KAJALA ALIA SEGEREA SIYO SEHEMU YA MATANUZI
Happiness Katabazi
MSANII wa filamu nchini, Kajala Masanja, jana alimwaga machozi na kuujia juu upande wa jamhuri katika kesi inayomkabili ya utakatishaji fedha haramu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akiushinikiza ulete mashahidi haraka kwani mahabusu anakoishi siyo sehemu ya starehe.
Kajala alitoa shinikizo hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, muda mfupi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rsuhwa (TAKUKURU), Leonard Swai, kuikumbukusha mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao, lakini akadai hilo halitaweza kufanyika, kwa sababu hajaja na mashahidi na anaomba kesi hiyo iahirishwe.
Baada ya wakili huyo kumaliza kutoa maelezo hayo, ndipo Kajala akanyosha kidole na kuomba ruhusa ya mahakama ili aweze kuzungumza jambo.
“Mheshimiwa hakimu, hivi huyu wakili wa serikali anafikiri kule Segerea ninakoishi kwa sasa ni sehemu ya starehe? Mahabusu kunatisha, wewe wakili wa serikali lete mashahidi kesi isikilizwe,” alidai Kajala huku akitokwa na machozi.
Kwa upande wake, Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 9 ambapo upande wa jamhuri unatakiwa ulete mashahidi wake ili waanze kutoa ushihidi.
Machi 27, mwaka huu, ilidaiwa na wakili Swai kuwa mbali na Kajala, mshtakiwa mwingine ni mumewe, Faraja Chambo, wanakabiliwa na makosa matatu, kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama la kuhamisha umiliki wa nyumba iliyoko Kunduchi Salasala, eneo ambalo halijapimwa jijini Dar es Salaam.
Shtaka la pili ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010, walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo, ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa Emilian Rugalia, ambaye ndiye waliyemuuzia kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007. Na shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha, ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14, 2010 huku wakijiua ni kinyume cha sheria hiyo.
Chambo naye yuko mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, kwa sababu anakabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha haramu, iliyofunguliwa mahakamani hapo, ambapo kwa mujibu wa sheria, kosa hilo halina dhamana.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei Mosi mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment