WAHANDISI JWTZ WATUMIKE WAKATI WOTE
Na Happiness Katabazi
JUKUMU mojawapo la msingi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa amani, ni kusaidia mamlaka za kiraia kulinda usalama wa wananchi na mali zao na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada ya uokoaji wakati wa majanga na kukarabati miundombinu inapoharibika.
Katika kusaidia shughuli za kijamii, JWTZ kwa muda wote wa uhai wake, imeweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujizolea sifa nyingi kutokana na mchango wake, hasa katika uokoaji na urejeshaji miundombinu ya barabara na madaraja wakati wa mafuriko na Majanga mengine.
Jukumu hilo limekuwa likifanywa na wanajeshi wote, wakiongozwa na wahandisi wa medani wa JWTZ wenye makao makuu yao eneo la Sangasanga -Ngerengere mkoani Morogoro, ambao wamebobea katika fani hiyo.
Wahandisi wa medani ndio watalaamu ambao wakati wa vita huwezesha vikosi kusonga mbele kwa kuonyesha njia, kwa kufanya doria na kuchagua sehemu nzuri ya kupitisha vikosi, zana na vifaa. Wao pia husafisha njia kwa kutegua mabomu, kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Kwa misingi hiyo basi, binafsi naona bado kuna haja kwa taifa letu kuanzisha utaratibu wa kuwatumia wahandisi wa JWTZ wakati wa amani ili taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo katika sekta ya miundombinu.
Jeshi letu hivi sasa lina hazina ya wataalam wa kila fani, lakini baadhi yao taaluma zao hawazitumii ipasavyo kutokana na serikali kutowapa fursa ya kutumia ujuzi wao wakati wa amani.
Tunaosoma Kwenye vyuo HIvi sasa ni mashahidi Kwani Wanajeshi Wengi na wanausalama toka vyombo mbalimbali Vya dola wamejiandikisha vyuoni humo ili wajiendeleze kielimu Katika fani mbalimbali.
Sote ni mashaidi kwamba inapotekea maafa, wahandisi wa JWTZ wamekuwa wakisukumizwa kutengeneza barabara, kuokoa majeruhi nk., lakini hali hiyo ya pilikapilika hawaipati wakati wa amani.
Pamoja na kuwa na fani ya uhandisi, lakini wanajeshi wote wamefundishwa ukakamavu , nidhamu ya Hali ya juu na kazi zao huzifanya ndani ya muda unaotakiwa na kwa uaminifu na uzalendo.
Ni barabara, madaraja mengi tunayashuhudia yamejengwa na raia wa kawaida, tena kwa gharama kubwa, yakiaribika mapema kwasababu yamejengwa chini ya kiwango na wakandarasi waliokosa vifaa na uzalendo. Pia yamekuwa yakichukua muda mrefu kukamilika, na mara nyingine tunaambiwa serikali ndiyo imekuwa ikichelewesha fedha za kuwalipa makandarasi na wakati mwingine tunaambiwa makandarasi hao ni wazembe.
Hakika habari kama hizi hazipendezi kusikiwa maskioni mwa mwananchi yeyote mpenda maendeleo, kwani sote tunafahamu taifa lisilo na miundombinu ya uhakika ni wazi litakuwa linajirudisha nyuma kimaendeleo kwani shughuli za uzalishaji zitakwama kwa kuwa mazao au mawasiliano hayasafirishwi kwa wakati muafaka, hivyo kufanya pato la wananchi na taifa kwa ujumla kukosekana na bidhaa kukosekana sokoni.
Wakati umefika kwa serikali ya awamu ya nne ambayo kwa bahati nzuri inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa alikuwa ni ofisa wa jeshi hili, ione jinsi ya kuwashirikisha wahandishi wa JWTZ kwenye ujenzi wa miundombinu ya taifa hata wakati wa amani.
Kwani hivi sasa serikali inatumia fedha nyingi kuleta makandarasi toka nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakati jeshi lina wahandisi wengi tu wasiotumiwa ipasavyo. Endapo serikali itakubali kuwatumia wahandisi medani, ni wazi kwamba serikali itatumia fedha kidogo kwa ajili ya kulipa gharama za uhuduma hiyo.
Yawezekana wakawapo watakaosema kuwa jeshi halina vifaa vya kutosha vya kuweza kufanya shughuli hiyo, sawa, lakini hatuoni sababu ya JWTZ kutowezeshwa ili waweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitakuwa ni mali yetu ya kudumu na tutakuwa tukivitumia muda wowote tunapovihitaji kuliko hali ilivyo hivi sasa ambako tunatoa tenda kwa wahandisi wa nje ambao huongeza gharama kwa kuingiza vifaa vya ujenzi na bado hujinufaisha kwa kuviuza mara wanapomaliza kazi zao.
Tujiulize kipi bora, kuendelea kuwatumia makandarasi toka nje ya nchi kwa gharama kubwa ambao wakimaliza kazi wanaondoka na vifaa vyao au taifa lijinyime na kununua vifaa vyake na kutumia wahandisi wake katika ujenzi wa miundombinu ya taifa letu?
Lengo langu si kupiga vita makandarasi wa nje ili wasipewe tenda, la hasha! Ila kwa kuwa serikali kila kukicha imekuwa ikidai kuwa haina fedha za kutosha kutokana na bajeti ya taifa kuwa tegemezi kwa wafadhali, sasa kwanini hicho kidogo tulichonacho kisizunguke humu ndani ili wananchi na taasisi nyingine za serikali ziweze kufaidika nacho?
Naamini fedha za kununulia vifaa vya ujenzi wa miundombinu kote nchini tukiwa na nia ya dhati tunaweza kuzipata, kwani nchi yetu ina utajiri mwingi wa rasilimali, ambao tukiutumia vizuri, unaweza kutupatia haraka fedha hizo.
Nitoe pia changamoto kwa JWTZ , chini ya Mkuu wa Jeshi hilo , Jenerali Davis Mwamunyange kwamba, kama kweli nayo ina nia njema na taifa hili na inapenda kuona miundombinu ya taifa lao ikiimarika, pia nayo ina jukumu la kuiomba serikali iiwezeshe na kisha iwaruhusu kufanya kazi za kuboresha miundombinu wakati wa amani.
Huu ni wakati wa zama za maendeleo ya sayansi na teknolojia na hivyo vinapaswa kuikumbuka JWTZ pia na njia mojawapo ya kulifanya liende sambamba na maendeleo hayo, ni kupanua wigo wa utendaji wake na ninafikiri njia mojawapo ni kwa kujishughulisha katika ujenzi wa taifa kwa kutumia wataalamu lililonao.
Hizi si zama za wanajeshi wetu kutembea na silaha wakati wote au kushinda messi wakinywa Pombe za JWTZ ambazo zinauzwa KWA bei rahisi au kunyang'ang'Anyana wanawake na raia mitaani, bali kubadilika ili liwe jeshi la ujenzi wa taifa, huku likihakikisha amani na usalama kwa nchi yetu.
Rais Kikwete haitoshi kuona ukiteua baadhi ya maofisa wa JWTZ kuwa wakuu wa mikoa na wilaya. Tunataka kuona wahandisi medani wa jeshi hilo wakitumiwa na serikali yako katika shughuli za ukarabati na ujenzi wa miundombinu ili taifa lipate maendeleo kwa haraka kama sote tunavyotamani.
Wanajeshi madaktari na fani nyingine ndani ya jeshi hilo, tunaona hivi sasa wamekuwa wakitumia fani zao vizuri kwa sababu kuna hospitali zinazoeleweka ndani ya jeshi hilo na hasa ukizingatia Baada ya mgomo wa madaktari , serikali iliipandisha hadhi Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam , Kuwa Hospitali ya Rufaa, zimekuwa zikitoa uhuduma ya matibabu hata kwa raia.
Ni vyema tutambue kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, hivyo basi Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe na si wageni. Sote kwa pamoja tujifunge mkanda bila kubaguana katika kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa taifa na naamini tutafanikiwa.Waandisi wa JWTZ watumike wakati wote hapa nchini, siyo tu kuwatumia wakati wa mafaa na Kuwapeleka Katika nchi zenye vita Kama Darfur, Congo na kwingineko.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Aprili 4 Mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment