Header Ads

Bunge Lisilo Meno Halitufai!

Na Happiness Katabazi

AWALI ya yote namshukuru Mungu kwa kunifikisha siku ya leo salama, ninamshukuru kwa kunipa nguvu ya kuandika makala hii.

Baada ya kushukuru, sasa nipaze sauti yangu, niwapigie kelele kwanza wabunge na kisha Bunge kwa ujumla wake na mwisho serikali yetu.

Kwa muda wote ambao nimekuwa nikifuatilia shughuli za Bunge letu, nimekuwa nikiliona kama taasisi isiyokuwa na nguvu hata ya kufanya yale ambayo inaruhusiwa kisheria, Bunge lisilokuwa na haki ya kukagua na kujadili mikataba kati ya serikali na wawekezaji.

Katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita, Watanzania walisubiri kwa hamu kusikia wabunge wakijadili mkataba mbovu kabisa uliosaniwa hivi karibuni kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Pamoja na huo, ipo mikataba mingine ambayo naamini Watanzania walikuwa na hamu ya kuwasikia wawakilishi wao wakiijadili mikataba kuwa ni pamoja na ile ya wawekeaji wa sekta ya madini ambayo Rais Jakaya Kikwete alikwishakiri kuwa ina upungufu na akaahidi kuwa itafanyiwa marekebisho.

Nimejiridhisha kabisa kuwa serikali inafanya makusudi kukataa kuitoa mikataba hii kwa wabunge, kwa sababu inatambua kuna 'madudu' ya ajabu katika mikataba hiyo, ndiyo maana ilikataa kutoa mkataba wa kampuni ya Richmond licha ya Kamati ya Uwezeshaji na Biashara kuagiza ipewe mkataba huo.

Cha ajabu, wakati kamati hiyo ikinyimwa mkataba huo, maudhui ya mkataba huo yalichapishwa katika magazeti binafsi.

Sote tunajua misingi ya demokrasia na utawala bora ni kuwa na Bunge huru na lenye meno.

Kitendo cha kuwanyima wabunge haki ya kujadili mikataba ambayo serikali inaingia na wawekezaji ni ishara kwamba, mhimili mmoja wa dola unaoitwa serikali, unakaidi na kukataa kudhibitiwa au kuwajibika kwa chombo cha uwakilishi wa wananchi kinachoitwa Bunge. Huu ndiyo mwanzo wa ufisadi.

Sasa tunajua kwamba mikataba bomu inayoruhusu rasilimali ya nchi hii kuporwa na wageni ni kitendo cha makusudi chenye maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wakuu wa dola walio katika serikali.

Tuchukulie mfano wa Richmond. Kampuni hii inasadikiwa kuwa ilipewa mkataba na serikali kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004.

Wote tunajua kwamba Richmond haikuwa na uwezo wa kujenga vinu vya umeme, ingawa serikali iliipatia mkataba wa dola zaidi ya milion 178.Matokeo ya Kampuni ya Richmond kushindwa kukidhi matakwa ya mkataba, ni kukosekana kwa umeme.

Ili kukwepa aibu hii, wafadhili wa kashfa hii waliibua Kampuni ya Dowans.
Hawa eti wamenunua mkataba wa Kampuni ya Richmond. Hata Mtanzania wa kijijini kabisa sasa anajua kinachochezewa hapa ni kodi ya wananchi kutokana na kutokuwa na watu makini wa kutetea maslahi yao.

Tuukumbuke msemo wa ‘kikulacho ki nguoni mwako’. Msemo huu ni kielelezo cha vitendo vinavyofanywa na watendaji wa serikali yetu ambao baadhi yao sasa wanaonekana kuingiwa na roho ya ufisadi wa kuiba fedha za wananchi kwa kiwango cha kutisha.

Ni hawa ndiyo wasiotaka mkataba baina na Richmond na serikali ujadiliwe bungeni na wanataka vyombo vya habari viwashangilie na kuwasifu kwa ufisadi huu.

Matarajio ya Watanzania ya kusikia kilichomo katika mkataba kupitia kwa wawakilishi wao bungeni yameyeyuka, wawakilishi wao hawawezi kufanya kile wanachokitaka wananchi kwa sababu tu wamenaswa katika ndoano waliyojiingiza ya uanamtandao.

Hawako tayari kuwapigania wananchi wao waliowatuma wakawawakilishe bungeni, badala yake wanaonekana ku0shindana kuwaramba miguu viongozi serikalini katika kile kinachoonekana kusaka uteuele katika bodi za mashirika na tume mbalimbali.

Midomo yao wameitia gundi kali (super glue) na wanaisifu serikali bungeni, lakini 'uswahilini' wakiwa katika vijiwe vyao vya moja baridi na moja moto huku wakibadilisha mawazo na wananchi wa kawaida, wanakuwa vinara wa kuiponda kwa kila aina ya maneno ya kashfa na wakati mwingine matusi kabisa.

Najiuliza, hawa ni wawakilishi wa namna gani kama si wanafiki na watu waliojaa nidhamu za woga, watu wanaoishi kwa staili ya mbwa anayebweka kukiwa shwari, lakini akiona mwizi anakimbia na kufyata mkia?

Nimetafakari na kujiuliza kwa muda mrefu kidogo kuhusu wabunge hawa. Hivi tatizo lao ni nini? Ni kukosa elimu ya kutosha au ni uwoga na njaa? Imani niliyonayo sasa ni kwamba inawezekana kuna rundo la wabunge walio na upeo mdogo wa kusoma na kuielewa miswada mingi iliyondikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo hawataki hata kuisikia. Naamini udhaifu wao huu ndiyo kiini cha tatizo hili.

Ninamini hivyo kwa sababu nina hakika mbunge aliyeghushi vyeti vya elimu yake hana ubavu wa kumdhibiti kiongozi anayeghushi au kuweka saini mikataba bomu. Nayakumbuka maneno ya karibuni kabisa ya mbunge mmoja aliyediriki kusema; ‘Bunge lina meno ya plastiki’.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili April 29,2009

1 comment:

Christian Bwaya said...

Nimesoma makala haya gazetini. Nakubaliana na wewe kwa asilimia mia moja.

Karibu!

Powered by Blogger.