RAIS KIKWETE NA KILIO CHA MAKANJANJA
Na Happiness Katabazi
“DALILI mbaya za kuwatumia waandishi wa habari wasiozingatia misingi ya kitaaluma, maarufu kama ‘makanjanja’, inaweka fani hiyo katika hatari ya kupoteza heshima yake katika jamii”
“Kutokana na hali hiyo , nawaagiza wamikili wa vyombo vya habari nchini, wahariri na wanahabari , kuzingatia maadili ya taaluma ya habari ili kuinusuru taaluma hiyo isiangamie kutokana na kuvamiwa na ‘makanjanja’.
Maneno haya ameyasema rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kwenye sherehe za uzinduzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Alisema iwapo hatua za mara moja hazitachukuliwa mapema,basi wanahabari na wamiliki ndiyo watakaokuwa watu wa kwanza kujuta , hali itakayosabisha kuanza kusemana na kuchimbana wenyewe, ambapo tayari kuna mwelekeo wa mashaka na kwamba dalili zake zimeishaanza.
Binafsi nilipata fursa ya kumsikiliza Rais Kikwete wakati akihutubia kwenye dhifa hiyo, ila nimebaini kwamba hao waliomuandalia hotuba aliyoitoa wamempotosha rais wetu, kwani wameshindwa kutofautisha ‘makanjanja’ ni waandishi wa namna gani na ‘waandishi mtandao'ni wapi.
Kwa sisi wanahabari, ‘makanjanja’ tunaowajua ni wale matapeli wasio na taaluma yoyote ya kuandika habari na ambao hawana vyombo vya kuandikia, lakini hupita hapa na pale kudandia shughuili na dhifa kwa kisingizio cha kuandika habari huku wakidanganya kuwa wanafanyiakazi chombo hiki au kile.Hivyo ‘Makanjanja’ wamekuwa wakijulikana kwa sifa ya kugombea vyakula na kudai fedha (mishiko au mikukuta) kutoka kwa vyanzo mbalimbali. Wakishajaza matumbo yao na kupewa mshiko, hutoweka wasijulikane walipoishia.
Ndugu wasomaji hivi sasa ndani ya vyombo vya habari kuna kundi moja linalojumuisha baadhi ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi ambao ni watu wazima na taaluma zao lakini kwa makusudi kabisa wameamua kujigeuza kuwa ‘waandishi mabazazi’ ambao moja ya kazi yao kubwa ni kuwakumbatia wanasiasa wachafu ambao huwajaza mapesa mfukoni ili waweze kuwachafua wanasiasa wengine, hata kama wanaoshambuliwa ni watu waaminifu na waadilifu ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya umma.
Ndugu Wananchi kundi hilo dogo ,limeamua wazi wazi kuzika maadili ya taaluma yao, heshima zao mbele ya waandishi wadogo na jamii inayowazunguka na badala yake wameamua kuacha kuandika habari zenye ukweli kwa maslahi ya taifa letu na badala yake wamekuwa wakishinda kwenye vikao vya kupanga fitna za kuwachafua baadhi ya viongozi na watu wengine wenye heshima kwenye jamii ili waonekane siyo mali kitu mbele ya jamii.
Kundi hili linatumiwa na baadhi ya viongozi wa CCM na serikali kwa malipo ya fedha, safari za nje ya nchi, na kuwalipia gharama za kwenye vyuo, ili liweze kuwachafua mahasimu wao kupitia kalamu. Kupitia kazi ya kundi hilo, baadhi ya viongozi wa CCM, serikali na watu wenye heshima kwenye jamii wameishaingia kwenye ugomvi wa chini chini na baadhi ya viongozi wenzao kwa sababu ya kundi hilo ambalo limekuwa likitumiwa kuandika habari za kuwachonganisha na kuwachafua viongozi wengine.
Ni kundi hili hili ndilo limekuwa likipendwa na kulelewa na baadhi ya vigogo hao na waandishi wa habari ambao ni makini na wenye kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika utendaji wao wa kila siku, viongozi hao wamekuwa wakiwabagua.
Mfano mkubwa wa kundi hili ni wale waandishi wanamtandao waliotumiwa kwa takriban miaka kumi na mbili iliyopita kujenga hoja ya kuwa Watanzania wanawapenda wanasiasa wa mtandao. Waandishi hawa walitumika kikamilifu kuiweka serikali ya awamu ya nne madarakani.
Ukiangalia kwa makini makundi haya mawili kama nilivyoyaeleza , utabaini kundi la ‘waandishi mabazazi’ ndiyo lenye madhara makubwa kwa taifa kuliko lile kundi la ‘makanjanja’. Nasema kundi hili lina madhara makubwa kwa sababu lina vitambulisho vya kufanyia kazi ya uandishi wa habari (press card), kutwa linaambatana na viongozi kwenye safari za ndani na nje ya nchi, lina sauti ndani ya vyombo vya habari, wameajiriwa na wamekuwa wakivujishiwa siri za ndani ya serikali kupitia hao wanaowatumikia ambao nadiriki kuwaita wanasiasa mafisadi.
Kwa ujumla, Rais mwenyewe umekuwa ukiwatumia waandishi hawa mabazazi katika misafara yako na uliwatumia katika kampeni zako. Hivyo changamoto yako Rais lianzie kwako, hapo Ikulu na timu ya waandishi wako, na pia kwenye mtandao wako ambao bado upo na unakutumikia. Tuwe wakweli kwa taifa letu, na mungu atatubakiri kwa hilo.
Rais umetoa changamoto kubwa sana, unataka nchi yenye vyombo vya habari vyenye viwango na madili. Hata hivyo hatuoni juhudi za kuwawezesha waandishi kielimu zikipewa kipaumbele isipokuwa tunaona sasa wakubwa mnasomesha waandishi wenu, wakuwasifu na kuwalamba miguu.
Pia tunaona mfumuko wa vyombo vya habari vya wakubwa, vyenye lengo la kuwasifu wenye vyombo na kuwabomoa wahasimu wao. Rais, hayo ndiyo mambo yanayobomoa badala ya kujenga tasnia ya habari na hapo tulitegemea tusikie sauti yako ikiunguruma.
Kama yote yaliyosemwa ni kweli, tulitazamia tukusikie rais ukizungumzia uhuru wa wanahabari kuandika habari, haki ya wanahabari kupewa habari na wajibu wa viongozi wakuu kutoa majibu haraka na yanayotosheleza wakihojiwa na wanahabari.
Hivyo Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) halina maana kubwa kwa Watanzania kama siyo shirika huru, lisiloendeshwa kiserikali kwa madhumuni ya kuitetea serikali. Kwa nini hao waliokuandalia hotuba hawakukuambia kuwa habari tunazochapisha ni asilimia tano tu ya habari zote hivyo asilimia 95 zimefichwa kwenye mafaili ya serikali chini ya kinga ya usiri. Kwa nini hawakukuambia pia kuwa habari tunazopewa na viongozi wako ni za uhusiano mwema tu na nyingi zimesukwa kuficha ukweli?.
Hata hivyo waandishi wa habari wenye misimamo yao wamekuwa wakivutana vikali na kundi hilo na hatimaye kundi la waandishi wenye msimamo wanaoneka kushinda vita dhidi ya wahuni hao kwani hivi sasa kundi hilo linakabiliwa na wakati mgumu kwani kila habari ya wanayoiandika kwa lengo la kumchafua mtu asiye na hatia, zimekuwa zikikosolewa wazi.
Hivyo basi nilitegemea aliyemwandalia Rais wetu hotuba aliyoitoa kwenye uzinduzi wa (TBC), angemwandalia haya ili rais aweze kusimama hadharani na kulikemea kundi hili la waandishi mabazazi, kuliko kumwandalia hotuba inayokemea ‘makanjanja’. Tunajua kuwa mkuki ni mtamu kwa nguruwe lakini kwa binadamu ni mchungu.
Waliomwandalia rais hotuba hiyo bila shaka ni wale waandishi wa habari wa kundi la mtandao ambao ni sehemu ya kundi la waandishi mabazazi. Wasingeweza kumwambia Rais kuwa aliwatumia vibaya wakati wa uchaguzi, ila yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo, Rais akubali sasa kukemea kundi hili kwa kuwa ni hatari kwa taaluma ya habari hata kama lilimsaidia kuingia madarakani.
Hivyo rais wetu sisi tumepokea changamoto yako kwamba tuzingatie maadili, tutazingatia, lakini namimi nakupa changamoto hii, uwashikishe adabu baadhi ya wanasiasa wa chama chako ili wawe waadilifu. Sisi waandishi wa habari kazi yetu ni kutafuta ukweli na kuutangaza kwa wananchi.
Ikiwa viongozi wengi tulio nao ni wachafu, sisi tuwape sifa gani? Ikiwa kazi kubwa ya viongozi tulio nao ni kuendeana kwa waganga wa kienyeji na kisha kupora fedha za umma sisi tu tufiche habari hizo?
Kwa nini maadili yanaonekana kutoweka kwa waandishi wa habari tu lakini wanaowapotosha hatuwakemei?
Naamini kuwa ukiwaonya viongozi wako na kuwashikisha adabu, ni dhahiri ufisadi unaojitokeza katika tasnia ya habari utakoma. Lakini kama rais utashindwa kuwadhibiti watu hao ipo siku watakugeukia wewe mwenyewe na kuanza kukupaka matope mbele ya jamii. Hatutaki tufike huko.
Mungu Ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika
0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,April 17,2008

No comments:
Post a Comment