Header Ads

DPP kijana anayeingia ofisini na msahafu wa Sheria


ELIEZER MBUKI FELESHI

.Ndiye DPP mpya Tanzania, ana miaka 39
.Apania kumfuta tongotongo Rais Kikwete
.Aliungurumisha kesi ya MV Bukoba
.Adai ilijaa mambo ya ajabu, ataka kutungia kitabu
.Uhaba wa wanasheria wampasua kichwa

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete, alimteua mwanasheria mwandamizi wa serikali, Eliezer Mbuki Feleshi (39), kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Uteuzi wa Feleshi ambaye alijizoelea sifa nyingi wakati wa kesi ya MV Bukoba aliposhiriki kama mwendesha mashitaka msaidizi na mchango mkubwa alioutoa katika tume ya kuchunguza mauaji ya wafanyabishara wanne wakazi wa Mahenge, ambayo iliwatia hatiani polisi, umekuwa ukielezwa na baadhi ya watu kama muarobaini wa ofisi hiyo. Katika makala hii MWANDISHI WETU HAPPINESS KATABAZI, anamuhoji jinsi alivyoupokea uteuzi huo, na pia alivyojiandaa kukabiliana na changamoto za ofisi hiyo.

Swali: Kuteuliwa kwako na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) katika umri mdogo ulionao, kumedhihirisha jinsi rais alivyo na imani na utendaji kazi wako, umeupokeaje uteuzi huo?
Jibu: Nimeupokea kwa heshima kubwa. Natambua kuwa rais ananiamini na ndio maana akafikia uamuzi wa kunitwisha mzigo huu mzito katika umri mdogo nilionao.
Lakini uteuzi wangu nina hakika umezingatia sifa zilizowekwa kikatiba za mtu anayestahili kuteuliwa kushika wadhifa huu, binafsi ninafarijika kwamba, Mheshimiwa Rais aliisoma katiba kabla ya kuniteua, na aliporidhika, ndipo akaniteua.
Ni fahari kwangu, familia yangu, vijana wenzangu na taifa kwa ujumla, kuwa na vijana wanaoweza kuaminiwa na kukabidhiwa majukumu makubwa kama hili la kuongoza ofisi nyeti na kubwa.
Kazi iliyopo ni kuhakikisha kuwa simuangushi rais wangu na Watanzania kwa ujumla, nimepania kuwaonyesha kuwa vijana tunaweza kazi.

Swali: Umejipanga vipi kuthibitisha kuwa unaweza?

Jibu: Jambo la msingi ambalo nitalizingatia siku zote, nitakapokuwa katika ofisi hii, ni kutekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia taratibu na misingi ya sheria ambayo ndio muhimili mkuu wa ofisi hii.
Misahafu ya sheria haidanganyi hata siku moja, na mimi ni muumini wake mkubwa, siku zote nimekuwa muumini wa sheria na ninaziishi, na kwa imani yangu hiyo ambayo imenipa mafanikio tangu nikiwa ngazi za chini, naamini nitafanya kitu kitakachomtoa tongotongo rais wangu.
Mimi na wenzangu tumeshajipanga, na bado tunaendelea kujipanga, sina cha kueleza zaidi katika hili…, unajua ofisi kama hizi ndugu yangu mambo mengine yanabaki ya kiofisi, lakini ninachotaka kuwaambia Watanzania ni kwamba, nitaiendesha ofisi hii kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.
Bahati nzuri ni kwamba, kuna maofisa wengi tu hapa waliobobea katika fani ya sheria ambao utendaji wao, ninaamini kabisa kuwa hauna shaka hata kidogo, na tangu awali nilikuwa nikifanya nao kazi pamoja, na kwa ushirikiano wa dhati.
Majukumu tuliyokuwa tukitekeleza pamoja hapo awali, si kwamba yatabadilika baada ya mimi kuingia ofisini hapa, hapana, kimsingi ni yale yale, lakini ninachotaka tufanye kwa sasa ni kuhakikisha tunasonga mbele kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuwa nyakati zinabadilika kwa kasi sana.
Na ieleweke kuwa ofisi ya DPP ni ya kikatiba, si ya mtu binafsi, wala haitawaliwi kwa msingi wa umri, bali inaongozwa na mtu anayeonekana kuwa na sifa ya kupewa wadhifa huo. Watangulizi wangu waliteuliwa kushika wadhifa huo si kwa kuwa na umri mkubwa, bali kwa kuwa walikuwa na sifa za kuongoza ofisi hii.

Swali: Kuna malalamiko mengi ya kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi, hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?

Jibu: Kesi ni ushahidi, na ushahidi unapatikana kwa kuukusanya. Jamii inao wajibu wa kushirikiana na taasisi zinazofanya upelelezi ili kuharakisha kazi ya kukusanya ushahidi. Kwa nyakati fulani wananchi wamekuwa waoga kutoa ushahidi au wakati mwingine kuutoa kwa wasiwasi.
Kuna wakati wapelelezi wamezorota kufanya kazi zao na kuna wakati wamejitahidi, ila wanakwamishwa na nyenzo.
Kwa sababu hiyo, sipingi kuwa kuna malalamiko kama hayo kutoka kwa jamii, yapo, na ili kukabiliana na hali hiyo, nitaanza kwa kulifanyia kazi tatizo la vitendea kazi, pili ofisi yangu itafanya jitihada za makusudi za kuwaomba wananchi kushirikiana na waendesha mashitaka katika kukusanya ushahidi.
Kikubwa ni kuwaelimisha wananchi kuwa, wanayo sehemu yao ya kutoa taarifa dhidi ya wapelelezi wasio waadilifu, hasa kama wapelelezi wanawazungusha kupokea ushahidi wanaowapelekea, ninaamini nitafanikiwa kuondoa malalamiko hayo.

Swali: Idara yako ina wataalamu mahiri wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?

Jibu: Wataalamu wazuri wapo, ila ukweli ni kwamba, hawatoshi. Hili ni tatizo. Mmmm, ni tatizo hili... Nchi ni kubwa na inayo mahitaji mengi. Na idara hii ni eneo lenye changamoto nyingi na kubwa. Hivyo kuna kila sababu ya kuwatambua kwa karibu wataalamu wachache waliopo na kuwathamini, na hili ni kwa idara zote zilizo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Swali: Kuna mpango wa kutenganishwa kwa wapelelezi wa kesi za jinai na waendeshaji wa kesi za jinai, utekelezaji wake utaanza hili?

Jibu: Inatakiwa ieleweke kuwa, hapatakuwa na wakati wa mpelelezi na mwendesha mashitaka kufanya kazi bila ushirikiano wa karibu, kutokana na kutegemeana kwa kazi zao.
Kinachokusudiwa kufanyika ni kuiwezesha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwa na waendesha mashitaka wa kutosha ili wao kama waendesha mashitaka, wafanye kazi ya kuendesha mashitaka na wapelelezi waimarishe kazi ya kupeleleza na kuwasaidia waendesha mashitaka kupata ushahidi.
Hivyo askari polisi wanaoendesha kesi leo kwa kupewa kazi hiyo na DPP, watapata fursa nzuri ya kufanya kazi za kupeleleza kesi za watuhumiwa mbalimbali.
Uimarishaji wa mkakati huu ulishaanza, na mwaka ujao wa fedha tunatumaini, baadhi ya maeneo ya nchi yetu, wataanza kushuhudia kesi zikiendeshwa na maofisa kutoka ofisi ya DPP, kuanzia ngazi ya wilaya.

Swali: Hili la kutengenisha majukumu haya likifanyika, ofisi yako itakuwa na mamlaka gani ya kuhakikisha kesi zinaendeshwa katika muda unaotakiwa?

Jibu: Upelelezi ni taaluma iliyo na mafunzo, mbinu na miiko yake, na haitegemei zoezi la kutenganisha kazi ya upelelezi na uendeshaji mashitaka. Hivyo tangu awali wapelelezi wanatakiwa kupeleleza kesi kwa umahiri na haraka.
Lakini ni matarajio yangu kuwa Ofisi ya DPP itakapoanza kuendesha kesi nchi nzima au katika maeneo machache, polisi waliokuwa awali wanahusika kwenye zoezi la kuendesha mashitaka, watapata fursa nzuri ya kuongeza nguvu kwenye eneo la upelelezi.

Swali: Unazungumziaje madai kuwa baadhi ya mawakili wa serikali hawana ujuzi wa kutosha, na kwamba mishahara midogo inawafanya baadhi yao, wajihusishe na vitendo vya rushwa?

Jibu: Ujuzi haununuliwi, unatokana na mafunzo na utendaji wa mtu mwenye bidii ya kujifunza, kuna mawakili wengi wanafanya kazi vizuri ingawa wana mishahara midogo.
Mshahara mdogo si kigezo cha kula rushwa. La msingi ni kuangalia jinsi ya kumwezesha wakili awe na mshahara mzuri, utakaomwezesha kupangilia mambo yake kwa uhakika, aweze kununulia vitabu vya kujisomea na nyenzo nyingine za kazi, jambo ambalo viongozi wetu wanapaswa kuliangalia kwa jicho makini.

Swali: Una maoni gani kuhusu watu wanaopinga mamlaka makubwa aliyonayo DPP?

Jibu: Katiba iko wazi, na sioni sababu ya kuliongelea hili. Huenda kinachoweza kuangaliwa ni kama kuna ukiukwaji au matumizi mabaya ya madaraka ya DPP. Unajua DPP kama taasisi, hawezi kuwa na tatizo, ila tatizo linaweza kuwa kwa mtu anayeweza kutumia madaraka hayo vibaya, kitu ambacho kitahitaji ushahidi.

Swali: Unaridhika na mfumo wa uendeshaji mashitaka hapa nchini?

Jibu: Siyo mmbaya, naweza kusema unaridhisha, lakini pia ni lazima nikiri kuwa kuna mapungufu yanayosababishwa na uhaba wa vitendea kazi.
Kama nilivyoeleza awali, wataalamu hawatoshi na kuna tatizo la mashahidi kutokupatikana kuja kutoa ushahidi, na hasa katika maeneo yaliyo na mila na desturi za kufanya mapatano ya kutozana fidia.

Swali: Ni tukio gani unalolikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?

Jibu; Ninayo mambo mengi, lakini kubwa ni kesi ya MV Bukoba ambayo nilikuwa mwendesha mashitaka, nikimsaidia Wakili Mkuu wa Serikali W.C. Magoma.
Kesi hii ilikuwa ya mauaji, mamia ya watu walipoteza maisha yao, mashahidi wengi walipokuja mahakamani na kutoa ushahidi, ilinibidi kuwa makini sana, kulikuwa na mambo ya ajabu sana katika kesi hiyo, ni vigumu kuelezea, labda kama kuna siku nitaandika kitabu, nitaeleza kwa unaga ubaga.
Mahakama ilikuwa ikigubikwa na simanzi kila siku kesi hii ilipokuwa ikisikilizwa, kama binadamu, hata mwendesha mashitaka kuna wakati unakuwa na majonzi kama hao waliofiwa na ndugu na jamaa zao, lakini kazi kwanza, nilikuwa natakiwa kusimamia ukweli.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana zaidi.

Jibu: Nimezaliwa Julai mosi, mwaka 1967, katika Kijiji cha Malya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, nikiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa wa familia yetu ya mzee Mussa Mbuki Feleshi na mama yangu Ruth N’gweshemi.
Baba yangu alikuwa mchungaji wa Kanisa la African Inland Church na mama alikuwa mama wa nyumbani.

Baba yangu alifariki mwaka 1973 kwa ajali ya gari na mama yeye alifariki mwaka 1991, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nimesoma Shule ya Sekondari Shinyanga, baadaye nilijiunga na Shule ya Sekondari Galanos mkoani Tanga ambako nilisoma kidato cha tano na sita.

Baada ya kumaliza kidato sita nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Ruvu).
Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991, nikichukua shahada ya kwanza ya sheria na kuhitimu mwaka 1994. mwaka 2003 nilirudi tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma shahada ya uzamili ya sheria (Masters in Law), nilihitimu mwaka 2005.
Kabla ya kuteuliwa kuwa DDP, nilikuwa Mwanasheria wa Serikali na kituo changu cha kazi kilikuwa mkoani Mwanza.

Hivi sasa ninasoma Shaha ya Udaktari wan Sheria PhD in Law Criminology and Penology. Nina mke mmoja, Suzana Majija, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana mkoani Mwanza na tuna watoto wanne.

0755 312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, April 15,2007

No comments:

Powered by Blogger.