Header Ads

Huyu ndiye Augustino Ramadhani; Jaji Mkuu Mteule wa Tanzania


Mapema wiki hii Rais Jakaya Kikwete, alimteua aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Augustino Ramadhani (62) kuwa Jaji Mkuu mpya, Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, alifanya mahojiano maalumu na Jaji Mkuu huyo mteule na katika makala hii amezungumzia historia ya maisha yake kwa mapana na masuala mengine mbalimbali yanayohusu Mahakama ambayo ni mhimili mahususi.

Swali: Umepokeaje uteuzi wa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania?

Jibu: Nimepokea uteuzi huu kwa furaha. Na nimechukulia kwamba Rais Kikwete ana imani nami na pia ameridhishwa na utendaji kazi wangu na kabla ameamini kuwa mimi nitaendeleza yaliyofanywa na watangulizi wangu yaani Jaji Augustino Saidi, Jaji Francis Nyalali na Jaji Barnabas Samatta.
Sikutazamia, uteuzi umenijia ghafla. Hivyo nataka nipate muda wa kujipanga ili siku za usoni aliyeniteua asione alichagua mtu asiyestahili kushika wadhifa huu.

Swali: Watanzania wangependa kusikia kauli yako kwamba ni mambo yapi umejipanga kuyafanya katika uongozi wako?

Jibu: Ni mapema mno kusema nimejipanga kuanza kukabiliana na jambo gani maana nafasi hii ni ya kuteuliwa, labda kama nafasi hii ingekuwa ya kisiasa ningeweza kutamka mapema namna hii kwamba nimejipanga kufanya nini.
Sipendi kuwadanganya Watanzania kwamba ooh, nitafanya ili na lile, kwakuwa mimi ni mwanasheria mwandamizi, hivyo leo hii nikurupuke na kusema kitu ambacho sijakifanyia utafiti, nitakuwa nadhalilisha taaluma ya sheria na Mahakama kwa ujumla.
Nitakapoingia ofisi mpya nakuona ofisi hiyo mambo yanaendeshwaje, kuna ‘miba gani’, na kushirikisha wenzangu hapo ninaweza kutoa kauli ya nini tumejipanga kukifanya.
Ila ninachoweza kuwahakikishia wananchi ni kwamba, nimelenga kusimamia mambo matatu. Moja nitahakikisha haki inapatikana haraka iwezekanavyo, maana imekuwa ni tatizo linalolalamikiwa na watu wengi wanapotafuta haki katika vyombo vya sheria.
Nitahakikisha pia haki inapatikana bila rushwa na kwamba nitajipanga na watendaji wenzangu kuona ni jinsi gani tutakabiliana na tatizo hilo.
Pia nitahakikisha haki inapatikana kwa gharama nafuu, maana haki imekuwa ikipatikana kwa gharama kubwa hasa inapokuja gharama za kuwalipa mawakili, lakini nitaweka mipango na wenzangu na kuandaa mazingira ya kupatikana haki kwa gharama nafuu.

Swali: Kuna malalamiko mengi ya ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?

Jibu: Maoni yangu. Si ucheleweshwaji wa kesi za mauaji tu, bali kesi zote zinacheleweshwa. Kwa upande wa kesi za jinai, kuna sababu tatu ninaweza kuzitaja kuwa zinachangia ucheleweshwaji wa kusikiliza, upande wa kwanza ni serikali ambao waendesha mashitaka huwa wanasema upelelezi kwa kesi fulani bado haujakamilika.
Na sisi kama Mahakama ni vigumu kujua ni matatizo gani yanawakabili katika upelelezi, kwa kweli hili ni tatizo kubwa na kila kukicha limekuwa likipigiwa kelele.
Upande wa pili ni mshitakiwa mwenyewe, wakati mwingine unachelewesha kuleta mashahidi mahakamani ila hali hiyo katika upende huu wa mshitakiwa hutokea mara chache mno.
Upande wa tatu ni Mahakama yenyewe, sasa kwenye Mahakama yenyewe kuna mambo ambayo yanasababisha kesi kuchelewa kusikilizwa. Uchache wa vyumba vya kuendeshea kesi na mfano halisi pale Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ina vyumba vinne tu vya kuendeshea kesi, hapa Mahakama ya Rufani ina vyumba viwili vya kuendeshea kesi. Sasa majaji ina wabidi wasubiriane kuendesha kesi na kesi nyingine zinachukua muda mrefu wakati zikiendeshwa.
Jingine linalochangia ucheleweshwaji wa kusikiliza kesi ni uhaba wa majaji na mahakimu, hili ni tatizo na hata kama unao mahakimu na majaji wengi, lakini vyumba vya kuendeshea kesi ni vichache kama ilivyo sasa hapa nchini, bado tatizo kesi kuchelewa kusikilizwa litakuwa pale pale.
Tatizo jingine la ucheleweshwaji ni uhaba wa nyenzo, leo hii hapa majaji na mahakimu kurekodi mienendo ya kesi kwa mkono badala ya kutumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti kama ilivyo kwa mahakama za nje. Kwa hiyo muda mwingi sisi majaji na mahakimu kuandika. Mfano Mahakama ya Afrika Mashariki, majaji wake wanatumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti.
Halafu pia katika hili la nyenzo, kutokuwepo kwa mfumo wa kompyuta ‘computerization’, unakuta jaji anaandika hukumu kwa mkono kisha hukumu hiyo inapelekwa kuchapwa kwa mchapaji sasa unakuta hukumu moja inaandikwa mara mbili.
Kwa hiyo hayo matatizo niliyoyataja hapo juu yanachukua muda mwingi na si siri yanachangia ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi kwa wakati.

Swali: Mahakama yako ina majaji, mahakimu na wataalamu wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?

Jibu: Majaji, mahakimu na watalaamu katika mhimili wa Mahakama hawatoshi na kuna haja waongezwe kwa kuwa uchache wao nao ni sababu moja wapo inayopelekea ucheleweshwaji wa kesi.

Swali: Unazungumziaje madai kwamba kuna mahakimu hawana ujuzi wa kutosha na kwamba mishahara midogo wanayopata inawafanya baadhi yao wajihusishe na vitendo vya rushwa?

Jibu: Wakisema mahakimu hawana uzoefu wa kutosha nitawaelewa, siyo hawana uzoefu, hili nakataa kwakuwa mahakimu wote wamehudhuria kozi katika vyuo husika na kozi zao zinatofautiana kwa muda, kwani mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya kozi zao huwa ni za muda mfupi tofauti na mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi, kwakuwa hao ni wanasheria kamili, ila nasema hivi kinachotakiwa hapa ni kwa mahakimu hao kupenda kujifunza zaidi kila mara bila kuchoka kwa kuwa elimu haina mwisho na mtu au kiongozi yeyote anayependa kujifunza mara kwa mara anapata fursa ya kujua vitu vingi na uzoefu wake unaongezeka na ninatoa changamoto kwa watendaji wote wa mahakama kupenda kujisomea na kuifunza.
Kweli mishahara ni midogo kama ilivyo sekta nyingi nyingine, lakini mishahara kuwa midogo siyo sababu ya mfanyakazi wa Mahakama kuchukua rushwa kwa sababu kuna wanaopata mishahara minono na kila kukicha wanapokea na kudai rushwa. Binafsi yangu nasema hivi rushwa ni urafi wa mtu binafsi.

Swali: Unaridhika na mfumo wa Mahakama ya Tanzania?

Jibu: Hadi sasa mfumo wa Mahakama hapa nchini unaridhisha ila nitahakikisha ninakaa na wenzangu kuona ni jinsi gani tunaweza kuuboresha zaidi.

Swali: Ni tukio gani unalikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?

Jibu: Tukio ambalo sitalisahau lilikuwa ni kule kufiwa na baba yangu mzazi, Mathew Douglas Ramadhani, Machi mosi mwaka 1962, nilikuwa na umri wa mika 15, tukio hili lilinishtua sana na siwezi kulisahau kwa sababu nilikuwa bado mtoto mdogo, nilikuwa nikiwaza nani angenisomeshwa.
Tukio lililonifurahisha ni siku nilipomuoa mke wangu kipenzi Luteni Kanali Saada Mbarouk, ambaye anafanya kazi Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Nilifunga naye ndoa Novemba mosi mwaka 1975.

Swali: Ni kitu gani kilikutuma kujiunga na fani ya sheria?

Jibu: Nilipenda kusoma sheria kwanza pale Tabora Sekondari (Tabora School) nilipokuwa nasoma kuliwa na mwalimu akiitwa Butterworth, alikuwa akitufundisha somo la historia tangu kidato cha kwanza hadi cha sita, yeye alikuwa mwanasheria, sasa huyu vile alivyokuwa anazungumza ni tofauti na walimu wengine kwa namna alivyokuwa anabishana na kuchukulia mambo tofauti na walimu wengine.
Basi tangu hapo alinivutia na zaidi ya hapo marehemu baba yangu alisomea somo la sheria, alichukua shahada ya BA na moja ya masomo ya hiyo digrii ilikuwa ni sheria na nyumbani kulikuwa na vitabu vya sheria na katika maktaba ya nyumbani.
Lakini si hivyo tu baba yangu mzaa mama, Masoud Than, alikuwa mkalimani wa mahakama na babu alimlea mama Justine Dodo naye alikuwa mkalimani wa jaji enzi za ukoloni na kutembea naye miji mingi hapa Tanganyika. Sasa haya yote nalazimika kusema yalifanya nipende sheria na hadi nikaenda kuisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Swali: Unafikiri idadi ya wanawake waliobahatika kuchaguliwa kuwa mahakimu na kuteuliwa kuwa majaji wanatosha na kama hawatoshi nini kifanyike?

Jibu: Majaji na mahakimu wanawake hawatoshi na chakufanya Mahakama iwezeshe wanawake ili waweze kufikia vigezo vinavyotakiwa ili siku moja wateuliwe kuwa majaji au wachaguliwe kuwa mahakimu.
Nasema kuwa idadi ya majaji wanawake ni ndogo, kwa mifano hai, mfano mmoja wapo unapatikana hapa Mahakama ya Rufani, mahakama hii ina jumla ya majaji 13 na watatu kati yao ni wanawake waliosalia ni majaji wanaume. Sasa hii ni tofauti kubwa sana.
Hapo awali Mahakama ya Rufaa ilikuwa na jaji mwanamke mmoja tu ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kuwa hakimu hapa nchini anaitwa Eusebio Mnuo, na Rais Jakaya Kikwete alivyoingia madarakani akateua majaji wawili katika mahakama hii nao ni Jaji Natalia Kimaro na Engela Kileo.

Swali: Ni changamoto zipi zinaikabili Mahakama ya Tanzania?

Jibu: Changamoto ni nyingi, moja ya changamoto kubwa inayotukabili ni kutoa haki zote katika mashauri ya jinai na madai haraka, kupiga vita rushwa na suala la rushwa nalitazama katika sehemu mbili ya kwanza ni rushwa ya kweli na ya pili rushwa ya kudhaniwa.
Hivyo watendaji wa Mahakama wanatakiwa waweke juhudi kwamba kusiwepo na mazingira ya rushwa ya kweli na ya kudhaniwa. Na changamoto ya tatu inayoikabili mhimili mahususi wa Mahakama ni kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wengi kwakuwa haki ina gharimu hasa inapokuja suala la mawakili, sasa tuhakikishe haki inapatikana kwa wote wenye madai yao mahakamani.

Swali: Hivi sasa kuna mchakato wa waumini na taasisi ya dini ya Kiislamu wanataka irejeshwe Mahakama ya Kadhi, nini msimamo wako na kama ikija itakaaje katika mtiririko wa mahakama?

Jibu: Kwa kweli kuhusu hili la Mahakama ya Kadhi siwezi kulizungumzia kwakuwa ninavyofahamu mimi suala hili lipo kwenye mchakato katika ngazi husika hata hivyo sina taarifa rasmi kama utekelezaji wa suala hilo umefikia wapi, hivyo binafsi siwezi kuzungumzia jambo kama sina taarifa za uhakika.

Swali: Huoni wakati umefika wa shughuli za Mahakama ya Tanzania kuendeshwa kwa Kiswahili ili wananchi waridhike na maamuzi yanayotolewa, kwakuwa hivi sasa mahakama zinaendeshwa kwa lugha ya Kiingereza na wananchi wengi wanaona hawatendewi haki na hasa unapofikwa wakati wa mawakili wa pande mbili wanapobishana kisheria wawapo mahakamani?

Jibu: Nakubali kwamba ipo haja ya kuendesha shughuli za mahakama kwa lugha ya Kiswahili. Na kwakweli tayari limefanyika hilo la kuendesha mahakama kwa kutumia lugha ya taifa, sasa hivi mahakama za mwanzo zinaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na sehemu kubwa ya Mahakama za Wilaya.
Lakini hata Mahakama ya Rufani tunaendesha Kiswahili inapobidi kuwa kanuni za Mahakama ya Rufani zinaruhusu kuendesha mashauri kwa Kiswahili au Kiingereza ila kumbukumbu lazima ziandikwe kwa lugha ya Kiingereza.
Na ninaamini ikitumika lugha ya Kiswahili mahakamani itaondoa manung’uniko ya wananchi na itasaidia watu waone haki inavyotendeka.

Swali: Huoni wakati umefika sheria zote za nchi ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili kama ilivyo Katiba ya Tanzania ambayo ndiyo pekee imeandikwa kwa lugha ya taifa?

Jibu: Katika hili siwezi kusema wakati umefika kwa sababu hadi sasa hakuna maneno ya Kiswahili yaliyowekwa katika lugha ya kitaaluma ya sheria (many legal technical terms yet produced) yakipatikana hapo tunaweza kusema wakati umefika sheria za nchi ziandikwe katika lugha ya Kiswahili.

Swali: Wadhifa huu mpya wa ujaji mkuu, huoni kwamba unaweza kukuzuia usiendelee kupiga kinanda kanisani?

Jibu: Kwanza kabisa kupiga kinanda nachukulia kama ibada, yaani kama vile ninavyokuwa na uhuru wa kwenda kusali hivyo ninao uhuru wa kuingia kanisani na kupiga kinanda.
Kwahiyo ieleweke uteuzi huu hautanizuia kupiga kinanda kwani hata nilivyokuwa Jaji Mkuu Zanzibar nilikuwa nahudhuria ibada na kupiga kinanda hata Jumapili ijayo (leo) nitakwenda kanisani St. Albano kusali na kisha nitapiga kinanda kama kawaida.
Enzi nasoma Tabora School ndipo nilipojifunza kupiga kinanda na mwanangu aitwaye Francis ndiye anayeonyesha kufuata nyayo zangu katika upigaji kinanda.
Licha ya kupendelea kupiga kinanda pia napenda kucheza mpira wa kikapu, na nimeanza kucheza mchezo huu tangu nasoma hadi nilivyokuwa ndani ya JWTZ niliupenda sana mchezo huu hadi nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Basketball Association (TABA, sasa BFT baada ya kuwa shirikisho) na mimi na wanamichezo wengine akiwemo Ofisa Habari na ofisa Utamaduni Manispaa ya Kinondoni Iddi Chaulembo, mwaka 1972 tulifufua chama hicho mkoani Iringa kitaifa.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana?

Jibu: Nimezaliwa Desemba 28, mwaka 1945 Zanzibar mjini nikiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane, wa kike wanne na wanaume wanne. Ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana.
Nimesoma shule mbalimbali za msingi Mpwapwa mkoani Dodoma 1952 -1953 nikaenda Town School-Tabora nikasoma darasa la tatu hadi la nne mwaka 1954-1956 na darasa la sita na saba nilisoma Kazel Hill sasa inatwa Shule ya Msingi Itetemia mwaka 1957-1958. Na darasa la nane tu mwaka 1959 nikarudi kusoma Mpwawa.
Mwaka 1960-1965 nilijiunga na Tabora School kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwakuwa nilifaulu nilichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966, na nilisoma shahada yangu ya Sheria na ilipofika Machi 1970 nilihitimu masomo.
Na mwishoni mwa Machi mwaka huo huo wa 1970 nikajiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), niliingia jeshini kama mwanasheria raia mpaka kipindi cha mafunzo ya kijeshi nikaenda kwenye mafunzo na kisha nikarudi kuitumikia JWTZ.
Ilipofika mwaka 1971 nikapewa kamisheni kambi ya Mgulani nikawa Luteni (nyota mbili). Nikaendelea na jeshi hadi mwaka 1977, nikahamishiwa Brigedi ya Faru-Tabora nikiwa na cheo cha Meja.
Sasa mwaka 1978, wewe mwandishi ulikuwa hujazaliwa, ndiyo mzee Aboud Jumbe Mwinyi, wakati huo akiwa ni rais akaniita Zanzibar na kuniteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na kipindi hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.
Aidha Oktoba 1978 niliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Na ilipofika Machi 1979 nilirudishwa JWTZ na baada ya muda mfupi nikapelekwa kwenye vita ya Uganda , nikiwa na cheo cha Luteni Kanali na kwenye vita hiyo nilikuwa naendesha mahakama za kijeshi.
Vita ilipokwisha nikarudi Zanzibar. Januari 8 mwaka 1980 nikaapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati huo nikiwa na cheo cha Luteni Kanali. Nikaendelea na Ujaji Mkuu Zanzibar hadi Septemba 1989 alipoapishwa Jaji Mkuu Zanzibar Hamid Mahamod Hamid.
Hata hivyo Juni 23 mwaka 1989 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania hadi mapema wiki hii nilivyoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Nilipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa Bara ndiyo sababu ya kuacha ujaji Mkuu Zanzibar.
Januari 1993 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na niliendelea na nafasi hiyo hadi Januari 2003 na Oktoba 2002 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambapo kipindi changu cha miaka mitano katika tume ZEC kinamalizika Oktoba mwaka huu.

Mwaka 1997 nilistaafu JWTZ nikiwa na cheo cha Brigedia, na niliagwa kwa heshima zote za kijeshi licha sikupewa mafao yangu kwakuwa mafao hayo yameunganishwa kwenye kazi yangu ya ujaji hivyo mafao yangu yote nitalipwa wakati nikistaafu kazi hii ya Ujaji Mkuu, kama mungu atanipa uzima.

Novemba 2001, niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki nafasi ambayo natakiwa nimalize kipindi changu cha miaka sita Novemba mwaka huu.
Nina mke mmoja ambaye Mungu ametujalia tumebahatika kupata watoto wanne, wawili ni wasichana na wawili ni wavulana.
Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Francis (30) huyu ni mwanasheria na anafanyakazi ya uwakili Manchester, Uingereza, Brigeth, huyu ana shahada ya Uandishi wa Habari na anafanyakazi ICAP hapa nchini, Marina ni mfamasia, yuko Liverpool, Uingereza na Mathew naye ni mfamasia, anafanya kazi Liverpool.”

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu: 0755 312 859, barua pepe: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 22,2007

4 comments:

Anonymous said...

Asante sana kwa habari hii. Imenisaidia kumfahamu Jaji A. Ramadhani.

Kazi njema!

Unknown said...

happy nimepitia mahojiano haya
muhimu.. safiiii sanaaaa
natumaini wadau wengi watasimama
hapa pia kucheki mambo yakoo...
kila la kheri...
www.haki-hakingowi.blogspot.com

kahangwa said...

kazi nzuri happy,
kupitia kwako tumemfahamu japo kiasi huyo mteule. binafsi ningetamani umwulize maswali ya nyongeza kwa kila jibu lake. matharani,antofautishaje utendaji wa mahakama ya kiraia na ya kijeshi;hao wanawe walioko majuu kwenda kwao huko kuna mahusiano yoyote na nyadhifa alizopitia;n.k?

Anonymous said...

Dada happy ungekuwa karibu ningekukumbatia kwa furaha endeleza wembe huohuo maana serikali yetu imevamiwa na vibaka wa uchumi,ila wasisahau hata mabutu alikwa na ngome nzito lakini wananchi wakisema ENOUGH IS ENOUGH waache waibe kwa sasa lakini vitawatokea puani itabidi tufilisi mpaka mali ya mjukuu ikibainika ilitoka kwenye serikali hiyo.Muganyezi

Powered by Blogger.