu na kuwashughulikia kikamilifu,na ili ninaushaidi nalo.

Kazi ya kudhibiti rushwa ni kweli wanaweza kuachiwa (TAKUKURU) lakini hata masuala ya kiutendaji nayo mathalani uzembe wa makarani kupoteza mafaili tunahitaji kuwaachia TAKUKURU? La hasha huu ni wajibu wa mahakama moja kwa moja na haukwepeki.

Mahakama zetu zinapaswa kuwa na kompyuta za kutosha, printa, magari au walau hata pikipiki kwa mahakimu na vitendea kazi vingine ili kazi ziweze kufanyika kwa urahisi. Aidha ilipaswa kila hakimu wa mahakama ya wilaya kuwa na kompyuta kwajili ya kurahisisha ufanisi wake wa kazi mathalani uchapaji wa maamuzi madogo madogo ya mahakama kama vile ruling na order mbalimbali.

Aidha ni jambo la aibu sana hadi sasa kwa mahakama kutokuwa na tovuti(website) ambayo maamuzi na hukumu mbalimbali za mahakama zingekuwa zinapatikana.

Nasema ni jambo la aibu kwa sababu mahakama nyingi duniani tayari zina mitandao na tovuti na idara nyingi za serikali yakiwamo mashirika na taasisi binafsi yana tovuti kwaajili ya kutolea na kupokelea taarifa mbalimbali.

Leo hii hakimu au jaji anataka asome hukumu labda ya kesi ya Takrima, mgombea binafsi nk. ina mlazimu atafute ‘Law report’ au aingie gharama ya kuja Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,ndiyo apate nakala hizo za hukumu.Mahakama ingekuwa imefungua tofuti yake hakimu au jaji huyo asingelazimika kufunga safari kuja hapa hapa na badala yake kule mkoani alipo angefungua tovuti ya Mahakama ya Tanzania na angeweza kupata na kuisoma vema hukumu hizo na nyingine nyingi.

Je, nini kinashindikana kwa mahakama zetu, je,ni kukosekana kwa vipaumbele au kutojua?

Kuwepo kwa mtandao wa kompyuta, tovuti(website) kungesaidia mambo mengi sana kwani mahakama zilizoko wilayani na mikoani zingeweza kupata mawasiliano moja kwa moja na Mahakama Kuu.Mahakimu wangeweza kupata rejea za kesi mbali mbali ambazo hazijaripotiwa kupitia katika mtandao huu.

Aidha kusingekuwa na haja ya kusubiri muda mrefu uamuzi utoke kwani ukishasomwa tu unawekwa kwenye mtandao,mtumiaji anaufungua na kuutumia.
Vilevile Jaji wa chumba kimoja angeweza kujua jaji mwenzie ameamua nini na hivyo kuepusha mlundikano wa maamuzi mengi yanayotofautiana kuhusu jambo moja.

Baadhi ya ufisadi nilioutaja katika makala hii si wa kubuni wala kutunga.Upo na unatokea kila siku mashaidi ni wananchi wanao hudumiwa na mahakama hizo ,mimi mwenyewe ni Mwandishi wa Habari wa gazeti hili kwa miaka zaidi ya mitano sasa nimekuwa nikiandika habari za mahakamani toka mahakama za Mwanzo hadi mahakama ya Rufaa hivi sasa nimeshuudia baadhi ya ufisadi huo na hasa umekithiri katika mahakama za chini ukiachilia mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

Naweza kusema kwamba kupungua kwa matatizo niliyokwisha yataja hapo juu kunatokana kwa namna moja na udhibiti na usimamizi wa karibu uliopo kutoka kwa Majaji,Wasajili wa mahakama na uchache wa mashauri yanayofika Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu.

Kwa aina nyingine uwepo wa vitendea kazi vya kisasa japo havikidhi maitaji, umechangia sana kuleta ufanisi katika mahakama hizo mbili .Hivyo niimani yangu kwamba iwapo maslahi ya watumishi wa mahakama yataboreshwa kama ya wenzao wa mahakama Kuu na Rufaa,vifaa vikaongezwa,mazingira ya utendaji kazi yakaboreshwa na usimamizi mzuri ukawepo basi hata mahakama za chini zitakuwa na ufanisi mzuri ukilinganisha na sasa.

Binafsi nina imani na Jaji Mkuu Agustine Ramadhani ambaye pia ni Brigedia Mstaafu wa Jeshi la Wananchi(JWTZ) ambaye kabla ya kuapishwa nilifanya naye mahojiano maalum ofisini kwake kuhusu historia ya maisha yake na amejipanga vipi kuongoza Mahakama ya Tanzania, ambapo aliniambia kwamba kwake ni mapema mno kutamka kuwa amepanga kufanya jambo gani na kuomba Watanzania wampe muda aingie kwenye ofisi mpya ya (Ujaji Mkuu),aangalie ofisi hiyo ina miba gani, na akae na wenzake wajadiliane mambo mbalimbali kisha anaweza kutamka kwamba amejipanga kufanya mambo gani.

Jaji Mkuu umeishaingia ofisi mpya na kiti umeishakikalia na sasa umeishaanza kukizoea na hata ile miba uliyosema nafikiri umeishaanza kuiona.

Sisi kama wananchi tuna wajibu wa kukusaidia kwa kukuonesha wapi uozo ulipo, na wapi panatukera na kutuchefua ili wewe na timu yako mjue pa kuanzia. Ombi letu kwako ni hili mahakama ifungue Tovuti yake,itandaze masanduku ya maoni katika kila makahakama na watumishi wasiyowaaminifu washughulikiwe mara moja bila kuoneana haya.

Hizo ni changamoto zinazokabili mahakama zetu na Jaji Mkuu Ramadhan unapaswa kuzifanyiakazi ili hadi ya mahakama iweze kuwepo kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Bila kazi ya ziada,hadhi ya mahakama ya Tanzania inakwisha.

Mungu Afrika,Mungu inusuru Tanzania

0755 312859; Email:katabazihappy@yahoo.com,website:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Jumapili Septemba 30, mwaka 2007

2 comments:

Ansbert Ngurumo said...

Wagira mahyo! Ninkushoma. Egi epicha yawe ekaba ekunulize!

Simon Kitururu said...

Hili jambo limenitisha sana...
Asante kwa kutustua kuhusu hili swala.

Powered by Blogger.