Header Ads

CCM IJIFUNZE ALAMA ZA NYAKATI

Na Happiness Katabazi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetokana na chama cha TANU na Afro-Shiraz, vilivyokuwa vikiamini na kuhubiri kuwa rushwa ni adui wa haki.

Wakati wazee wetu wakipigania uhuru na hata baada ya kupatikana, mahubiri ya viongozi wetu wa CCM na serikali yao yalikuwa yakikisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki.

Miaka michache iliyopita, CCM iliwashangaza Watanzania iliposema rushwa ni takrima. Hili liliwashangaza wengi kwa sababu katika historia ya taifa hili na katika miaka 45 ya uhuru wa nchi yetu, hakujawahi kutokea mabadiliko ya kuhalalisha rushwa mpaka hivi majuzi CCM ilipotamka kuwa rushwa ni takrima, na kwamba ni utaratibu wa Kiafrika kumkarimu mtu.

CCM ililivalia hili njuga na kulipeleka bungeni, na kwa sababu ndiyo chama dola, likapita, ikawa sheria ya nchi. Kwa kuwa wapinzani bungeni ni wachache, hawakuweza kuuzuia muswada ule usiwe sheria, ikatumika turufu ya wengi wape.

Wanaharakati wakaichachamalia sheria ile na kuipeleka mahakamani, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Nola vikapaza sauti kwa nguvu kuipinga sheria hiyo. Mahakama ikasikia kelele hizo, ikatamka kwamba vipengele vya takrima kwenye sheria ya uchaguzi vinahalalisha rushwa, na hivyo ni kinyume cha katiba ya nchi.

Hii maana yake ni kwamba, CCM na serikali yake, vilikuwa vimehalalisha rushwa, na kwa maana nyingine ni kwamba, wale wote walio bungeni walikuwa wamepata uongozi kwa rushwa.

Ukiihalalisha rushwa kwenye uchaguzi, utapata viongozi wa aina gani? Ikiwa uongozi unaweza kupatikana kwa fulana, kofia, pilau, fedha n.k je, unaweza kusema tuna uongozi wa kiadilifu?

Siku zote uongozi uliopatikana kwa rushwa, huzaa serikali ya wala rushwa. Takrima iliyohalalishwa na serikali yetu, ndiyo matokeo ya ufisadi unaojionyesha hivi sasa serikalini. Tujiulize, kama tuna viongozi walioingia madarakani kwa kutoa takrima, ufisadi unaoiandama serikali yetu utakwisha?

Unaweza kuueleza vipi uongozi unaopora nyumba za serikali, kisha kuanza kupangisha maofisa wa serikali kwenye mahoteli ya kitalii kwa mabilioni ya fedha za walipa kodi?

Sasa Watanzania wanajiuliza, kwa nini mikataba ya madini inatiwa saini kwa siri? Wanajiuliza kwa nini madini kama dhahabu, tanzanite n.k hayawaletei manufaa Watanzania, badala yake yanawanufaisha wageni na makuadi wao wenyeji?

Lakini Watanzania tunasahau wale tuliowakabidhi madaraka, wanahitaji kurejesha fedha zao walizonunulia uongozi. Hii ndiyo siri ya mikataba kuwekwa saini kwa siri vichochoroni na katika mahoteli ughaibuni.

Hivyo hakuna sababu ya kushangaa kwanini serikali inashiriki kwenye rushwa, kwa sababu hao tuliowakabidhi madaraka wanatumia nafasi zao za uongozi kufanya biashara za kifisadi ili pesa yao irudi katika kipindi kifupi, na wajilimbikizie nyingine za kununulia kura kwenye uchaguzi ujao.

Leo hii tunapigia kelele rushwa ndani ya CCM, lakini ile kashfa ya rushwa na ufisadi katika ununuzi wa rada, IPTL, BoT zimeishia wapi? Tunapigia kelele rushwa katika uchaguzi wa CCM wakati tumefumbia macho rushwa ya Richmond.

Mbona Watanzania tumekuwa taifa linaloongozwa kwa jazba za msimu, kwa maana kwamba tumekuwa wepesi kusahau haraka hoja ya leo mara jambo jipya linapoibuka.

Hebu turudi kwenye hoja yetu ya msingi, hawa wanachama wa CCM wanaolalamika kuwa wenzao wametoa rushwa, akiwemo Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa na Katibu Mkuu wa CCM, mstaafu Philip Mangula ni vyema tuwasikilize.

Wanachosema ni kweli, kwa vile tunawajua ni watu wazito ndani ya CCM, hatuhitaji ushahidi mkubwa zaidi kwamba CCM inanuka rushwa.

Lakini mbona waheshimiwa hawa wanatetea haki hiyo ndani ya chaguzi za CCM tu? Mbona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais hatukuwaona makada na wanachama wa CCM wakivalia njuga kupiga vita rushwa? Au mkuki kwa nguruwe mtamu, lakini kwa binadamu mchungu?

TAKUKURU sasa imewakamata na imesema itaendelea kuwakamata watoa rushwa na tayari imeishawafikisha mahakamani baadhi ya wabunge wa chama hicho na wengine kuwaachia, hilo ni jambo zuri na la kusifiwa kwa sababu unapokuwa na chama tawala kilichojaa wala rushwa, ni dhahiri kitazaa serikali ya wala rushwa.

Lakini TAKUKURU mbona haikufanya hivyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka juzi? Au wanafanya hivyo kwa sababu Rais Jakaya Kikwete kasema hataki rushwa? Je, Kikwete asingesema wangefanya kamatakamata hiyo?

Jambo jingine ambalo ni jema lililotokana na uchaguzi ndani ya CCM, limetuonyesha kwamba kile ambacho CCM imekuwa ikiwashutumu wapinzani kuwa wanaking’ang’ania kimejidhihirisha kuwa kweli, kwamba kumbe hata miongoni mwa wanachama wake wakiwemo viongozi ni walafi wa madaraka.

Hawakubali kung’atuka, wanahodhi vyeo ndani ya CCM kama vile wameumbiwa na Mungu vyeo hivyo na hakuna mwanachama mwingine mwenye haki ya kuvishika vyeo hivyo.

Inashangaza kwa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM - Taifa, Philip Mangula, ambaye alitangaza kung’atuka katika siasa kwenda kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa Iringa, pia wapo ambao walikwishakuwa na nyadhifa za Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Katibu Mwenezi Mkoa au Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa zaidi ya miaka kumi, lakini bado wanang’ang’ania na kugombea tena.

Ingawa ni haki yao kugombea, lakini wanaong’ang’ania kufanya hivyo ili kulinda maslahi binafsi, hawa kamwe hawapaswi kuvumiliwa.

Kimsingi matokeo ya vigogo kugaragazwa, ni karamu ya wapiga kura, ni ushindi kwa wanademokrasia ndani ya CCM.

Lakini pia inawezekana ikawa hizi ni dalili za mwanzo za chama hiki kumeguka na kuwa
katika kambi mbalimbali zinazogombea madaraka, ikizingatiwa kuwa wanamtandao wana haraka ya kujijenga na kutwaa hatamu za uongozi wa chama wakati wakongwe hawajawa tayari kung’atuka.

Uchaguzi wa CCM haujaonyesha kama chama sasa kitakuwa bora kuliko kilivyokuwa awali, ubora wa viongozi wapya bado haujaonekana, hivyo hatuna sababu ya kuwaweka katika mizani ya juu kwa sifa, hatutajua wanatofautiana nini na waliowatangulia.

Nashawishika kuamini kuwa, viongozi wapya hawana agenda ya kuliletea taifa hili heri. Tunachokiona ni mabadiliko ya sura na jinsia, lakini wanachopigania ni kupata fursa ya kupora, kujilimbikizia mali na vyeo.

Kwani waziri kuwa mjumbe wa NEC, ni ajabu, kwa sababu haifahamiki atawasaidia vipi wananchi, kama si kujiimarisha ndani ya chama chake ili awe kwenye kinyang’anyiro cha urais?

Tunachokiona ni wabunge, manaibu waziri na mawaziri wengi kuomba uongozi ndani ya chama, hasa nafasi ya ujumbe wa NEC ili waweze kujilimbikizia madaraka vizuri, hawa nawaita walafi na hawana jipya, isipokuwa kuweka sawa matumbo yao.

Natuma salamu zangu kwa wanasiasa wakongwe walioangushwa kwenye uchaguzi huu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, ambaye amekuwa mwanachama wa TANU tangu mwaka 1960 hadi 1977 na mwanachama mwanzilishi wa CCM .

Pia amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 37 sasa, pamoja na nyadhifa nyingine za juu alizowahi kushika tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka sasa.

Pia Philip Mangula, aliyekuwa mwalimu wa siasa katika kilichokuwa Chuo cha Itikadi Kivukoni, baadaye Mkuu wa Mkoa na kisha akawa Katibu Mkuu wa CCM Taifa kwa kipindi chote cha uongozi wa Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Benjamin Mkapa. Na wengine wote waliongushwa katika kinyang’anyiro huku wakiwa wamekaa madarakani kwa muda mrefu, someni alama za nyakati!

Nawapa pole kwa vile ninyi ni wahanga wa ari, nguvu na kasi mpya. Msife moyo, kwani hao waliowagalagaza nao siku yao inakuja, waswahili wanasema “mwosha huoshwa, tena akioshwa hulipuliwa”. Kama waliwaondoa kwenye kinyang’anyiro kwa hila, basi ipo siku nao watafanyiwa hivyo hivyo au zaidi ya hivyo.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

0755 312 859;katabazihappy@yahoo.com;
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Septemba 16,2007

4 comments:

Anonymous said...

Nimependa sana kusoma makala yako katika toleo hili. umesema kweli kabisa kuwa watu walio ndani ya CCM wanapaswa wasilalamike kuwa rushwa ipo ndani ya CCM. Kwa kwa kuwa wao ndio walioasisi rushwa hiyo then umesema kweli kuwa wao ndio wanaotoa rushwa katika uchaguzi huko Tanzania . Napenda sana makala yako na Mungu akubariki sana.
Josh Michael
colorado USA

Anonymous said...

Nam! hakika makala hii ni nyeti!

Hatuna budi kuyakubari wayasemayo wapinzani, wanaharakati na wengine japo wachache wenye kuona mbali na walio na uchungu na Taifa hili.

Mimi ninacho mshukuru mungu ni kwamba, anazidi kufichua ama kuanika na kudhihilisha kile wanacho kisema wazalendo!

Mwenyezi hujidhihilisha kupitia njia zisizo fikirika kirahisi.

Nina imani pia kuwa tutazidi kuona na kusikia mengi siku za usoni!

Kwa Wapenzi wote, wenye kuitakia mema na wanao penda kuiona nchi hii ikipiga hatua ya maendeleo ya watanzania (Wote)ambao leo hii tu-hohe hahe,....Muumba awazidishie heri katika kila jambo katika kuinusuru Tanzania!

Shukurani kwako H.Katabazi nawe mtanzania mwenye machungu ya kuona kuwa siku moja Tanzania inanukia marashi na SIYO rushwa na Maisha ya heri kwa wanchi yao Tanzania.

Anonymous said...

Congrants Happiness,
I am really impressed by your articles and i feel we need to go further and understand the root cause of some of the problems that have been going on for a long time.
I think what we need more on your blog, is a clear cut analysis on the current issues, how did we get ourselves there and how we are going to overcome these issues that have been decapitating the economy of our beloved country.Otherwise, i am such a fun and i wish you well...tuku pamoja ...aluta continua
George in Bermuda

Anonymous said...

tunamshukuru haki ngowi kwa kutupa hamasa kila mara kupitia hapa kila unapo andika makala mpyaa. ni ushirikiano mzuri ulioje..
happines kazana tupo nyuma yako

Powered by Blogger.