Header Ads

SERIKALI IWE MAKINI NA UTITIRI WA MAKANISA

Na Happiness Katabazi

IBARA ya 19(1) ya Katiba ya nchi, inasema kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.

Ibara ya 19(2) inasema kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Kwa mujibu wa vifungu hivyo vya ibara hizo, tunaona taarifa zilizolisibu Kanisa la Assemblsy of God la Mikocheni B’ linaloongozwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM)Mchungaji Dk.Getrude Rwakatare hivi karibuni kwamba watoto wachawi wawili, waliokuwa wanasafiri kwa ungo walivutwa na kudondoka katika eneo la ibada la kanisa hilo, ni za kusikitisha sana.

Kwanza, habari hizo zina lengo la kupambanisha imani ya kichawi na imani ya Mungu. Lakini zote ni imani, na tayari ibara 19(1) ya Katiba inampa kila mtu haki ya kuwa na imani anayoitaka.

Hao wanaoamini katika kusafiri kwa ungo nao wana imani inayolindwa na katiba sawa na wanaoamini imani ya Yesu.Kwa hiyo tunashangaa ni kwanini watu waanze kuadhiriana kwa mambo yasiyo ya msingi, au labda ni ya kitapeli, ya kutafuta biashara ya waumini.

Lakini tujue kwamba, hili linatia dosari kwa wale wanaotangaza na kueneza dini, japo ibara 19(2) imewalinda na kuwahakikishia kwamba serikali haitaingilia shughuli za uendeshaji wa jumuiya za dini, watakapofanya mambo yanayoweza kuvunja amani ya jamii au hata kuhatarisha maisha ya waumini wao, dola haitakuwa na budi kuingilia kati.

Uhuru wa kuabudu hauwezi kutumika pale baadhi ya wachungaji watakapogeuza taasisi za dini kuwa vyombo vya ufisadi, ambapo matendo machafu yanayovunja maadili, biashara chafu zinazoenda kinyume cha sheria na utapeli wa kawaida unafanyika.

Tukumbuke mfano mmoja wa Uganda pale mchungaji mmoja aliyeitwa Kibwetere alipoangamiza wafuasi wake kwa kutumia wafuasi wa dini.

Jambo kama hilo hilo liliwahi kutokea Novemba 18 mwaka 1978 nchini Guyana, ambapo James Warren aliyejulikana kwa jina la Jim Jones alipounda kanisa lake kule Guyana katika visiwa vya Caribbean na kuua waumini wake 900 kwa sumu ya cyanide, wanaenda kumuona Yesu.

Basi, kwa kuwa dunia imejaa matapeli wa aina hii na dini sasa hivi zimekuwa biashara kubwa hapa nchini ambapo baadhi ya wajanja anakimbilia huko, ingefaa jamii itahadharishwe kuwa si kila anayehubiri dini ni kweli ni mtumishi wa Mungu.

Wapo manabii na watumishi wa Mungu feki wengi sana huko mitaani na yafaa wananchi wachukue tahadhari, kwani hawa wanasingizia kufanya miujiza lukuki na kutoa upako kwa jinsi ambavyo ni ya kushangaza.

Hivi sasa kuna kanisa limetangaza kutoa misukule. Yaani mtu aliyefariki miaka mitano au zaidi iliyopita, eti mchungaji anaweza kumrudisha? Hii inatisha!

Wanajua wananchi wengi wako katika hali ngumu ya maisha, wanakabiliwa na umaskini wa kupindukia, maradhi yasiyoponyeka kama ukimwi, kansa, na msambaratiko wa maisha ya ndoa, basi kwa kuhisi kuwa wana ufumbuzi wa haya yote, wanafanya ibada feki za kuwahadaa wananchi.

Kwa upande mwingine, tunaitahadharisha serikali kwamba utitiri wa taasisi za kidini ni ishara mbaya kwa utawala uliopo madarakani.

Ina maana kwamba hayo matatizo tuliyoyataja hayajapatiwa ufumbuzi na wananchi wamekata tamaa, hivyo ni rahisi kughiribiwa na wajanja wanaotumia dini kujinufaisha.

Tusije tukashangaa yale ya Jim Jones na Kibwetere yakitokea hapa Tanzania na hilo linaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Tujiulize maswali, je, hawa watoto matapeli ambao Jeshi la Polisi Kinondoni lina rekodi zao, waliwezaje kumhadaa mchungaji mwenye aiba ya upako wa Roho Mtakatifu kama Dk.Rwakatare?

Tujiulize pia kazi iliyofanywa na taasisi za dini kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, na baada ya hapo, mbona viongozi wa dini na madhehebu ya Kikristo walishiriki kuwarubuni waumini wao kupigia kura mgombea waliyemtaka kwa madai kuwa mgombea huyo alikuwa amechaguliwa na Mungu wao?

Je, huo haukuwa utapeli wa wazi? Walikutana wapi na Mungu wao akawanong’oneza kwamba mwanasiasa huyo alikuwa chaguo lake?

Tangu lini mtu asiyemwamini Yesu kuwa ni mwana wa Mungu na Mungu kamili kwa sura ya binadamu na kwamba alikufa na kufufuka, akawa chaguo la Mungu wa Wakristo?

Mbona hata baadhi ya viongozi wa dini wametumia nafasi zao za dini kujitafutia vyeo kwenye vyama vya siasa?
Je, hizo sadaka na michango wanayopokea kutoka kwa mafisadi na hizo shughuli za uchangishaji wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa kidini unaofanywa na wanasiasa na baadhi ya mafisadi wanaojulikana, ndiyo njia muafaka ya kueneza shughuli za dini?

Sasa mwananchi wa Tanzania akimbilie wapi, akienda kwenye dini anakuta ufisadi, akienda kwenye jamii anakuta ufisadi, akienda kwenye siasa anakuta ufisadi, sasa kimbilio la Mtanzania litakuwa wapi?

Matukio ya kiimani yanayotokea katika baadhi ya makanisa siku hizi, yatufumbue macho na masikio ya kila mmoja wetu, kwani nyakati zimebadilika, viongozi wametugeuka na hakuna wa kumuamini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Machi 3,2008

1 comment:

Anonymous said...

happiness katabazi

kwa ujumla naunga mkono hoja yako ya serikali kuwa makini na kudhibiti tabia mpya ya kila mtu kuwa na kanisa lake. ijapokuwa hukuwa na mifano mingi ya hapa nchini, ni wazi kuwa huo ni moto unaofuka kuna siku utalipuka na kuangamiza jamii. kuna kisa cha karibuni kabisa huko nyanda za juu kusini ambapo waumini wa kanisa moja walihamia msituni kumsubiri yesu. hii inashangaza.

imani ya dini ni very sensitive, na inahitaji kuwa makini katika kuishughulikia. lakini hiyo isiikatishe tamaa serikali au kuhofu kuwa italaumiwa kwa hatua itakazochukuwa.

mbali na uliyoyaeleza, hivi karibuni kumezuka mtindo wa kila dhehebu la kikristo au kanisa kutaka lipewe eneo lake maalum la kuzikia pale muumini wao anapofariki. mimi hujiuliza kwani akizikwa katika makaburi ya mchanganyiko na waumini wenzake wa madhehebu mengine ya kikristo kuna ubaya gani. wenye kutaka maeneo hayo hudai kuwa yale ni makaburi ya rc au sabato au anglikan na sisi tunataka eneo letu.

hili ni jambo la aibu. hivi kuna yesu wa rc au wa wasabato au lutheran pekee? yesu ni mmoja na kama wote tunamkubali iweje dhehebu litake eneo lake pekee yake la kuzikia? huo si ubaguzi na kujitenga? ingekuwa ni imani tofauti kama waislam au wahindu au budha isingekuwa tatizo lkn imani moja sasa kwa nini watu wajitenge?

hivi kwa utitiri huu wa makanisa kila kukicha serikali kweli itaweza kulipa kila kanisa eneo lake la kuzikia? au hawa wanaoanzisha madhehebu mapya wanataka serikali ishindwe kuwapa maeneo baadae waiilaumu na kuiita ya kishetani?

umefika wakati sasa kudhibiti madhehebu au anaeanzisha kanisa lake atoe hoja ya msingi kwa nini asifuate madhehebu yaliyopo kama rc, lutheran, sabato, angilikan nk. iwapo hoja yake itakuwa ya msingi basi anaweza kuruhusiwa lkn kama hoja hana basi serikali isikubali.

kuhusu kujitenga kwa kuwa na maeneo ya kuzikia maiti kimadhehebu hili lisiruhusiwe kabisa. maeneo ya kuzikia yatengwe kwa imani za kidini na sio kwa imani ya kimadhehebu kwa kila mkristu kuwa na eneo maalum kulingana na kanisa lake.

ahsante. kama kuna maoni yoyote kutoka kwa msomaji, nitumie sms (usipige) kupitia 0713 414234

Powered by Blogger.