Header Ads

NAMLILIA DITOPILE




Na Happiness Katabazi

ILIKUWA juzi saa 4:39, asubuhi, nikiwa nimeketi sebuleni na kunywa chai nyumbani kwetu Sinza ‘C’, nilipokea simu kutoka kwa mfanyakazi mwenzangu ambaye ni mchora katuni aitwaye, Said Michael ‘Wakudata’ akiniambia rafiki yako, Brother Ditopile, amefariki dunia.


Nilishtuka na ghafla mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio huku mikono ikitetemeka na kusababisha simu yangu ya kiganjani kuanguka kwenye zulia.

Kwakuwa hapo sebuleni nilikuwa nimekaa na mama yangu mzazi na kaka zangu, mama yangu alishtuka, akanikaribia na kuniuliza kulikoni? Ndipo nilipomweleza kwamba nimepokea simu inayosema rafiki yangu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (60) amefariki dunia.

Kwakuwa mama yangu naye alikuwa akimfahamu Ditopile, alishikwa butwaa. Kwakuwa siku hizi taarifa za kuzushiana vifo zimekuwa za kawaida ndani ya taifa hili, sikutaka kuziamini moja kwa moja taarifa hizo, niliamua kuokota chini ile simu yangu na kuanza kupiga kupitia namba zake (Ditopile) zote nne, ambazo nilizitumia kuwasiliana naye mara kwa mara.

Nilipokuwa napiga simu kwenye line zote hizo, line zote zilikuwa hazipatikani. Ndipo nilipochukua uamuzi wa kumpigia simu aliyekuwa Katibu Mkuu wa timu ya Ashanti, Arafat Said, kwa kuwa marehemu alikuwa ni mlezi wa timu hiyo, kumuuliza kuhusu tukio hilo, naye alinithibitishia ni kweli. Nikabaki nimejiinamia kwa simanzi kutwa nzima na kuishia kumwombea kwa Mungu.

Mara ya mwisho kuwasiliana na Ditopile ilikuwa ni Ijumaa saa mbili usiku ya wiki iliyopita.
Alinipigia akaanza kwa kunitania kwamba muda si mrefu nitakuwa mkwe wake kwa mtoto wake wa kiume aitwaye Ramadhani, ambaye yupo masomoni Uingereza.


Nikamjibu kwa kumtania kwamba sitakuwa tayari kuwa na baba mkwe ambaye ni chakaramu kama yeye, akajibu kwamba hiyo ndiyo tabia yake tangu mdogo, hivyo hawezi kuibadili ukubwani na kwamba yeye ataongoza msafara wa wazee wa Pwani kwenda kwa mzee Katabazi kumchumbia paparazzi (yaani mimi), ili familia yake iwe na mwandishi wa habari, kwani waandishi wa habari ambao enzi za uhai wake alipenda kuwaita paparazzi, walimuandika sana kwa mabaya yake na mazuri yake.

Baada ya kunieleza hayo, nilimweleza kwamba kuna mtoto wako aitwaye Ramadhani Mzuzuri, mapema wiki iliyopita alitembelea blog yangu na kuniachia ujumbe wa kupongeza kazi zangu, nami nilimuliza Ramadhani kwakutumia e- mail kwamba Ditopile ni baba yake na kama ni baba yake basi mimi rafiki yake.

Nilivyomweleza hivyo Ditopile, akaniambia hiyo ni sababu moja wapo iliyosababisha anipigie simu siku hiyo na akanieleza kweli yule ni mtoto wake.Baada ya kumaliza hadithi hiyo akaniomba nimsaidie kufahamu kesi yake imepangwa lini na kwa jaji yupi.


Nilimwambia kuwa nipe sekunde chache nitoe kitabu changu cha kumbukumbu ili niweze kukutajia tarehe, nikamweleza kwamba kesi yake itatajwa kwa mara ya kwanza Aprili 24 mwaka huu, mbele ya Jaji Njegafibili Mwaikugile.

Alishukuru na kuniambia: “Eh siku hiyo mapaparazzi wenzio wamejiandaaje kuja kunipiga picha?” Nilimjibu huku tupo timamu na kwamba siku hiyo tutahakikisha tunazingira pembe zote za Mahakama Kuu bila yeye kujua ili kuhakikisha tunaipata sura yake.Akacheka sana, akasema mapaparazzi mna taabu kweli.


Namlilia rafiki yangu Ditopile kwani tangu atoke jela nimekuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara kwa simu. Ila mara ya mwisho kuonana naye ana kwa ana na kuzungumza naye kwa takriban saa mbili ilikuwa ni Desemba 9, 2006 ndani ya Gereza la Keko alipokuwa amewekwa rumande.

Kama inavyofahamika, waandishi wa habari huwa hawaruhusiwi kuingia magerezani, lakini mzee Ditopile alimtuma mtu anipigie simu niende kumuona gerezani, ila nikifika pale gerezani nijitambulishe kwa jina bandia la Koku Katabazi, nimetokea mkoani Kagera na kwamba nivalie mavazi ya gauni kubwa na kitambaa kichwani ili maofisa magereza wa gereza hilo wasinitambue.

Kweli nilifanya hivyo na kabla ya kufikia sehemu ya kujiandikisha kwenye daftari la wageni, nilinunua maji chupa makubwa na mkate na tayari kusubiri niitwe jina la kuingia kumuona Ditopile.

Nilivyoitwa jina hilo, nilishtukia nadakwa kiaina na ndugu na jamaa wa mzee Ditopile na wakanieleza nisiwe na wasiwasi watanipeleka gerezani anapolazwa.

Kweli ilipofika zamu yangu, niliingizwa ndani ya gereza huku nikiambatana na ndugu yake mmoja ambaye ni mtu mzima kiumri, nikapandishwa sehemu ya kuzungumzia wageni ambapo ni hatua tano kutoka chumba alichokuwa akilala yeye na wenzake maarufu kwa jina la ‘Sick Bay’.

Baada ya kufika na kuketi kwenye kiti, Ditopile alitoka chumbani akaja kuzungumza nami, nilishindwa kujizuia nilibubujikwa machozi. Akaniita jina langu akisema na ujanja wako wote unalia? Nilimjibu kuwa jela si kuzuri, hasa anapopelekwa mtu unayemfahamu.
Akanijibu kwamba yote ni mipango ya Mungu na tumuachie Mungu.

Nilianza kumuuliza maswali ya hapa na pale kwamba ni kweli alikuwa amemuua yule dereva wa daladala, Hassan Mbonde (33), alisema ni kweli Novemba 4 mwaka 2006, alimuua kwa kumpiga risasi, ila hakuwa amekusudia kufanya tukio hilo, kwani dereva wa daladala aliligonga gari lake na alipowaambia kwanini waliligonga, dereva huyo alimtukana kwa kumuonyesha ishara ya kidole cha katikati.

“Happiness, kwakweli kwa utu uzima niliokuwa nao, wadhifa niliokuwa nao kweli mtu dereva alinigonga na nilipomhoji alinitusi kwa kutumia kidole cha katikati ya mkono wa kulia…kwakweli niligadhabika sana nikajikuta nachomoa silaha na kumfyatulia, licha ya kwamba halikuwa lengo langu.

“Siwezi kukana kwamba sikumuua yule dereva, ila nilimfyatulia risasi kutokana na hayo aliyonifanyia, ila naomba Mungu na ninaendelea kumuomba Mungu anisameheme, kwani hata vitabu vya Mungu vinakataza binadamu kutoana roho…hivyo tuiachie mahakama ndiyo itaamua,” alisema Ditopile.

Baada ya kumaliza mazungumzo yetu siku hiyo ambayo taifa likikuwa likisherehekea uhuru wake, nilimuaga kwamba nakwenda, akanisii nisimtupe kwa sababu yupo jela, niwe napita kumjulia hali na kumpatia taarifa mbalimbali, nikamkubalia.

Baada ya kuondoka gerezani hapo, kilichofuata, alikuwa akiletwa kwa nyakati tofauti katika Mahakama ya Kisutu na hatimaye Mahakama Kuu ambapo ndipo kituo changu cha kufanyia kazi.

Machi 9, mwaka jana, viwanja vya Mahakama Kuu viligeuka kuwa uwanja wa mapambano kabla na baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, kufikishwa mahakamani hapo na kutolewa kwa dhamana.

Mapambano hayo yalifanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni ndugu wa mshitakiwa Ditopile dhidi ya waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia mwenendo wake. Nami nilikuwa mmoja wao.

Machi 10, 2007 ambayo ilikuwa siku ya Jumamosi asububi, nikiwa na Mwadhiri Mwandamizi wa Sheria na Katiba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, nilipokea simu ikisema: “Sura yangu mnaitakia nini au mmetumwa na waganga wenu muichukue mkaniroge?”
Nikamuuliza aliyenipigia alikuwa nani, akanijibu kuwa: “ Ni mimi mzee wako Ditopile.” Nilicheka.

Nikacheka sana, ila nikamweleza wazi kabisa kwamba sikufurahishwa na vurugu zilizofanywa na ndugu zake, kwani zilikuwa zikizuia waandishi wasifanye kazi yao, pia lionyesha kuwa familia yake ina watu wa namna gani. Akasema tumsamehe, na nilipomhoji ni kwanini anavaa kofia kubwa ‘pama’, alisema anaivaa kwa makusudi ili wapiga picha wasiipate sura yake kwa urahisi.

Akaniambia kuwa: “Wewe ni mwandishi gani umeingia gerezani kuniona ukashindwa kupiga picha mazingira ya Gereza la Keko?”

Nikamjibu kuwa nisingeruhusiwa. Akaniambia pamoja na sheria kukataza yeye alitumia mbinu zake za kijeshi na alifanikiwa kupiga picha mazingira ya gereza hilo na jinsi mahabusu wanavyolala na wala hajawahi kukamatwa na askari magereza na picha hizo amezihifadhi nyumbani kwake.

Kwa wale wanaomfahamu marehemu, lazima watakubaliana nami kwamba Ditopile alikuwa ni mtoto wa mjini, mwenye kupenda masihara na mzaa, muwazi na mwongeaji kupita kiasi, na mara nyingi nilipokuwa nikionana naye au kuzungumza naye alikuwa akiniasa nipende kusali, kuishi vizuri na watu na alinisisitiza nijiendeleze kielimu, kwani elimu ndiyo mkombozi katika ulimwengu wa sasa.

Pia aliniasa kufanya kazi kwa bidii na kwamba ujumbe huo niusambaze hata kwa vijana wenzagu.Aliniambia kuwa wakati akisoma Chuo Kikuu wakati wa likizo alikuwa na ubao wa kuuza mboga na matunda katika Soko la Ilala, hivyo alikuwa akifanya biashara hiyo.

Pia aliwahi kuuza magazeti ya Daily News katika mitaa ya Masaki na Oysterbay. Na alisema kazi hizo zilikuwa zinamsaidia kuongeza kipato. Baada ya kuniambia kwamba aliwai kufanya kazi hizo, nilimwangalia usoni nikajikuta naangua kicheo kwa sauti ndani ya ofisi yake ya mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Akauliza: “Unacheka hizo kazi?” Akaniambia mwanangu hadi leo hii mnatuaona tunateuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, mkae mkijua tumetoka mbali.”

Hatukuishia hapo, tuliendelea kuwasiliana kwa simu na hata Januari 6 mwaka huu, baada ya yeye kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba waandishi wa habari, Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, wamemwagiwa tindikali, alinipigia simu akasema yupo mkoani Lindi, akasema amesikitishwa na tukio hilo na kwakuwa haishi utani aliniambia wakati umefika sasa mapaparazzi tuanze kuvaa ‘pama’ kama yeye ili watakapotumwagia tindikali isituingie machoni.

“Mapaparazzi anzeni kuvaa pama kama mimi ili mkimwagiwa tindikali isiwaingie machoni au wasilianeni na mimi niwaonyeshe duka niliponunua pama langu,” alisema.
Niliishia kucheka.

Ndugu msomaji mapema mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba Ditopile alikuwa akiuza asali, na kweli hadi anafariki dunia alikuwa akifanya biashara hiyo, ambayo aliwahi kunieleza kwamba inamuingizia kipato kizuri.


Baada ya taarifa hizo kutangazwa, alinipigia simu akiniambia kwamba: “Waandishi hamna dogo, mimi kuuza asali imekuwa nongwa?” Akaniambia mbona Mwenyekiti wenu wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Reginald Mengi, anauza soda za Coca Cola amuandiki? Mbona bosi wako Freeman Mbowe anauza pombe kwenye ukumbi wake wa Billicanas auandiki? Nilishindwa kumjibu kwani nilicheka sana, akaniambia usicheke.

Katika viongozi wa CCM hakika naweza kusema kiongozi ambaye nilikuwa naye karibu kikazi na aliyekuwa akinipa ushauri mbalimbali alikuwa ni Ditopile, alinichukulia kama mwanawe, hakika Ditopile nakulilia.

Hakuwa na majivuno kama walivyo viongozi wengine, hata wakati alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani nilipokuwa nikipata nafasi, nilikuwa nikipita kumsalimia ofisini kwake.

Ni Ditopile huyu huyu, siku moja kabla ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika utawala wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete, kwenda kujitangaza rasmi kugombea urais katika ofisi za Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Pwani, Kibaha, alinipigia simu saa tatu usiku akiniambia: “Wewe si unataka ‘scoop’” (habari moto), akaniambia kesho saa mbili asubuhi panda gari kisha shuka stendi ya mabasi Kibaha.



Nilipomuuliza kuna habari gani mbona hataki kuniambia, akaniambia Nimwamini yeye na kwamba kesho yake nifike bila kukosa.

Kwakuwa nilikuwa nikimuamini na kumheshimu, kesho yake ambayo ilikuwa ni siku ya Jumapili, nilifanya hivyo nikapanda gari la kwenda Kibaha pale Ubungo, na kabla ya gari kuondoka Ubungo, alinipigia simu akiniuliza nilikuwa nimefika wapi, nikamweleza ndiyo tunaondoka Ubungo, akasema sawa.

Lile gari lilipofika stendi ya Kibaha, ghafla nilipokea simu nyingine kutoka kwake akiniuliza nilikuwa nimefika wapi, nikamwambia nimefika stendi ya Kibaha, ilikuwa saa 3 asubuhi.

Akaniambia nikodishe teksi nimwambie dereva anipeleke CCM Mkoa wa Pwani, nilifanya hivyo. Nilipoanza kuingia ile njia ya vumbi kuelekea kwenye ofisi hizo, nikaona kumepambwa bendera za CCM. Nikamuuliza yule dereva kulikoni? Akaniambia kuwa hata yeye alikuwa anashangaa.

Nilipofika kwenye ofisi hizo za CCM saa nne asubuhi nikakuta wafuasi na viongozi wa CCM wametanda huku viti vikiwa vimepangwa na nikabahatika kumkuta mpiga picha wa TvT, sasa TBC, Chris, nikamuuliza kulikoni? Akaniambia Kikwete siku hiyo anakuja kujitangaza rasmi kwamba atagombea urais.

Aidha, baada ya dakika chache, Ditopile akaniambia: “Umekwishafika?” Nikamjibu, ndiyo.
Akasema: “Eh umekuta nini au umesikia nini?” nikamwambia nimeambiwa kwamba muda mfupi ujao Kikwete atatangaza rasmi azima yake ya kugombea urais, akasema ni kweli na akaniambia hiyo ndiyo ‘surprise’ yake kwangu na kamwe sitakuja kumsahau kwani tukio lile lilikuwa ni la kihistoria. Ni kweli sitamsahau.

Wana CCM walitutangazia kwamba Kikwete angefika pale saa tano kujitangaza lakini alifika saa saba na nusu mchana. Na ilipofika saa sita Ditopile na alinitafuta na kunitambulisha kwa mkewe aitwaye Tabia, kasha tulisalimiana.

Nakumbuka enzi za uwahi wake aliwahi kuniambia kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari akawa anasema anafuata masharti yote ya daktari. Na alikuwa aishi utani, nakumbuka kuna siku nikiwa ofisini kwake Pwani nilimkuta anakunywa chai na mkate wa kumimina nikamuuliza kulikoni na mikate ya kumimina asubuhi, akasema ni miongoni mwa kitafunio anachokipenda.

Nasema tukio hili sitalisahau kwakuwa lilihudhuriwa na wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam na walianza kufika eneo hilo saa tano hadi saa saba.

Baadhi ya wahariri walionikuta hapo walishikwa butwaa na kuniambia wewe umepataje taarifa hizo, nikawaambia kwa njia zangu hasa ukizingatia kipindi hicho nilikuwa bado mwandishi mchanga sana na hata nilivyoandika habari ya tukio lile nakumbuka habari ile nilinyimwa ‘by line’ na mhariri wangu bila sababu za msingi.

Nakulilia Ditopile ambaye haupo tena nasi duniani, ila mazuri uliyoachia tutayafuata na kuyatekeleza kwa vitendo.Hata hivyo Ditopile kama walivyo binadamu wengine alikuwa na upungufu na udhaifu na mabaya yake, hatutayafuata.


Mwanasiasa wa siku nyingi Ditopile amefikwa na mauti Jumapili iliyopita. Alifikwa na mauti katika Hoteli ya Hilux ya mjini Morogoro.

Nimemfahamu Ditopile kwa miaka sita sasa na hadi sasa kuna baadhi ya watu ukiwaeleza kwamba Ditopile ana elimu ya chuo kikuu wanakukatalia kutokana mzaha wake.

Ditolipe ndiye mwasisi wa msemo wa ‘halo halo’. Ambaye amekuwa akisema yeye si mtu wa kuja, bali yeye ni mzaliwa wa jiji hili na amezaliwa wodi ya ‘Makuti’ enzi hizo ilikuwa ndani ya Hospitali ya sasa Taifa ya Muhimbili.


Ditopile aliitimu shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, aliajiriwa na Chama cha TANU kama Katibu Msaidizi, Makao Makuu. Na kutokana na utendaji wake mwaka 1980 alikwishafikia cheo cha Katibu Msaidizi Mkuu Daraja la Kwanza.

Machi 1983, aliteuliwa kuwa Katibu wa Wilaya wa CCM katika wilaya za Serengerema na Tabora mjini. Nyota yake ilianza kung’ara, na mwaka 1982 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM .Mwaka 1996 hadi 1997, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara.

Ditopile alikuwa ni miongoni mwa vijana sita waliokuwa wameamua kujiunga na utumishi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) mara baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu mwaka 1973.

Baada ya kujiunga na utumishi wa TANU , Ditopile alijiunga na Chuo cha Itikadi na Propaganda Kivukoni, wakati ule kikiitwa Chuo cha Chama. Baada ya kumaliza mafunzo ya Itikadi na Propaganda, alirudi makao makuu ya chama, na hapo alipewa jukumu la kuanzisha maktaba ya CCM ambayo hadi leo ni ya chama tawala.


Pia alikuwa ni mtumishi mwaminifu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakati wa utumishi wake alikwenda katika Chuo cha Maofisa Monduli, alikochukua mafunzo ya uafisa wa jeshi.

Pamoja na nyadhifa hizo , Ditopile aliwai kuwa mbunge wa Jimbo la Ilala katika miaka ya 1980. Aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Naibu Waziri wa Mawasiliano.

Pia alipata kuwa mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kigoma, Lindi, Dar es Salaam na Tabora.
Ditopile alizaliwa Machi 7, mwaka 1948 katika Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam. Alisoma Shule ya Msingi Mchikichini, Dar es Salaam kati ya mwaka 1956 na 1959.


Mwaka 1960 hadi 1963, alisoma Shule ya Kati Magomeni, Dar es Salaam.
Kati ya mwaka 1964 hadi 1967, alisoma Shule ya Sekondari ya Aga Khan, ambayo kwa sasa inajulikana kama Tambaza.

Mwaka 1968 hadi 1969, alihitimu Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Tanga. Julai 1970, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1973. Lakini makala hii haita kamilika kama sitaandika kwamba marehemu Ditopile alikuwa ni rafiki wa karibu wa familia ya Rais Kikwete.

Na hakuna ubishi kwamba katika uhai wake marehemu alikuwa ni miongoni mwa watu waliopigana kufa na kupona ili Kikwete ateuliwe na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Na kweli hilo walifanikiwa.

Lakini naweza kusema bahati haikuwa upande wake, kwani ndani ya miaka miwili na miezi minne, tangu kijana wake Kikwete ashike kiti cha urais, Ditopile alikumbwa na kesi ya kuua bila kukusudia, na kusababisha kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa moka.

Pia katika kipindi hicho kifupi cha utawala wa kijana wake, Ditopile amekumbwa na mauti. Hivyo hakuweza kufaidi matunda ya utawala wa kijana wake.

Ditopile anatarajiwa kuzikwa leo katika shamba lake lilipo Kinyerezi, Dar es Salaam.

Ditopile sisi tulikupenda, lakini Bwana amekupenda zaidi.

Mungu ailaze roho yako mahala pema peponi. Amina.

Namlilia Ditopile.



0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne.April 22,2008

No comments:

Powered by Blogger.