Header Ads

Profesa Chachage:Mbegu itakayoota kesho



Na Happiness Katabazi

KWA binadamu wanaozaliwa na mwanamke, wakaishi, wakafanya mambo yao, wakifa inaleta kihoro na msiba kwa watu wengi.

Lakini wapo wengine ambao utamani kuamini walizaliwa na mwanamke wakaishi katika jamii ya binadamu wakifa japo si mila njema kushangilia kifo, watu ukaa na kusema afadhali shetani kachukua mtu wake. Labda kila binadamu upenda kujua lipi kati ya haya mawili yatatokea siku ya kifo chake.

Na Julai 12 mwaka jana, katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walikusanyika watu wa matabaka yote, wenye hadhi, makabila na jinsia zote wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, walikuja kutoa heshima za mwisho kwa msomi.

Ni nani huyo? Si mwingine ni hayati Profesa Chachage Chachage (51).Chachage ni nani? Alifanya nini hata makundi hayo yakaitwa na kifo chake? Hakuna msomi mwingine ndani ya nchi hii ambaye kifo chake kilivuta wingi wa watu kama hawa.

Nilimfahamu Profesa Chachage. Naweza nikasema mimi nilikuwa ni mwandishi wa mwisho kuzungumza naye kuhusu fikra zake wakati alipokaribia kuhitimisha safari yake hapa duniani.

Ilikuwa ni Jumamosi, siku moja kabla ya kufa kwake, kiasi cha saa 4:30 hivi usiku nikiwa sebuleni nyumbani kwetu Sinza ‘C’. Nilipatwa na mshawasha wa kuzungumza kwa njia ya simu yangu ya mkononi na Profesa Chachage, ambaye alikuwa ni miongoni mwa vyanzo vyangu vya habari nyeti.

Ambaye kabla ya kukumbwa na mauti alikuwa akiniambia ataki katu katu kuitwa mwanaharakati, akitaka aitwe Mwanamapinduzi, kwa maelezo kwamba wanaharakati wengi ni wanafki na wasanii. Na kweli nikazoea kumwita jina hilo.

Kwa nini nilipata mshawasha wa kuzungumza naye siku hiyo? Mezani kwake, kulikuwa na maswali kadhaa ambayo nilikuwa nimemwandikia, nikitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa ajili ya habari na makala, ambavyo nilitarajia kuchapisha katika gazeti.

Nilizungumza naye kwa takriban dakika tano, kabla ya kuniambia kwamba muda huo alikuwa Kibaha, mkoani Pwani, kikazi. Baada ya kuniambia yuko Kibaha , nilipata hamu ya kutaka kujua kazi anayoifanya huko.

Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi juu ya shughuli iliyokuwa imempeleka huko. Hata hivyo kabla ya kumaliza mazungumzo yetu, alinidokeza kwamba katika safari hiyo alikuwa ameongozana na rafiki yake mkubwa, na ambaye pia alikuwa mtu muhimu kwangu katika kazi yangu ya uandishi wa habari, Dk. Abuu Mvungi.

Bila hiana, nilimwomba Profesa Chachage kunipatia simu yake ili naye nimsalimie. Alifanya hivyo, tukaanza kutupiana ‘madongo’ ya utani kama ilivyokuwa ada yetu pindi tunapokutana katika mihangaiko mbalimbali.

Baada ya kumalizana na Dk. Mvungi, Profesa Chachage alirudisha simu yake katika masikio yake, huku nikiendelea kumdadisi ni nini hasa kilichokuwa kimewafanya wanamapinduzi hao wawe Kibaha muda huo.

“Happiness, Jumanne nitakuwa ofisini. Usijali, njoo nakuahidi, kisha nitajibu maswali yako ambayo uliniletea wiki tatu zilizopita, usijali, ” aliserma.

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya mwisho ya Profesa Chachage.
Wapo waliomfahamu marehemu kama mwandishi wa vitabu, mwanafalsafa na mpenzi wa muziku wa Bongo Flavor.

Mimi nilimfahamu kama mtu mwenye fikra za kimapinduzi, mwandishi wa vitabu na mpigania haki na masilahi ya umma, mkweli.
Leo Watanzania wa kada mbalimbali hususan jumuiya ya wasomi, tunaadhimisha mwaka mmoja tangu kufariki kwake, Professa Chachage Seith Chachage.

Professa Chachage alifariki dunia ghafla Julai 9 mwaka jana, saa 5:00 usiku, akiwa katika ukumbi wa mikutano Kibaha, ambako alikuwa ameongozana na jopo la wasomi wanne waliopewa kazi mahususi, ya kuandika ripoti kuhusu hali ya Muungano na migogoro ya kisiasa Zanzibar na namna serikali inavyoweza kuitatua.

Kazi hiyo walikuwa wametumwa na serikali zote mbili, ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kabla ya kifo chake, habari zilisema Profesa Chachage alianza kulalamika kuhusu hali ya joto iliyokuwa katika chumba hicho cha mikutano, ingawa inaelezwa kwamba wasomi wenzake hao walimwona kama anatania kutokana na ukweli kwamba chumba hicho kilikuwa na ubaridi unaotokana na viyoyozi vilivyomo ndani ya chumba hicho, na vyote vikiwa vinafanya kazi barabara kiasi cha baadhi ya waliokuwamo kuhisi baridi kali.

Katika malalamiko hayo, ilielezwa kwamba Professa Chachage alichukua chupa ya maji, baada ya kunywa maji, habari zinasema aliendelea kutokwa jasho jingi, hali iliyomfanya asimame kitini kwake, akijaribu kujikongoja ili atoke nje kupata upepo.

Hata hivyo, kabla hajafika nje, ghafla alianguka na kupoteza fahamu. Hapo ndipo wenzake walizinduka na kuanza kushika hiki na kile kwa nia ya kunusuru uhai wake.

Kama wasemavyo wahenga, ‘siku ya kufa nyani miti yote huteleza’.
Siku na muda ambao Mwenyezi Mungu amepanga kuchukua roho ya mja wake, binadamu hawezi kuukwepa.

Akiwa njiani akipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha, alikata roho.
Huo ndio ukawa mwisho wa safari ya maisha yake duniani, Profesa Chachage, kipenzi si cha jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanafunzi wa Idara ya Sosiolojia waliopo na waliopita.

Nikiri kwamba pamoja na kulisikia jina la Profesa Chachage tangu nikiwa katika Shule ya Msingi Mugabe, jijini Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza nilishikana mikono na profesa huyo mwaka jana kabla ya kifo chake.

Ilikuwa Jumamosi moja, Januari mwaka jana, saa moja jioni, pale UDASA Club. Aliyenikutanisha ana kwa ana na bingwa huyu wa sosiolojia ni aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria wakati huo, Dk. Sengondo Mvungi.

Tangu siku hiyo, hadi kifo chake, Profesa Chachage na mimi, tuliishi kama chanda na pete.

Katika mambo ambayo sitayasahau, ni msimamo wake kuhusu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Uhandisi ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo Rais Kikwete alikifungua mwaka jana.

Enzi ya uhai wake, alitaka kuwe na utaratibu mzuri unaolinda masilahi ya wasomi kwa maana kwamba wasomi walipwe vizuri ili waweze kuishi kutoka na utaalamu wao badala ya hali ilivyo hivi sasa, ambapo wasomi wanajikuta wakiwa wabangaiza mitaani, wakifanya biashara ya kuuza machungwa, mchicha au kufuga kuku, ng’ombe na nguruwe ili waweze kujikimu.

Kwa hiyo, ndiyo maana hayati Profesa Chachage alisimamia kidete suala la mishahara na masurufi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tunaweza kusema kwamba wasomi wa UDSM walimtambua kwa hilo na walimuunga mkono, na hadi sasa wameshapata awamu ya kwanza ya nyongeza ya mishahara waliyoahidiwa na serikali.

Kuhusu suala la wasomi kulitumikia taifa lao kizalendo, huo ndio ulikuwa msimamo wake kiitikadi kwamba katika kila taifa wasomi lazima wawe wana mageuzi wanaotetea haki za walio wengi.

Hilo hata yeye mwenyewe katika uhai wake hakuweza kulifanikisha, japo aliandika mengi akilipigania hilo. Hakulifanikisha kwa sababu linahitaji pawepo idadi ya kutosha ya wasomi wenye msimamo huo ili waweze kulitekeleza.

Hivi sasa wasomi walio wengi wanapendelea kujiunga ama na CCM, kuunga mkono sera zake, au kukaa kimya ili kutetea masilahi yao binafsi na kushibisha matumbo yao na familia zao.

Wasomi wengi hivi sasa wanadhalilisha taaluma zao kwa kuunga mkono au kutumika kubuni miradi ya kifisadi na ya kuuza nchi, na wanafahamika.

Nitaendelea kumkumbuka na kuheshimu mchango wa Profesa Chachage kwa vitendo, kwani nakumbuka katika uhai wake alijaribu kutetea nafasi ya vyuo vikuu kuhusu mfumo wa elimu.

Yeye alisimama kidete kupambana na mrengo wa kibwanyenye unaotaka kugeuza vyuo vikuu kuwa taasisi za kufanyia miradi ya kiuchumi.

Na katika hili, alipambana na katiba mpya ya chuo iliyokuwa ikipendekezwa na enzi za uongozi wa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Methew Luhanga, ambayo ingekigeuza chuo kuwa taasisi ya kibiashara badala ya wajibu wake wa kutoa elimu ya juu na kufanya utafiti.

Katika harakati zake hizo aliwaongoza na kuwashawishi wasomi katika chama chao cha (UDASA) na katika chama cha wafanyakazi wa (RAAWU) kupinga katiba hiyo.

Hata hivyo katiba mpya ya chuo hicho imepatikana baada ya yeye kufariki.

Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walionyesha dhahiri kumkubali na kumuenzi mwanamapinduzi huyu kwa sababu walikubali kuanzisha Mfuko wa Profesa Chachage, kwakukatwa mishahara yao.

Wasomi wa UDSM wana haki ya kumuenzi marehemu Chachage, labda enzi za uhai wake alifahamika kwa watu wengi lakini mambo yalivyo, mwanamapinduzi huyu atapendwa zaidi na Watanzania baada ya kifo chake.

Yale aliyoyapigania na hayakupatikana katika uhai wake na wala Tanzania ya leo haitapa faida ya mchango wake.

Hata hivyo kesho watapatikana kina Profesa Chachage wengine watakao chukua kurunzi aliyoiwasha kuwaangazia Watanzania wa kizazi chao kuona njia ya kufika kwenye maendeleo.

Profesa Chachage, sasa marehemu ametoka wapi?
Alizaliwa Januari 8, mwaka 1955 katika Kijiji cha Mtwango, wilayani Njombe, Iringa.

Kwa asili, yeye ni kutoka kabila la Wabena, ambalo ni moja ya makabila makubwa mkoani humo, ukiacha Wahehe.

Si siri, marehemu alikuwa ni mwanamapinduzi wa kweli na asiye na woga katika kutetea haki na masilahi ya umma na itachukua muda mrefu kumpata msomi mwenye sifa kama za marehemu.

Pia kifo chake ni pigo kwa jumuiya ya wanachuo, duru za wasomi ndani na nje ya nchi.

Profesa Chachage, ambaye ameacha mjane na watoto wanne, kwa mara ya kwanza alitunukiwa shahada ya kwanza ya Sosiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1982.

Baada ya ya kuhitimu, na kuwa miongoni mwa wanafunzi bora alipewa kazi ya kufundisha shuleni hapo akiwa kama Mkufunzi Msaidizi, kabla ya kuendelea na masomo ya shahada ya pili na ya uzamili chuoni hapo katika fani yake hiyo mwaka uliofuata.

Mwaka huo wa 2000, akiwa na cheo chake hicho cha Profesa Mshiriki, Chachage alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na akakabidhiwa dhamana ya kuongoza kitengo cha Utafiti na Uchapishaji cha chuo kikuu hicho hadi 2003.

Kuanzia mwaka 2003 hadi anafariki dunia, Profesa Chachage alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Sosiolojia na pia Mwenyekiti wa UDASA.
Lakini pia, Profesa Chachage ameandika mada na vitabu kadhaa, ambavyo vitatumika katika vyuo vikuu na vyuo vingine vya elimu ya juu nchini.

Moja ya vitabu na mada zake zilizotia fora katika ulimwengu wa mazingira ya Tanzania, ni Makuadi wa soko huria, ambacho, pamoja na mambo mengine, Profesa Chachage anayaangalia madhira ya wakulima wa korosho wanayoyapata kutokana na sera mbovu za nchi, dhidi ya wanunuzi wa zao hilo.

Vitabu vingine ni pamoja na Honourable Teacher (Mheshimiwa Mwalimu), Dhima ya Fasihi na Sudi ya Yohana, ambavyo amevitunga katika mfumo wa hadithi. Pia vipo Fasihi na sanaa na uhusiano wake na Kiswahili, Kivuli na almasi za bandia.

Profesa Chachage, binafsi nakutakia mapumziko mema huko uliko. Najua utakutana na wana mapinduzi magwiji, kama Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba na wengine wengi.
Usisahau kuwaeleza mbinu mpya ya ukoloni unaolinyemelea Bara la Afrika.

Pia umweleze Mwalimu Nyerere kile chama chake alichokiasisi cha CCM, kimejaa makundi madogo na makubwa, lililoyafunika kwa sasa ni kundi la ‘wanamtandao’ na si tena chama cha wakulima na wafanyakazi, bali hivi sasa chama hicho ni cha wafanyabiasha na matajiri.

Aidha, umweleze kwamba makada wa chama chake wengi wao hawawezi kugombea nafasi za uongozi bila kupewa baraka na ‘sangoma’.

Pia hivi sasa ni nadra sana kuwa kiongozi kama si mwanamtandao, mpika majungu, mfitini na bingwa wa kutumia vyombo vya habari ili vikupambe.

Nilazima pia uwe hodari na mahiri wa kujikomba kwa wakubwa na kuwasifia hata kama utendaji wao ni mbovu.Tafadhari usisahau kumweleza haya.

Umweleze ile migomo ya vyuo vikuu inaendelea kama kawaida na ubinafsishaji na uingiaji wa mikataba yenye utata imeshika kasi.

Pia umweleze hivi sasa tofauti kati ya maskini na wenye nacho, ambayo alikuwa akiipinga kila siku hivi sasa imeanza kuota mizizi.

Najua umekutana na wasomi wenzako kutoka pande nne za dunia pamoja na walalahoi kadhaa waliopoteza maisha kutokana na taabu walizozipata katika harakati zao za kutetea mazingira mazuri na bora ya elimu, ambayo sasa yameanza kuharibiwa na mitazamo pamoja na sera mbovu za wanasiasa na watunga sheria.

Mwisho kabisa, pamoja na pengo kubwa uliloliacha kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na familia yako, lakini kumbuka kwamba wale marafiki zako tuliokuwa tukikata karibu usiku mzima kutakiana heri kwa kugongeana bilauri, nasi umetuacha taabani.

Mimi nitaendelea kukuenzi daima kwa kuandika ukweli na kukemea maovu kama ulivyokuwa ukiniusia kila mara.

Naahidi kuwa jasiri kwa kusema na kuandika ukweli katika kutetea masilahi ya wanyonge wa nchi yetu.

Profesa Chachage ambaye alizikwa kijijini kwake Mtwango, Njombe, mkoani Iringa, atakumbukwa pia na wale aliokuwa akichangia nao katika ‘upigaji pafu’ wa sigara.

Hao nao wataendelea kukulia na kuuenzi mchango wako, umewaacha bila mlezi wala mshauri. Watakukumbuka daima.

Mungu alikuumba na akakutwaa. Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahala pema peponi.

Amina.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu Julai 9,2007

No comments:

Powered by Blogger.