Header Ads

HAKIMU AKWAMISHA KESI YA KIBANDA

Na Happiness Katabazi UPANDE wa Jamhuri katika kesi kuruhusu na kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na wenzake jana ulijikuta ukishindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kama ilivyopangwa kwasababu Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Waliarwande Lema kuwa na udhuru. Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda mbele ya Hakimu Binge Mashabara aliikumbusha mahakama kuwa kesi jana ilikuja kwaajili kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali na kwamba wao upande wa jamhuri wapo tayari kwaajili ya kuwasomea maelezo hayo ya awali. Lakini Hakimu Mashabara alisema upande wa jamhuri hautaweza kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kwasababu hakimu Lema ambaye ndiye anayesikiliza kesi hiyo tangu ilipofunguliwa yupo nje ya ofisi amekendwa kuudhuria semina na hivyo anaiarisha kesi hiyo hadi Mei 15 mwaka huu. Mbali na Kibanda washtakiwa wengine ni mwandishi wa makala hiyo Samson Mwigamba na Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando, Juvenalis Ngowi, Isaya Matamba, John Mhozya na Frank Mwilongo. Machi 7 mwaka huu, Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda. Shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake ni la kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti Na.229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwamba Novemba 30 mwaka 2011, Makunga akiwa na wadhifa huo alichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011, iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Magereza na Polisi wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Aprili 25 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.