Header Ads

ZIARA ZA MAWAZIRI SI JIBU LA HOJA ZA WAPINZANI

Na Happiness Katabazi

HOJA ya wapinzani kuhusu tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa maadili kwa viongozi, ugumu wa bajeti na ufujwaji wa rasilimali za nchi, zimeichanganya Serikali kiasi cha mawaziri na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenda mikoani kujaribu kuondoa sumu hiyo.

Utetezi unaotakiwa utolewe na serikali si kwenda kuhutubia wananchi mikoani, ni kukaa chini na kuangalia wapinzani wametoa hoja zipi na serikali kuzijibu kwa vitendo na kitaaluma.

Mfano, Mbunge wa Karatu Dk. Willibrod Slaa, (CHADEMA) anaposema kwamba Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), alinyimwa mikataba ya ujenzi wa minara pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hawezi kujibiwa kwa mawaziri, manaibu wao na makada wa CCM kwenda kuwahutubia wananchi.

Nasisitiza na kutoa ushauri wa bure kwa Serikali, dawa ya hoja za wapinzani si kuwatoa viongozi hao wa serikali katika ofisi zao na kwenda kutangatanga mitaani kuhutubia wananchi, tena kwa kutumia fedha za walipa kodi na fedha za CCM wakati baadhi ya wana CCM wanalia njaa.

Na hata hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti habari kwamba uchaguzi wa CCM Mkoa wa Mara ulishindwa kufanyika baada ya kukosekana kwa posho za wajumbe hadi kada mmoja na mfanyabiashara wa mkoa huo, kuokoa jahazi kwa kutoa mamilioni ya fedha zake kwa ajili ya posho za wajumbe wa mkutano huo na hatimaye ukafanyika.

Ziara hizo hazina maana yoyote zaidi ya ufujaji wa fedha za umma. Binafsi najiuliza kama ni kwenda kunadi Ilani ya CCM leo hii, ina maana wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, iIlani hiyo haikunadiwa, na kama haikunadiwa vizuri ni vipi CCM ilishinda kwa kishindo?

Serikali ijibu hoja na kama inaona wapinzani hususan Dk. Slaa amechafua jina la viongozi, basi akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Hiyo ndiyo dawa ya kujibu hoja za wapinzani.

Dk. Slaa anaposema Kampuni ya Meremeta haimilikiwi kwa asilimia 100 na serikali, badala yake inamilikiwa kwa asilimia 50 na asilimia 50 iliyobaki inamilikiwa na Kampuni ya Trinex ya Afrika Kusini, je, uzushi uko wapi katika hili?
Je, hati ya Brela ya kutambua usajili wa kampuni hiyo uliofanywa kwenye visiwa vya wakwepa kodi huko Uingereza je, ni uongo?

Dk. Slaa ameuliza katika hoja yake kwamba, je, Serikali ya Tanzania haikushiriki kwenye ufisadi kwa kufungua kampuni ya wakwepa kodi, kwanini serikali haitaki kueleza ilipofungua kampuni Uingereza katika visiwa vya Ilse of Man ilikuwa inakwepa kodi ya nani?

Na je, ni halali kwa serikali yetu kuanzisha kampuni hizo zinazotuhumiwa kuwa ni za kifisadi? Hoja kama hii isipojibiwa vizuri Watanzania tutaichoka serikali.
Labda ni vizuri pia kuuliza Kampuni ya Meremeta ilifanya biashara gani kustahili kulipwa mabilioni kutoka BoT na iliingizia taifa faida gani?

Sisi wananchi wa kawaida tukiamini kwamba Kampuni ya Meremeta iliundwa kwa madhumuni ya kuchota fedha za BoT na kuzipeleka nje ya nchi, tutakuwa tumekosea?
Kwaninii hata ilipofilisika hatuambiwi nani aliteuliwa kama mufilisi wa kampuni hii? Kwani serikali haijaeleza kuhusu madeni yote ya kampuni hiyo mufilisi.

Watanzania tunataka kujua, hiyo Trinex ya Afrika Kusini iliyolipwa kwa fedha za walipa kodi ni ya nani? Sasa haisaidii serikali kutapatapa na kukurupuka kujibu kashfa hii wala kuwahutubia wananchi hakutasaidia serikali kujikosha.

Hoja ya Dk.Slaa tumeielewa na hii ni mara ya pili nasisitiza inahijati majibu thabiti na si ya ‘mipasho’. Serikali ijue kwamba wananchi si mbumbu kiasi cha kutong’amua ukweli wa mambo.

Alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam, Mzee Kingunge Ngombare-Mwiru, aliwabeza wapinzani na kusema hoja zao zimejaa uzushi, uongo na wana wivu, kwa sababu CCM iliwashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, na sasa wanaona wivu kwamba serikali inatekeleza ahadi za kuleta maisha bora, imejenga shule nyingi za sekondari.

Kitu ambacho mzee Kingunge amesahau ni kwamba tayari serikali ipo madarakani na yeye ni waziri na hakuna mpinzani aliyekwenda mahakamani kupinga kutokuitambua serikali iliyopo madarakani.

Kwa hiyo, hoja ya Kingunge hata kama alitumwa na serikali kama alivyodai, ni ya kukurupuka na ailengi wala kujibu hoja ya vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Kwa kuwa hoja ya wapinzani ni ufisadi, wizi wa mali za umma na uvunjwaji wa maadili ya viongozi unaofanywa na viongozi wakuu wa ngazi za juu za serikali na CCM, jibu la mzee Kingunge liko nje ya mada.

Hata pale Kingunge alipo wadharau na kusema serikali ina mengi ya kufanya na kwamba haitawafuatilia wapinzani mikoani kujieleza kwa wananchi, tayari serikali hiyo hiyo ya kina mzee Kingunge imesalimu amri na imeteua timu yake ya viongozi kwenda kuzima moto wa wapinzani.

Kwani Mawaziri, Manaibu Waziri na Bendi ya TOT-Plus, Katibu Mkuu wa CMM Yusuf Makamba na makada wengine , wamepangwa mikoani wakijaribu bila mafanikio makubwa kujikosha mbele ya wananchi na kujaribu kukanusha hoja za wapinzani.

Kinachojidhiirisha ni jinsi serikali inavyojikang’anya katika suala hili. Haionekani serikali ina majibu yanayoeleweka kukanusha hoja za wapinzani. Hivyo kila kigogo aliyeguswa na tuhuma hizo anakurupuka na kutoa maelezo yake yanayopingana na vigogo wenzake kana kwamba serikali haina msemaji mmoja wa kueleweka.

Chakuchekesha zaidi ni pale baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi walipotishia bila mafanikio makubwa kumshitaki Dk. Slaa, gazeti la Mwanahalisi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto.

Kitendo cha kutotimiza vitisho vyao kinaonyesha uwoga walionao wa siri nyingi zinazowahusu kufichuliwa mahakamani.

Tunawapa ushauri waheshimiwa watuhumiwa wa ufisadi kwamba wakubali kujiuzulu badala ya kungoja wananchi kufumuka kwa maandamano yanayoweza kusababisha ghasia na wao wenyewe kucharazwa bakora na umma wenye 'hasira takatifu'.

Ieleweke wazi kwamba japo Watanzania wanasemekana kuwa ni binadamu ambao nyonga yao ya hasira iliondolewa na wakunga walipozaliwa, itafika siku vifuko vyao ya nyonga vitajaa nyongo ya hasira takatifu na watakapoanza maandamano itakuwa ni vigumu kuwadhibiti.

Tunaamini bado nchi yetu ina viongozi angalau wachache wenye busara ya kutambua ukweli, hivyo kuwashauri watuhumiwa wa ufisadi kung’oka madarakani.

0755 312859;katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Alhamisi ya Oktoba 4,mwaka 2007

7 comments:

Anonymous said...

Katika Makala yako ya leo umesema kama vile critical thinker na ndio maana ya usomi. Wao CCM kama wanataka kwenda huko kupiga soga basi wameseme maswali ya Msingi na kutoa majibu sio Umbumbu wao katika suala hili.. Waseme kama Mkataba wa Buzwagi amesainiwa au vipi?? Waseme pia kama Kampuni ya Meremeta ipo Tanzania au vipi na pia waseme kwa Kisomi kwa watu sio kusema tu hoo wapinzani tunahitaji majibu sio utapeli wao. Pia Happy ujue kuwa sio wataichoka CCM tumeshaichoka Tayari sasa hivi tunasubiri wakati ufike tuu...CCM hivyo Mna nini nyie watu??Mbona matapeli wa watu wenu na watoto wenu wenyewe?? hivyo mnafanya kama vile sio NCHI yenu..!! Wewe Makamba na Wao timu yako Tumewachoka Kabisa.
Josh Michael Colorado Marekani
PS: Ukiona na kujua utumbo ndani ya CCM ni Kinyaa kitupu

Anonymous said...

Dada Happy hao majambazi wa kalamu wanaogopa kujiuzulu maana wanajua kufanya hivyo kwanza watakosa hadhi ya kulipwa mafao yao na pili watajiweka katika hali mbaya zaidi maana watakuwa wameacha mwanya wa kupatikana kwa ushahidi.Sisi tuache wajidanganye kuwa tumelala uchaguzi ukifika tuwaondoe kwa kura maana hawataki kutoka kwa hiyari yao na hapo ndio tutapata serikali ya kuwashughulikia kisawasawa!

Anonymous said...

Makala yao ni nzuri na umeonyesha ni jinsi gani watu wanavyohitaji majibu ya msingi na si 'mipasho' kama mwenyewe ulivyoiita. Inasikitisha kwa nchi ambayo wananchi wake wengi ni mafukara kiasi cha kushindwa hata kupata mlo mmoja kwa siku, viongozi wanadirik kutekeza rasilimali za nchi kwa ziara zisizo na tija! Hii serikali yenye wizara 60, isiyojali gharama, isiyojali watu wake, itiayo nta masikioni, yenye kiburi, yenye ufedhuli - inajidanganya. Za mwizi ni 40, na inaelekea40 ndo inakaribia. Watajibalaguza lakini kwa taarifa yao wananchi wameshaanza kujua ukweli na UKWELI UTATUWEKA HURU. Dawa yao imeshachemshwa na sasa tutawalazimisha wainywe na hakika wataimeza na tutaona mwisho wake! UNGU IBARIKI TANZANIA.

Anonymous said...

baada ya kuipitia taarifa ya serikali kuhusu buzwagi naona kodi itaanza kutozwa mwaka 2009! mi hili kwa upeo wangu mdogo na kulinganisha ugumu wa maisha nakuwa siielewielewi serikali yetu,
kwa mfano mfuko wa sementi huku morogoro sasa ni shilingi elfu 15!
wangeanza sasa kuchukua kodi yao 2009 ni mbali sana

Simon Kitururu said...

Kazi kweli kweli!Mungu ibariki Tanzania!

Anonymous said...

Dada kazi kwako na wivu wako...wewe upendi CCM au vipi? basi Chadema wakiingia madarakani utakuwa mwandishi mkuu wa Rais Freeman Mbowe.
John

Rashid Mkwinda said...

Huyu jamaa wa mwisho ambaye ameamua kuficha jina lake ana mtazamo ule wa mwaka 47, hajui nini kinaendelea chini ya jua hili, lakini itafika mahali naamini atakubali zipi chenga na zipi chuya kwani wengi tulikuwa wa aina hii na sasa tumebadilika.

Angalia jinsi nchi ilikotekea ilipo na kule inakoelekea ndipo utakapo jua nini kilichopo na nini kinahitajika katika kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini katika falsafa iliyoasisiwa serikali ya awamu ya tatu MKUKUTA

Powered by Blogger.