Header Ads

KESI ZA EPA ZAGUSA BOT

Na Happiness Katabazi

WAFANYAKAZI wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuunganishwa na watuhumiwa wengine wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Wafanyakazi waliofikishwa mahakamani hapo ni Mkuu wa Kitengo cha Madeni BoT, Iman Mwakosya, Kaimu Mkuu wa Idara ya Madeni, Ester Komu, na Wanasheria Sophia Joseph na Bosco Kimela.

Watuhumiwa hao waliunganishwa kwenye kesi ya jinai namba 1162 ya mwaka huu na watuhumiwa wengine waliokuwepo ambao ni Rajab Maranda na Farijala Hussein.

Mbele ya Hakimu Henziron Mwankenja, Wakili wa Serikali, Edga Luhoga, alidai Farijala na Maranda wanakabiliwa na mashitaka sita katika kesi hiyo ikiwemo kughushi, kulaghai, kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanganyifu na kwamba washitakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa BoT wanakabiliwa na shtaka moja la kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kusababisha wizi huo kutendeka.

Luhoga alidai katika tarehe tofauti mwaka 2005, Farijala na Maranda, kwa makusudi walighushi hati za usajili wa makampuni kwa maelezo zimetolewa na BRELA na kwamba wao ni washirika katika Kampuni ya Money Planers&Consultant Ltd na kufanikiwa kujipatia ingizo la sh bilioni 2.6 kwenye akaunti yao kutoka BoT.

Wakili wa serikali alidai kwamba watuhumiwa hao walidanganya kuwa wameteuliwa kukusanya deni la Kampuni ya BC.Grancel&CoLtd ya Ujerumani.

Watuhumiwa hao walikana walikana tuhuma hizo na kuelezwa kuwa dhamana ipo wazi kwa masharti ya kila mmoja kutoa sh milioni 450, hati za mali zisizohamishika, kuacha hatia za kusafiria mahakamani, masharti ambayo walishindwa kuyatekeleza na kupelekwa rumande hadi Novemba 21 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa.

Aidha, katika mashitaka mengine, watuhumiwa Farijala na Maranda wanakabiliwa na tuhuma ya kughushi, kulaghai na kujipatia ingizo la fedha na kuiba sh milioni 207, mali ya BoT; hata hivyo wafanyakazi hao wa BoT wanakabiliwa na shitaka la kuzembea mpaka fedha hizo zikaibiwa.

Katika kesi hiyo, hakimu alisema dhamana ipo wazi na masharti ni kwamba kila mtuhumiwa anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaotoa bondi ya sh milioni 69 na kila mtuhumiwa atoe fedha taslimu sh milioni 104 palepale mahakamani; masharti ambayo walishindwa kuyatekeleza. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 20 mwaka huu.

Wakati huohuo, watuhumiwa Davis Kamungu na Godfrey Moshi wanaokabiliwa na kesi nyingine zinazohusiana na wizi wa EPA, waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Washitakiwa hao walifikishwa juzi mahakamani hapo.

Hata hivyo, kwa upande wa mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kiasia Jayantkumar Chandubhai Patel “Jeetu Patel, Devendra K.Vinodbhai Patel, Amit Nandy na Ketan Chohan ambao jana walifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutimiza masharti ya dhamana, wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo. Kesi yao itatajwa Novemba 20 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, mtuhumiwa Johnson Lukaza naye anaendelea kusota rumande hadi hapo mamlaka husika zitakapokwenda kutathmini nyumba ambazo hati zake zimewasilishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kudhaminiwa.

Mpaka jana jumla ya watuhumiwa 17 wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na tuhuma za wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Novemba 8 mwaka 2008

No comments:

Powered by Blogger.